Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema
wakati akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa kujadili program mpya mbili za
masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa na Ugavi, Usimamizi mfumo wa uzalishaji na
usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo hicho.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo akichangia wakati wa Mkutano huo.
Wadau mbalimbali wakifuatilia
kwa makini majadiliano kuhusu program mpya mbili za masomo katika ngazi ya
Shahada ya Uzamili katika Biashara ya Kimataifa na Ugavi, Usimamizi wa mfumo wa uzalishaji na
usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na CBE.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria katika chuo
hicho kujadili program mpya mbili za masomo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika
Biashara ya Kimataifa na Ugavi, Usimamizi
mfumo wa uzalishaji na usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo
hicho.
Na. Aron Msigwa – Dar es salasam.
Tanzania bado inahitaji wataalam waliobobea
katika Biashara ya Kimataifa na wale wanaosimamia mfumo wa uzalishaji,
usambazaji na utunzaji wa bidhaa mbalimbali
hususan mazao ya chakula ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama
kubwa ya uagizaji, utunzaji, usambazaji na hasara ya kuharibika kwa mazao inayowakumba wafanyabiashara walio wengi
kabla ya kufikisha bidhaa zao kwa walaji.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam
na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Emanuel Mjema wakati
akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa kujadili program mpya mbili za masomo
katika ngazi ya Shahada ya Uzamili (Masters)katika Biashara ya Kimataifa na Ugavi, Usimamizi wa mfumo wa uzalishaji na
usambazaji, zinazotarajiwa kuanza kutolewa na chuo hicho.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo zinazowakumba
wakulima na wafanyabiashara walio wengi hasa wale wa matunda ambao hupoteza karibu
asilimia 40 ya mazao yao, lazima hatua madhubuti zichukuliwe kwa kuwajengea
uwezo wa kitaalamu vijana wa Kitanzania ambao wataweza kukabiliana na
changamoto ya wakulima kupata hasara kwa kuhakikisha mazao yanayotoka kwenye
maeneo ya uzalishaji yanafika yakiwa salama.
‘Leo tuna mkutano wa wadau kwa sababu CBE tuko katika hatua za mwisho
za mchakato wa kuanzisha Programu mpya za Shahada za uzamili katika katika
masuala ya Ugavi (Procurement and Supply Chain Management) pia Shahada ya
Uzamili katika Biashara ya Kimataifa (International Business Management) ili
tuweze kutoa mafunzo yatakayowasaidia watanzania’’
Amebainisha kuwa mazao kama matunda mara
nyingi yamekuwa yakiharibika katika hatua ya kuvunwa, kusafirishwa na
kuhifadhiwa jambo linalowasababishia hasara wakulima pamoja na wasafirishaji
kwa kuwa hawana ujuzi na utalaam wa usimamizi wa bidhaa na mazao yao.
Aidha, ameongeza kuwa asilimia 40 ya
gharama hizo hutumika katika masuala ya usafirishaji na ufuatiliaji wa bidhaa husika kuifikisha kwa
mlaji na kusisitiza kwamba gharama hizo husababishwa na mfumo mzima unaopaswa
kupitiwa kabla ya kuifikisha bidhaa husika sokoni jambo ambalo lingerekebishwa
kwa kuwa na wataalam wa kutosha kusimamia sekta hiyo.
"Tanzania tunahitaji wataalam
waliobobea katika eneo hili, tumekuwa na changamoto nyingi, mfano
mfanyabiashara akinunua mahindi kutoka wilaya
ya Mpanda au Namanyele anayapata kwa bei ya chini kwa kuwa eneo lile lina
wazalishaji wengi, akiyasafirisha
kuyaleta jijini Dar es salaa gharama yake inapanda karibu mara tano gharama hii
ni ile inayoletwa na mfumo wa usambazaji wa bidhaa husika" Amesisitiza
Prof. Mjema.
Amesema uanzishwaji wa Programu hizo
utayaangalia masuala mbalimbali yakiwemo ya ufungaji wa bidhaa husika, maghala
ya kuhifadhia bidhaa hizo, suala la usafirishaji na usimamizi wa bidhaa husika
yakiwemo mazao ya kilimo kuhakikisha kuwa hayaharibiki kabla ya kuwafikia
walaji.
Kuhusu uanzishwaji wa programu ya Biashara
ya Kimataifa amesema kuwa kutokana na uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi,
watanzania wengi sasa wanafanya biashara ya Kimataifa na wengi wao wanakosa
weledi katika kufikia matarajio ya biashara zao.
Amesisitiza CBE imeliona eneo hilo kuwa
linapaswa kutazamwa na kufanyiwa kazi ili Watanzania wanaofanya Biashara ya
kimataifa waweze kupata mafanikio katika
biashara za Kimataifa, kuelewa changamoto za biashara hiyo na vitu
vinavyotakiwa kuzingatiwa ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.
"Uchumi wa Tanzania unakuwa kwa
kasi, tunaanzisha programu hizi ili
kuwawezesha watanzania kujua kwamba katika biashara za Kimataifa kuna
changamoto gani, lazima tuwaandae watanzania kuingia katika uchumi wa dunia
wakiwa na utaalam na uelewa wa kutosha kuhusu mikataba ya kimataifa na biashara
ya kimataifa ili kukidhi haja ya nchi na mahitaji ya kimataifa"
Amesisitiza Prof. Mjema.
Amesema kuwa uanzishwaji wa programu ya
Suppy Chain Management unatumia mtaala wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa
(ITC) ambao pia unakubalika na Shirika
la Kimataifa la Biashara (WTO) kwa kuwa
unatumika kufundishia duniani kote na kuongeza kuwa mtaala huo wameushusha
katika ngazi ya Taifa kwa kuangalia hali halisi ya mazingira na changamoto
zinazoikabili Tanzania katika masuala ya Ugavi.
"Wahitimu wa fani ya Usimamizi wa
Mfumo wa Usambazaji wa bidhaa mbalimbali (Supply Chain Management) watakaopata
vyeti vyetu vya kuhitimu wataweza kufanya mtihani wa ITC utakaowawezesha
kukidhi viwango vya kimataifa na kuwawezesha wahitimu hao kukubalika duniani
kote katika fani hiyo" Amesisitiza Prof. Mjema.
Naye Mshauri Msimamizi kutoka SCM na
Mwakilishi wa Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) Tanzania, Bw. Pamphill
Kiluwa akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa uanzishwaji wa program ya
Biashara ya Kimataifa na ile inayohusika na Ugavi na Usimamizi wa mfumo wa Uzalishaji,
Usambazaji na Utunzaji wa bidhaa kutoka kwa mzalishaji kwenda kwa mlaji
unalenga kuzalisha wataalam wenye weledi wa kutosha .
Amesema kuwa uzalishaji wa wataalam hao
utaweza kukidhi haja ya wateja kulingana na mahitaji yao ndani na nje ya nchi
kwa kukidhi mahitaji yaliyopo katika masuala ya Ununuzi, usafirishaji ,uhifadhi
wa bidhaa na vifaa mbalimbali katika ngazi ya Taifa na Kimataifa.
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa chuo
hicho Dkt. Michael Haule akizungumzia
programu hizo amesema kuwa zitakuwa
mkombozi kwa Watanzania huku akisisitiza kuwa kumekuwa na mapungufu katika
masuala ya Ugavi na Manunuzi hasa upande wa kununua,kupakia na kusafirisha
bidhaa mbalimbali kutoka eneo la uzalishaji hadi kumfikia mlaji wa mwisho na
kusisitiza kuwa uanzishwaji wa programu hizo
Amesema Shahada ya Biashara ya Kimataifa
itawaezesha wahitimu kufanya kazi katika mashirikia na taasisi za kimataifa za
ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa
ufundishaji wa kozi hizo utachukua miezi 18.
Dkt. Haule amebainisha kuwa ufundishaji wa kozi hizo chuoni hapo
utatumia mbinu na Teknolojia ya kisasa
kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa njia ya mtandao huku akibainisha kuwa chuo
hicho sasa kiko katika hatua za mwisho za majadiliano yanayohusisha wadau
mbalimbali kupata ushauri wa kitaalam ili kiweze kuufanyia kazi kuboresha
mitaala hiyo kabla ya kuwasilisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)
kwa ajili ya usajili ili ianze kutumika ikiwa ni hatua ya mwisho.
Aidha, amesema kuwa katika kufanikisha
hatua mbalimbali za mchakato wa kuanzishwa kwa program hizo mpya, wataalam wa CBE
walitembelea mikoa 17 wakihoji waajiri, wanafunzi , wananchi na wadau
mbalimbali maeneo ya uzalishaji ili kupata uhakika wa mahitaji halisi ya soko
la kozi hizo nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment