Kwanza lazima niseme tu mwaka 1989 ulikuwa mgumu kwa timu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na hata kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) na hata ile ya Tanzania Bara, ambayo ilishiriki kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.
Matokeo ya ajabu zaidi yalikuwa klabu ya Simba, ambayo ilijikuta ikinusurika kuteremka daraja mwaka huo, lakini kikubwa zaidi ni kule kushangazwa na ubora wa timu ya wajenzi ya MECCO kutoka Mbeya, ambayo mwaka huo ilikuwa imepanda daraja la kwanza.
MECCO, ambayo ilikuwa inaundwa na wachezaji kama Epharaim Kayeta, Nassib Abbas, Betwell Africa, Abeid Kasabalala, Rashid Mandanje, Danford Ngesi, Charles Makwaza na wengineo, ilifanikiwa kuwabana mbavu Simba chini ya kocha Mohammed Hussein Hassan 'Msomali' ikiwa na wachezaji Moses Mkamdawire, Juma Shamte (alitokea Tukuyu), Omari Hussein 'Kakakuona' (alitokea Maji Maji), Dan Muhoja, Michael Kidilu, John Mkelele, Edward Chumila, Raphael Paul, Ramadhani Lenny, Adam Selemani (alitokea Reli), Malota Soma, Adolf Kondo, Sunday Juma, Aston Pardon, Twaha Hamidu, Iddi Selemani (alitokea Sifa United ya Manzese), Abubakar Kombo, Augustine Haule, Rashid Salum 'Killer' (alitokea Ndovu SC), Niva Mtawa, Suleiman Mathew Luwongo (alitokea kwa watani wao Yanga), Clement Kazamala, Daniel Manembe, Juma Limonga (alitokea Reli) na Ally Machella (kutoa Temeke Rangers).
Mechi ya kwanza baina ya Simba na MECCO ilifanyika jijini Dar es Salaam Februari 25, 1989 ambapo Simba ilibanwa mbavu na kuambulia suluhu mbele ya vijana hao waliokuwa wakitandaza boli kwa kiwango kikubwa.
Walau Simba ilikuwa imefuta aibu ya vigogo kuumbuliwa na timu hiyo, kwani tayari MECCO, katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo iliyoanza Desemba 31, 1988, ilikuwa imeichapa Yanga bao 1-0 ambalo lilipachikwa wavuni na Ephraem Kayeta kwenye Uwanja wa Sokoine.
Hata hivyo, Simba haikujua kwamba vijana hao walikuwa imara, na walipokutana katika mechi ya marudiano Juni 24, 1989, wakachezea kichapo cha mabao 3-2! Haya yalikuwa maajabu ya mwaka na ndiyo matokeo yaliyozidi kulididimiza jahazi la Simba mpaka ikanusurika kuteremka daraja. Zilizoshuka mwaka huo ni RTC Kigoma na Kurugenzi Dodoma.
Wenzao Yanga walifanikiwa kulipa kisasi kwa MECCO baada ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Taifa Julai 26, 1989.
Msimamo kamili wa ligi hiyo hadi kufikia mwisho ulikuwa hivi:
P W D L GF GA Pts
Yanga 26 14 8 4 26 12 36
Pamba 26 14 7 5 25 15 35
Pilsner 26 9 15 2 23 13 33
Maji Maji 26 8 13 5 28 27 29
Ushirika 26 8 11 7 24 22 27
Ndovu 26 7 12 7 23 18 26
Sigara 26 7 12 7 20 25 26
Coastal 26 8 9 9 26 27 25
MECCO 26 6 12 8 23 26 24
African Sports 26 6 11 9 25 25 23
Nyota Nyekundu 26 5 13 8 20 22 23
Simba 26 5 11 10 22 27 21
--------------------------------------------------------------------------
RTC Kigoma 26 6 6 14 22 30 18
Kurugenzi Dom 26 4 10 12 18 34 18
No comments:
Post a Comment