Na Immaculate
Makilika -MAELEZO
Ni ukweli
usiopingika kwamba dunia imeingia katika maendeleo ya teknolojia yanayopelekea
matumizi ya vifaa vya kisasa na vyenye utaalamu wa hali ya juu katika kufanya
shughuli mbalimbali, ambazo hapo awali zilifanywa kwa kutumia nguvu kubwa na
idadi kubwa ya watu na kwa muda mrefu.
Maendeleo
hayo ya teknolojia yamejidhihirisha katika nyanja nyingi mojawapo ni hii ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano. Ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano
umerahisisha mawasiliano na unatoa fursa kwa jamii kwa ujumla kuwa huru zaidi
katika kutekeleza majukumu yake.
Serikali
inatoa fursa kwa wananchi kutoa hoja na kero zao popote pale walipo kwa
kuanzisha tovuti katika wizara, taasisi na ofisi zake ambazo zinawezesha
wananchi kupata tarifa muhimu na kwa urahisi kuhusu wizara, ofisi ama taasisi husika
na serikali kwa ujumla.
Katika
kuzingatia maendeleo hayo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, mwaka 2006
Rais wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, aliitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati
huo chini ya Idara ya Habari -MAELEZO
kuanzisha, kuratibu na kusimamia Tovuti ya Wananchi.
Dhamira kubwa
ya kuanzishwa kwa tovuti hii ni kutokana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 18 toleo la mwaka 2005, maagizo ya
Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003; na dhana ya Serikali inayozingatia
Haki za Binadamu na Utawala Bora kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 19 ya
Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Aidha, tovuti
hii inatoa fursa kwa wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali yao, kuwawezesha
watanzania popote walipo duniani kuweza kuwasilisha hoja zao, maoni na
malalamiko serikalini kwa kutumia mtandao wa intaneti .
Vile vile, Tovuti
ya Wananchi inarahishisha upelekaji wa hoja za wananchi kwenda kwa maafisa
husika wa serikali ili zifanyiwe kazi na kujibiwa na kuiwezesha serikali
kurudisha majibu na kutoa maelezo ya kina kuhusu hoja zinazopokelewa kutoka kwa
wananchi kupitia njia za intaneti na ujumbe mfupi (SMS).
Malengo hasa
ya kuanzishwa kwa tovuti ya wananchi ni:
Kuimarisha na
kupanua dhana ya uwazi na uwajibikaji Serikalini dhana ambayo ni nguzo muhimu
ya utawala bora. Kusaidia mapambano dhidi ya rushwa, uonevu, unyanyasaji na
maovu mengine katika jamii kwa kusaidia mawasiliano ya haraka na vyombo husika
vya dola.
Malengo
mengine ni pamoja na kuiwezesha Serikali kupata maoni ya wananchi juu ya vipaumbele
vyao vya maendeleo na kuhusu ubora wa huduma mbalimbli wanazopatiwa na
watumishi wa umma kwa lengo la kuziboresha pamoja na kuiwezesha Serikali kupata
hoja na takwimu zitakazoiwezesha kubuni mbinu mikakati mipya ya mageuzi ya
kiuchumi na kijamii ili nchi yetu ipige hatua kubwa zaidi ya maendeleo na
kuifanya ifikie uchumi wa kati ifikapo 2020.
Katika
hotuba ya bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyowasilisha Bungeni na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye, alisema kuwa Wizara imeratibu
utoaji wa ufafanuzi kuhusu hoja na kero mbalimbali za wananchi kwa serikali
zilizowasilishwa kupitia Tovuti ya Wananchi. katika kipindi cha mwezi Julai,
2015 hadi Machi, 2016. Jumla ya hoja 93 zilipokelewa. kati ya hizo, hoja 70
zimepatiwa ufafanuzi na hoja 23 zimeendelea kufanyiwa kazi.
Lakini pia Tovuti ya Wananchi imepokea jumla ya hoja
117,336 tangu ilipoanza kazi mwaka 2007 hadi kufikia Machi mwaka 2016, kati ya
hizo hoja 78,328 zimeshughulikiwa, huku wananchi
48 walitembelea Idara ya Habari- MAELEZO na kuwasilisha hoja zao. Hoja hizo
zimeshughulikiwa.
Wananchi
hao ni pamoja na wananchi wa mtaa wa Zavara katika kata ya Chanika ambao eneo
lao lilivamiwa. Hoja yao iliwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala na kushughulikiwa.
Mtoto mwenye saratani aliwasilisha hoja yake na kupelekwa Wizara ya Afya na
kufanikiwa kupata matibabu nchini India.
Aidha,
wananchi wengi waliowasilisha hoja zao zilizohusu kucheleweshwa kwa kusikilizwa
kwa kesi zao mahakamani, hoja zao zilishughulikiwa na kesi zao zilisikilizwa na
kutolewa maamuzi.
Tovuti hii inamwezesha Mtanzania yeyote aliyeko
mahali popote duniani penye mtandao wa intaneti au mwenye simu ya mkononi
kuwasiliana na Maafisa Wakuu wa Wizara yoyote ili kutoa maoni, ushauri, pongezi
au malalamiko au kuiuliza swali serikali moja kwa moja.
Hoja huwasilishwa Serikalini kwa kutumia intaneti
kwa kufungua anwani ya tovuti – www.wananchi.go.tz – bonyeza
sehemu iliyoandikwa weka hoja. Njia nyingine ya kuwasilisha hoja ni kwa
kuandika ujumbe mfupi kwa kutumia simu ya mkononi. Hii itatumika mara baada ya
namba ya kutuma na kupokea ujumbe huo itakapokuwa tayari, kwa kuandika barua
kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO S.L.P 8031 au tembelea ofisi za Idara
ya Habari – MAELEZO zilizopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam karibu na
Makao Makuu ya Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Hoja zinapotumwa huingia moja kwa moja katika
Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali. Iwapo mtumaji hana uhakika
na sehemu ambapo anataka hoja yake aielekeze, hoja hiyo huingia moja kwa moja
makao makuu ya Tovuti ya Wananchi, Idara ya Habari – MAELEZO, waratibu wa
Tovuti huiwasilisha hoja hiyo Wizara au taasisi inayohusika.
Hoja hizo hutafutiwa majibu na Maafisa wa Wizara
husika ambao nao huyatuma majibu hayo kwa mtuma hoja ndani ya siku tano za kazi, kwa kupitia njia
aliyoitumia mtuma hoja.
Baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya
nchi wameweza kuwasilisha kero zao kupitia na Tovuti hii ya Wananchi, ambapo
walipatiwa majibu ya hoja zao, kama vile Bibi Valeria Luzebigo aliweza kupata
majibu ya vipimo kutoka kwa mkemia Mkuu wa Serikali kufuatia kifo cha baba yake
mzazi.
Aidha Bwana Saidi Bundela, mkazi wa Dar es Salaam mwenye
ulemavu wa miguu alipatiwa msaada wa magongo ya kutembelea na Rais Msaaafu Dkt.
Jakaya Kikwete. Naye BwanaGeofrey Bwananali, mkazi wa Dar es Salaam ameendelea
kupatiwa msaada wa matibabu ya ngozi baada ya kuwasilisha matatizo yake kupitia
tovuti hii.
Ni wakati sasa kwa watanzania walioko ndani na nje
ya nchi kutumia fursa hii ya maendeleo ya teknolojia hasa
matumizi ya Tovuti ya Wananchi katika kuwasilisha hoja na kero mbalimbali,
ambazo zinalenga kuboresha hali ya wananchi pamoja na utendaji wa Serikali kwa
maendeleo ya Taifa.
Tovuti ya
Wananchi imekuwa msaada mkubwa kwa watumiaji. Ni wito kwa kila Mtanzania
kutumia haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni yake kwa uhuru kupitia Tovuti hii.
Ikumbukwe kwamba mawasiliano hai katika maisha ni kama mishipa ya damu mwilini.
MWISHO
No comments:
Post a Comment