Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 1 November 2014

UCHAGUZI WA KURA ZA MAONI CCM TIMBWILI TUPU KIBAIGWA


Na Mwandishi Wetu
Kibaigwa: UCHAGUZI wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeingia dosari katika mji mdogo wa Kibaigwa mkoani Dodoma baada ya kukumbwa na kashfa za rushwa na ukiukwaji wa taratibu na kanuni.

Eneo linalodaiwa kukumbwa na mizengwe hiyo ni Mtaa wa Mpakani ambapo mshindi wa kura hizo za maoni, Jeremiah Mark Mtagwa, anadaiwa kutumia rushwa na kuanza kampeni mapema.
Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Oktoba 31, Bw. Mtagwa alishinda kwa kupata kura 237 dhidi ya kura 163 za mpinzani wake Japhet Malongo.
Aidha, inaelezwa kwamba, mizengwe hiyo ilianza wakati wa kampeni za wagombea kujinadi kwa wapiga kura Oktoba 27, ambapo msimamizi wa uchaguzi huo, Bi. Ruth Mesomane, ambaye ni Katibu Mwenezi wa Kata ya Kibaigwa, anadaiwa kumnyima fursa Bw. Malongo kujieleza na hatimaye kuvunja mkutano.
Akizungumza na mtandao huu, Bw. Malongo, ambaye alikuwa akitetea nafasi yake, alisema baada ya kunyimwa fursa ya kujieleza wakati wa kampeni, alilazimika kulalamika wilayani ambapo uongozi wa CCM Wilaya ya Kongwa uliahidi kwenda kulishughulikia suala hilo kesho yake.
"Kesho yake Katibu wa CCM wa wilaya Bw. Ally Kidunda alikuja akiwa ameongozana na Katibu Mwenezi wa Wilaya, Bw. Lepupuma pamoja na katibu wa UWT na UVCCM na wakaagiza kwamba kwa mujibu wa taratibu wagombea wote lazima wapewe nafasi sawa ya kujieleza na kuulizwa maswali, jambo ambalo halikuwa limefanyika," alisema Malongo.
Aidha, inaelezwa kwamba, uongozi wa wilaya uliagiza uchaguzi huo ufanyika Oktoba 31 na kwamba Katibu wa Wilaya ndiye angekuja pia kuangalia, hata hivyo, katibu huyo hakuweza kufika jana na kuagiza uongozi wa Kata ndio usimamie kama kanuni zinavyoelekeza.
Taarifa zinasema, msimamizi wa uchaguzi huo, Bi. Mesomane, aliuendesha uchaguzi huo katika mazingira yanayoashiria wimbi la rushwa huku akimzuia Bw. Malongo kuingia ukumbini baada ya zoezi la kura kufanyika.
"Nilitolewa nje wakati wa kupiga kura, sawa, lakini baada ya pale wakanikataza nisiingie, lakini naambiwa mwenzangu aliingia kupitia mlango wa pembeni na ndipo mchezo wa uchakachuaji ulipofanyika.
"Pia kwa kuwa nilikwishahisi mchezo mchafu, niliomba niteue mawakala wawili, lakini wakanikatalia na kusema wakala ni mmoja tu... niliongoza katika kituo cha Nguvu Kazi kwa kupata kura 116 dhidi ya 14, lakini kwenye kituo cha Mpakani ambako uchakachuaji ndiko ulikofanyika, nilipata 47 dhidi ya 223," alisema Malongo.
Inaelezwa pia kwamba, msimamizi huyo wa uchaguzi alipiga simu polisi akidai kulikuwa na fujo na kwamba anaomba ulinzi, lakini mkuu wa kiuo cha polisi Kibaigwa, Afande Massawe, alipofika hapo akashangaa kukuta hali ya utulivu huku watu wakisubiri matokeo.
Katika hali ya kushangaza, matokeo hayo yalitangazwa na wakala wa Bw. Malongo, Petro Mwenda, badala ya msimamizi wa uchaguzi, ambaye pamoja na viongozi wengine, walikuwa wamejifungia.
Blogu hii ilimtafuta msimamizi wa uchaguzi, Bi. Mesomane, ambaye alishusha lawama kwa Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Richard Kapinye, kwamba ndiye anayemuunga mkono Bw. Malongo na kumtuhumu kuchukua watu kutoa matawi mengine kwenda kupiga kura.
"Najua aliyekwambia atakuwa Diwani tu, anamtetea huyo mgombea wake," alilalamika Bi. Mesomane huku akishindwa kufafanua ni kwa vipi anaweza kuwatambua wapiga kura kwamba wameletwa na nani wakati kura ni za siri.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Bw. Ally Kidunda, alikiri kupokea taarifa kwa simu kuhusu sakata hilo, lakini akasema anasubiri rufaa ya maandishi ili kuchunguza na kujua ukweli kabla hawajachukua hatua.
"Nimepokea malalamiko hayo yasiyo rasmi, lakini tutashughulikia suala hili kwa makini zaidi kwa sababu hatupendi chama kiingie kwenye kashfa za rushwa na mikanganyiko mingine," alisema.
Hata hivyo, alisema kwamba Kibaigwa kumekuwa na changamoto kubwa za kisiasa na kuonya kwamba kuna kikundi cha wafanyabiashara wanaowatumia wanasiasa kuhakikisha wanawaweka madarakani watu wanaowataka.
Blogu hii ilimtafuta pia Bw. Mtagwa, ambaye alikanusha vikali madai yote na kusema ni njama za kisiasa zinazofanywa dhidi yake.
"Mimi ndiye nimekuwa nikifanyiwa fitna mfululizo, nimelalamika hayo kwa maandishi, sasa nashangaa ninapogeuziwa kibao tena kama eti nimefanya ama kushiriki kumhujumu mwenzangu asishinde," alisema.

No comments:

Post a Comment