Servacius Likwelile, Katibu Mkuu Hazina
Na
Benny Mwaipaja, WFM
KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa
Tanzania imejipanga kuimarisha mapato yake ya ndani ili kutekeleza kikamilifu
Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.
Dkt.
Likwelile, amesema hayo Mjini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku 2
unaowahusisha wataalamu wa Uchumi na Mipango wapatao 170 kutoka nchi nzima.Amesema
kuwa misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo imekuwa ikipungua kila wakati, hatua
ambayo imeifanya Serikali kuendelea kujipanga kukabiliana na nakisi ya Bajeti
yake ili kukuza maendeleo.
"Mikopo
yenye riba nafuu nayo imepungua, sasa hivi unaenda kukopa kibiashara, kwa uchumi
wetu huu hatuwezi kumudu" alisisitiza Dkt. Likwelile
Ameeleza
kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuimarisha miundombinu ya
barabara, reli, bandari na mambo mengine, hali inayohitaji fedha nyingi ambazo
zitapatika kwa kukusanya kodi mbalimbali.
Amewataka
wataalamu hao wa uchumi na mipango kujadili na kuibuka na mipango itakayosaidia
kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo wa Pili wa Maendeleo wa Taifa unaotarajiwa
kugharimu shilingi Trilioni 107.
Akifungua
mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wataalamu hao kutoa
mapendekezo ya kitaalamu wakizingatia changamoto mbalimbali zikiwemo za kupanda
kwa gharama za mafuta duniani.
Vilevile,
amewakumbusha umuhimu wa kutumia takwimu sahihi wakati wa kupanga namna bora ya
kutekeleza mpango huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na watanazania kuwaletea
maendeleo ya haraka
"Takwimu
ndizo zinazotoa picha halisi ya matatizo yanayowakabili watanzania ukiwemo
umasikini, ambapo zikitumika vizuri zitasaidia kupanga namna bora ya wananchi
wanavyoweza kuondokana na umasikini huo" Alisisitiza Dkt. Mwakyembe
Kwa
upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri, amesema
kuwa Tanzania imedhamiria kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo
mwaka 2025.
Amesema
kuwa hatua hiyo itafikiwa kwa kuelekeza nguvu kubwa katika uanzishwaji na
uendelezaji wa viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwanri
amesema kuwa hatua hiyo itakuza uchumi wa nchi kwa kuongeza kipato cha wananchi
pamoja na ajira na akasisitiza umuhimu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii na
kujitolea utaalamu na nguvu zao zote kufanikisha malengo hayo.
No comments:
Post a Comment