Rais John Magufuli
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
TAREHE 23/06/2016
UTAFITI
MIEZI
8 TOKA MHE RAIS JOHN MAGUFULI AMECHAGULIWA KUWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu waandishi wa habari habari za leo na pole
kwa majukumu mazito ya ujenzi wa Taifa. Taarifa yetu itajikita katika maeneo
makuu mawili, Mkutano Mkuu wa CCM na UTAFITI wa Miezi 8 ya Mhe Rais John
Magufuli.
Taasisi ya CZI ni taasisi huru isiyo ya kiserikali
ambayo inajihusisha na ushauri wa mambo ya HABARI na kijamii, pamoja na tafiti
mbalimbali. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, tulizunguka nchi nzima
na kuuliza wananchi maswali ya papo kwa papo, ama kwa njia ya simu ama kwa
kuhoji kimakundi kulingana na umri wa wahusika.
Tulihoji Watanzania 2,3oo wa kada mbalimbali katika
maeneo kadha wa kadha tuliyotembelea kuanzia umri wa miaka 14 hadi 18 na
kuanzia wenye umri wa miaka 18 hadi 30 na kuanzia miaka 30 hadi 60.
KUNDI
LA 1 UMRI MIAKA 14-18
Kundi hili baada ya kuhojiwa wanaamini Rais John Magufuli
ataleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, na atarejesha nidhamu ya masomo shuleni
kuanzia shule za awali, msingi nasekondari kwa vijana wenye umri kuanzia miaka
7 hadi 18.
Asilimia 78 ya vijana hao kwenye ngazi ya elimu ya
msingi na sekondari wanaamini Mhe Rais Magufuli atasaidia kuleta mageuzi kwenye
elimu ikiwa ni pamoja na kuondoa tatizo la madawati, mitaala na nidhamu ya
walimu, huku asilimia 22 ya vijana hao wakisema Mhe Rais huenda asifanikiwe
kwenye harakati zake za mageuzi kwenye sekta ya elimu. Pia kundi hili linaamini
kuondolewa kwa michezo shuleni kutazidi kudidimiza maendeleo ya michezo nchini.
KUNDI
LA II UMRI MIAKA 18-30.
Watanzania kuanzia miaka 18-30, asilimia 82
wanaamini serikali ya Rais Magufuli italeta mageuzi kwenye elimu hususan kwenye
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na kumaliza tatizo la mabweni ya
kulala wanafunzi wa vyuo vikuu. Pia kada hiyo inaamini rais anaweza kupunguza
tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na vijana nchini Tanzania. Sababu
kuu ambayo inawafanya waseme hayo inatokana na kupambana na wafanyakazi hewa
katika taasisi za serikali ambazo zimekuwa zikichangia kukosekana kwa ajira kwa
vijana. Lakini sababu nyingine ya kuongezeka kwa ajira ni msimamo wa serikali
wa kufufua na kuanzisha viwanda vipya, hasa vya mazao ya kilimo ili kuongeza
mnyororo wa thamani kwa mazao ya kilimo.
Aidha asilimia 18 ya kada hii haiamini kama
serikali ya awamu ya tano italeta mageuzi yoyote nchini na wanasema ni kawaida
ya serikali kuwapa matumaini wananchi wake lakini mwishoni mambo hubaki
vilevile kama awamu zilizopita.
KUNDI
LA III UMRI MIAKA 30-60
Watanzania wenye umri wa miaka 30-60 waliohojiwa
wanasema kuna uwezekano watumishi wa umma wakarejesha imani kwa serikali
kutokana na juhudi za Mhe. Rais anavyopambana na ufisadi na rushwa kwa dhati.
Aidha kada hii asilimia 89.0 wanaamini Mhe Rais
atamaliza matatizo ya wazee kwa kuanza kuwalipa posho kwa mwezi lakini pia
wanaamini nidhamu ya watumishi itaongezeka miongoni mwa watumishi wa umma
pamoja na binafsi kutokana na namna serikali inavyopambana na watumishi hewa na
utumbuaji majipu unaoendelea kwenye serikali ya awamu ya tano.
Aidha kada hii inaamini umoja na mshikamano wa Watanzania
utaendelea kuimarika na moyo wa kusaidiana kwa wananchi wa Tanzania utadumu na
kuimarika pia.
Vile vile kada hii inasema Rais Magufuli anazidi
kuwa maarufu huku wapinzani wakionekana kupoteza umaarufu kutokana na kushindwa
kubuni mbinu mpya ya mapambano ya kisiasa.
Asilimia 11 ya kada hii inaamini serikali ya awamu
ya tano haitaleta mageuzi yoyote kwa wazee na nidhamu kwa watumishi wa
umma haitabadilika kutokana na aina ya
viongozi wanaowasimamia watumishi hao ambao wengi wao siyo waadilifu na siyo
watendaji na wafuatiliaji wa mambo kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa ujumla wake mhe rais anakubalika kwa asilimia
89% huku akiwa amewapiku Edward Lowasa na Mhe Jakaya KIkwete ambao wao
wamegawana zilizobaki. Jakaya Kikwete akiwa na asilimia 7% huku Edward Lowasa
akiwa na asilimia 4%.
Mikoa ambayo tulikwenda ni Dodoma, Mara, Geita, Ruvuma,
Arusha, Manyara, Kusini Pemba, Wete Pemba, Kaskazini Unguja, Tabora, Kigoma, Pwani,
Morogoro, Simiyu, na Tanga, na kuhoji wananchi takriban 2,300.
MAFANIKIO YA
MIEZI NANE (8) YA UTAWALA WA RAIS DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI
Mara
tu baada ya kutangazwa mshindi hata kabla ya kuapishwa Novemba 5, 2015 watu
wengi walibeza kama angeweza kutekeleza yale aliyoyasema. Wapo waliosema kwamba
asingeweza kupambana na rushwa na ufisadi kwa sababu mfumo huo umeanzia ndani
ya CCM. Walizungumzia kuhusu suala la kufumua mfumo wa uendeshaji wa Serikali,
kuijenga upya CCM, pamoja na namna ya kushirikiana na upinzani. Wengine
wakahoji muundo wa baraza la mawaziri utakavyokuwa hasa kwa vile lililopita
lilikuwa kubwa mno.
Hata
hivyo, katika kipindi cha miezi nane tu, amefanya mambo makubwa mengi kana
kwamba amekuwepo madarakani kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa hata ahadi zake
nyingi amekwishazitekeleza na nyingine anaendelea kuzitekeleza. Tutajaribu
kukumbusha machache kati ya mengi aliyoyafanya katika kipindi hicho.
Alielekeza Shs. 225 milioni
zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya pongezi za Wabunge Dodoma
kutumika kununua vitanda vya hospitali ya Muhimbili na Shs. 15 milioni tu ndio
zitumike kwa ajili ya sherehe hiyo.
1.
MPANGO
MAHUSUSI WA KURUDISHA NIDHAMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA (UTUMBUAJI MAJIPU)
Kurudisha nidhamu kwa
watumishi wa umma ilikuwa moja ya agenda zake na ahadi aliyoirudia Zaidi ya
mara 100 wakati wa kampeni zake na hata sasa bado anaendelea kusema. Watanzania
wamekuwa na kilio cha muda mrefu kwamba wamekuwa wakishindwa kupatiwa huduma
muhimu na watendaji wa serikali, ambao wengi wao hawatekelezi wajibu wao
ipasavyo.
Itakumbukwa kwamba, hata kabla hajaunda Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli alifanya mambo
makubwa kadhaa ambayo hayakutegemewa. Kwanza alifanya ziara mbili kubwa za
kushtukiza ambapo Novemba 6, 2015 ikiwa ni siku moja tu baada ya kuapishwa
alitembea kwa miguu kutoka Ikulu hadi Wizara ya Fedha ambako alipita katika
ofisi moja baada ya nyingine na baadaye alifanya kikao na watendaji. Novemba 9
alifanya ziara nyingine ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
ambako alivunja Bodi ya Wakurugenzi, alimwondoa Kaimu Mkurugenzi wa hospitali
hiyo, Dk. Hussein Kidanto na kuamuru mashine muhimu za vipimo za CT-Scan na MRI
kutengenezwa haraka huku akitoa sehemu ya mshahara wake kumlipia mgonjwa mmoja
aliyekuwa anahitaji kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.
Ni katika kipindi hicho
ambapo Serikali, katika zile zile ziara za kushtukiza zilizofanywa na Rais
mwenyewe na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Watanzania walishuhudia vigogo wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakiswekwa ndani, kusimamishwa, kutenguliwa teuzi zao na wengine kufikishwa
mahakamani kwa makossa mbalimbali, yakiwemo uzembe, rushwa na ufisadi na matumizi
mabaya ya madaraka. Tumeona watendaji wa mamlaka nyingi za umma wakiendelea
kusimamishwa/kufukuzwa kazi kama Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, UHAMIAJI
na TRL. Hii imerudisha nidhamu kwa watumishi wa UMMA na kuleta ufanisi katika
utoaji wa huduma kwa wananchi.
2.
MPANGO
WA KUBANA MATUMIZI
Itakumbukwa kwamba, Rais
Magufuli alipunguza kupunguza sherehe na dhifa za kitaifa na Jumatatu ya Novemba 23, 2015, alitangaza kufutwa kwa Sherehe
za Uhuru Desemba 9 na kuagiza fedha za maandalizi ya sikukuu hiyo zitumike
kutatua matatizo mengine, ikiwemo kufanya upanuzi wa Barabara ya Morocco-Mwenge
huku akiagiza siku hiyo itumike kusafisha mazingira ili kupunguza matatizo ya
kipindupindu nchini. Alifuta sherehe za Muungano na kuelekeza kwamba fedha hizo
zitumike kupanua barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege jijini Mwanza hadi mjini.
Aliagiza pia taasisi hizo zifanye vikao vyao katika kumbi maalum za idara zao
badala ya kwenda mikoani ama kukodi kumbi za hoteli huku watu akijilipa posho
nyingi wakati vikao hivyo ni vya kiutendaji tu.
Tumeshuhudia katika uteuzi
wa viongozi wa serikali ya Awamu ya 5, Mh. Rais amezuia shamlashamla za
kupongezana viongozi wa serikali wanapoteuliwa na kufanya uteuzi wa serikali ya
awamu ya Tano kutumia bajeti ndogo katika siku hizo za uteuzi. Mfano, uteuzi wa
Wakuu wa wilaya, Mawaziri na wakuu wa Mikoa hakukuwa na shamlashamla kama
ilivyozoeleka katika awamu zilizopita.
Hili limesaidia kuokoa
fedha nyingi ambazo zimekwenda kufanya shughuli za maendeleo ya wananchi. Wale waliodhani kwamba utendaji wa Dk. Magufuli ni mfumo wa kujilundikia
majukumu bila utekelezaji (Slack Management Style) walikosea sana, kwa sababu
tangu wakati ule tumeshuhudia watendaji wengi wazembe, wala rushwa na mafisadi
wakiwajibishwa huku wengine wakifikishwa mahakamani.
3.
WATUMISHI
HEWA
Suala la kuwepo kwa
watumishi hewa, ambalo lilikuwa linalalamikiwa kwa muda mrefu, safari hii Rais
Magufuli alilitumbua ambapo tulishuhudia kwamba kumbe kulikuwa na watumishi
hewa zaidi ya 12,000 waliokuwa wanalipwa mabilioni ya fedha ambazo ziliingia
kwa maofisa wajanja. Kuonyesha kwamba hakuwa na mzaha hata kidogo, alimfuta
kazi mara moja Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga baada ya kugundua kwamba alimdanganya
kwamba mkoa wake haukuwa na mtumishi hewa hata mmoja wakati haikuwa hivyo.
Mabilioni mengi ya fedha yameokolewa kutokana na zoezi hilo katika Serikali za
Mitaa.
4.
SAFARI
ZA NJE KWA WATUMISHI WA UMMA NA VIONGOZI WA KISERIKALI
Rais Magufuli alianza mara
moja kwa kutangaza kufuta safari zote za nje za mafunzo na ziara kwa maofisa na
watendaji wa Serikali katika harakati za kubana matumizi huku akibainisha
kwamba, safari hizo zililigharimu Taifa mabilioni ya fedha wakati nyingi
hazikuwa na tija. Akasema yeyote ambaye alitaka kusafiri ilikuwa lazima apate
kibali maalum kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au kwake yeye. Siyo siri kwamba
hili limeondoa zile ‘safari za kufanya shopping’ ambazo maofisa wengi wa
serikali walizitumia kutafuna fedha za umma na kuitia doa Serikali ya CCM.
Uamuzi wa Mh. Rais
kurudisha utaratibu wa vibali vya kwenda nje, umeokoa pesa nyingi sana ambazo
zilikuwa zinatumika na viongozi mbalimbali wa serikali kusafiri kwenda nchi za
nje safari ambazo zilikuwa hazina tija kwa taifa. Kwa kulitekeleza hili hata
yeye mwenyewe katika kipindi cha miezi 8 ya utawala amesafiri mara 2 tu, kwenda
Rwanda na Uganda. Huu ni mfano ambao unatakiwa kuigwa na kuungwa mkono na
watanzania wote walio na dhamana katika sekata ya umma.
5.
ELIMU
BURE (CHEKECHEA MPAKA KIDATO CHA NNE)
Katika kufuata Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, ameweza kupeleka TShs bilioni 18 kwa ajili ya
kutekeleza mpango huo wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari. Hivi sasa
tunashuhudia idadi kubwa ya udahili wa wanafunzi wa shule za msingi na kuongeza
idadi kubwa ya uhitaji wa madawati hasa kwa shule za msingi. Wazazi wengi
wameitikia na kuamua kupeleka watoto wao shuleni haya ni matokeo ya Utekelezaji
wa Sera ya Elimu bure katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
6.
PUNGUZO
LA KODI KWA WAFANYAKAZI (PAYE) UKUSANYAJI WA MAPATO
Serikali makini hukusanya
kodi! Rais Magufuli katika kipindi kifupi tu ameweza kusimamia vyema ukusanyaji
wa kodi akianza kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wakwepaji
sugu. Lakini pia Serikali imeweza kupunguza kiasi cha kodi ya PAYE kwa 2%
katika mishahara ya wafanyakazi kila mwezi na kuondoa makali ya kodi kwa
wafanyakazi wake.
7.
VITA
DHIDI YA MAFISADI
Mh. Rais pia ameweza
kuanzisha mahakama ya mafisadi kwa lengo la kupambana na mafisadi ambao
wamelifikisha taifa la Tanzania kwa wizi mkubwa wa mali za umma pamoja na
matumizi mabaya ya fedha za serikali. Hili alilisema katika kampeni na
amelitekeleza kwa asilimia 80 akionyesha dhamira yake ya kushughukia watu wa
namna hiyo.
Katika sherehe za kuanza
mwaka wa kimahakama Mh. Rais aliweza kuahidi na kutoa jumla ya Tshs Bilion 12
ili kuharakisha utendaji wa mahakama jambo ambalo halijawahi kufanyika na kila
mwaka awamu zilizopita bajeti haitoshelezi kwa muhimili huu. Fedha hizo
zilikabidhiwa kwa Idara hiyo mwezi Februari 2016.
Ajabu ni kwamba, kasi ya kuwawajibisha watumishi wa umma ikaanza kupingwa
na baadhi ya wapinzani, hususan wale ambao walikuwa wanaahidi kwenye kamepni
zao kwamba wangeweza kupambana na ufisadi! Siyo siri kwamba, tayari kasi yake
hiyo ilikuwa imewapoteza wapinzani hata kabla hajaunda baraza la mawaziri –
wakati huo akiwa na wasaidizi watatu tu – Katibu Mkuu Kiongozi, Makamu wa Rais
na Waziri Mkuu!
8.
UJENZI
WA MABWENI KWA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Mh. Rais amehaidi kujenga
mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam jambo ambalo
lilipigiwa kelele sana na wanafunzi katika awamu zilizopita lakini leo
litafanyika kupitia Mh. Rais wa awamu ya Tano kama alivyo ahidi.
Yako mengi sana
aliyoyatekeleza ambayo hayawezi kutosha hapa, lakini Rais Magufuli, ambaye
kimsingi ameisongesha mbele Tanzania katika kipindi kifupi, anaweza kufanya
mambo makubwa zaidi hasa atakapokabidhiwa uenyekiti wa taifa wa CCM, chama
tawala na kikongwe kabisa barani Afrika, kwa sababu huko nako ataondoa mfumo
mbovu wa uongozi unaokifanya chama hicho kilalamikiwe na kiwe agenda kuu ya
wapinzani kila mara.
Wale wanaobeza utendaji
wake wanapaswa kukaa kimya, kwani Wananchi waliomweka madarakani ndio
watakaompima na kumhukumu, kwa sababu hakuna aliyetegemea kama serikali hii
ingeweza kuondoa Service Charge kwenye umeme wa majumbani ambapo wananchi
walikuwa wanaumizwa sana na hili jambo.
Mwenye nia njema na
maendeleo ya taifa hili, anapaswa kuiunga mkono kwa dhati kabisa serikali ya
Dk. Magufuli kwa utendaji huu na siyo kumhujumu, kumbeza ama kutoka visingizio
vyovyote vile.
KUELEKEA MKUTANO MKUU
WA CCM TAIFA JULAI 23 MWAKA HUU.
Ndugu zangu Watanzania, wakati wanachama wa CCM
wakijiandaa na Mkutano Mkuu wa chama hicho kikiwa na ajenda moja tu kumkabidhi
Rais John Magufuli uenyekiti wa CCM, wanachama wa chama hicho wanapaswa
kutambua mambo kadhaa ambayo yanampa umuhimu wa kipekee Rais Magufuli kupewa
nafasi hiyo na wajumbe wa mkutano mkuu, pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Chama cha Mapinduzi kina rasilimali nyingi:
1. Rasilimali watu
2. Rasilimali Ardhi, Majengo na Viwanja
3. Wananzuoni wa kila taaluma
4. Wafanyabiashara ndogondogo (machinga)
5. Wafanyabiashara wa kati na wakubwa
6. Wanachama wake wanaozidi milioni 9
7. Mashabiki wake wanaozidi milioni 28.9
8. Wakulima
9. Wavuvi
10. Wafugaji nk.
Lakini pamoja na utajiri huo, bado chama hicho
hakiwezi kujiendesha na wanategemea Ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, pamoja na wafadhili ambao wengine siyo wasafi kwenye rekodi za kodi.
Ndugu waandishi wa habari, baada ya kutafakari kwa
kina tumegundua kwamba, Mhe Rais Magufuli anazo agenda nzuri za kukiendeleza
chama hicho kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo pindi atakapopewa chama hicho.
Agenda hizo ni:
Mosi:
Kuhakikisha chama kinajitegemea kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo
itakifanya kijiendeshe chenyewe bila kutegemea wafadhili.
Pili:
Miradi ambayo ipo tayari ijulikane na iwekwe wazi na iwanufaishe wanachama na
wananchi kwa ujumla.
Tatu:
Kuongeza wanachama zaidi wa chama hicho.
Nne:
Kuwa na wanachama wanaokipenda chama hicho na wenye uzalendo na chama hicho na
nchi yao.
Ndugu waandishi wa habari, kwa mtazamo huo
tunawaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu
waone umuhimu wa kumpa Mhe Rais Magufuli kura za kutosha ili awe mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi.
Aidha, kuna taarifa za baadhi wa wanaCCM wachache
ambao wamekuwa wanazunguka mikoani na wilayani wakieneza taarifa za uongo
kwamba Rais Magufuli mwenyewe ndiye hataki kuwa mwenyekiti wa chama.
Ndugu wananchi na waandishi wa habari, tunawaonya
hao wanaoeneza uongo huo waache mara moja kwa kuwa uongo na uzushi huo haulengi
kukijenga chama na watu hao huenda wakajikuta kwenye wakati mgumu kama
wataendelea kuzusha na kueneza uongo huo.
Tunawaomba Watanzania wazidi kumuombea rais wetu
kwa kuwa anaonyesha nia ya dhati kuhakikisha nchi inapata maendeleo, kwani hata
wakati aliposhiriki jubilee ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania alisikika
akiwataka benki kuu kuhakikisha wanalinda thamani ya shilingi pamoja na kushusha
mfumko wa bei.
Kama mnavyojua, moja ya matatizo makubwa kwa
watanzania hasa wa kipato cha chini ni mfumko wa bei ambao umekuwa unawatesa
kila mwaka bila serikali kutafuta njia mbadala za kupunguza mfumko huo, lakini
rais wa awamu ya tano Mhe Magufuli na serikali yake wanapambana kuondoa kero
hiyo kubwa kwa Watanzania.
Tudumishe umoja, mshikamano na Amani. Mungu
Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeandaliwa
na:
David
Saire Manoti-Mwanasiasa Kijana
Raphael
Nyang’i Awino- Mwanasiasa kijana
Cyprian
Musiba Nyamagambile- Mwandishi/Mtafiti
Dotto
omary Nyirenda - Mwanadiplomasia kijana
Daniel Mahelela - Mtafiti
Juma
George Chikawe-Mwanasheria
No comments:
Post a Comment