Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama
Wanafunzi 297,488 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza Kidato cha Nne na mtihani wa Maarifa wa mwaka 2014, utakaoanza Jumatatu ijayo.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema kati yao 245,030 ni watahaniwa wa shule na 52,458 ni watahaniwa wa kujitegemea.
Alisema watahiniwa wote walioandikishwa kufanya mtihani mwaka 2014 wamegawanyika katika makundi ya watahaniwa wa shule, watahiniwa wa kujitegemea na wanaofanya mtihani wa maarifa.
Mhagama alisema watahiniwa hao wa mwaka 2014 ni pungufu ya watahiniwa 122,369 ikilinganishwa na watahiniwa 367, 399 wa mwaka 2013.
Aidha alisema kati ya watahiniwa hao, 51 ni wasioona na wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa kwa ujumla ni 356.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea walioandikishwa ni 52,458 ambapo wanaume ni 25,774 na wanawake 26,684 sawa na asilimia 50.87.
Alisema watahiniwa wa kujitegemea walioandikishwa mwaka huu ni pungufu ya 8,049 ikilinganishwa na watahiniwa 60,507 walioandikishwa mwaka 2013.
Mhagama alifafanua kuwa karatasi ya pili imeongezwa kwa lengo la kuwafanya watahiniwa wa kujitegemea kuwa na alama zitakazounganishwa na alama za karatasi ya kwanza kwa uwiano maalum uliowekwa, kama inavyofanyika kwa watahiniwa wa shule.
Alisema jumla ya watahiniwa wa mtihani wa maarifa walioandikishwa ni 14, 723 wakiwemo wanaume 5,940 na wanawake 8,783.
Alisema watahiniwa wa maarifa walioandikishwa mwaka 2014 ni pungufu ya 3,491ikilinganishwa na watahiniwa 18,214 walioandikishwa mwaka 2013.
Kwa upande wa vituo vya mitihani, Mhagama alisema kuwa jumla ya shule 4,419 zina watahiniwa wa shule, na vituo 920 zina watahiniwa wa kujitegemea, huku vituo 620 vimeandikisha watahiniwa wa maarifa.
Alitoa wito kwa maafisa elimu wote wa mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa salama na tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment