Gari la Kampuni ya Wengert Windrose Safaris likiwa limeshikiliwa kituo cha polisi mkoani Arusha baada ya kukutwa na shehena ya bangi. |
Na Mwandishi Wetu
BIASHARA ya utalii imekuwa na ushindani mkubwa si nje bali hata ndani ya nchi yetu. Ushindani wa kibiashara unadhihirishwa na jinsi ambavyo makampuni ya ndani na nje yanavyopigana vikumbo kutafuta njia na mbinu za kuwapiku washindani wao.
Hilo ni jambo la kawaida kabisa.
Hakika pale ambako hapana ushindani basi ni wazi pia kwamba hapatakuwapo na tija kwani mama wa biashara huria ni ushindani na hilo hakuna wa kubishana. Hata hivyo, kuna mvutano ambao umeanzishwa na kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited, kampuni tanzu ya Friedkin Conservation Fund (Friedkin Family Tanzania) dhidi ya serikali ya Tanzania ambao hauna tija kwa pande zote mbili na ambao unahitaji kumalizwa kwa sababu umeendelea kuikosesha nchi mapato.
Kampuni nyingine ni Tanzania Game Trackers Safaris Limited na Mwiba Holdings Limited.
Kampuni hiyo imeingia katika mvutano na serikali kuanzia mwaka 2013 wakati msimu mpya wa uwindaji wa kitalii ulipoanza, hasa pale walipokosa moja ya vitalu walivyoomba katika utaratibu wa ushindani. Kitalu hicho kilijulikana kwa jina la Lake Natron Game Controlled Area (North). Baadaye kitalu hiki kilikuja kujulikana kama Lake Natron Game Controlled Area (East), ambacho kiligawiwa kwa Green Mile Safari Company Limited baada ya ushindani.
Kitalu hiki cha uwindaji wa kitalii ndicho kimekuwa luba na kufanya mahusiano kati ya kampuni hiyo na serikali kuyumba sana hadi leo takriban miaka mitatu baada ya kampuni hiyo kukosa umiliki katika mchakato wa ushindani. Katika mazingira ya kawaida kampuni ya kigeni inayofanya biashara hapa nchini kwa kutumia sheria za Tanzania haina budi kukubaliana na sheria, na kama kuna kutoridhika na chochote inatakiwa kwenda mahakamani kutafuta haki.
Hata hivyo, baada ya kampuni hiyo kwenda mahakamani mara kadhaa kutafuta haki ya kumilikishwa kitalu hicho ikashindwa kuipata imeamua kuendeleza vita dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyombo vya habari. Tena vita hiyo ambayo inaendeshwa kwa kutumia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi ilihamishiwa hadi katika Baraza la Congress la Marekani.
Shehena ya bangi ikishushwa kwenye gari la Kampuni ya Wengert Windrose Safaris katika kituo cha polisi mkoani Arusha baada ya kukamatwa. |
Kampuni ya Wengert ikafikia hatua ya kuliaminisha Baraza hilo kwamba imetendewa ndivyo sivyo nchini kwa kunyang'anywa kitalu kinyume cha sheria na kwamba kitendo hicho kimefanyika kinyume cha sheria.
Katika kulighadhibisha Baraza hilo Wengert wakadai kwamba imenyang'anywa kitalu na kupewa kampuni nyingine ya kigeni. Hiyo ya kudai kwamba imenyang'anywa kampuni ya Kimarekani na kupatiwa kampuni nyingine ya kigeni ni katika ile ile tabia ya kutaka kuwachochea watunga sheria hao wa Marekani kwa kutumia kigezo cha kwamba wao ni bora zaidi hivyo haiyumkiniki akanyang'anywa Mmarekani halafu apewe mgeni mwingine!
Uchochezi huo ukatumika kwa malengo ambayo kampuni ya Wengert ilitaka.
Baraza la Congress la Marekani lilimwandikia Rais wa Marekani, Barack Obama, barua likiituhumu Idara ya Wanyamapori kwa kuinyanga’anya kampuni ya Wengert kitalu na kukitoa isivyo halali kwa Kampuni nyingine, jambo ambalo halikuwa kweli. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kampuni iliyogawiwa kitalu hicho ni ya Kitanzania.
Kampuni hiyo haikutaka kusema ukweli kwamba uamuzi wa kutogawiwa kitalu ulitokana na maamuzi ya kamati ya ugawaji wa vitalu na kamwe sio kutokana na uamuzi wa Idara ya Wanyamapori.
Vitalu hugawiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii baada ya kushauriwa na kamati ya ugawaji wa vitalu. Tuhuma hizo za uongo zilipelekwa mbele ya Baraza la Congress baada ya rufaa yao waliyokata kupinga ugawaji wa vitalu kukataliwa. Ni wazi kabisa kwamba ushawishi uliofanywa kwa Baraza la Congress kwa kutumia mbinu chafu na uongo uliokithiri ulilenga katika kuiweka katika shinikizo serikali ya Tanzania ili iende kinyume na maamuzi yake halali yaliyofanayika kwa mujibu wa sheria.
Wengert walikwenda mahakamani mara kadhaa kupinga maamuzi hayo ya serikali na mara zote wamegonga ukuta. Wiki iliyopita walishindwa kwa mara ya nne mahakamani katika jitihada zao za kutaka kuthibitisha kwa kutumia vielelezo wanavyodai ndivyo halali kwamba kuna makosa katika ugawaji wa vitalu katika eneo la Lake Natron Game Controlled Area. Imefikia hatua kampuni ya Wengert inadai kwamba nyaraka rasmi za Serikali ya Tanzania ni batili na kwamba yenyewe ndiyo ina ramani halali na nyaraka mbalimbali kutoka serikalini.
Inachekesha sana kwamba kampuni ya kigeni inakuja nchini na kuamua kupambana na serikali yetu kwa ajili ya kulazimisha umiliki wa kitalu cha uwindaji wa kitalii kwa kila njia ikiwa ni pamoja na kuvifunga midomo vyombo vya habari kwa kutumia mbinu chafu. Kwa taarifa rasmi za kiserikali ni kwamba kampuni hiyo, pamoja na kampuni nyingine za Friedkin Family Tanzania, zimekuwa zikiwatumia watumishi wake na mawakala mbalimbali kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya makampuni mengine ya uwindaji wa kitalii.
Aidha, kampuni hiyo pia imekuwa ikiendesha kampeni chafu dhidi ya viongozi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kutaka kuthibitisha kwamba viongozi hao wanafanya maamuzi yasiyozingatia sheria. Ukweli ni kwamba kampuni hizo ndiyo zimekuwa mstari wa mbele kutotii sheria za nchi.
Tabia hii ilishamiri sana wakati wa awamu iliyopita. Kumekuwapo na jitihada za kuitaka kampuni hiyo iendelee kufanya shughuli zake za kitalii katika maeneo halali iliyokabidhiwa na serikali ya Tanzania lakini kila uchao kumekuwapo na tuhuma za kila aina dhidi ya wadau wengine wa sekta ya utalii na serikali kutoka kwa kampuni hizo.
Mtuhumiwa ambaye ni dereva wa gari hiyo akiwa ameshikiliwa na polisi. |
Aidha, katika kuthibitisha uwezo wake wa kufanya mambo ya hovyo upo ushahidi kwamba watumishi au mawakala wa kampuni hiyo walichimba mashimo katika kiwanja kidogo cha ndege kilichopo kwenye moja ya vitalu vya washindani wao eti tu kwa sababu uwanja huo waliutengeneza wao wakati wanamiliki kitalu hicho.
Swali kubwa linalojitokeza katika vurugu hizi za makampuni haya ya Kimarekani ni kwamba nani anayewachochea na kuwavimbisha kichwa kiasi cha kuidhalilisha serikali ya Tanzania huku wakiwa nchini? Kwa nini hadi leo hatusikii hatua za kinidhamu na hata kisheria dhidi ya kampuni hizii ambayo inaonekana kila uchao yanazidisha mapambano dhidi ya serikali yetu? Tusiruhusu mwekezaji yeyote yule kutupanda kichwani, hata kama anatoka taifa linalojigamba kuwa taifa kubwa duniani! Tunachohitaji kwa wawekezaji ni wao wanufaike na sisi pia tunufaike.
No comments:
Post a Comment