Kikosi cha SC Villa cha mwaka 2015
KAMPALA,
UGANDA
KWA baadhi ya wanasoka, daima hucheza kufa
na kupona ili kushinda, hususan fedha zinapopewa kipaumbele; lakini zaidi ya
yote mchezo huo ndio maarufu zaidi hapa nchini.
Lakini kuna mechi kadhaa ambazo matokeo
yake ni ya kupangwa, hali ambayo imewafanya hata mashabiki wa soka nchini humo
kugoma kabisa kwenye viwanjani kutazama mechi za soka.
Yafuatayo ni matukio ya kashfa za kupanga
matokeo nchini Uganda.
1. SC
VILLA VS AKOL FC, 2003
Katika moja ya kashfa kubwa katika soka ya
Uganda, SC Villa na Express FC zilikuwa zinakabana kuwania ubingwa wa soka
nchini humo. Huku zikiwa zimesalia memchi mbili ligi kufikia tamati, timu hizo
zilikuwa zinalingana kwa pointi lakini Villa ilikuwa na faida ya mabao 7 dhidi ya
Express, hali iliyomaanisha kwamba ubingwa huo ungeweza kuamuliwa kwa tofauti
ya mabao.
Kufuatia mlolongo wa ushindi wenye utata wa
Express, Villa ikajua kwamba ilitakiwa kufunga mabao mengi zaidi kuipiku
Express. Kichekesho kikaanzia kwa Akol ikiwa njiani kutoka Lira kwenda Uwanja
wa Namboole.
Saa chache kabla ya mechi, baadhi ya
wachezaji wa Akol waliruka kwenye basi huko Bwaise na kutokomea kusikojulikana,
wakiwatuhumu wenzao kwamba walikuwa wamepewa fedha na mchezaji wa Villa Dan
Obote, mchezaji wa Akol, kuuza mechi hiyo.
Wale waliosalia walijitetea kwamba wenzao
waliokimbia walikuwa wamepewa maelekezo na rais wa Fufa wa wakati huo, Denis
Obua, kutocheza mechi hiyo ili kuinyima Villa mabao mengi.
Mwisho wa picha, ni wachezaji 9 tu
waliobakia kucheza na Villa ikapa ushindi wa mabao 22-1. Majogoo hao wakatwaa
ubingwa kwa tofauti ya mabao.
2.
NSAMBYA VS WEMBLEY BOYS, 1984
Kabla Nsambya FC haijacheza na timu ya
vijana ya Express FC maarufu kama Wembley Boys katika memchi ya Ligi Daraja la
Kwanza, walikuwa na kibarua kigumu cha kushinda mechi tatu zilizosalia ili
kuipiku Cooperative FC, ambayo ilikuwa imemaliza mechi zake zote, ili kufuzu
kwa Ligi Ndogo ya Kanda.
Siyo tu kwamba Nsambya ilitakiwa kushinda,
lakini ilihitaji kuizidi Cooperative iliyokuwa inaongoza kwa tofauti ya mabao 19.
Kabla ya mechi timu zote mbili ‘zilikubaliana’ kupanga mechi hiyo na mwamuzi wa
mechi hiyo George Kyambadde aliripotiwa kuwepo kwenye mpango huo. Nsambya ikashinda
kwa mabao 18-1.
Hata hivyo, kwenye ripoti yake mwamuzi
akaandika matokeo yalikuwa 18-0. Cha kushangaza, mwamuzi huyo huyo ndiye
aliyechezesha mechi iliyofuata ya Nsambya dhidi ya Foods & Beverages FC, ambayo
Foods waliigomea na kuvunjika huku Nsambya ikiongoza kwa 2-1, wakidai kulikuwa
na upendeleo. Nsambya ikaendelea kuichapa Spear Motors 1-0 na kufuzu. Na
hatimaye klabu hiyo ikapanda kwenye Ligi Kuu ya mwaka 1985.
3.
UGANDA AIRLINES VS TOBACCO, 1986
Katika kuwania nafasi ya mshindi wa pili
kwenye ligi nyuma ya SC Villa, Tobacco ilihitaji karamu ya mabao katika mechi
yao ya mwisho dhidi ya Airlines ili kuipiku Coffee. Hiyo pia ingewawezesha
kushiriki Kombe la Washindi Afrika.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Bugembe
ambako timu mwenyeji Tobacco iliishindilia Airlines mabao 12-0 na kuipiku Coffee
FC. Wiki moja kabla, Airlines ilikuwa imeichapa KCC FC 1-0 lakini ikaamua
kuiuza mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Charles Masembe.
Kwa kuhisi mchezo mchafu, baadhi ya maofisa
wa Airlines walijaribu kuingilia kati, wakaingia uwanjani, lakini wachezaji wao
wakamuomba mwamuzi awalime kadi nyekundu na hivyo ndivyo kocha wao Sam Mayanja alivyotolewa
nje. Pamoja na chama cha soka kuunda kamati ya uchunguzi, hakuna aliyeadhibiwa.
4.
EXPRESS VS KCC, 1983
Katika kilele cha ligi, Express ilihitaji
ushindi wa mabao sita dhidi ya KCC ili kumaliza ya kwanza mbele ya vinara SC
Villa.
Inaripotiwa kwamba katika kilele cha mechi
hiyo iliyochezwa Nakivubo, maofisa wa timu zote walikubaliana kupanga matokeo
ya mchezo huo ili kuondoa utawala wa Majogoo.
Siku ya mechi, mechi hiyo ilikuwa kama ya
mazoezi huku wachezaji wa KCC wakiwa hawako makini kabisa wakati mashabiki wao
waliungana na wale wa Express kushangilia kila bao la Express katika ushindi wa
6-0 siku hiyo. Baadaye Express ikalazimisha sare ya 1-1 na SC Villa na kutwaa
taji lao la kwanza katika miaka 18.
5. KCC
VS UCB, 1981
Timu iliyokuwa ikishika nafasi ya nne UCB
FC ilikuwa kizingiti cha KCC FC kutwaa taji lao la tatu mfululizo. Ili kuiacha
mbali SC Villa iliyokuwa inashika nafasi ya pili, timu hizo mbili zilikutana na
‘kupanga’ matokeo ili KCC itwae ubingwa na baadaye, KCC waipishe UCB kwenye
nusu fainali ya Kombe la Uganda.
Kilichofuata kilikuwa kichekesho. UCB haikujaribu
hata shuti moja golini; KCC ikashinda 1-0. Kwa upande wa mechi ya Kombe la
Uganda, wachezaji wa KCC, hususan Godfrey Kateregga, alikuwa amebaki peke yake
na kipa wa UCB Jimmy Bossa Jnr lakini badala ya kufunga akageuka na kupiga pasi
ndefu nyuma kwa kipa wake John Tebusweke. UCB ilishinda lakini katika
kichekesho kingine, Coffee FC ikawashinda kwa mikwaju ya penalti kwenye fainali.
6.
SIMBA VS KINYARA, 2003
Katika raundi ya mwisho ya mechi, Kinyara
FC yenye maskani yake Masindi ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja na
ilitakiwa kuifunga timu ngumu ya Simba, ambayo ilikuwa katikati ya msimamo wa
ligi. Inaripotiwa kwamba baadhi ya wachezaji wakala njama za kuinusuru Kinyara.
Katika mechi yao, walinzi wagumu kupitika
wa Simba walikuwa wanazungushwa kirahisi na washambuliaji wa Kinyara huku
mashabiki wachache kwenye Uwanja wa Nakivubo ukijiuliza kulikoni. Kinyara ikashinda
2-0 na kuepuka kushuka daraja. Uongozi wa Simba inayomilikiwa na Jeshi uliamua
kuunda tume ya kunguza tuhuma za rushwa lakini haikuzaa matunda.
7.
MAROONS VS NILE, 1980
Timu mbili za mjini Jinja zilikuwa
zimekabana koo kuwania taji na walikuwa na tofauti ya pointi moja tu dhidi ya
viongozi wa ligi hiyo Nytil, ambayo ilikuwa imemaliza mechi zake zote. Siku ya
mwisho ya msimu huo, Nile FC ikakutana uso kwa macho na Maroons kwenye Uwanja
wa Nakivubo.
Nytil ilitegemea sare ili itwae ubingwa kwa
tofauti ya mabao wakati Nile ilihitaji ushindi kunyakua taji kwa tofauti ya
pointi. Kabla ya mechi ya Nakivubo, kulikuwa na hujuma nyingi kwenye kambi ya
Maroon zilizofanywa na mabosi wa Nile na Nytil.
Kwenye mechi yenyewe, Maroons ilionyesha
upinzani mkubwa, na hadi mapumziko ngoma ilikuwa 0-0. Baadaye, baadhi ya
wachezaji wa Nile, wengi wao ambao walikuwa wamechezea Maroons siku za nyuma,
waliingia kwenye chumba cha kubadilishia na Nile na inaelezwa mpango ukasukwa.
Mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili,
Nile ilipachika bao rahisi kuliko yote bila kubughudhiwa na wachezaji wa
Maroons na ikafanikiwa kutwaa ubingwa.
8.
STATE HOUSE VS PAMBA, MBALE HEROES, 1999
State House FC ilikabiliwa na tishio la
kushuka daraja na ilihitaji kushinda mechi zake mbili zilizosalia. Hata hivyo,
ikitambua kwamba ilikosa ujasiri wa kunusurika, ikaamua kula njama za kushinda
kwa mlango wa nyuma.
Mechi dhidi ya timu iliyoshuka daraja ya
Pamba haikufanyika kufuatia kutoonekana ghafla kwa wachezaji wa Pamba kabla ya
kuonekana dakika chache baada ya mwamuzi Hussein Bugembe kupuliza kipyenga cha
kumaliza mchezo. Hizo zilikuwa pointi tatu na mabao mawili.
Baadaye walikuwa wakutane na Mbale Heroes, ambayo
siku chache kabla ilikuwa imetwaa kombe la Kakungulu. Siku ya mechi, Mbale FC
haikuonekana – wakidai kwamba mechi hiyo ilikuwa imeahirishwa.
Wakati kamati ya ligi ilipobaini njama hizo
na kupanga tarehe mpya za mechi hiyo, Heroes wakagoma kucheza wakidai kwamba
hawakuwa na umuhimu nayo. Lakini katika mtikisiko mwingine, Fufa ikaamua kupunguza
timu kutoka 22 hadi 16 – na kwa maana hiyo State House ikawa imeshuka.
9. UCB
VS BONDO, 1986
Fufa ilikuwa imeagiza kwamba timu mbili
zinatakiwa zipande daraja na tano zishuke. Shirikisho pia likatoa maelekezo
kwamba timu tatu zilizoshuka daraja zinapaswa kucheza na zile ambazo zilifuzu
kwa Ligi Kuu Ndogo.
Hatari ya kushuka daraja ilizikabili timu
za Buikwe Red Stars, Uganda Breweries (Bell) na Uganda Commercial Bank (UCB) ambazo
zilipangwa dhidi ya KK Cosmos, Bondo (Arua), Mbale Heroes na Mbarara United kwenye
Uwanja wa Bugembe. Timu za Ligi Kuu ambazo zilidhani kwamba ingekuwa mteremko
zikajikuta zikishindwa kupata nafasi ya kupanda daraja.
Klabu mbili, Buikwe na UCB zinadaiwa
zikatenga fungu kubwa kuihonga timu ya Bondo ambayo tayari ilikuwa imetoka kwenye
mashindano hayo na ndipo timu hizo mbili zilipoifunga timu hiyo kutoka Arua
mabao 9-0 na 13-0 na kurejea Ligi Kuu.
10.
KCC VS POSTA, 1995
Msimu wa 1995 ulikuwa mbaya zaidi katika
historia ya KCC. Pamoja na kuajiri makocha wawili, timu ilishindwa kutoa
upinzani kwa Express FC na SC Villa kutwaa ubingwa. Baada ya kumfukuza kocha Fred
Mugisha, Paul Ssali akachukuliwa kuinusuru timu yake ya zamani.
Lakini mambo yakashindikana. Kwa kuwa klabu
ilikuwa imehusishwa na upangaji matokeo wa mechi kadhaa, wachezaji wakaanza
kuachia mechi mbalimbali. Posta FC ambayo ilikuwa imefika fainali ya Kombe la
Kakungulu dhidi ya Express ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja na ili
inusurike, ilitakiwa kuifunga KCC na haikuwa na uwezo wa kuifunga timu hiyo
ngumu.
Kikao kikaandaliwa na maofisa wa klabu zote
mbili siku moja kabla ya mechi na kilichofuata kilikuwa historia. KCC ikacheza
mchezo mbovu zaidi katika historia yake.
Wachezaji waliachia magoli kwa sababu timu
hiyo haikuwa inashuka daraja ikiwa katika nafasi ya sita. Posta ikashinda 3-2
na kubaki Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment