Peter Tino (kulia) akiwa na Kitwana Manara.
MATUMAINI ya Zambia kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika Lagos, Nigeria, mwaka 1980 yalipata kipigo kikubwa siku ya Jumapili, Novemba 11, 1979 wakati timu yao ya taifa, KK XI wakati huo, ilipotoka sare ya 1-1 na Taifa Stars ya Tanzania na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye uwanja wa Dag Hammarskjoeld mjini Ndola.
Rais Kenneth Kaunda, Waziri Mkuu Daniel Lisulo na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Chama na Serikali walikuwa miongoni mwa maelfu ya wapenzi wa soka ambao walishuhudia Zambia ikitolewa katika raundi ya tatu kwenye mchezo ambao ingeweza kuifunga Tanzania.
Zambia sasa ni lazima isubiri hadi mwaka 1982 kwa mashindano mengine. Lakini kwa Tanzania, imekuwa ni ndoto ambayo imegeuka kuwa kweli na imewawezesha kusonga mbele kwenye fainali za kombe hilo mjini Lagos kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo nchini humo.
Kulikuwako na fadhaa kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka wa Zambia ambao kwa muda wote walikuwa wakiishangilia na kuomba dua timu yao iifunge Taifa Stars, baada ya Stars kushinda bao 1-0 mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza hapo Oktoba 28, 1979. Lakini badala yake wakaona matumaini yakiponyoka kama tonge la ugali mkononi.
Mtu ambaye Zambia haitamsahau kwa 'ukatili wake mkubwa' ni mshambuliaji Peter Tino ambaye alifunga bao zuri katika dakika ya 85. Mkwaju wa Tino ulipishana na kipa Vincent Chileshe aliyetoka langoni kukabiliana na Tino. Goli hilo kwa hakika liliwanyamazisha na kuwahuzunisha maelfu ya Wazambia waliofurika uwanjani kuangalia pambano hilo la kihistoria.
Zambia iliuanza mchezo kwa nguvu zote na kwa uhodari mkubwa, juhudi ambazo ziliipatia bao la kuongoza katika dakika ya 42, mfungaji akiwa Alex Chola. Ilikuwa ni Zambia iliyokuwa ikicheza mchezo wote uwanjani, huku wachezaji wa Tanzania wakilazimika kucheza kwa kujihami zaidi.
Zambia ilizidi kupamba moto kwa kushambulia goli la Tanzania na kuwafanya watazamaji kuwa na matumaini kwamba vijana wao wangeshinda kwa uhakika kabisa dhidi ya Taifa Stars.
Walinzi wa Tanzania Daudi Salum, Salim Amir na Jella Mtagwa hawakusalimu amri hata kidogo kwa mashambulizi ya Zambia. Mshambuliaji hatari wa Zambia Godfrey 'Ulcar' Chitalu hakupewa mwanya hata kidogo na walinzi hao.
Washambuliaji wa Zambia walilishambulia lango la Tanzania bila kupumzika. Kipa wa Taifa Stars, Juma Pondamali alizuia kwa ujasiri mkubwa mikwaju mikali ya washambuliaji wa Zambia akina Chitalu, Alex Chola na Peter Kaumba.
Kabla ya goli la Chola, Chitalu alikuwa amekosa goli la wazi kutokana na krosi ya Jani Simulambo ambayo ilikuwa moja ya krosi nyingi zilizopigwa langoni kwa Tanzania. Na katika kasi yake ya kawaida, Chitalu alifanikiwa kuichomoka ngome ya Tanzania katika kipindi fulani, lakini kipa alikuwa macho kuokoa hatari hiyo.
Zambia, ambayo ilikuwa imepania kulipa kisasi cha kufungwa Dar es Salaam, haikukata tamaa na bahati ya bao ilikuja wakati Chola alipopata pasi ya Chitalu na kuirudisha tena kwake. Chitalu alitoa tena pasi kwa Chola na bila makosa mchezaji huyo akafunga kilimi cha mashabiki wachache wa Tanzania waliokuwepo uwanjani hapo.
Katika kipindi cha pili, Watanzania walikuja juu na kwa moto zaidi kwani Hussein Ngulungu, Thuwein Ally na nyota wa mchezo Tino waliwatoa jasho walinzi Bernard Mutale na Simbule na kuwaweka katika wakati mgumu.
Katika juhudi za kuongeza ukali wa mashambuli ya Zambia, kocha Brian Tiler alimtoa Peter Yambayamba na kumwingiza Bizwell Phiri na Pele Kaimana aliyeingia badala ya Evans Katebe. Tanzania nayo ilimtoa Thuwein na kumwingiza Mohammed Salim.
Katika hatua hiyo, Zambia walikaribia kupata bao la pili sekunde chache baadaye, lakini nafasi hiyo ilipotezwa na Chitalu ambaye alikuwa amebanwa sana na Mtagwa ambaye hakukubali kusalimu amri.
Tanzania nayo ilikaribia kusawazisha katika dakika ya 75 wakati shuti kali la nahodha Leodgar Tenga lilipookolewa na kipa Chileshe. Hapo hapakuwa na mzaha kwa upande wa Taifa Stars, hatua ambayo iliwafanya wachezaji wa Zambia wacheze kwa kujihami na bao lao.
Huku dakika zikiwa zinayoyoma, Chitalu alikatiza uwanja na mpira, akapiga chenga walinzi wawili wa Tanzania, lakini kipa Pondamali akamsimamisha kabla ya kupiga shuti. Hapo ndipo ilipoonekana dalili ya kuzama kwa Zambia, kwani Chitalu, Chola na Pele walikuwa wakipiga shuti zao zilizokuwa zikiokolewa kwa ujasiri mkubwa wa Pondamali. Hali hiyo sasa iliifanya Tanzania kuja juu na wachezaji wakafanikiwa kubomoa mbinu ya wapinzani wao katika sehemu ya kiungo, hivyo kuwawezesha kucheza watakavyo katika eneo hilo bila matata. Ndipo Tino alipozamisha matumaini ya Zambia kwa shuti lake ambalo liliwanyanyua Watanzania wachache uwanjani, wakacheza dansi kwa furaha ya kwenda Lagos.
Kocha wa Tanzania Slawomir Wolk kutoka Poland alisema baada ya mchezo kwamba Zambia ilipoteza mchezo huo kwa vile wachezaji wa Stars walikuwa wakijua kila mbinu na maarifa ya wapinzani wao.
Tukio moja tu uwanjani lilikuwa la kuonyeshwa kadi ya njano kwa kipa Pondamali kwa kupoteza wakati. Alisema Slawomir: "Tulicheza vibaya katika kipindi cha kwanza. Tulichanganyikiwa, lakini tukajisahihisha baada ya mapumziko. Hata hivyo, tuna furaha kwamba tumepita na tunakwenda katika fainali huko Lagos."
Katika mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma Pondamali, Leopard Tasso Mukebezi, Mohammed Kajole/Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.
No comments:
Post a Comment