Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 3 November 2014

KAMATI YA BUNGE YAITAKA TPDC KUKABIDHI MIKATABA 26

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.PICHA|MAKTABA 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge imeutaka uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwasilisha mikataba 26 kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) leo saa 4:00 asubuhi.
Ofisi hiyo imechukua hatua hiyo baada ya TPDC kutowasilisha mikataba 26 ya gesi wiki iliyopita mbele ya kamati hiyo ya Bunge inayoongozwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah amemwandikia barua kaimu mkurugenzi mtendaji wa TPDC akimtaka kuwasilisha mikataba hiyo kama ilivyoagizwa na kushindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa.
“Nafanya rejea agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) la Januari 26, 2012 na agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) la Oktoba 27, 2014 kutaka kuwasilisha mikataba 26 ya uzalishaji na ugawanaji mapato pamoja na taarifa za upitiaji wa mapato hayo,” inasema barua hiyo ya Kashililah.
“Nafanya rejea barua yako Kumb. CAB.135/39/01/53 ya Oktoba 28, 2014 ukiiomba PAC ikupe muda zaidi wa kuandaa mikataba na nyaraka zilizoombwa na Kamati.
“PAC imepitia na kutafakari, na kuazimia; TPDC ipewe siku nne hadi Jumatatu (leo) saa 4:00 asubuhi iwe imewasilisha mikataba 26 ya uzalishaji na ugawanaji mapato pamoja na taarifa ya mapitio ya mikataba hiyo mbele ya kamati hiyo.
“Pia Kamati kujadili taarifa ya ukaguzi wa hesabu za TPDC kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013.”
Awali PAC iliituhumu Wizara ya Nishati na Madini kwa kugoma kuwasilisha mikataba 26 ya gesi na iliwatimua kikaoni watendaji wa TPDC baada ya kushindwa kuwasilisha mikataba hiyo na mapitio yake wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa bodi ya TPDC, Michael Manda na kaimu mkurugenzi wa shirika hilo, James Andilile waliahidi kikao cha PAC kuwasilisha mikataba hiyo wiki iliyopita, lakini hawakutekeleza.
Naye kaimu mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe aliliambia gazeti hili kuwa iwe isiwe lazima mikataba hiyo iwasilishwe katika kamati kwa ajili ya kupitiwa na kusisitiza kuwa kamati ina haki ya kupata nyaraka yoyote inayoihitaji na anayezuia anakwenda kinyume na Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.
Katika utetezi wake TPDC ilieleza kuwa mikataba ya Serikali ina utaratibu wake wa kuipata, huku wakisema kamati inatakiwa kuipata kupitia ofisi za Bunge na kwamba aliyewaelekeza hivyo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Licha ya watendaji hao kuahidi kuwasilisha nyaraka za mikataba hiyo baada ya kueleza kuwa wanaweza kupewa adhabu kali, Filikunjombe alisema jambo hilo halijatekelezwa.
“Tumepata taarifa kwamba Wizara ya Nishati na Madini imesema haiwezi kutoa mikataba hiyo hadi iwasiliane na wawekezaji wao,” alisema.
“TPDC ni shirika la umma na hiyo mikataba wataileta tu. Kamati inafanya kazi kwa mujibu wa sheria hivyo mikataba tunayoiomba siyo nyaraka za siri au ambazo zimesainiwa na rais zisitolewe.”
Akijibu tuhuma hizo, Profesa Muhongo alisema: “Hatuwezi kuishi katika malumbano na katika mazingira hayo hatuwezi kuendelea. Sina muda wa kujibishana nao, wao wachukue hatua wanazoweza.
“Nchi haiwezi kufuta umasikini kwa malumbano bila kufanya kazi kwa vitendo na uadilifu.”
Huu ni wakati wa kuwa na viongozi wenye upeo mkubwa. Mitaji na kazi zenye kufuta umasikini ndiyo ‘injini ya kukuza uchumi wetu.”
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment