Kikundi cha Agape
Kikundi cha Tumaini
Kikundi cha Upendo
Kikundi cha Ebenezer
Kikundi cha Kijamii cha Wanawake (CBO) cha Atue Women Empowerment kilichoko mkoani Iringa kinaota ndoto za mafanikio, na ndoto hizi zitatimia tu ikiwa watafanikiwa kupata kiasi cha Shs. 50 milioni kuongezea mtaji kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki.
Mradi huo, kwa mujibu wa Mratibu wa kikundi hicho, Bi. Emery Kiwanga, unaweza kuwakwamua kiuchumi na hivyo kuondokana na utegemezi sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za wananchi kujiletea maendeleo wenyewe.
Katika mahojiano maalum na www.brotherdanny5.blogspot.com, Bi. Kiwanga alisema, ufugaji huo wa nyuki siyo tu kwamba utawaletea manufaa kiuchumi, bali pia utasaidia kuihamasisha jamii katika suala zima la utunzaji wa mazingira ambalo kikundi kimelenga kulipigia kampeni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Tunajishughulisha na kilimo cha msimu, lakini tumeona kwamba kupitia umoja huu tuanzishe mradi wa pamoja wa akinamama ambao utakuwa mwanzo wa kukuza uchumi wetu pamoja na kutunza mazingira, kwani ufugaji wa nyuki unahitaji mazingira rafiki yasiyoharibiwa," alisema.
Bi. Kiwanga alisema kwamba, wazo la kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki kwa kikundi hicho walilipata baada ya kufanya ziara katika shamba la Mheshimiwa Mizengo Pinda mkoani Dodoma, ambapo baada ya kupata elimu ya kutosha, wakaona wanachelewa wakati fursa zipo za kuiletea jamii maendeleo.
"Badala ya kukopeshana visenti kidogo kwa ajili ya biashara ndogo ndogo ambazo hazina faida kubwa kiasi kwamba wengine wanashindwa hata kurejesha mikopo, tumeona ni bora tuwe na mradi endelevu utakaoinufaisha jamii yote kwa ujumla," alisema.
Ili kufanikisha mradi huo, Bi. Kiwanga alisema wanahitaji wahisani mbalimbali wawasaidie kiasi cha Shs. 50 milioni ambazo watazitumia kwa ajili ya kununua shamba, mizinga pamoja na miundombinu mingine ya kuanzisha ufugaji huo wa nyuki mkoani Iringa.
Alisema lengo kubwa ni kuhakikisha kila mwanakikundi kati ya 100 wanaounda kikundi hicho, anamiliki mizinga mitano, hivyo wanahitaji kuanza na mizinga 500.
"Kwa kweli wanawake tunahitaji tujikomboe, lakini kikundi chetu chenye mchanganyiko wa wanawake wa rika mbalimbali, kinaweza kabisa kufanya mambo makubwa ya maendeleo na tunaiomba jamii itusaidie tufikie malengo yetu," alisema.
Akizungumzia historia ya kikundi hicho, Bi. Kiwanga alisema kwamba kilianzishwa mwaka 2011 kabla ya kupata usajili rasmi mwaka 2013 kama Community Based Organization (CBO) katika Manispaa ya Iringa.
"Atue ni kifupi cha vikundi vidogo vinne, ambavyo ni Agape, Tumaini, Upendo na Ebenezer, na kwa sasa kina jumla ya wanachama 100," alibainisha.
Alisema malengo ya kikundi hicho ni kuwajengea uwezo wanawake wote Tanzania, wakianza na wanawake wa Manispaa ya
Iringa.
"Tangu tulipoanza tumekuwa tukichangiana na hatimaye kukopeshana baada ya kuhamasisha wanawake waanzishe biashara ndogo ndogo kwa nia ya kuondokana na utegemezi
ambao mara nyingi huwaweka wanawake katika mazingira hatarishi.
"Lakini pia tunatoa elimu ya ujasiriamali ili kujijengea uwezo binafsi (kwa kila mwana kikundi), kujenga nidhamu ya fedha, udhibiti wa fedha na matumizi, mikopo na vyanzo vingine vya
mapato tukilenga kuwa kikundi cha mfano katika maendeleo kwa njia ya kuweka na kukopa fedha kutoka
katika taasisi za fedha," anafafanua.
Aliongeza kusema kwamba, kwa
kuzingatia Mkakati wa Serikali wa kusaidia kupambana na umaskini kupitia awamu
ya pili ya Mpango wa Taifa wa Kupambana
na Umaskini na Kukuza Uchumi (MKUKUTA II) na Malengo ya Milenia, kikundi kimelenga kutumia fursa zinazopatikana
katika maeneo yanayokizunguka, pamoja na ubunifu na kujifunza kwa wengine,
kuhakikisha kinaanzisha miradi endelevu kwa ustawi wake na jamii kwa ujumla badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali.
Kuhusu vyanzo vya mapato kwa sasa, Bi. Kiwanga alisema wanategemea zaidi michango ya wanachama ambayo ndiyo hutumka kukopeshana kwa ajili ya kuendeleza biashara ndogo ndogo.
"Changamoto yetu kubwa ni ukosefu wa mtaji. Hadi wakati huu chanzo chetu kikuu cha mtaji
ni ada pamoja na michango mingine ya wanachama, kiasi ambacho hakiwezi
kutosheleza malengo, ni changamoto ambayo wakati mwingine huwafanya wanachama washindwe
kuendelea hata na miradi waliyoianzisha," alisema.
Naomba mawasiliano ya hicho kikundi
ReplyDelete