Sehemu ya jengo la Mapokezi na Nyumba ya kulala watalii hifadhi ya taifa Gombe iliyoko mkoani Kigoma.
Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe akitoa ufafanuzi juu ya hifadhi hiyo kwa mwandishi wa makala hii
Kiongozi mkuu wa Sokwe Mtu 110 walioko katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe mkoani Kigoma akifahamika kwa jina la Ferdinand ana miaka 57. (Picha zote na Hastin Liumba, Kigoma).
Na Hastin Liumba, KigomaHIFADHI ya Taifa ya Gombe ni moja kati ya Hifadhi (16) za Taifa Tanzania,ambapo Hifadhi ya hii ni moja kati ya hifadhi mbili za Taifa Tanzania ambazo zinaambaa na Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 56.
Hifadhi hii ni miongoni mwa Hifadhi tatu za Taifa Tanzania ambazo kuna wanyama adimu wanaoitwa Sokwemtu, nyingine ni Mahale mkoani Kigoma na Kisiwa cha Rubondo katika Ziwa Victoria Mkoani Mwanza.
Hayo yameelezwa na kaimu mhifadhi wa hifadhi ya Gombe Susuma Kusekwa alisema hayo wakati akiongea na mwandishi wa makala hii baada kutembelea hifaadhi hiyo hivi karibuni.
Kusekwa anasema Hifadhi ya Taifa ya Gombe ilianzishwa mwaka 1943 kama Pori la Akiba (Game Reserve) baada ya kuwaondoa wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya eneo hilo mwaka 1942.
Anabainisha mwaka 1960 mtafiti Mama Jane Goodall ambaye ni Mwingereza alifika Gombe na kuvutiwa na kuguswa na uhifadhi wa Sokwemtu na hivyo kuanza shughuli za utafiti wa wanyama hawa adimu.
Mhifadhi huyo alisema ilipofika mwaka 1965 juhudi za mama huyu Jane zilileta matunda ya kuanzisha kituo cha utafiti wa Sokwemtu na mazingira yake.
Aidha ndani ya miaka mitatu baadaye 1968 eneo hili lilipandishwa hadhi na kuwa ‘Hifadhi ya Taifa’ na juhudi zaidi ziliongezeka kwa kushirikiana kati ya watafiti na uongozi wa Hifadhi kuzoesha Sokwemtu kuwakaribia wanadamu ili waweze kutumika kwa shughuli za utalii na ndipo baada ya miaka kumi baadaye mwaka 1978 shughuli za utalii zilianza.
Alisema kwa ujumla hifadhi hii ni ya kujivunia kutokana na mambo mengi yaliyopo ambapo Hifadhi ipo kilomitam 16 Kaskazini mwa mji wa Kigoma (ni rahisi kufikika) ikiambaa na ziwa Tanganyika kwa umbali wa kilomita 14 (kuanzia pale kwenye mpaka wetu na kijiji cha Mtanga hadi mpaka wetu na kijiji cha Mwamgongo.
Anaongeza Hifadhi hii inapakana na vijiji vipatavyo vitano vikiwemo Mwamgongo, Mtanga, Mgaraganza, Bubango na Chankele ambapo wakazi wake shughuli zao kubwa ni Uvuvi.
Mhifadhi huyo Hifadhi haipo mbali na nchi za jirani za Burundi kwa upande wa Kaskazini ambapo ni mwendo wa saa moja na nusu kwa boti za kawaida zinazoendeshwa kwa injini.
Alisema upande wa Magharibi Hifadhi inapakana na Ziwa Tanganyika na baada ya Ziwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kusini mwake ikiwemo Zambia.
Aidha aliogeza nchi hizo zote zina eneo la Ziwa kwa mgawanyiko ambapo nchi ya Tanzania ni asilimia 41, Kongo asilimia 45, Burundi asilimia 8 na ni asilimia Zambia 6.
Alisema Ziwa Tanganyika ni la kwanza kwa urefu duniani likiwa na ukubwa wa kilomita 673 na la kwanza duniani kwa ujazo wa maji baridi takribani Kilomita za ujazo 18,900.
Alisema ziwa lina hifadhi 17 ya maji baridi duniani, pia kina chake ni cha pili kwa ukubwa mita za ujazo 1,470 duniani baada ya Ziwa Baikar lililopo nchini Urusi ambalo lina kina cha 1,700.
‘Tunafurahi kuona sehemu ya Ziwa Tanganyika imehifadhiwa katika kiwango cha juu ambapo Hifadhi ya Taifa ya Mahale ina sehemu yenye ukubwa wa kilometa za mraba 96 za maji na Gombe kilometa za mraba 21 za maji.
Aidha anasema Inaaminika zipo aina zaidi ya 340 za viumbe hai ambapo zaidi ya aina 300 ni za samaki katika ziwa Tanganyika na asilimia kubwa ya samaki hao hawapatikani penginepo duniani na viumbe wengine ni pamoja na nyoka wa kwenye maji, mamba, viboko na vyura.
Anasema ni miongoni mwa Hifadhi Tatu za Taifa Tanzania ambazo zina wanyama hawa adimu Sokwemtu wapatao 110 nyingine ni Mahale ikiwa na Sokwemtu wapatao 800, na Rubondo Sokwemtu wapo 30.
Kusekwa anaongeza na hivyo kufanya idadi ya Sokwemtu 940 kuwa ndani ya mipaka ya hifadhi ambayo inalindwa katika ngazi ya juu ya sheria mama ya Hifadhi za Taifa Tanzania.
Anasema kati ya Sokwemtu 2,606 tu walioko nchini Tanzania, 1,666 wapo nje ya mipaka hii ya Hifadhi za Taifa Tanzania na ni maeneo hatarishi ya Masito Ugala yaliyozungukwa na makambi ya wakimbizi na kingine ni utafiti wa Sokwemtu umeanza tangu miaka ya 1960.
Anasema sifa nyingine ina vyanzo vingi vya maji vinavyotokea Hifadhini na kumwaga maji Ziwa Tanganyika yakiwemo maporomoko ya kuvutia ya Kakombe na Mkenke.
Aidha aliongeza Hifadhi ina sehemu ya maji ya Ziwa Tanganyika ambalo lina sifa za kipekee duniani ambapo ni ziwa refu kuliko yote duniani likiwa na umbali wa kilomita 673 kutoka Kaskazini hadi Kusini mwa Ziwa.
Kingine anabainisha ni la pili duniani kwa kina kirefu cha kilomita 1.47 likifuatia baada ya Ziwa Baikar lililopo Urusi mkoa wa Syberia likiwa na kina cha kilomita 1.7.
Aidha Kusekwa anaongeza ni la kwanza duniani kwa ujazo wa maji baridi, kilometa za ujazo 18,900 sawa na 17 ya maji baridi duniani na si hivyo tu lina aina mbalimbali za samaki zaidi ya aina 300. Na wako viumbe wengine wa majini kama mamba, viboko, nyoka aina ya cobra wa majini na vyura.
Shughuli za Hifadhi
Kusekwa anasema shughuli za Hifadhi zimegawanyika katika makundi mbalimbali kama ulinzi (Protection), ikolojia, ujirani mwema, utalii na utafiti chini ya Taasisi ya Jane Goodall (JGI).
Anasema Hifadhi imeendelea kuwa salama na yenye mafanikio mbalimbali tangu ilipoanzishwa na mafanikio hayo ni pamoja na Sokwemtu kuendelea kuwepo ambapo wakati inaanzishwa (1968) walikuwepo Sokwemtu 150 hadi sasa wapo wapatao 110 hii imewezekana kutokana na sababu tajwa hapo juu.
Alisema baadhi ya sababu zilizopelekea kupungua kwa idadi hiyo ya Sokwe ni magonjwa hasa Polio miaka ya nyuma, homa ya mapafu, kuwindwa na wananchi miaka ya nyuma na hata kuzeeka kama ilivyo kwa wanyama wengine.
Ulinzi katika hifadhi
Kaimu mhifadhi huyo anasema kitengo cha ulinzi kimekuwa na majukumu makubwa ya kuhakikisha usalama wa wageni wa kiofisi, watalii, watumishi, rasilimali za shirika na maliasili zilizomo hifadhini kimeboreshwa zaidi.
Kuhusu Utalii
Kusekwa anasema ni vyema kufahamu shughuli zinazofanyika hifadhini ambazo huvutia watalii kuja na kuona rasilimali hizi adimu,utalii wa kuona Sokwe ni kivutio kikubwa cha kwanza na pia kutembelea maporomoko ya maji ya Kakombe na Mkenke.
Alisema Wanyama wengine waliopo ni pamoja na nyani wa kijivu, kima wa mkia wa blue, mwenye mkia mwekundu na Chotara, Mbega mwekundu, Pongo na Nguruwe pori.
Alisema juhudi mbalimbali zimefanyika ili kukuza utalii katika hifadhi na katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008/09 hadi sasa kumekuwa na ongezeko la wageni wote waliotembelea hifadhi.
Ikolojia na Utafiti
Anasema shughuli za kuhakikisha ikolojia iliyosalia ya wanyama hawa inaendelea kulindwa zinafanyika kwa kushirikisha juhudi mbalimbali zikiwemo za ulinzi, kuhakikisha utafiti unaofanyika hauleti madhara yoyote kwa wanyama na hata inapobidi wanyama hawa kupatiwa matibabu.
Aidha ikolojia ambazo zinazofanyika hifadhini ambazo ni pamoja na kusimamia tafiti zinazofanyika ndani ya hifadhi, kwa kupitia kitengo cha Utafiti cha Gombe Stream Research Centre (GSRC) chini ya Taasisi Jane Goodall ambacho kinasaidiana na watafiti wa nje wanaokuja kufanya utafiti Gombe.
Anaeleza utafiti wa mama na mtoto (Mother Infant Relationship), wapo kina mama wenye watoto katika kundi la Kasekela ambao wameteuliwa na kufuatwa kila mwezi, ili kuratibu tabia zao na za watoto wao (tangu miaka ya 1960),Utafiti wa kuratibu afya za Sokwemtu (Health Monitoring Project),Utafiti wa kuratibu sokwe na mazingira upande wa kusini mwa hifadhi (Kalande).
Alisema utafiti wa kuratibu madawa asilia na chakula cha Sokwemtu,utafiti wa nyani ndani ya Hifadhi ya Gombe, utafiti wa kuangalia chotara (hybrids) kati ya Kima (Cercopithecus mitis) na Nkunge (Cercopithecus ascanius).
Changamoto za hifadhi
Kusekwa anasema pamoja na mafanikio zipo changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi zaidi, kati ya hizo kubwa ni ya usalama wa wanyama hawa adimu kupatiwa ulinzi zaidi na pia kuhakikisha wanapata mahitaji yao ya kila siku ya chakula kutoka katika mazingira wanayoishi.
Aidha kwa muda mrefu miundombinu mibovu ya usafiri imechangia kupunguza idadi ya wageni wanaotembela Mkoa wa Kigoma hususani Hifadhi ya Gombe. na tunatumaini barabara ya Kidahwe- Nyakanazi na Mpanda-Uvinza itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Kingine ni mwamko mdogo miongoni mwa jamii kuhusu shughuli za uhifadhi na utalii wa ndani au wa kiikolojia na kiutamaduni na uwajibikaji mdogo miongoni mwa jamii zinazoizunguka hifadhi katika kutekeleza miradi ya Ujirani Mwema “SCIPs”.
Wito kwa Serikali
Anaiomba Serikali kusaidia kuunganisha shughuli za uhifadhi na za utalii kwa kuunganisha shughuli za utalii kwa nchi jirani kwa kupitia Balozi zilizopo Kigoma mjini za Kongo na Burundi ili kufufua utalii uliokuwepo miaka ya nyuma kabla ya kuvunjika kwa amani katika nchi hizi za jirani hususani Burundi na Kongo.
Aidha Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuhifadhi maeneo yaliyosalia ya makazi ya Sokwemtu wapatao 1,870 walioko nje ya mipaka ya Hifadhi hasa eneo la Masito Ugala na nje ya mipaka ya Hifadhi ya Mahale na Mpanda.
Alitoa shukrani za pekee zinatolewa kwa ujio wenu katika Hifadhi ya
Taifa ya Gombe na Kigoma kwa ujumla. Sisi wana Gombe tunaamini kwamba
kwa pamoja tutaweza kushirikiana na kutangaza utalii wetu wa ndani na
nje ya nchi.
hastinliumba@gmail.com-
No comments:
Post a Comment