Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango
HOTUBA YA WAZIRI
WA
FEDHA
NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI
YA FEDHA KWA
MWAKA 2016/2017
1.
Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17. Pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu
vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni
Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida
kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali;
Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya
Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za
Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo
Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha
matumizi ya Serikali wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
2.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa
baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama
hapa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa
Makamu wa Rais na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya
nchi yetu. Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa
tena kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza
Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa
kuwa Mbunge wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe
Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu
Tukufu. Kadhalika, natumia fursa hii
kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kuongoza
mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.
3.
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia
niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu wa kitaifa: Mama Janet
Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu wa Rais), Mama
Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani Mganga (mke wa Mhe.
Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na Mama Saada El-Maamry
Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza viongozi wetu
vizuri. Asante kwenu wote na Mungu
awabariki.
4.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine
natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na
Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968
Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya
madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai
nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa
wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata”
mwisho wa kunukuu. Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba
nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi
yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na
kuwa sehemu ya Bunge hili. Napenda pia
kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa
na Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania. Nampongeza pia Dkt. Thomas
Kashililah, Katibu wa Bunge na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
kwa kuratibu vyema shughuli za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia
kumpongeza Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za
umma kwa wakati.
5.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana
Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia,
Mbunge wa Mtwara vijijini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege,
Mbunge wa Kalambo, kwa kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa
mapendekezo na ushauri. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za
kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya
Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016
na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
6.
Mheshimiwa Spika,
napenda kumpongeza
Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano
anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kumshukuru
Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa
uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru
Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi
wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti
hii.
7. Mheshimiwa
Spika,
Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo
wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na
ushauri wao. Kipekee niwashukuru wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa
masuala ya kodi (Task Force) na kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think
Tank) kwa ushauri wao mzuri walionipa.
8. Mheshimiwa
Spika, kwa
kukamilisha shukrani hizi, napenda kutoa shukrani maalum kwanza kwa Prof. Benno
Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, mwalimu wangu na mfano bora wa maisha
yangu kikazi. Amenilea kitaaluma na
kikazi tangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Benki ya Dunia, na ameendelea
kunishauri katika utumishi wangu Serikalini. Ninamshukuru sana kwa uzalendo na
unyenyekevu wake na ninamtakia kheri na afya njema yeye na familia yake. Pia
ninapenda kutoa shukrani maalum kwa rafiki yangu mpenzi, mke wangu Mbonimpaye
kwa kunitunza vizuri, lakini hasa kwa kuniombea msaada wa Mungu siku zote
akishirikiana na watoto wetu, wanafamilia wengine na marafiki zetu. Asanteni na
Amani iwe kwenu! Aidha nawashukuru viongozi wa dini mbalimbali na watanzania
wote ambao waliitikia rai ya Rais wetu Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
kumuombea na wanatuombea sana na sisi wasaidizi wake ili tujitoe na kuwatumikia watanzania, na hasa maskini, kwa bidii na
unyenyekevu. Mungu awabariki! Kadhalika,
nawashukuru sana wananchi wa kijiji cha Kasumo, wilaya ya Buhigwe nilikozaliwa,
pamoja na wananchi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Asanteni kwa kunilea
na kwa mapenzi yenu mema.
9.
Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye kauli mbiu ya “Hapa
Kazi Tu”. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kweli ya kutekeleza ahadi
zake zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020, Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025
ili kukidhi kiu na matarajio ya Watanzania. Malengo makuu ya kiuchumi ya Bajeti
hii ni mawili. Kwanza ni kutatua matatizo yanayowakabili wananchi ili
kuleta matumaini mapya ya maisha mazuri zaidi kwa wananchi wetu, hasa wa kipato
cha chini. Lengo hili litahusisha kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa
Serikali, hususan kurejesha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, na kuondokana na
ufanyaji kazi kwa mazoea, pia kuimarisha uadilifu na usimamizi wa matumizi ya
mali za umma na rasilimali za Taifa. Pili ni kujenga uchumi wa kipato
cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini utulivu wa uchumi na uendelezaji
wa viwanda vitakavyoongeza ajira hasa kwa vijana wetu nchini na kuongeza tija
kwenye kilimo ili kuongeza kipato katika sekta hii inayotegemewa na wananchi
wengi.
10.
Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa
Rais akifungua Bunge hili tarehe 20 Novemba 2015, alibainisha maeneo
yanayolalamikiwa sana na wananchi, na kuelekeza Wizara, Ofisi na Taasisi husika
zijipange ipasavyo kutatua malalamiko hayo kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali. Naomba niyarejee kwa kifupi. Kwanza ni rushwa katika maeneo yote ya
utoaji huduma kwa wananchi; Pili, ni upotevu wa mapato, ujangili, wizi,
ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha, uzembe na urasimu katika maeneo
mbalimbali; eneo la tatu ni huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu
bora na afya; eneo la nne ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji,
vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji, wananchi na wamiliki wa mashamba
pori na uvunjaji wa sheria za ardhi.
11.
Mheshimiwa Spika, eneo la tano ni
huduma zisizoridhisha za usafiri na usafirishaji kutokana na uchakavu wa
miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa majini; na udhaifu mkubwa wa shirika
la ndege. Eneo la sita ni upungufu katika utoaji haki ikiwa ni pamoja na
mlundikano wa kesi mahakamani, wananchi kubambikiwa kesi na polisi, makazi duni
na ukosefu wa vitendea kazi kwa askari; eneo la saba ni kodi na tozo za kero
kwenye mazao, uhaba wa zana na pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi, uhaba wa
masoko ya uhakika, maghala, maafisa ugani na huduma za ugani, na uvuvi haramu;
na eneo la nane ni uwezeshaji mdogo kwa makundi maalum hususan wazee, walemavu,
wanawake, watoto, vijana, wafanyakazi, wasanii, wanamichezo, wachimbaji wadogo
na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
12.
Mheshimiwa Spika, baada ya rejea hiyo, naomba
niseme tena kwamba mkazo mkuu wa Bajeti hii ni kutekeleza azma ya Serikali ya
awamu ya tano ya kutatua kero za wananchi. Aidha, Serikali itatekeleza azma ya
kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha Taifa
letu kufikia hadhi ya kipato cha kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio
wengi ifikapo mwaka 2025.
13.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha miundombinu ya
msingi kama vile ya maji, umeme na usafirishaji kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo
ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo
yanayotumika kama malighafi viwandani. Ili kufanikisha hilo, mkazo mkubwa
utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa rasilimali
hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuibua
vyanzo vipya vya mapato, na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki - EFDs ili kuongeza makusanyo na vile vile
kudhibiti matumizi yasiyokuwa na tija. Hivyo, kauli mbiu ya Bajeti za nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua
fursa za ajira” (Industrial growth
for job creation). Kwa msingi huo, Bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17
imeongezwa kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 40 ya bajeti yote tofauti na
miaka yote ya nyuma ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 25. Bajeti hii pia inalenga kujenga mazingira
mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza ili kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa
ndani na nje katika kuendeleza viwanda na kilimo.
I.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA
BAJETI YA MWAKA 2015/16
14. Mheshimiwa
Spika, mpango na bajeti ya
Serikali mwaka 2015/16 ililenga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 22.49
kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni
13.99 zilikuwa ni makadirio ya mapato ya ndani zikijumuisha mapato ya
Halmashauri; shilingi trilioni 2.32 ni mikopo nafuu na misaada kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo; shilingi trilioni 4.03 ni mikopo ya kibiashara ya
ndani; na shilingi trilioni 2.14 ni mikopo ya kibiashara ya nje. Aidha, kiasi
cha shilingi trilioni 16.57 kilipangwa kutumika kwenye matumizi ya kawaida na
shilingi trilioni 5.92 kwenye matumizi ya maendeleo.
Mapato
15.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mapato ya ndani yanapatikana, sera za mapato
za mwaka 2015/16 zililenga kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija; kuongeza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato; na kuongeza wigo wa mapato. Sera hizo zililenga kukusanya mapato ya kodi ya
shilingi trilioni 12.36, mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 1.11 na
mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 521.9.
16.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha
Julai 2015 hadi Aprili 2016, jumla ya makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya
Halmashauri) yalikuwa shilingi trilioni 11.48 sawa na asilimia 99 ya makadirio
ya kukusanya shilingi trilioni 11.55 katika kipindi hicho. Mapato ya kodi
yalikuwa shilingi trilioni 10.17, sawa na asilimia 100 ya lengo, mapato yasiyo
ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 967.2 sawa na asilimia 105 ya lengo na mapato
yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 344.1, sawa na asilimia
79 ya makadirio kwa kipindi hicho.
17.
Mheshimiwa
Spika, mwenendo huo mzuri wa
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi umetokana na
juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika ukusanyaji wa mapato na
kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi, tozo na ada mbalimbali. Hata hivyo, mapato ya Halmashauri
hayakufikia lengo kutokana na mifumo ya ukusanyaji mapato isiyoridhisha pamoja
na kodi ya majengo kutokusanywa kwa kiwango kilichotarajiwa kulingana na fursa
zilizopo.
Misaada
na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
18.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ilitarajia kupata shilingi trilioni 2.32
kutokana na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo. Hadi Aprili, 2016, misaada na mikopo nafuu iliyopatikana ni shilingi
trilioni 1.15, sawa na asilimia 65 ya lengo la kipindi hicho. Kutofikiwa kwa
lengo kumetokana na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kuweka masharti mapya na
kubadilika kwa sera ndani ya nchi zao zinazohusiana na misaada kwa nchi
zinazoendelea.
Mikopo yenye masharti ya Kibiashara
19. Mheshimiwa
Spika,
mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi trilioni 6.18 ambapo
shilingi trilioni 4.03 ni kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 2.15 kutoka vyanzo vya
nje. Fedha hizo zililenga kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia dhamana za
Serikali za muda mfupi na hatifungani za Serikali zilizoiva. Hadi Aprili, 2016
Serikali ilikopa kutoka vyanzo vya ndani shilingi trilioni 3.94 sawa na
asilimia 97.8 ya lengo. Kati ya hizo, shilingi trilioni 2.56 zilikuwa kwa ajili
ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na hatifungani zilizoiva na
shilingi trilioni 1.39 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, kwa
upande wa mikopo ya nje, Serikali ilisaini mikataba yenye
jumla ya Dola za Kimarekani milioni 674.3 na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya usafirishaji, awamu ya pili ya
mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam pamoja na mradi wa maji safi na
maji taka Arusha. Hata hivyo, hali ya soko la mitaji ulimwenguni ilikuwa mbaya
na kusababisha kuongezeka kwa gharama za
mikopo mipya kwa kiwango kikubwa na hivyo kuathiri upatikanaji wa mikopo ya
nje.
Matumizi
20. Mheshimiwa
Spika, Bajeti
ya mwaka 2015/16 pamoja na mambo mengine ililenga kugharamia Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015; kukamilisha miradi iliyoanza kutekelezwa; na kulinda mafanikio
yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, maji pamoja na maendeleo ya
jamii. Hadi Aprili, 2016 Serikali ilitoa
mgao wa matumizi wa shilingi trilioni 16.86 kwenye mafungu mbalimbali sawa na
asilimia 89.9 ya lengo la kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni
13.65 zilikuwa ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na shilingi trilioni
3.21 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Miradi ya maendeleo
iliyogharamiwa kwa kutumia fedha za ndani ni pamoja na: usambazaji wa umeme
vijijini, ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, ukarabati wa reli ya
kati, ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I na II, na usambazaji wa
maji mijini na vijijini.
Ulipaji wa Madai
21. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali
yaliyohakikiwa ya makandarasi, wahandisi washauri, watumishi na wazabuni wa
huduma na bidhaa kulingana na upatikaji
wa fedha. Hadi Aprili 2016, Serikali imelipa jumla ya shilingi trilioni 1.13,
kati ya fedha hizo: shilingi bilioni 689.5 ni kwa ajili ya makandarasi na
wahandisi washauri; shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya walimu na malimbikizo ya
mishahara ya watumishi; shilingi bilioni 10.0 kwa ajili ya Jeshi la Polisi;
shilingi bilioni 211.0 kwa ajili ya mikataba ya kijeshi; na shilingi bilioni
194.0 kwa ajili ya ankara za umeme kwa Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi
za Serikali.
Mafanikio
na Changamoto katika Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2015/16
22.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi
kumi ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16, Serikali imefanikiwa kutekeleza
shughuli muhimu za Bajeti licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa. Baadhi ya
mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kufikia
wastani wa shilingi trilioni 1.02 kwa mwezi mwaka 2015/16 ikilinganishwa na
wastani wa shilingi bilioni 904.0 kwa mwezi mwaka 2014/15; kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa
kutumia fedha za ndani bila ya kupata msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama
ilivyozoeleka kwa chaguzi zilizopita; na kuanza kwa utekelezaji wa elimu ya
msingi bila malipo.
23.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni
kuongezeka kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka
wanafunzi 99,069 mwaka 2014/15 hadi 123,798 mwaka 2015/16; kulipa malimbikizo
ya madai yaliyohakikiwa ya makandarasi, wazabuni wa huduma na bidhaa na
watumishi.
24.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na mafanikio hayo, zimejitokeza changamoto kadhaa
zikiwemo: ukwepaji wa kodi
unaohusisha wafanyabiashara na watumishi wasio waadilifu; uelewa mdogo wa
Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani; mwitikio mdogo wa wafanyabiashara
katika matumizi ya mashine za kielektroniki yaani EFDs pamoja na wananchi
kutodai stakabadhi zitokanazo na mashine hizo katika ununuzi wa bidhaa na
huduma; mazingira magumu ya ukusanyaji wa kodi katika sekta isiyo rasmi; uwepo
wa wafanyakazi na wanafunzi hewa; na kuwepo kwa mahitaji makubwa yasiyowiana na
uwezo wa mapato, yakiwemo mahitaji ya kuboresha miundombinu hususan ya maji,
reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara.
Usimamizi wa Deni la Taifa
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa
kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Katika kuhakikisha kuwa deni la taifa
linasimamiwa kikamilifu, Serikali inakamilisha uaandaji wa Sera ya Usimamizi wa
Deni la Taifa na kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada
SURA 134 ili iendane na Sera hiyo. Sera hiyo itatoa dira ya muda mrefu katika
usimamizi wa deni la Taifa na hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na usimamizi
madhubuti wa deni la Taifa. Aidha, Sera hiyo itatoa mwongozo wa kukuza na
kuongeza ufanisi wa soko la fedha la ndani pamoja na kusaidia utekelezaji wa
Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 kwa ufanisi zaidi.
26.
Mheshimiwa
Spika, hadi Machi, 2016 Deni la
Taifa lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 20.94 ikilinganishwa na Dola za
Kimarekani bilioni 19.69 Juni, 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 6.34.
Kati ya kiasi hicho, Deni la Serikali lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 17.93
na Deni la nje la sekta binafsi lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 3.01.
Aidha, Deni la Serikali liliongezeka kwa asilimia 6.01 ikilinganishwa na Dola
za Kimarekani bilioni 16.92 Juni, 2015. Ongezeko hilo lilitokana na mikopo ya
ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi
iliyoendelea kutekelezwa kutokana na mikopo hiyo ni pamoja na ujenzi wa
barabara na madaraja nchini, mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa
njia ya umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi
yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi
wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
27.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na kuendelea
kuongezeka kwa Deni la Taifa, bado ni himilivu. Hii inathibitishwa na Tathmini
ya Uhimilivu wa Deni la Taifa (Debt Sustainability Assessment) iliyofanyika
Mwezi Septemba, 2015 ambayo ilionesha kuwa deni hilo ni himilivu katika kipindi
cha muda wa kati na mrefu.
Madeni
ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Serikali
28. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali iliahidi
kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutoa hatifungani maalum. Hata
hivyo, katika hatua za mwisho za kukamilisha mikataba ya makubaliano kati ya
Serikali na mifuko ili kutoa hatifungani maalum, kulijitokeza masuala
mbalimbali yakiwemo utofauti katika ukokotoaji wa deni pamoja na michango ya
watumishi hewa. Kutokana na tofauti hizo, Serikali kupitia Mkaguzi wa Ndani
Mkuu ilianza kufanya uhakiki kwenye mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii. Mkaguzi wa
Ndani Mkuu amekamilisha uhakiki kwenye Mfuko wa PSPF na mara zoezi
litakapokamilika kwenye mifuko mingine, Serikali itatoa hatifungani maalum kwa
mifuko yote ya hifadhi ya jamii. Serikali itafanya pia maboresho katika sekta
hii ya hifadhi za jamii ili kuleta ufanisi na tija.
II.
BAJETI YA MWAKA 2016/17
Shabaha na Misingi ya
Bajeti ya Mwaka 2016/17
29. Mheshimiwa Spika,
kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchambuzi wa mwenendo wa viashiria vya uchumi
jumla na maoteo katika kipindi cha muda wa kati - financial programming, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha
mwaka 2016/17 ni kama ifuatavyo:-
(i)
Pato
Halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2016 kutoka 7.0 mwaka 2015;
(ii)
Kuendelea
kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na
asilimia 8.0 mwaka 2016;
(iii)
Mapato
ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la
Taifa mwaka 2015/16, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.9 ya Pato la
Taifa mwaka 2016/17;
(iv)
Mapato
ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka asilimia
12.6 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16;
(v)
Matumizi
ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya Pato la Taifa mwaka
2015/16 hadi asilimia 27.0 mwaka 2016/17;
(vi)
Nakisi
ya bajeti inakadiriwa kuwa asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka
makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2 mwaka 2015/16;
(vii) Nakisi katika urari wa malipo
ya kawaida kuwa asilimia 7.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 na kupungua hadi
asilimia 7.5 mwaka 2016/17; na
(viii) Kuwa na akiba ya fedha za
kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka
nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne Juni 2017.
30. Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo hayo
yatafikiwa kwa kutegemea misingi ya Bajeti ifuatayo:-
(i)
Kuendelea
kuwepo kwa amani, usalama, utulivu na utengamano nchini, kikanda na duniani;
(ii)
Utulivu
wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia;
(iii)
Kuwepo
kwa hali nzuri ya hewa nchini na katika nchi jirani;
(iv)
Kuendelea
kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii kama vile Pato
la Taifa, biashara ya nje, ujazi wa fedha, mapato, matumizi na huduma za jamii;
(v)
Kuimarika
kwa sera za fedha na za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na
tofauti kati ya riba za amana na za mikopo;
(vi)
Kuendelea kuimarika na kutengemaa kwa uchumi wa dunia;
na
(vii) Ushiriki wa sekta binafsi
katika uchumi utaongezeka hususan kwenye uwekezaji katika viwanda.
Sera za Mapato kwa mwaka 2016/17
31. Mheshimiwa
Spika, Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuongeza na kuimarisha
ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika
mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza
utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Katika kufanikisha
azma hii, sera za mapato kwa mwaka 2016/17 zimejielekeza kwenye maeneo
yafuatayo:
(i)
Kusimamia
kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa
mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
(ii)
Kuendelea
kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi
ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
(iii)
Kuimarisha
ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za
serikali;
(iv)
Kuendelea
kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija; na
(v)
Kuendelea
kuimarisha usimamizi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara bandarini, kwenye
viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki
zinakusanywa.
Misamaha
ya Kodi
32.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali itaendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi kwa taasisi za
kidini na wawekezaji ili kuhakikisha inakuwa na tija kwa Taifa. Katika
kutekeleza hili, Serikali itafanya marekebisho ya sheria husika ili kuondoa
matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Marekebisho hayo yatawasilishwa katika
muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016. Pamoja na mambo mengine, marekebisho
hayo yatalenga kuwataka wanufaikaji kulipa kodi kwa bidhaa watakazoagiza na
baadae kuwasilisha maombi ya kurejeshewa kodi hiyo baada ya uhakiki kufanyika.
33.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutangaza na kutoa taarifa za
wanufaika wa misamaha ya kodi kila robo ya mwaka ili wadau waweze kufahamu
sekta au taasisi iliyonufaika na misamaha hiyo na maeneo ilikoelekezwa. Utaratibu
huu utasaidia kudhibiti wafanyabiashara, taasisi na makampuni yanayotumia
vibaya misamaha hiyo kwa kujinufaisha wao binafsi na watumishi wa umma wasio
waadilifu.
Mapato
yasiyo ya Kodi
34.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2016/17, usimamizi wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi
ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo utakuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Uamuzi wa kuipatia TRA jukumu hili
unatokana na uzoefu na mifumo ya ukusanyaji wa mapato waliyonayo nchi nzima
lakini pia mafanikio na uzoefu wa nchi nyingine kama Ethiopia na Rwanda. Aidha,
Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya
kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi
na kudhibiti upotevu wa mapato. Miongoni mwa makusanyo yanayolengwa ni pamoja
na: tozo, faini kama vile za mahakama na usalama barabarani, ada, viingilio
kwenye hifadhi za Taifa na viwanja vya michezo pamoja na vibali vya kuvuna
maliasili.
35.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuziruhusu
baadhi ya taasisi za Serikali kutumia mfumo wa kubakiza maduhuli – retention. Utaratibu huu umekuwa ukipunguza
mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kuzinufaisha taasisi chache. Hivyo, kuanzia
mwaka 2016/17, Serikali itafuta utaratibu huo. Uamuzi huu ni kwa mujibu wa Sheria
ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 kifungu 58 (a) mpaka (c) ambayo inaelekeza
mapato yote ya Serikali yakusanywe na kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Sambamba na matakwa ya Sheria ya Bajeti, tathmini iliyofanyika kuhusu utaratibu
wa retention ilibaini kuwa:
(i)
Taasisi
zinazohusika na utaratibu wa “retention” zimeacha majukumu yao ya msingi na
kuegemea zaidi kwenye shughuli za ukusanyaji mapato. Mifano ni pamoja na Wakala
wa Misitu na Kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi;
(ii)
Baadhi
ya taasisi zenye mfumo wa “retention” zinapata fedha nyingi na kuonekana
kujinufaisha zaidi wakati Wizara, Idara na Taasisi zingine zinakabiliwa na
uhaba wa fedha. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa maombi kutoka taasisi
nyingine kutaka kujiunga na utaratibu huu;
(iii)
Taasisi
zilizo kwenye mfumo wa “retention” bado zinalipwa mishahara asilimia 100 kutoka
kwenye mfuko mkuu wa Serikali; na
(iv)
Utaratibu
huu wa “retention” umesababisha idara ambazo awali zilikuwa zikichangia Mfuko
Mkuu wa Serikali kupitia maduhuli kutochangia na hivyo kupunguza mapato ya Serikali.
36.
Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, kuanzia sasa mapato yote
yatakusanywa na kuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kila fungu
litapewa fedha kulingana na bajeti yake. Wizara ya Fedha na Mipango kwa upande
wake itahakikisha kwamba fedha kutoka Mfuko Mkuu zinagawiwa kwa Mafungu
mbalimbali bila kuchelewa kulingana na mapato yaliyokusanywa.
Sera za Matumizi kwa Mwaka
2016/17
37.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2016/17, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya
fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.
Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa
fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo.
Katika kutimiza azma hii, Serikali itachukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo:
(i)
Kuwianisha
matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi ili kuepuka
malimbikizo ya madai. Maafisa Masuuli wanaagizwa kuzingatia maelekezo ikiwemo
kuingia miadi baada ya kupokea mgao wa fedha (exchequer) na siyo kabla;
(ii)
Kuhakikisa
malipo kwa wazabuni na watoa huduma yanafanyika kwa kuwasilisha Hati za Ununuzi
- LPOs zitokanazo na IFMS;
(iii)
Kuwasilisha
Bungeni marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuziba mianya ya upotevu
wa fedha katika ununuzi wa umma na kuhakikisha ununuzi unawiana na thamani ya
fedha itakayotumika;
(iv)
Kudhibiti
matumizi ya taasisi za Serikali yasiyo na tija na kufanya tathmini ya gharama
za uendeshaji ili kuchukua hatua stahiki kwa maendeleo ya nchi;
(v)
Kuendelea
na zoezi la kuunganisha Halmashauri zote nchini kwenye mfumo wa malipo ya
kibenki ili kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha
kwamba malipo yanafika kwa wakati;
(vi)
Kuhakikisha
kuwa mashirika ya umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara
yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali; na
(vii) Kuimarisha ufuatiliaji na
tathmini ya matumizi ya fedha za umma hususan katika miradi ya maendeleo.
Maeneo ya Vipaumbele
38.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu ya Hali ya Uchumi, Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 una maeneo makuu manne (4) ya vipaumbele:-
(i) Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; (ii)
Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu; (iii) Mazingira Wezeshi
kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji; na
(iv) Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango. Ili kufikia malengo hayo,
mikakati itakayotumika ni pamoja na: kuhamasisha wawekezaji na sekta binafsi
kuwekeza katika viwanda na maeneo mbalimbali nchini hususan kupitia mfumo wa
ubia baina ya serikali na sekta binafsi (PPP); kuondoa vikwazo kwa kuimarisha
mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; na kuimarisha usimamizi,
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.
Kuongeza Uzalishaji Viwandani
39. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo
awali, kauli mbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira”. Katika
kufikia azma hii, Serikali imelenga kutekeleza mikakati mbalimbali
itakayochochea uwekezaji katika viwanda. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja
na: kufanya uthamini wa ardhi na mali na kulipa fidia kwa maeneo maalum ya
uwekezaji yaliyotengwa nchini; kugharamia tafiti za viwanda kupitia taasisi za
TIRDO, TEMDO, CAMARTEC na COSTECH; kuendeleza miundombinu ya viwanda vidogo
kupitia SIDO; kuanzisha kongane za viwanda (industrial clusters); na kuwezesha upatikanaji
wa teknolojia rahisi na nafuu kwa ajili ya viwanda. Katika mwaka 2016/17,
Serikali imetenga fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 50.9 katika fungu 44 na fungu 46 ambazo pamoja na
mambo mengine zitagharamia utekelezaji wa maeneo niliyoainisha hapo juu.
40. Mheshimiwa
Spika, kama
alivyoelekeza Mhe. Rais wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge lako Tukufu, Serikali
itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi. Katika mwaka 2016/17, Serikali itakamilisha
tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuweka mikakati ya namna bora ya
kuviendeleza. Baadhi ya viwanda hivyo ni viwanda vya nguo, viwanda vya mazao ya
mifugo, viwanda vya kusindika mazao yakiwemo mazao ya mpira, korosho, tumbaku,
miwa na mpunga. Katika kutekeleza jukumu hilo, fedha za maendeleo zimetengwa katika
Mafungu mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza mashamba; na kuimarisha uzalishaji
wa mazao ya kilimo, na ya mifugo. Pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi
katika viwanda, Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya wawekezaji waliokiuka
masharti ya mikataba ya mauzo ya viwanda walivyobinafsishiwa.
41. Mheshimiwa
Spika, katika kuboresha
mazingira ya uwekezaji wa viwanda, Serikali imetenga fedha za kuboresha
miundombinu ya uwekezaji hususan ya umeme, maji, barabara, bandari na reli. Aidha,
Serikali imedhamiria kuondoa urasimu usio wa lazima na kuharakisha utoaji wa
maamuzi ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Vilevile, zipo
hatua mahsusi za kodi zinazopendekezwa katika Bajeti hii ambazo zina lengo la
kushawishi na kuhimiza uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Serikali pia
itaimarisha upatikanaji wa mikopo ya uendelezaji wa viwanda kupitia Benki ya
Rasilimali pamoja na taasisi nyingine za fedha.
42. Mheshimiwa
Spika, Serikali kupitia balozi
zetu na Diaspora, itaimarisha diplomasia ya uchumi katika nchi mbalimbali hasa
zile zilizoendelea pamoja na nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ikiwemo Jamhuri
ya Watu wa China, India, Korea Kusini, Afrika Kusini na Brazil ili kushawishi
wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na hivyo kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa
na uchumi wa viwanda. Vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya
uwekezaji nchini ambayo yatahamasisha kampuni za kigeni zilizoko hapa nchini
kuwa mabalozi wetu na kuvutia kampuni nyingine za nje wanakotoka kuja kuwekeza
hapa nchini. Hivyo, kama nilivyoeleza awali, jukumu la kuboresha mazingira ya
uwekezaji litapewa kipaumbele katika Bajeti ya mwaka 2016/17.
HATUA ZA KUTATUA KERO ZA WANANCHI
43.
Mheshimiwa Spika; bajeti hii itajikita kutatua kero katika maeneo yaliyolalamikiwa na
wananchi kama nilivyoeleza hapo awali. Baadhi ya hatua za kibajeti na kiutawala
zitakazochukuliwa ni kama ifuatavyo:
Rushwa katika
Utoaji wa Huduma
44.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na suala la rushwa na
ufisadi, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 ili kuwezesha uanzishwaji
wa mahakama ya mafisadi. Aidha, Serikali imetenga jumla
ya shilingi bilioni 72.3 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili
kuiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Vile vile katika
bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali imetenga shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya kuiwezesha
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukagua na
kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Hatua za
Kuzuia Upotevu wa Mapato
45.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itadhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha ufuatiliaji wa mara kwa mara katika
maeneo mbalimbali ya biashara, bandarini, viwanja vya ndege na mipakani;
kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kufanya kaguzi za kitaalam hasa katika
sekta za madini, maliasili, ardhi, mafuta na gesi asilia; kuhimiza matumizi ya
mifumo ya kieletroniki katika kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, pamoja
na kupunguza misamaha ya kodi.
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali inawapongeza wafanyabiashara walioitikia matakwa ya
Sheria Ya Usimamizi wa Kodi ambayo inamtaka kila mfanyabiashara isipokuwa wale
ambao wametangazwa rasmi na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato kutotumia mashine za
EFD kutoa risiti kila anapouza bidhaa au huduma. Hata hivyo, kuna baadhi ya
wafanyabiashara ambao bado wanakaidi matakwa haya ya kutumia mashine hizo.
Napenda kuwasihi wafanyabiashara hao kuanza mara moja kutumia mashine hizo
vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya
leseni zao za biashara na hawataruhusiwa kufanya biashara hapa nchini kwa
kipindi kisichopungua miaka miwili. Aidha, kwa
upande wa Serikali, ili kuwa na usimamizi mzuri wa fedha za Serikali na
kuhakikisha kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa, kwa mamlaka niliyopewa chini
ya Sheria ya Fedha za Umma pamoja na kanuni zake malipo yote lazima
yaambatanishwe na ankara za madai au stakabadhi (tax invoice) zilizotolewa na
mashine za EFD. Kwa sababu hiyo kuanzia tarehe 1 Julai 2016, ni marufuku kwa
Wizara, Taasisi, Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kufanya biashara na wazabuni na wafanyabiashara wengine ambao hawatumii mashine
za kielektroniki - EFDs. Aidha, malipo yatakayofanywa bila stakabadhi au Ankara
zisizokuwa za mashine za EFD ni lazima ziambatanishwe na ushahidi kuwa
mfanyabishara husika ametangazwa rasmi na Kamishna wa Mapato kutotumia mashine
za EFD.
Hatua za
Kudhibiti Matumizi
47.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kupunguza na
kudhibiti matumizi bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa na
hivyo kuhakikisha uwepo wa ufanisi katika matumizi ya Serikali. Baadhi ya hatua
hizo zimeainishwa katika Mwongozo wa kutayarisha Mpango na Bajeti ya mwaka
2016/17 niliouwasilisha hapa Bungeni Februari, 2016. Miongoni mwa hatua hizo ni
pamoja na:
(i)
Kuhakikisha mikutano yote ikiwa ni pamoja na
mikutano ya bodi, mafunzo na semina inatumia kumbi za Serikali na Taasisi za
Umma;
(ii)
Kutoa kipaumbele kwa Taasisi za Umma katika kutoa
huduma kwa Serikali kama vile bima, usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi,
matangazo na usafiri;
(iii)
Kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni
pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara;
(iv)
Kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa watumishi ili
kuepuka malipo yasiyostahili. Aidha, Serikali itaendelea kufanya sensa ya
watumishi wote;
(v)
Kudhibiti utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili
kuepuka utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasio stahili;
(vi)
Kuendelea kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja na bidhaa
moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa
bei;
(vii)
Kuendelea kudhibiti gharama
za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi;
(viii)
Kupunguza na kuondoa matumizi
yasiyo na tija katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadhimisho na sherehe za
kitaifa, matamasha, machapisho na safari za ndani na nje ya nchi zisizo na tija;
(ix)
Kuhimiza matumizi ya nakala
laini (soft copy) za machapisho mbalimbali hususan yanayozidi kurasa 50 ili
kupunguza gharama za uchapishaji na kutunza mazingira; na
(x)
Kudhibiti matumizi ya Taasisi na
Mashirika ya Umma yasiyowiana na majukumu yao ya msingi na yasiyo na tija.
Kero katika
Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
48. Mheshimiwa Spika, azma kuu ya Serikali ni kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa
mtazamo wa kibiashara, kukuza viwanda na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo
na sekta hii. Hata hivyo, bado sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa
zikiwemo kodi na tozo za mazao zisizo na tija, uhaba wa pembejeo, vifaa duni,
masoko, na uhaba wa maafisa ugani.
49.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni
1.56 sawa na asilimia 4.9 ya bajeti yote ukiondoa deni la Taifa kwa ajili ya
kugharamia shughuli mbalimbali katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji zikiwemo
ununuzi wa pembejeo; kuboresha upatikanaji wa masoko; kuongeza upatikanaji wa
zana bora na za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi; na kuongeza maafisa ugani.
50. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria
kupunguza ama kuondoa kabisa ushuru na kodi mbalimbali za mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi zisizo na tija. Nitaeleza hatua mahsusi muda mfupi ujao. Aidha,
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania itaendelea kutoa mikopo ya riba nafuu na
masharti yanayozingatia hali halisi ya sekta ya kilimo ili kusaidia kuleta
mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kijungujiko (subsistence farming) kwenda kilimo cha kibiashara. Katika mwaka
2016/17, Benki ya Kilimo itaendelea kutangaza na kupanua huduma zake kwa
wananchi mikoani.
Migogoro ya
Ardhi
51. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na
juhudi za kutatua migogoro katika Sekta ya ardhi ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji, vijiji
na hifadhi, wananchi na wawekezaji, uvunjaji wa sheria za ardhi na umiliki wa mashamba
pori. Katika kukabiliana na
migogoro hiyo, Serikali imetenga shilingi bilioni bilioni 5.0 kwa ajili ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi; shilingi
bilioni 13.0 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umilikishwaji wa ardhi; na shilingi
bilioni 8.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji wa ardhi. Aidha, Serikali
imetenga shilingi bilioni 33.4 kwa ajili ya programu ya kuwezesha umilikishaji
wa ardhi na uwekaji wa kumbukumbu utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.
Vilevile, Serikali itaendelea kusajili migogoro ya ardhi katika maeneo
mbalimbali nchini na kutafuta ufumbuzi kulingana na mazingira ya eneo husika
ili kupunguza migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi.
Huduma zisizoridhisha
za Usafiri na Usafirishaji
52.
Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea kukabiliana
na kero zinazotokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, bandari na
viwanja vya ndege. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga shilingi trilioni 5.47
sawa na asilimia 25.4 ya bajeti yote ukiondoa Deni la Taifa, kwa ajili ya miradi
ya ujenzi na uchukuzi. Baadhi ya maeneo yanayohusika ni;
(i)
Ujenzi wa miundombinu ya
barabara – kiasi cha shilingi trilioni 2.18 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa
barabara hasa zenye kufungua fursa za kiuchumi na kukarabati barabara zilizopo
(ii)
Uchukuzi – kiasi cha shilingi
trilioni 2.49 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga reli ya kati kwa kiwango
cha standard gauge; ununuzi wa ndege mpya tatu za abiria; ununuzi wa meli mpya
ziwa Viktoria; ukarabati wa meli katika ziwa Viktoria na ziwa Tanganyika; uboreshaji
wa miundombinu ya bandari; na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Aidha,
Kiasi cha shilingi bilioni 161.4 kimetengwa katika Mfuko wa Reli kwa ajili ya
ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni pamoja na ukarabati wa na Reli.
Umeme
53.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.13 sawa na
asilimia 5.3 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa ili kugharamia upatikanaji
wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani. Baadhi ya
miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kuongeza kasi ya usambazaji umeme
vijijini kupitia REA na kukamilisha miradi ya umeme inayoendelea ikiwemo
kuongeza mitambo mingine yenye uwezo wa kufua MW 185 katika mradi wa Kinyerezi – I na Kinyerezi II. Serikali itahakikisha kuwa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) linakuwa na uwezo kifedha ili lijiendeshe lenyewe na
kuwa na ushindani katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo nafuu ili
kupunguza gharama kwa wazalishaji na walaji.
Upatikanaji
duni wa huduma za afya, maji na elimu.
54.
Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingi katika maeneo haya, ikiwemo kukosekana kwa upatikanaji wa uhakika wa
maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani; na huduma bora
za afya. Aidha, kuna changamoto za ubora wa elimu na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu kwa wakati. Bajeti ya mwaka 2016/17 imejielekeza katika kutatua changamoto hizo kama
ifuatavyo:
Elimu
55.
Mheshimiwa Spika, sekta ya elimu imetengewa jumla ya shilingi trilioni 4.77 sawa na asilimia 22.1 ya bajeti yote
bila kujumuisha Deni la Taifa. Fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya kugharamia
shughuli mbalimbali za elimu zikiwemo: Elimu Msingi bila malipo; gharama za
uendeshaji wa shule ikiwemo chakula, ununuzi wa vitabu, na mitihani; mikopo na
ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu; na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
elimu katika ngazi zote
Afya
56.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za afya kwa
wananchi, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.99 sawa na asilimia
9.2 ya bajeti yote bila
kujumuisha Deni la Taifa kwa ajili ya sekta ya
afya. Baadhi ya maeneo yanayohusika ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi (reagents) ambayo
yametengewa shilingi bilioni 180.5; ulipaji wa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
shilingi bilioni 71.0; na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za
afya katika ngazi zote.
Maji
57. Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 1.02 sawa na asilimia 4.8 ya bajeti yote bila
kujumuisha Deni la Taifa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji
wa maji safi na salama nchini. Baadhi
ya shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa miundombinu
ya maji mijini na vijijini; ulipaji wa madeni ya wakandarasi na utekelezaji wa
shughuli za Mfuko wa Maji.
Mazingira Wezeshi kwa
Sekta Binafsi
58.
Mheshimiwa
Spika, kama nilivyoeleza hapo juu, katika bajeti ya
2016/17 Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya kufanya biashara, ikiwa ni
pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ya reli, barabara, bandari, maji na kuhakikisha
upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika maeneo
mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kupitia kodi, tozo na ada mbalimbali ili
kuzipunguza au kuziondoa zile ambazo zinalalamikiwa na wananchi na wawekezaji
wa ndani na nje. Miongoni mwa jitihada zitakazochukuliwa na Serikali ili kuongeza ushiriki
wa sekta binafsi katika uchumi ni pamoja na kuboresha huduma za upatikanaji wa
mikopo kwa sekta binafsi, kuimarisha soko la mitaji, kukuza utaratibu wa ubia
kati ya sekta ya umma na sekta binafsi - PPP, na kuboresha mazingira ya kufanya
biashara kwa kuboresha miundombinu ya umeme, usafirishaji, maji, usambazaji wa
gesi asilia, mfumo wa kodi, kuweka
vivutio mbalimbali, kuondoa urasimu usio wa lazima na kupambana na rushwa.
Uwezeshaji kiuchumi
wa Makundi Maalum
(i)
Maendeleo Vijijini
59.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ambapo
shilingi milioni 50 ziliahidiwa kwa kila kijiji ili kuwawezesha wananchi kuanzisha
na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa
(SACCOS) na vikundi vingine vya kiuchumi. Katika kutekeleza ahadi hii, Serikali
imetenga shilingi bilioni 59 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu kwa awamu.
Mpango huu utaanza kutekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya
kukamilisha utaratibu wa matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha kuwa fedha hizi
zinatumika ipasavyo.
(ii)
Vijana, Wazee, Wenye Ulemavu, Wanawake na Watoto
60.
Mheshimiwa Spika, Bajeti
ya 2016/17 imezingatia mahitaji ya makundi maalum ya vijana, wazee, wenye ulemavu,
wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Katika mwaka 2016/17 Serikali
imetenga shilingi bilioni 2.4 kwa
ajili ya uboreshaji
wa miundombinu ya makazi ya wazee na mahabusu za watoto; na chakula, dawa na
mahitaji mengine ya watoto walio katika mazingira hatarishi. Katika
mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imetenga asilimia 5.0 ya mapato ya ndani ya
kila Halmashauri kwa ajili ya vijana. Aidha, shilingi bilioni 1.0 zimetengwa
chini ya Fungu 65 (Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu,
kifungu cha 2032 mradi namba 4945) kwa ajili ya kuendeleza vijana. Vilevile,
shilingi bilioni 5.0 zimetengwa Fungu 65, kifungu cha 2002 mradi namba 6581 kwa
ajili ya kuendeleza ujuzi kwa vijana ambao hawana ajira na walio kwenye soko la
ajira.
61.
Mheshimiwa Spika,
katika bajeti ya 2016/17, Serikali imetenga asilimia 5.0 ya mapato ya ndani ya
kila Halmashauri kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya maendeleo ya wanawake
katika Halmashauri husika. Vilevile, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.95 kwa
ajili ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi chini ya Fungu 53 (Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kifungu cha 3001 mradi namba
4950). Kuhusu watu wenye ulemavu, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa vifaa
vilivyotengenezwa mahsusi kwa ajili yao vinasamehewa kodi ili viweze kupatikana
kwa bei nafuu. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha shule maalum za watoto
wenye ulemavu na kugharamia mahitaji yao ili kuwajengea mazingira mazuri zaidi
ya kujifunzia.
(iii)
Wasanii, Wabunifu na Wanamichezo
62.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2016/17 Serikali kupitia Fungu 96 imetenga jumla ya shilingi
bilioni 3.0 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya sanaa, ubunifu, utamaduni
na michezo ikiwa ni pamoja na: kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa Mfuko wa
Maendeleo ya Sanaa na Ubunifu; kusimamia urasimishaji wa shughuli
za Sanaa; kusimamia na kudhibiti filamu zitakazoingia sokoni bila
kufuata taratibu; na kuratibu uendeshaji wa kazi za sanaa nchini.
(iv)Wachimbaji Wadogo wa
Madini
63. Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwezesha
wachimbaji wadogo wa madini ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao na
hivyo kuongeza ajira, kukuza kipato cha wachimbaji na wananchi wanaozunguka
maeneo ya uchimbaji madini. Katika mwaka 2016/17 Serikali inakusudia kutekeleza
yafuatayo: kuwapatia ruzuku; kuwapatia mafunzo; kuwatengea maeneo maalum ya
uchimbaji; kuimarisha soko; pamoja na kuziwezesha taasisi zinazohusika na
ukaguzi wa usalama wa migodi ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika. Kiasi
cha fedha kilichotengwa kwa madhumuni haya katika bajeti ya 2016/17 ni shilingi
milioni 900 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo.
(v)
Wafanyakazi
64. Mheshimiwa
Spika, ili kuboresha kipato cha wafanyakazi, siku ya Mei Mosi Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliagiza
kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara (PAYE) kipunguzwe kutoka asilimia
11 hadi asilimia 9 ili kupunguza makali ya maisha kwa wafanyakazi. Agizo hilo litaanza
kutekelezwa Julai Mosi 2016. Aidha, kuanzia mwaka ujao wa fedha Serikali
itaanza kuwasilisha mchango wa mwajiri wa asilimia 0.5 ya mshahara kwenye Mfuko
wa Fidia kwa wafanyakazi ili watumishi wa umma wapatapo ajali mahali pa kazi
waweze kulipwa na Mfuko. Kadhalika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya
kuwezesha watumishi wake kujenga ama kununua nyumba kupitia Bodi ya Mfuko wa
Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali, pamoja na Watumishi Housing
Company.
(vi)Vyombo vya Ulinzi na
Usalama
65. Mheshimiwa Spika, Serikali
inavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kujipambanua
kwa nidhamu ya hali ya juu katika kazi zao. Hata hivyo, Serikali inawaelekeza Maafisa
Masuuli wa Mafungu husika kujipambanua vivyo hivyo kwa nidhamu kama hiyo katika
matumizi ya fedha na mali za umma. Aidha, katika mwaka 2016/17, utaratibu wa
kutoa misamaha ya kodi kwenye maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama utasitishwa
na nitaeleza utaratibu mpya baadaye. Kadhalika, Serikali itaendelea kujenga
nyumba za makazi kwa askari ili kukabiliana na uhaba wa makazi kwa askari
nchini.
III. MABORESHO YAMFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO
66. Mheshimiwa
Spika,
napenda kuwasilisha sasa mapendekezo ya hatua mpya za kufanya marekebisho
ya mfumo wa kodi, ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada
chini ya Sheria mbalimbali na kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa
mapato ya Serikali. Aidha, marekebisho haya yanalenga pamoja na mambo mengine,
kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta
ya viwanda, kilimo, usafirishaji na kukuza ajira. Marekebisho hayo yanahusu
Sheria zifuatazo:-
a.
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
c.
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
d.
Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82;
e.
Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124;
f.
Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399 (sambamba na Sheria ya kodi
ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289; Sheria ya Fedha za Umma ya Serikali za
Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015; na Sheria ya Rufani
za Kodi, SURA 408);
g.
Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu), SURA 370;
h.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
i.
Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria
nyingine mbalimbali; na
j.
Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara
zinazojitegemea;
a)
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani, SURA 148
67.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani kama ifuatavyo: -
(i)
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
maharage ya soya baada ya kubaini kuwa, mazao haya yalisahaulika kuingizwa
kwenye orodha chini ya kifungu cha 3 cha jedwali la misamaha linalojumuisha mifugo,
mazao ya kilimo ambayo hayajasindikwa na chakula cha binadamu;
(ii)
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
mbogamboga zote na mazao ya mifugo yakiwa hayajasindikwa
kama yanavyoonekana kwenye Ushuru
wa Pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sura ya 2 na 3 (mazao ya mifugo
yasiyosindikwa), sura ya 7 (matunda na karanga), sura ya 8 (nafaka), sura ya 10
(unga wa nafaka) na sura ya 11 (mbegu za mazao). Hatua hii inakusudia kutoa
msamaha wa kodi ya VAT kwenye mazao ya chakula ambayo hayajasindikwa ili kuwezesha
upatikanaji wa lishe bora ya msingi kwa gharama nafuu;
(iii)
Kuongeza vitamini na virutubishi kwenye orodha ya
vifaa na madawa muhimu yaliyoidhinishwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kupata msamaha wa kodi. Vitamini na
virutubishi hivyo huongezwa kwenye vyakula ili kuboresha lishe kama njia mojawapo
ya kuimarisha afya ya jamii;
(iv)
Kuongeza madawa ya kutibu maji yanayotumiwa na
binadamu kwenye orodha ya vifaa na madawa muhimu yaliyoidhinishwa na Waziri wa
Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kupata msamaha wa
Kodi ya Ongezeko la Thamani. Madawa haya ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya ya
msingi kwa kutumia maji salama. Waziri wa Maji na Umwagiliaji atatakiwa
kuwasilisha orodha ya madawa hayo kwa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto ili ayajumuishe kwenye orodha hiyo;
(v)
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma
za utalii hususan kuongoza watalii, kuendesha watalii, utalii wa majini,
kuangalia wanyama na ndege wa porini, kutembelea hifadhi na usafirishaji wa
watalii ardhini. Hatua hii inachukuliwa kama ilivyokusudiwa wakati wa kutunga
Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, ambayo ilianza kutumika rasmi Julai
2015, lakini kwa kutambua mikataba iliyokuwepo wakati huo kati ya watoa huduma
za utalii na watalii waliokuwa wanatarajia kuja nchini, ilikubalika kusubiri
kukamilika kwa makubaliano hayo kwa mwaka unaomalizika. Huduma hizi pia hutozwa
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nchi nyingine kama vile Kenya, Rwanda na Afrika
ya Kusini;
(vi)
Bidhaa zinazotengezwa Tanzania Bara na kuuzwa
Zanzibar zitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani upande wa Zanzibar, na bidhaa
zinazotengezwa Zanzibar na kuuzwa Tanzania Bara zitatozwa kodi hiyo upande wa
Tanzania Bara. Lengo la hatua hii ni kuondoa utaratibu uliokuwepo hapo awali wa
kufanya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenda Zanzibar kwa kuwa
Sheria ya Kodi hiyo inayotumika sasa haina kifungu kinachoruhusu marejesho ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenda Zanzibar kama ilivyokuwa kwenye sheria
iliyofutwa. Kwa kuwa kila upande wa Muungano una Sheria yake ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, kodi hii itatozwa sehemu ambako bidhaa au huduma
itatumika, yaani “destination principle”. Kwa msingi huo muhimu katika utozaji
Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itakuwa inakusanya
kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kupelekwa Zanzibar. Vile
vile, Tanzania Bara itakuwa inakusanya kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar
na kuletwa Tanzania Bara;
(vii)
Kufanya marekebisho katika orodha ya misamaha ya
bidhaa za petroli chini ya kifungu cha 15 cha Jedwali la misamaha la Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 ili kujumuisha pia bidhaa za lami
zenye HS Code 27.13, 27.14 na 27.15 ambazo hazikujumuishwa katika Jedwali hilo;
(viii)
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima
ya vyombo vya usafiri wa anga vinavyotambulika katika HS Code 88.01 na Hs Code
88.02. Hatua hii inapendekezwa kwa kuzingatia kuwa sekta ya usafirishaji wa
anga bado ni changa kuweza kuhimili ulipaji wa bima kwa vyombo hivyo vya
usafiri. Hivyo kuna umuhimu wa kuhamasisha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga
na hatimaye kukuza utalii. Aidha, hatua hii itasaidia wawekezaji katika sekta
ya usafiri wa anga kutumia bima za hapa nchini badala ya nje kwenye mikataba ya
ukodishaji; na
(ix)
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye ada za
huduma za kibenki zinazotozwa na benki hizo ili kupanua wigo wa kodi isipokuwa
riba kwenye mikopo.
Hatua hizi za Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 136,140.3.
68.
Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho hayo kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali
itachukua hatua mbalimbali za kiutawala ndani ya Mamlaka ya Mapato ili
kuboresha makusanyo ya Kodi hii, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kabambe
ya ufuatiliaji wa makusanyo na hivyo kupanua wigo wa kodi. Ili kutekeleza azma
hii, Serikali itatekeleza yafuatayo:
(i)
kuhakikisha kuwa daftari la usajili wa walipakodi
linahuishwa kila wakati ili kuwa na taarifa sahihi za walipa kodi hao;
(ii)
kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wakubwa na
wa kati hapa nchini wanapatiwa mashine za kielektroniki na zinatumika
kikamilifu;
(iii)
kuendelea kuimarisha ukaguzi wa hesabu za
walipakodi ili kuwezesha kodi stahiki kulipwa kwa wakati; na
(iv)
Kuanzisha ofisi mpya za kusimamia mapato kwa ngazi
za wilaya katika mikoa ya kikodi kwenye Jiji la Dar es Salaam na vituo vipya
vya huduma kwa walipakodi katika maeneo mbalimbali ya majiji na miji mikubwa.
69.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza pia kufanya mapitio ya Sheria ya Uwekezaji ili iendane na
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa lengo la kudhibiti na kupunguza
misamaha ya kodi isiyo na tija.
Hatua za kiutawala kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 268,607.1.
b)
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa
(Excise Duty), SURA 147
70.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo: -
(i)
Kufanya marekebisho ya viwango maalum vya kodi
(specific duty rates) vya bidhaa zisizo za petrol kwa kiwango cha mfumuko wa
bei wa asilimia 5. Marekebisho haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa
inayotaka yafanyike marekebisho ya viwango hivyo vya ushuru kulingana na
mfumuko wa bei ili kuendana na thamani halisi ya fedha. Hata hivyo, marekebisho
haya hayatafanyika kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa.
Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:
a)
Ushuru wa vinywaji baridi, kutoka shilingi 55 kwa lita hadi shilingi 58 kwa
lita;
b)
Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 10 kwa lita hadi shilingi 11 kwa
lita;
c)
Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 210
kwa lita;
d)
Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo
haijaoteshwa (unmalted), mfano kibuku, kutoka shilingi 409 kwa lita hadi
shilingi 430 Kwa lita;
e)
Ushuru wa bia nyingine kutoka shilingi 694 kwa lita hadi shilingi 729 kwa
lita;
f)
Ushuru wa bia zisizo na kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu
kutoka shilingi 508 kwa lita hadi shilingi 534 kwa lita;
g)
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 192 kwa lita hadi shilingi 202
kwa lita;
h)
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka shilingi 2,130 kwa lita hadi shilingi
2,237 kwa lita;
i)
Ushuru wa vinywaji vikali kutoka shilingi 3,157 kwa lita hadi shilingi
3,315 kwa lita;
j)
Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka;
k)
Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi
11,289 hadi shilingi 11,854 kwa kila sigara elfu moja;
l)
Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa
hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 26,689 hadi
shilingi 28,024 kwa kila sigara elfu moja;
m) Sigara nyingine zenye sifa
tofauti na (k) na (l) hapo juu kutoka shilingi 48,285 hadi shilingi 50,700 kwa
kila sigara elfu moja;
n)
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi
24,388 hadi shilingi 25,608 kwa kilo;
o)
Ushuru wa “cigar” unabaki kuwa asilimia 30;
p)
Ushuru wa mafuta ya kulainishia mitambo kutoka shilingi 665.50 kwa lita
hadi shilingi 699 kwa lita;
q)
Ushuru wa grisi za kulainishia mitambo kutoka senti 75 kwa kilo hadi senti
79 kwa kilo; na
r)
Ushuru wa gesi asilia kutoka senti 43 kwa futi za ujazo hadi senti 45 kwa
futi za ujazo.
(ii)
Kuongeza ushuru wa bidhaa (excise duty) unaotozwa
kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambulika katika HS Code
94.01 na HS Code 94.03 kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 kwa lengo la
kuhamasisha matumizi ya samani zinazotengenezwa kwa kutumia mbao zinazozalishwa
hapa nchini, kuongeza ajira na kuongeza mapato ya Serikali;
(iii)
Kutokana na ugumu uliojitokeza katika kudhibiti
uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki, Serikali imeamua kupiga
marufuku utengenezaji, uuzaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki yenye
kipimo cha unene chini ya microns 50; na
(iv)
Kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada
zinazotozwa na watoa huduma wa simu katika kutuma na kupokea fedha badala ya
ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee. Katika utaratibu wa sasa,
baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya kwa kuhamishia sehemu kubwa
ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.
Hatua hizi za ushuru wa
bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 63,639.4.
c)
Sheria ya Kodi ya Mapato,
SURA 332;
71. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
(i)
Kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya
kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano
ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu
anayestahili kulipa kodi;
(ii)
Kutoza Kodi ya Mapato kwenye mapato yote
yatokanayo na hisa kwenye makampuni. Marekebisho hayo yatafanyika kwa kufuta
aya ya (d) katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 cha
tafsiri ya maneno “Investment Asset” (rasilimali za uwekezaji) iliyokuwa inatoa
msamaha wa kodi kwa wenye hisa chini ya asilimia 25 kwenye makampuni. Hatua hii
itaongeza wigo wa kodi kwa ujumla wake na kupunguza misamaha ya kodi;
(iii)
Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya
mapato yanayotokana na ajira kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9. Hatua hii
inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya muda mrefu ya
kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi hatua kwa hatua hadi kufikia kiwango cha
tarakimu moja. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imekuwa ikipunguza kiwango
cha kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/07 hadi kufikia
asilimia 9 inayopendekezwa sasa. Kutokana na mabadiliko hayo, viwango vya kodi
vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo:
Viwango vya sasa
Ngazi
|
Mapato
kwa Mwezi
|
Kodi kwa
mwezi
|
1.
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 170,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
2.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 170,000/=lakini
hayazidi shilingi 360,000/=
|
11% ya kiasi kinachozidi Shilingi 170,000/=
|
3.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini
hayazidi shilingi 540,000/=
|
Shilingi 20,900/= + 20% ya
kiasi kinachozidi Shilingi 360,000/=
|
4.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini
hayazidi shilingi 720,000/=
|
Shilingi 56,900/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi
540,000/=
|
5.
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 720,000/=
|
Shilingi 101,900/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi
720,000/=
|
Viwango vinavyopendekezwa
Ngazi
|
Mapato kwa Mwezi
|
Kodi kwa mwezi
|
1
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 170,000/=
|
Asilimia
sifuri (0%)
|
2
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 170,000/=lakini
hayazidi shilingi 360,000/=
|
9% ya kiasi kinachozidi shilingi 170,000/=
|
3
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini
hayazidi shilingi 540,000/=
|
Shilingi 17,100+ 20% ya kiasi kinachozidi shilingi 360,000/=
|
4
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini
hayazidi shilingi 720,000/=
|
Shilingi 53,100+ 25% ya kiasi kinachozidi shilingi 540,000/=
|
5
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 720,000/=
|
Shilingi 98,100+ 30% ya kiasi kinachozidi shilingi 720,000/=
|
(iv)
Kutoza kodi ya zuio kwenye malipo yanayofanywa
kwenye mifuko ya jamii yanayotokana na mapato ya uwekezaji ili kuweka misingi
ya usawa na haki katika utozaji kodi. Hatua hii inalenga kuweka wajibu kwa
makampuni wa kutoza kodi ya zuio kwenye malipo yanayofanywa kwenye mifuko ya
jamii kutokana na upangishaji, ukopeshaji, n.k; na
(v)
Kumpa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) mamlaka ya kukadiria mapato yanayotokana na pango kwa kuweka kiwango cha
ukomo wa chini wa thamani kulingana na hali halisi ya soko ili kutoza kodi
kwenye mapato hayo (rental income).
Hatua hizi za Kodi ya Mapato
kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 71,586.9.
72. Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho
hayo kwenye Kodi ya Mapato, hatua mbalimbali za kiutawala ndani ya Mamlaka ya
Mapato zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kabambe ya
ufuatiliaji wa makusanyo na kuanzisha ofisi mpya za kusimamia mapato katika
maeneo mbalimbali kwenye ngazi za wilaya na vituo vya miji. Hatua hii
itajumuisha kusajili walipakodi wapya, na kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji
wa walipakodi waliopo ili walipe kodi stahiki.
Hatua hizi za kiutawala kwa
pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
80,108.18.
d)
Sheria ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, SURA 82
73. Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza
Tozo ya kuendeleza ufundi stadi (Skills Development Levy) kutoka kiwango cha
sasa cha asilimia 5 hadi asilimia 4.5 ili kuwapatia nafuu ya mzigo wa tozo
waajiri na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari pasipo shuruti na hivyo
kuongeza mapato ya serikali katika muda wa kati. Hatua hii itapunguza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 28,403.4
e)
Sheria ya Magari (Kodi ya
Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124
74. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki),
SURA 124 kama ifuatavyo: -
(i)
Kufanya marekebisho ya viwango vya usajili wa
magari na pikipiki kutoka shilingi 150,000 hadi shilingi 250,000 kwa kila gari;
na kutoka shilingi 45,000 hadi shilingi 95,000 kwa kila pikipiki; na
(ii)
Kupandisha ada ya usajili wa namba binafsi za
magari kutoka shilingi 5,000,000 hadi shilingi 10,000,000 kwa kila baada ya
miaka mitatu ili kuhuisha viwango hivyo kulingana na thamani halisi ya fedha.
Hatua
hizi kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
26,915.9.
f)
Sheria ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania, SURA 399; Sheria ya kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289;
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya
mwaka 2015; na Sheria ya Rufani za Kodi, SURA 408
75. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399, Sheria ya
Kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, Sura 289, Sheria ya Fedha ya Serikali za
Mitaa, Sura 290, Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015 na Sheria ya Rufani za
Kodi, Sura 408 ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi ya
Majengo ambapo hivi sasa kodi hiyo inakusanywa na Halmashauri. Lengo la
marekebisho haya, pamoja na mambo
mengine, ni kama ifuatavyo;
(i)
Kuiwezesha
Mamlaka ya Mapato kukadiria Kodi ya Majengo na kufanya uthamini wa majengo
husika;
(ii)
Mamlaka ya Mapato Tanzania kupewa uwezo wa
kukusanya Kodi ya Majengo kwa kutumia utaratibu wake wa kawaida kupitia sheria
za kodi;
(iii)
Kuweka utaratibu wa namna ya kuhifadhi na
kuwasilisha Kodi ya Majengo itakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
kwenye Halmashauri husika;
(iv)
Kuwezesha taratibu za kutatua migogoro
itakayotokana na ukusanyaji wa Kodi ya
Majengo kusimamiwa na Sheria zinazotumika hivi sasa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania katika kusimamia migogoro ya kodi; na
(v)
Kufanya maboresho katika misamaha ya Kodi ya
Majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika mfumo wa utozwaji kodi hiyo.
g)
Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na
Majukumu), SURA 370
76. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu) SURA 370,
ili kuzitaka wakala na taasisi zote za usimamizi na udhibiti zilizo chini ya
Msajili wa Hazina kuchangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi katika Mfuko Mkuu
wa Serikali. Taasisi hizo zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Aidha,
napendekeza kuiondoa katika orodha hiyo taasisi ya AICC na kuwekwa katika
orodha ya taasisi zinazotakiwa kutoa gawio (dividend) kwa Serikali kwa kuwa ni
taasisi inayofanya biashara.
h)
Sheria ya Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
77. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti
(Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) jijini Arusha,
Tanzania, kuanzia tarehe 2 hadi 5 Mei, 2016. Katika kikao hicho, walikubaliana
kwa pamoja kufanya marekebisho ya viwango vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC
Common External Tariff “CET”) na kurekebisha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2016/17
kama ifuatavyo: -
78. Mheshimiwa Spika, marekebisho ya viwango
vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC Common External Tariff “CET”)
yaliyokubaliwa yalizingatia kwa sehemu kubwa katika kuendeleza uchumi wa
viwanda kwenye ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-
(i)
Tanzania kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ya saruji inayotambuliwa katika HS Code
2523.29.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha
na kulinda uzalishaji wa saruji hapa nchini ambao umekuwa ukiongezeka dhidi ya
ushindani wa bei ya saruji inayoingizwa nchini kutoka nje;
(ii)
Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi
asilimia 10 kwenye bidhaa za chuma (flat rolled products of iron or non-alloy
steel) zinazotambuliwa kwenye HS Codes: (HS Code 7208.54.00; HS Code
7208.90.00; HS Code 7208.52.00; and, HS Code 7208.53.00). Hatua hii inalenga
katika kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi hapa nchini. Utafiti uliofanywa na
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaonesha kuwa uzalishaji wa bidhaa za
chuma umekuwa ukiongezeka na uwezo upo wa kukidhi mahitaji. Hata hivyo kuna
ushindani usio wa haki kutoka kwenye bidhaa za vyuma zinazotoka nje ambazo ni
za bei ya chini na zisizo na kiwango bora;
(iii)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 10 kwenye bidhaa za nondo (bars and rods of iron and steel) kwa bidhaa
zinazotambulika chini ya HS Codes: (HS Code 7213.10.00; HS Code 7213.20.00; HS Code
7213.99.00; HS Code 7227.10.00; HS Code 7227.20.00; HS Code 7227.90.00; HS Code
7308.20.00; HS Code 7308.40.00; na HS Code 9406.00.90). Lengo la hatua hii ni
kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi
ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora na za bei ya chini kutoka nje ya nchi;
(iv)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0
badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa za chuma “iron and steel products”
zinazotambulika chini ya HS Code 7308.10.00 ambazo ni muhimu katika ujenzi wa
madaraja (bridge and bridge sections);
(v)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10
kwa mwaka mmoja badala ya asilimia 25 kwenye “automotive bolts and nuts”
zinazotambulika kwenye HS Code 7318.15.00. Aidha, ushuru huu unapunguzwa kwa
kuzingatia kwamba malighafi zinazotumika kutengeneza bidhaa hizi hazizalishwi
katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(vi)
Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa utaratibu
wa duty remission kwa wazalishaji wa “bolts and nuts” kwenye malighafi
zinazotambulika chini ya HS Code 7228.30.00 na HS Code 7228.50.00 kwa kutoza
kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha
wazalishaji kupata malighafi hizo kwa gharama nafuu kwa kuwa hazizalishwi katika
ukanda wa Afrika Mashariki;
(vii)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
kiwango cha sasa cha asilimia 10 kwenye nyavu za samaki zinazotambulika chini
ya HS Code 5608.11.00. Hatua hii inazingatia kuwa kuna watengenezaji wengi wa
nyavu za aina hii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(viii)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
kiwango cha sasa cha asilimia 10 kwenye bidhaa za “Oil and Petrol Filters” zinazotambulika kwenye HS Code 8421.23.00, na
“intake air filters” zinazotambulika kwenye HS Code 8421.31.00. Lengo la hatua hii
ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi
ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora na za bei rahisi kutoka nje ya nchi;
(ix)
Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza
asilimia 0 kwa utaratibu wa duty remission kwenye malighafi za kutengenezea
“air filters” za magari kwa wazalishaji wa hapa nchini;
(x)
Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza
asilimia 0 kwa utaratibu wa duty remission kwenye malighafi (splints) za
kutengenezea vibiriti zinazotambulika chini ya HS Code 4421.90.00. Hatua hii
imezingatia kwamba hakuna misitu ya kutosha na yenye mbao za kukomaa
zinazokidhi mahitaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xi)
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupunguza
msamaha wa Ushuru wa Forodha hatua kwa hatua kwenye Sukari (sugar and sugar
confectionery) kutoka kiwango cha sasa ambapo waagizaji wa sukari ya viwandani
hulipa asilimia 10. Kutokana na kupunguza msamaha huo, waagizaji watalipa
ushuru zaidi hatua kwa hatua. Upunguzaji wa msamaha utakuwa kama ifuatavyo:
Mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa asilimia 15, 2017/18 kiwango kitakuwa cha
asilimia 20, 2018/19 kiwango kitakuwa cha asilimia 25. Hatua hii inachukuliwa
kwa kuwa kiwango cha sasa cha asilimia 10 kinadidimiza viwanda vyetu vya ndani
na pia ni chachu ya matumizi mabaya ya misamaha husika;
(xii)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 10 za sasa kwa bidhaa zinazotambulika chini ya HS Code 7612 “Aluminium
Milk Cans”. Hizi ni bidhaa zilizokamilika tayari kwa kutumika hivyo zinatakiwa
kutozwa ushuru wa asilimia 25 unaostahili kwa bidhaa za namna hiyo. Lengo la
hatua hii ni kulinda wazalishaji wa ndani wenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizi
kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiii)
Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza
asilimia 0 malighafi zinazoagizwa na wazalishaji wa Aluminium cans
zinazotambulika chini ya HS Codes 7606.12.00 na HS Codes 7606.92.00. Hatua hii
inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa “aluminium cans” katika Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiv)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya
asilimia 35 kwenye ngano (Wheat grain) inayotambuliwa chini ya HS Code
1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa mwaka mmoja. Hatua hii imezingatia kwamba
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha ngano ya aina hii
na kuweza kutosheleza mahitaji. Aidha, itatoa unafuu kwa wazalishaji wa bidhaa
na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei ya bidhaa za ngano;
(xv)
Kuongeza kiwango maalumu cha ushuru kwenye mitumba
ya nguo na viatu kutoka kiwango cha sasa cha dola za kimarekani 0.2 kwa kilo
hadi dola 0.4 kwa kilo. Hatua hii imechukuliwa ili kudhibiti hatua kwa hatua
uingizaji nchini wa nguo za mitumba ambazo zimeonekana kuwa siyo salama kwa
afya za watu wetu. Aidha, Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
zimekubaliana kuzuia kabisa uingizaji wa bidhaa hizi baada ya miaka mitatu
kuanzia sasa. Hata hivyo Nchi hizi zimekubaliana kuweka mikakati ya kuimarisha
na kuhamasisha uzalishaji wa nguo na viatu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
ili kukidhi mahitaji. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji tayari imeandaa
mikakati madhubuti ya kuendeleza sekta za ngozi na nguo;
(xvi)
Kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25
au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (iron
and iron-alloy steel) kwa mwaka mmoja, zinazotambuliwa katika HS Codes: HS Codes 7210.41.00; HS Codes 7210.49.00; HS
Codes 7210.61.00; HS Codes 7210.69.00; HS Codes 7210.70.00; HS Codes
7210.90.00; HS Codes 7212.30.00; and HS Codes 7212.40.00. Lengo la hatua hii ni
kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi
ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi. Utafiti uliofanywa
na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko
kubwa la uzalishaji wa bidhaa za vyuma kupita mahitaji ya soko katika soko la
dunia. Hali hiyo imesababisha kushuka sana kwa bei na hivyo kuathiri viwanda
vyetu kutokana na ushindani wa bidhaa hizo kutoka nje. Hatua hii ya kuweka
viwango maalum vya kodi ni muhimu kulinda viwanda na bidhaa zetu (anti-dumping
measure);
(xvii)
Kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25
au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa
za chuma (Flat-rolled products of bars, rods, sections, angles, shapes, and
related products) zinazotambuliwa katika HS Codes: HS Codes 7214.10.00; HS
Codes 7214.20.00; HS Codes 7214.30.00; HS Codes 7214.91.00; and HS Codes 7214.99.00.
Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na
viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya
nchi;
(xviii)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo “metric ton’ kwenye
bidhaa za chuma (steel reinforcement bars, angles, sections zinazotambuliwa chini ya HS Codes: 7216.10.00; HS Codes
7216.21.00; HS Codes 7216.22.00; and HS Codes 7216.50.00.). Lengo la hatua hii
ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani
dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi;
(xix)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya
asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya kula (crude edible oil) yanayotambulika
katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika
kuhamasisha kilimo cha mbegu za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya
kutengeneza mafuta ya kula. Aidha, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
imeandaa mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya kuzalisha mafuta yanayotokana
na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fursa soko kubwa lililopo katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania inayo nafasi ya kuweza kuongeza
uzalishaji wa mbegu za mafuta;
(xx)
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 10 kwa bidhaa za karatasi zinazotambulika kwenye HS Codes: HS Codes
4804.11.00; HS Codes 4804.19.10; HS Codes 4804.19.90; HS Codes 4804.21.00; HS
Codes 4804.29.00; HS Codes 4804.31.00; HS Codes 4804.39.00; HS Codes
4804.41.00; HS Codes 4805.59.00; HS Codes 4805.11.00; HS Codes 4805.12.00; HS
Codes 4805.19.00; HS Codes 4805.24.00; HS Codes 4805.25.00; HS Codes
4805.30.00; HS Codes 4805.91.00, na HS Codes 4805.92.00. Hatua hii inachukuliwa
ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyozalisha karatasi za aina hiyo na
ajira;
(xxi)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa
za nondo zinazotambulika kwenye HS Codes HS Codes 7228.10.00; HS Codes
7228.20.00; HS Codes 7228.30.00; HS Codes 7228.40.00; HS Codes 7228.50.00; HS
Codes 7228.60.00; HS Codes 7228.70.00; na HS
Codes 7228.80.00. Lengo ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na
ushindani wa bidhaa kama hizo zinazoagizwa nje; na
(xxii)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 - kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa
za chuma zinazotambulika kwenye HS Codes 7212.40.00; HS Codes 7215.10.00; HS
Codes 7215.50.00; HS Codes 7215.90.00; HS Codes 7216.61.00; HS Codes
7216.69.00; HS Codes 7216.91.00; na HS Codes 7216.99.00.
79.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia
marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
(EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo: -
(i)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa
forodha ili kuongeza vifaa vya majokofu yanayotumika katika kuhifadhi maiti
yanayotambuliwa chini ya HS Code 8418.69.90 kwa matumizi ya hospitali na mamlaka
za miji (city councils);
(ii)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Chapters 84 and 69) linalotoa
msamaha wa ushuru wa forodha ili kuongeza vifaa vinavyotumika kwenye hospitali
kuteketeza na kuchoma uchafu (incinerator’s equipments and materials used in
hospitals to burn waste);
(iii)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuondoa msamaha wa ushuru
wa forodha unaotolewa kwenye sare za wafanyakazi wa hospitali. Msamaha huu unaondolewa kwa kuwa sare hizi
zinaweza kuzalishwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(iv)
Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu
wa “Duty remission” kwa wazalishaji wa hapa nchini wa malighafi zinazotumika
kutengeneza betri zinazofahamika kama “deep cycle batteries”. Hatua hii
inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa viwanda vya ndani kwa kuwa deep cycle
batteries zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zimesamehewa ushuru kupitia Jedwali
la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(v)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa
forodha ili kujumuisha chupa zinazotumika kwa ajili ya kukusanya damu kwenye
hospitali (blood collection tubes); na
(vi)
Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu
wa “Duty remission” kwa malighafi zinazotumika kuzalisha vifaa vya nishati ya
umeme wa jua (Solar equipments).
Hatua zote za Ushuru wa
Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato kwa kiasi cha shilingi milioni
42,850.6.
i)
Marekebisho madogo madogo
katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali
80. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera na ya kiuandishi katika
Sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya
kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika muswada wa
Sheria ya Fedha 2016.
81. Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha
utekelezaji wa Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015, na kuleta uwajibikaji katika
utekelezaji wa Bajeti ya Mfuko wa Mahakama na Mfuko wa Bunge napendekeza
kufanya marekebisho yafuatayo:-
(i)
Kurekebisha kifungu cha 29 kifungu kidogo cha 3
cha Sheria ya Utawala wa Bunge, SURA 115 (The National Assembly Administration
Act, CAP 115) ili kubainisha kuwa bajeti ya Mfuko wa Bunge itawasilishwa
Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya Bunge. Hivi sasa Sheria hii
imeweka sharti kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuwasilisha Bungeni
Bajeti ya Mfuko wa Bunge; na
(ii)
Kurekebisha kifungu cha 59 kifungu kidogo cha 3
cha Sheria ya Utawala wa Mahakama, SURA 237 (The Judiciary Administraion Act,
CAP 237) ili Bajeti ya Mfuko wa Mahakama iwasilishwe Bungeni na Waziri mwenye
dhamana na masuala ya mahakama. Kifungu hiki kwa sasa kimeweka sharti kwa
Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Mfuko
wa Mahakama.
j)
Marekebisho ya Ada na Tozo
Mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
82. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa
na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa
uchumi. Aidha, napendekeza kufuta baadhi ya ada na tozo ambazo zimeonekana kuwa
kero kwa wananchi na kikwazo katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara
hapa nchini. Tozo na ada ninazopendekeza kuzifuta ni kama ifuatavyo:
(i)
Mamlaka ya Chakula na Dawa
(Tanzania Foods and Drugs Authority – TFDA):
a)
Kibali cha kusafirisha chakula nje ya nchi kwa shilingi 50,000;
b)
Kushikilia dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya ndani
kwa shilingi 100,000;
c)
Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda
vya ndani kwa Dola za Kimarekani 50;
d)
Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda
vya nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
e)
Tathimini ya matangazo ya bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za
Kimarekani 50;
f)
Matangazo yanayofanyiwa tathimini fupi kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini
kwa Dola za Kimarekani 25;
g)
Kudurufu cheti cha usafi wa chakula, dawa na vifaa tiba vinavyotengenezwa
nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
h)
Kudurufu cheti cha vifaa tiba vinavyotengenezwa ndani ya nchi kwa Dola za
Kimarekani 30;
i)
Kudurufu cheti cha dawa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 50;
j)
Kushikilia vitendanishi vinavyotengenezwa nje ya nchi katika rejesta kwa
Dola za Kimarekani 150;
k)
Kushikilia vipodozi vinavyotengenezwa ndani ya nchi katika regesta kwa
shilingi 30,000;
l)
Ukaguzi wa kiwanda cha dawa cha ndani ya nchi kabla ya kusajiliwa kwa Dola
za Kimarekani 250;
m)
Wawakilishi wa makampuni ya dawa ya nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani
1,000;
n)
Malighafi za vipodozi zinazoingizwa nchini kwa shilingi 50,000,000;
o)
Malighafi za dawa zinazoingizwa nchini kwa shilingi 100,000,000;
p)
Kibali cha hospitali kununua dawa zenye madhara ya kulevya kutoka bohari
kwa Dawa ya shilingi 10,000;
q)
Ada ya uingizaji nchini wa dawa zenye madhara ya kulevya ya shilingi
50,000;
r)
Cheti cha kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa shilingi 50,000;
s)
Cheti cha utambuzi wa dawa inayosafirishwa nje ya nchi kwa 50,000;
t)
Ukaguzi wa kiwanda kidogo kipya cha kusindika chakula kwa shilingi 100,000;
u)
Cheti cha kuteketeza bidhaa;
v)
Cheti cha Afya kwa ajili ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa shilingi 50,000; na
w)
Kibali cha kufanya maonyesho ya biashara ya bidhaa inayodhibitiwa kwa
shilingi 200,000.
(ii)
Bodi ya Pamba:
a)
Mchango wa mwenge kwa kila kiwanda cha kuchambua pamba wa shilingi 450,000;
na
b)
Ada ya vikao vya Halmashauri za wilaya wanapojadili maombi mbalimbali ya
wafanyabiashara wa pamba ya shilingi 250,000.
(iii)
Bodi ya Chai: Kodi ya moto na uokoaji.
(iv)
Bodi ya Kahawa: Ada ya leseni ya kusindika
kahawa ya Dola za Kimarekani 250.
(v)
Bodi ya Korosho:
a)
Ushuru wa chama kikuu cha ushirika wa shilingi 20 kwa kilo;
b)
Ushuru wa kusafirisha korosho wa shilingi 50 kwa kilo;
c)
Gharama za mtunza ghala kwa shilingi 10 kwa kilo;
d)
Kikosi kazi kwa ajili ya ufatiliaji wa masuala mbalimbali kwa kuchangia
shilingi 10 kwa kilo; na
e)
Makato ya unyaufu.
83. Mheshimiwa Spika, napenda nilifahamishe
Bunge lako Tukufu pamoja na wananchi kwamba, hatua ninazopendekeza za kufuta
tozo na ada nilizozifanya ni za awali tu wakati Serikali inaendelea kufanya
uchambuzi na tathmini ya kina kuhusu tozo na ada zinazotozwa na mashirika,
taasisi na wakala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Serikali za Mitaa. Hatua hizi
ni endelevu katika kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya kufanya biashara
ili nchi yetu iweze kuwa na nafasi nzuri ya kiushindani katika biashara na
kuvutia uwekezaji. Aidha, lengo la hatua hizi ni pamoja na kuondoa kero kwa
wananchi na kuwapa unafuu katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi.
84. Mheshimiwa Spika, napendekeza pia
kurekebisha baadhi ya viwango vya ada na tozo mbalimbali kama zitakavyoainishwa
kwenye Sheria ya Fedha 2016 na nyingine kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GNs)
na Mawaziri wenye dhamana na ada na tozo hizo.
k)
Kodi na Tozo Kwenye Bidhaa za
Mafuta ya Petroli
85. Mheshimiwa Spika, kwa muda sasa bei ya
mafuta (petroli, dizeli na ya taa) imekuwa ikishuka katika soko la dunia, hali
ambayo imesaidia kuleta unafuu wa gharama katika shughuli za kiuchumi hususan
kwa wananchi masikini maana bei za mafuta haya zinagusa kila mtu. Hivyo,
Serikali imeamua kuwa Ushuru wa Barabara, Ushuru wa Petroli na Ushuru wa Bidhaa
kwenye mafuta ya petroli utabaki kama ilivyo sasa. Hivyo, Mfuko wa barabara na
Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini watumie fedha hizi vizuri.
l)
Misamaha ya Kodi kwa Majeshi
ya Ulinzi na Usalama
86. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu
Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi (Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Ongezeko la
Thamani na Ushuru wa Forodha) kwa majeshi ya Ulinzi na Usalama kupitia kwenye
migahawa na maduka maalum ambayo yanauza bidhaa mbalimbali kwa mahitaji ya
askari. Katika kufanya hivyo, kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa matumizi
mabaya ya misamaha hiyo. Aidha, kutokana na hali hiyo ya upotevu wa mapato,
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeondokana na utaratibu huu isipokuwa
Rwanda na Tanzania ambazo zinatoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama.
87. Mheshimiwa Spika, katika kikao cha Mawaziri
wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti kwa mwaka
2015/16, Serikali ya Tanzania ilitakiwa kuangalia njia mbadala ya kutoa unafuu
wa gharama kwa majeshi yake badala ya utaratibu wa kutoa misamaha. Ili
kuendelea kutoa huduma kwa majeshi hayo pasipo kupoteza mapato ya Serikali,
napendekeza kuwapatia posho majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama ili kuwawezesha
kununua mahitaji yao wenyewe. Dhamira ya hatua hii ni kusitisha msamaha wa kodi
kwa majeshi ili kuondoa uvujaji mkubwa wa mapato na wakati huo huo, kuendelea
kuwapatia askari wetu mahitaji yao muhimu kwa utaratibu mzuri zaidi. Aidha, lengo
la hatua hii ni kuhakikisha kuwa motisha unaotolewa unawanufaisha walengwa,
yaani askari, badala ya wajanja wachache kuendelea kunufaika na misamaha hiyo.
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
88. Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2016, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
IV.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2016/17
89. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za
uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka 2016/17, Sura ya Bajeti
inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 29.54 zinatarajiwa kukusanywa na
kutumika katika kipindi hicho. Bajeti ya mwaka 2016/17 inatarajiwa kuwa na ongezeko
la jumla ya shilingi trilioni 7.04 sawa na asilimia 31.1 ikilinganishwa na Bajeti
ya mwaka 2015/16 ya shilingi trilioni 22.49.
90. Mheshimiwa Spika, Serikali inalenga
kukusanya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri ya jumla ya
shilingi trilioni 18.46 sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote. Kati ya mapato
hayo, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 15.11 sawa na asilimia 13.8 ya Pato
la Taifa. Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri
ni shilingi trilioni 2.69 na shilingi bilioni 665.4 kwa mtiririko huo. Makisio
ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi
vinavyoonesha kwamba TRA kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zinazokusanya
maduhuli wana uwezo wa kukusanya kiasi hiki cha mapato. Hivyo, Serikali
itasimamia kwa karibu na kuziba mianya yote ya uvujaji wa mapato ya kodi na
yasiyo ya kodi ili kuhakikisha kuwa malengo ya ukusanyaji yanafikiwa.
91.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na
mikopo ya jumla ya shilingi trilioni 3.60 ambayo ni asilimia 12 ya bajeti yote.
Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 2.75
ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo; shilingi bilioni 372.1
ni misaada na mikopo kwa mifuko ya pamoja ya kisekta; na shilingi bilioni 483
ni misaada na mikopo ya kibajeti (GBS).
92. Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya
bajeti, katika mwaka 2016/17 Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni
7.48 kutoka katika vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni
5.37 zinategemewa kukopwa katika soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani
na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja na mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia
miradi ya maendeleo na kulipia malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa. Aidha, ili
kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu na kuhakikisha inatekeleza Mpango wa
Pili wa Maendeleo kikamilifu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.10
kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
93. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa za kuongeza
ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kugharamia, pamoja na mambo mengine, miradi
ya maendeleo. Utekelezaji wa miradi hiyo pia hutegemea mikopo ya nje ya
kibiashara ambayo upatikanaji wake hutegemea hali ya soko la fedha duniani.
Katika mwaka 2016/17, kuna miradi mikubwa hususan ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha standard gauge na
uimarishaji wa bandari ambayo matayarisho yake yanahitaji muda na umakini
mkubwa hasa uhakika wa upatikanaji wa fedha. Hivyo, utekelezaji wa miradi hii
unatarajiwa kuanza katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2016/17 baada ya
kutathmini hali ya upatikanaji wa fedha zaidi na kukamilisha maandalizi ya
msingi ikiwa ni pamoja na kumpata mkandarasi na kuingia mkataba. Matarajio ya
Serikali ni kuwa mkandarasi atakabidhiwa eneo (site) ndani ya miezi tisa (9) ya
kwanza ya 2016/17.
94. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi,
katika mwaka 2016/17 Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 29.54
kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 17.72
zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi
trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ambapo kiasi cha shilingi trilioni
8.70 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 3.12 ni fedha za nje.
95. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa
bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni kama
inavyooneshwa katika Jedwali, ukurasa wa 92 wa kitabu cha hotuba hii.
Mfumo wa Bajeti wa Mwaka 2016/17
V.
HITIMISHO
96.
Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wengi wamechoka na adha ya umaskini: Watanzania wanataka
kipato cha kuweza kukidhi mahitaji yao ya msingi. Wananchi wanataka huduma bora
zaidi hususan upatikanaji wa maji, elimu, afya, umeme na makazi; akina mama
wamechoka kutembea na ndoo za maji kichwani; watoto wetu shuleni wamechoka
kukaa chini na kugombania matundu machache ya vyoo; vijana wanataka ajira; kilio
cha mauaji ya kikatili ya albino ni fedheha kwa nchi yetu; wananchi bado
wananyimwa haki zao kutokana na kukithiri kwa rushwa; Watanzania wanataka nchi
yenye neema; Watanzania wanataka Serikali inayofanya kazi kwa ufanisi;
Watanzania wanataka mazingira safi na endelevu; Watanzania wanataka miundombinu
na usafiri wa kisasa na salama; Watanzania wanataka miji na makazi yaliyopimwa
na yaliyopangwa vizuri; na pia Watanzania wanapenda amani, utulivu, utangamano
na furaha. Hata hivyo, napenda nisisitize kuwa Tanzania mpya ambayo wote
tunaitamani iko mikononi mwetu!!
97.
Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha hotuba yangu napenda kuwaambia Watanzania wenzangu
siri ya maendeleo. Siri ya kuifikia Tanzania mpya tunayoitamani! Kwanza,
maendeleo hayaji hivi hivi! Maendeleo yanataka dhamira na utashi, juhudi na
maarifa; maendeleo yanataka vitendo, siyo maneno! Maendeleo yanataka pawepo
dira ya kutuongoza tunakotaka kwenda. Ili kufanikiwa, lazima kuyafahamu vizuri
mazingira tulipo na njia ya kupita, hususan fursa na hatari zilizo mbele yetu.
Maendeleo yanataka mwelekeo (focus), vipaumbele, malengo na viashiria vya hatua
iliyofikiwa; maendeleo yanahitaji nidhamu ya hali ya juu hususan katika
matumizi ya rasilimali (watu, fedha, muda, vitendea kazi na mali). Maendeleo
yanataka usimamizi makini wa utekelezaji. Hivyo, maendeleo yanataka hatua kali
za kumwajibisha yeyote anayekwamisha na kuhujumu juhudi zetu kwa kutotimiza
wajibu, uzembe, rushwa, ubadhirifu n.k. Maendeleo yanahitaji kujinyima au kujitoa
(sacrifice) na kwa maana hiyo yafaa Watanzania tujitafakari juu ya kujengeka
kwa utamaduni wa kuchangishana michango mingi ya sherehe za anasa na badala
yake tujielekeze kusaidiana katika masuala ya maendeleo kama ada za shule,
gharama za matibabu n.k. Aidha, maendeleo yanahitaji muendelezo wa hatua stahiki
badala ya kurukia mambo mapya kabla ya kukamilisha yaliyoanza kutekelezwa (consistency of action); Maendeleo yanapatikana
kwa kufanya kazi kwa bidii (hard work). Hivyo, maendeleo hayatakuja kwa kucheza
pool table na kunywa viroba muda wote;
maendeleo yanapatikana kwa kuthubutu (boldness) na kujiamini (self confidence)
na hatimaye kuamua kujitegemea.
98.
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niseme juu ya utegemezi kwa misaada kutoka kwa wahisani. Tangu
Uhuru wafadhili wameendelea kutupatia misaada ambayo imetoa mchango mkubwa
katika maendeleo ya Taifa letu. Hata hivyo, pamoja na kuwa lengo la misaada ni
kujazia uwezo wa taifa kutekeleza miradi ya maendeleo au kukabiliana na maafa,
ni vizuri watanzania wenzangu tukaelewa kuwa kwa upande mwingine misaada
inaweza kuwa sumu ya maendeleo! Misaada inaweza kuwa uchochoro wa sera na
miradi mibovu, inapoteza kujiamini na masharti yanayoambatana na misaada
yanapunguza uhuru wa kujiamulia mambo. Misaada pia inaweza kuchochea rushwa na kuzorotesha
jitihada za ndani hususan za ukusanyaji mapato. Mwanazuoni anayeitwa Sebastian
Edwards katika kitabu chake – Toxic Aid:
Economic Collapse and Recovery in Tanzania (2014) amefichua ukweli huo kwa
maneno yafuatayo, nanukuu:-
“After analysing in great depth Tanzania’s history during its first two
decades as an independent nation, it is clear to me that the official aid
community had a major responsibility in one of the most colossal collapses of a
poor country in the history of the modern world. When one adds and subtracts everything – the
misguided policies, the blunders, the growing corruption, and the socially
worthwhile projects- the balance is hugely negative. The inescapable conclusion of that exercise
is that during 1961-81 aid was worse than ineffective; it was toxic”! Mwisho
wa kunukuu.
Hivyo, ni muhimu sana kama
taifa tutambue jambo hili na tufanye kila linalowezekana kupunguza utegemezi
kwa misaada ya wahisani kwa kulinda utulivu wa uchumi, kujenga uwezo wetu
wenyewe hususan kukuza sekta ya viwanda ili kupanua wigo wa kukusanya zaidi
mapato ya ndani na kwa ufanisi zaidi. Ni muhimu sana tuweke msukumo zaidi wa
kukuza na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje pamoja na kuimarisha biashara
katika mahusiano yetu na nchi rafiki.
99.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho na muhimu sana ni kuwa maendeleo endelevu yanapatikana
haraka katika mazingira ya amani na usalama. Hivyo ni lazima tunu ya amani katika
nchi yetu ilindwe kwa nguvu zote.
100.
Mheshimiwa Spika, Rai yangu kwa watanzania: Mungu ametujalia rasilimali nyingi; Mama zetu
walizaa na wanaendelea kuzaa watoto wenye akili timamu, wabunifu na wenye uwezo
wa kutatua changamoto kuu na vikwazo kwa maendeleo ya Tanzania mpya. Hivyo,
tukiongozwa na uzalendo, uchungu wa nchi hii na uthubutu wa Rais wetu Mhe. Dkt
John Pombe Joseph Magufuli, lazima sasa tudhamirie kuigeuza Tanzania kuwa nguvu
kuu ya kiuchumi katika kanda hii ya Afrika (economic power house) katika
kipindi cha miaka kumi ijayo. Tukiwa na nia moja, inawezekana, na hakika Mungu
yuko upande wetu.
101.
Mheshimiwa Spika, ningependa pia kuchukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wenzangu na
wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matumizi ya muda ambao ni rasilimali
muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Watanzania wengi tunatumia muda vibaya
kwa mambo yasiyokuwa na tija na hatuzingatii muda katika kutimiza majukumu
yetu. Kwa upande wa watumishi wa umma, kumekuwa na mazoea ya kutumia muda mrefu
kwenye vikao na mikutano na kuacha majukumu ya msingi ya kuwahudumia wananchi.
Vilevile, wananchi hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa wamekuwa
wakitumia muda mwingi wa kazi kufanya mambo yasiyokuwa na manufaa kwao binafsi
na Taifa kwa ujumla, hususan; unywaji wa pombe, kucheza pool, uzururaji, kamari, sinema za mitaani, kukaa vijiweni na
kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo, natoa rai kwa
watanzania wote kuthamini matumizi mazuri ya muda kwa kufanya kazi kwa bidii
ili kuchochea maendeleo yetu binafsi na Taifa kwa ujumla.
102.
Mheshimiwa Spika, Ninapoelekea
kumalizia hotuba hii, napenda kusisitiza mambo yafuatayo ambayo yanalenga
kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ili kuweza kutekeleza
bajeti kama ilivyopangwa:
Kwanza, Serikali itaongeza msukumo katika matumizi ya mashine za EFD ili kuhakikisha
kila mfanyabiashara anatoa risiti za mashine za EFD na wanachi wanadai risiti
pale wanapofanya manunuzi ya bidhaa au huduma. Katika kutimiza azma hii Wizara
yangu itaunda Kikosi Maalum cha kufuatilia utekelezaji wa agizo hili katika
maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili kuhakikisha wale wote wataokiuka utaratibu
huu wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria. Ninapenda kutoa rai kwa viongozi
wote, hususan Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge, Madiwani na Viongozi wa Dini kuwa mfano
wa kuigwa kwa wananchi wetu kwa kuhakikisha kuwa tunadai risiti za EFD pale tunaponunua
bidhaa au huduma. Aidha, viongozi wote mnaombwa kuhamasisha wananchi kudai
risiti za EFD. Kila asiyetoa risiti na asiyedai risiti ajue anatenda kosa na
anasaliti jitihada zetu za kuijenga Tanzania mpya.
Pili, vituo
vyote vya kuuzia mafuta ya petroli vinaagizwa kukamilisha ufungaji wa mashine
za EFD kwenye pampu za kuuzia mafuta hayo ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016 ili
kuhakisha kuwa Serikali inakusanya kodi stahiki. Serikali itafanya ukaguzi
kwenye vituo vyote vya mauzo ya mafuta hapa nchini na kuchuka hatua za kisheria
kwa wale watakaokaidi agizo hili.
Tatu, katika kudhibiti misamaha ya kodi inayotolewa kwa wafanyabiashara,
watumishi wa umma, mashirika ya dini na taasisi zisizo za kiserikali, kuanzia
mwaka ujao wa fedha watalazimika kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazoagiza.
Kodi hiyo itarejeshwa kwa wanufaikaji baada ya ukaguzi kufanyika na
kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Aidha, Serikali itawataka wanufaika
kuwasilisha maombi yao Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kuagiza bidhaa
husika ili kupata kibali cha uagizwaji wa bidhaa hizo.
Nne, Maafisa Maasuuli wote wanaagizwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki
katika ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za
Mitaa, na Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na kudhibiti
upotevu wa mapato. Aidha, kodi na tozo hizo zitakazokusanywa zipelekwe benki ndani
ya masaa 24.
Tano, kuanzia mwaka ujao wa fedha utaratibu wa kubakiza sehemu ya makusanyo,
yaani mfumo wa retention umefutwa. Taasisi
zote zilizokuwa zikitumia mfumo huo zitalazimika
kuwasilisha mapato yote kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Utoaji wa fedha kutoka
Hazina kwenda kwenye taasisi hizo utazingatia utaratibu wa kawaida kulingana na
bajeti iliyoidhinishwa.
Sita, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia agizo la Serikali la kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo yaliyoainishwa ikiwa ni pamoja na:
safari za nje ya nchi, mafunzo nje ya nchi, posho za vikao, warsha na
makongamano, sherehe na maadhimisho ya kitaifa, ununuzi wa samani, ununuzi na
uendeshaji wa magari, n.k. ili kupata fedha zaidi na kuzielekeza kwenye miradi
ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Saba, Waajiri wanatakiwa kuwasilisha kodi ya mapato ya wafanyakazi – PAYE
pamoja na michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati. Aidha, kwa
wale wenye malimbikizo ya PAYE na michango, wanaagizwa kuwasilisha malipo hayo
kabla ya tarehe 31 Desemba, 2016 vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi
yao. Maafisa Masuuli, Wakuu wa Taasisi, Mashirika na Kampuni Binafsi wanaagizwa
kusimamia utekelezaji wa agizo hili.
Nane, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kutumia mfumo wa nakala laini (soft copy)
katika kusambaza nyaraka mbalimbali za Serikali zinazozidi kurasa 50 isipokuwa
kwa mafungu yanayotakiwa kusambaza nakala ngumu (hard copy) kutokana na matakwa
ya kikanuni/kisheria. Hatua hii inalenga kupunguza matumizi makubwa ya gharama
za kuchapisha na kudurufu nyaraka hizo na kulinda mazingira.
Tisa, katika mwaka wa fedha 2016/17 madai yote yanayohusu huduma za umeme, maji na simu yatalipwa moja
kwa moja (centrally) na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutumia bajeti za
mafungu husika. Aidha, Maafisa Masuuli wanaagizwa kulipa kwa wakati ankara za
huduma za umeme, maji na simu ili kuepuka malimbikizo ya madai mapya.
Kumi, Maafisa Masuuli wanaagizwa
kufanya ununuzi kwa kutumia Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa IFMS.
Aidha, wazabuni na watoa huduma wanaelekezwa kuhakikisha wanapatiwa Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa
IFMS. Hivyo, kuanzia mwaka 2016/17 Hati za ununuzi zitakazotolewa nje ya
utaratibu huu hazitatambuliwa kama hati halali za ununuzi.
103.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya utekelezaji wa bajeti niliyowasilisha yatategemea
ushirikiano wa kila mmoja wetu ili kufikia malengo yanayokusudiwa. Kama
nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2016/17 itategemea zaidi mapato ya
ndani katika utekelezaji wake, hivyo kila taasisi ya Serikali inahimizwa
kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la
mapato linalokusudiwa na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi wetu. Ninaomba
sote tushirikiane kwa pamoja na kila mmoja awajibike katika nafasi yake ili
tuijenge Tanzania ya viwanda.
104.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, niwashukuru kwa dhati wananchi wa Tanzania, hususan
wakulima, wafugaji na wavuvi, wafanyabiashara, watumishi wa umma na walioko
sekta binafsi, na Diaspora ambao wanafanya kazi kwa bidii kuchangia maendeleo
ya uchumi wa Taifa. Ninyi ndiyo
nguzo/muhimili wa Taifa linalojitegemea. Serikali inawathamini sana.
Ninawashukuru pia vijana, Taifa la kesho. Wale waliopo shuleni na vyuoni someni
kwa bidii mpate maarifa na ujuzi wa kuijenga nchi yenu. Na wale wengine tumieni
nguvu zenu na ubunifu wenu katika kilimo cha mazao ya thamani kubwa, ufugaji,
na huduma ikiwa ni pamoja na tasnia za ubunifu, muziki, filamu, komedi, mitindo
ambako bado kuna fursa tele za kujipatia kipato halali ili kukidhi mahitaji ya
maisha.
105.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wetu wa
Maendeleo wanaotarajia kuchangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kama
ifuatavyo: nchi za Canada, Jamhuri ya watu wa China, Denmark, Finland,
Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya Kusini, Marekani, Norway,
Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi,
pia taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Arab Bank for Economic Development
in Africa (BADEA), Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Global Fund,
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Organisation of the Petroleum Exporting
Countries (OPEC Fund), Saudi Fund, Kuwait Fund, na Umoja wa Ulaya. Aidha,
napenda kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera unaojulikana kama Policy Support
Instrument (PSI). Rai yangu kwa marafiki zetu ni kuwa: Endeleeni kutuunga mkono
hususan katika jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwavutia
wawekezaji kutoka katika nchi zenu na kututafutia fursa za masoko ya bidhaa
zetu. Mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi kutumia michango yenu kwa
ufanisi na uwazi.
HAPA KAZI TU! MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
106.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment