Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Mhe. Angellah Kairuki akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2016.
Na. Aron Msigwa – Dar es
salaam.
SERIKALI imetangaza utaratibu
mpya utakaofuatwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kuanzia Juni
16 hadi 23, 2016 ambapo imewaagiza Watendaji Wakuu katika Wizara, Idara
zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali kutenga siku moja ya kukutana na
watumishi katika sehemu zao za kazi kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali
zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, imewaagiza
watendaji hao kutenga siku nyingine moja kwa ajili ya kukutana na wananchi, kusikiliza
na kuzitafutia ufumbuzi kero zao zinazohusiana na huduma zinazotolewa na
Taasisi zao.
Akitangaza utaratibu huo
leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeamua kubadili mfumo wa
maadhimisho hayo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi na watumishi wa
umma katika maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa wakati
wa maadhimisho hayo Watendaji hao watatakiwa kukutana wananchi na kusikiliza
kero zinazohusiana na huduma zinazotolewa na taasisi zao pia kukutana na
watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi kusikiliza kwa lengo la kusikiliza
kero zinazowakabili zikiwemo za upandishwaji wa vyeo, madai mbalimbali na
taratibu mbalimbali kuhusu utumishi wa umma.
Amesema kuwa baada ya
maadhimisho hayo kila Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi ya Umma itapaswa
kuandaa taarifa jinsi ilivyotekeleza maagizo yaliyotolewa kwa kuiwasilisha
Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kabla ya Juni 30, 2016.
Ameeleza kuwa Tanzania
inaungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa
Umma Barani Afrika chini ya Kaulimbiu isemayo
Uongozi wa Umma kwa Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.
Mhe. Angellah
amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatajikita katika kuangalia mchango
wa Utumishi wa Umma katika ukuaji wa uchumi Barani Afrika, mchango wa Utumishi
wa Umma katika kuiwezesha Ajenda ya Afrika ya 20163 ambayo inaweka mkazo katika
maendeleo ya Afrika na Haki za Wanawake.
Amesisitiza kuwa malengo
na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa viwanda uliofungamanishwa
na maendeleo ya watu, Tanzania ikiwa imejiwekea malengo ya kupiga hatua katika
ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya viwanda.
Amesema ili kufikia
azma hiyo Serikali kupitia Utumishi wa Umma ina wajibu wa kuwawezesha wananchi
kushiriki katika shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi huku watumishi wa
umma wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi, kutoa huduma kwa
wananchi wote kwa wakati pasipo urasimu wala ukiritimba pia kuepuka vitendo vya
rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Katika hili Watumishi
wa umma lazima wawe na utendaji unaoweza kupimika, ili kulitekeleza hili kuanzia
tarehe 1 Julai tutaanzisha dhana ya mfumo wa utendaji wa taasisi mbalimbali kwa
lengo la kupima utendaji wa taasisi kulingana na matokeo tunayoyapata”
Amesisitiza.
Ameongeza kuwa
watumishi wa umma Serikalini wanatakiwa kuwa na utendaji unaojali matokeo,
kuepuka vitendo vya wizi, ufisadi na udanganyifu vinavyosababisha upotevu wa
fedha za Serikali.
Akizungumza kuhusu
Haki za Wanawake katika utumishi wa umma amesema kuwa Serikali itaendelea
kuhakikisha kuwa kuna uwiano wa jinsia katika
nafasi na fursa mbalimbali katika ajira , Uteuzi wa nafasi za uongozi , mafunzo
kazini na upandishwaji vyeo.
UFAFANUZI
KUHUSU WATUMISHI HEWA.
Kuhusu suala la kuwaondoa
Watumishi hewa katika orodha ya malipo ya Serikali Mhe. Angellah amefafanua kuwa tayari Ofisi
yake imekwishatoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi zote za Umma pamoja
na Mamlaka za Serikali za Mitaa yanayowataka kuwasilisha taarifa ya mwisho ya watumishi
hewa ifikapo Juni 15, 2016.
Amesema taarifa itakayowasilishwa
itatakiwa kubainisha majina , namba za utambulisho wa watumishi hewa/ cheki
namba, tarehe waliyotakiwa kuondolewa kwenye mfumo wa malipo na kiasi
kilichopotea na kile kilichookolewa ikiwa
imesainiwa na Mkuu wa Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi husika.
Ameeleza kuwa mara
baada ya kuzipokea taarifa hizo Serikali itazifanyia tathmini ili kupata
uhakika wa zoezi zima la kuondoa watumishi hao kuanzia kuanzia tarehe 15 Machi
2016.
“Kama mmekuwa
mkifuatilia taarifa mbalimbali Serikali tumekuwa tukilishughulikia kwa nguvu
suala hili la watumishi hewa kuanzia mwezi Machi mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli alipotoa maagizo ya kuwaondoa watumishi hewa katika orodha
ya malipo ya Serikali” Ameeleza.
Aidha, amebainisha
kuwa kuwa kuanzia Machi, 1, 2016 hadi Mei 30, 2016 watumishi 12,246
wameondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali zikiwemo
za kutimiza umri wa kustaafu kwa lazima au kufukuzwa kazi ,vifo,kuhitimishwa
kwa mikataba na ugonjwa.
Jumla ya shilingi
25,091,292,688.82 zingepotea kama watumishi hao wasingeondolewa kwenye mfumo wa
malipo ikilinganishwa na watumishi 10,295 walioondolewa kwenye mfumo hadi
Aprili 30, 201 huku kiasi kilichookolewa kikifikia shilingi 23,206,547,598.82 likiwa
ni ongezeko la watumishi 1,951 na shilingi 1,884,745,090.
No comments:
Post a Comment