Mwalimu Bahati
Kilungu Maziku.
Waganga wa jadi Elizabeth
au Shija Makandi Sweya (kushoto) na Regina
au Tatu Kashinje Nhende.
Bilia
Masanja Mhalala
Mganga wa jadi Abubakar Ally Magazi
Muhoja
John Shija
Na Daniel
Mbega, Kahama
WATU sita,
akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Katunguru iliyoko Kata ya Wendele, Tarafa ya
Msalala wilayani Kahama, wamekamatwa mjini hapa wakiwa na vipande sita vya
mifupa inayodhaniwa kuwa ya albino.
Taarifa zilizopatikana
mjini hapa zimeeleza kwamba, mwalimu huyo Bahati Kilungu Maziku (56), Msukuma
na mkazi wa Mtaa wa Mbulu katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, amekamatwa akiwa
na watu watano, wakiwemo waganga wa jadi watatu, katika harakati za kuuziana
mifupa hiyo.
Wengine waliokamatwa
ni mganga wa jadi Bi. Elizabeth au Shija Makandi Sweya (42), mkazi wa Busongwahala,
Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Bilia
Masanja Mhalala (39), Msukuma, mkulima na mkazi wa Mogwa wilayani Nzega, mke wa
Biria ambaye ni mganga wa jadi Regina au Tatu Kashinje Nhende (40), Msukuma na
mkazi wa Mogwa.
Aidha,
watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Muhoja John Shija (24), Mnyamwezi na mkazi
wa Isagenhe wilayani Nzega pamoja na mganga wa jadi na mfanyabiashara Abubakar
Ally Magazi (25), Mrundi na mkazi wa Nzega.
Taarifa za
uchunguzi wa awali zinaeleza kwamba, Mwalimu Bahati ndiye aliyesuka mpango
mzima akishirikiana na waganga wa jadi Bi. Shija Makandi ambaye ndiye
aliyeitafuta mifupa hiyo na Abubakar Magazi ambaye alikuwa apelekewe ili ‘kuibetua’
(kuitengeneza) na kuzalisha fedha.
Watuhumiwa
watano wanadaiwa kwamba walifunga safari kutoka Nzega hadi Kahama kwa Mwalimu
Bahati, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya awali, ndiye aliyejua ni wapi ambako
mifupa hiyo ingeuzwa, hivyo walikuwa wanakutana hapo kwa ajili ya kugawana
fedha.
Mifupa hiyo
inadawa kuhusishwa na tukio la kukatwa mkono wa kulia Bi. Muungu Masaga Gedi
(35) mwenye albinism, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata
ya Igoweko wilayani Igunga, ambalo lilitokea Mei 16, 2014 na kufunguliwa Jalada
Namba IGU/IR/1070/2014.
Katika tukio
hilo, mume wa majeruhi huyo, Mapambo Mashili, aliuawa kwa kukatwa mapanga na
watu wasiofahamika wakati akipambana na watu hao wasimdhuru mkewe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP
Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 21, 2015 na kwamba watu hao walikamatwa saa 7:00 mchana katika nyumba moja
ya kulala wageni inayofahamika kwa jina la Maji Hoteli iliyopo Phantom, Kata ya
Nyasubi mjini Kahama baada ya Polisi kuweka mtego kufuatia taarifa za
wasamaria wema.
Taarifa ya Kamanda
Kamugisha imesema kwamba, mnamo Mei 19, asubuhi, mkuu wa upelelezi wa Wilaya
ya Nzega alipata taarifa kuwa kuna mtu anauza viungo vya albino, ndipo walipoweka
mtego. Hata hivyo, alisemai kuwa walishindwa kuwakamata na baadaye mtu huyo
alihamishia biashara hiyo wilayani Kahama.
Hata hivyo,
jeshi la polisi bado linaendelea na msako dhidi ya watu wengine wanaotajwa
kwamba ndio walioitafuta mifupa hiyo, na kwa mujibu wa taarifa za awali, ndio
waliohusika na mauaji pamoja na kumjeruhi mama huyo.





No comments:
Post a Comment