Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango
Na
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali imelegeza msimamo wake
kuhusu kuondoa misamaha ya kodi
kwenye Taasisi za dini
badala yake itaongeza udhibiti ili kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha
hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa
ufafanuzi huo mjini Dodoma wakati akiongea na vyombo vya habari ili kutoa
ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti
Kuu ya Serikali iliyopitishwa Juzi na Bunge.
Amesema kuwa uamuzi huo wa serikali umefuatia
maombi na mapendekezo mbalimbali ya wadau yaliyoitaka serikali iendelee kutoa
misamaha ya kodi kwa Taasisi hizo kutokana na umuhimu wake wa kuisaidia jamii
kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo.
"Kwa kutambua
mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za
elimu, afya, maji; nimeamua kufuta utaratibu nilioutangaza katika hotuba ya
bajeti, badala yake serikali itaimarisha zaidi udhibiti wa misamaha
hiyo"Alisema Dkt. Mpango
Alizitaja baadhi ya
hatua zitakazochukuliwa kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo kuwa
ni kuzitaka Taasisi za dini kuwasilisha orodha ya vifaa vinavyotarajiwa
kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka wa kalenda, pamoja na kuthibitisha
kama vifaa vilivyosamehewa kodi mwaka uliotangulia vilitumika kwa mujibu wa
sheria
Aidha, utaratibu mpya utazitaka Taasisi hizo za
dini kuwasilisha majina ya watu waliowaidhinisha kuandika barua za maombi ya
msamaha wa kodi zikiainisha cheo, saini, picha, anuani na namba za simu za
wahusika.
"Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha TRA
kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa misamaha kama zimepata kibali cha Taasisi
husika zimetumika na zimetekeleza miradi iliyokusudiwa" Aliongeza Dkt.
Mpango
Dkt. Mpango alisema
katika utaratibu huo mpya, wameweka masharti ya kuzilazimisha Taasisi hizo za
dini kuiandikia serikali barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha waliyemteua
kutoa bandarini mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje
Alizitaja hatua
nyingine kuwa ni wakati wa kuomba msamaha wa kodi katika bidhaa zinazoingizwa
nchini, Taasisi za dini zitalazimika kupata barua ya uthibitisho kutoka kwa
Afisa Mtendaji wa serikali ya Mtaa ama kijiji na mkuu wa wilaya mahali Taasisi
au Mradi ulipo ili kuthibitisha uwepo wa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa
vinavyoombewa msamaha
Dkt. Mpango alifafanua
kuwa magari yatakayoingizwa kwa msamaha wa kodi yatalazimika kuwa na rangi
pamoja na namba maalumu za utambuzi mfano TEV 222 AXZ kama njia ya kudhibiti
matumizi yake.
Alionya kuwa Taasisi
ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa kodi itafutiwa usajili wake.
No comments:
Post a Comment