Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino amemsifu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwa ni miongoni mwa viongozi wa vyama vya soka duniani walioamua kuendesha soka kwa weledi kutokana na kuratibu mafunzo mbalimbali kwa makocha na waamuzi.
Salamu za Infantino zimetolewa na Msimamizi Mkuu wa kozi ya waamuzi nchini, Carlos Henrique kutoka Afrika Kusini akisema, “Infantino ana ripoti zote ya namna mpira wa miguu unavyoendeshwa duniani. Anasifu Tanzania kwa namna mnavyopiga hatua. Ana ripoti idadi ya makocha walivyokuwa wachache na sasa mna makocha wengine wako kwenye kozi.
“Mbali ya makocha, leo tuko nanyi waamuzi, ni hatua kubwa ambayo Rais Infantino amemsifu Rais wa TFF, Bwana Malinzi,” alisema Henrique.
Henrigue aliyeka waamuzi hao kujikita zaidi kusoma namna sheria 17 za mpira wa miguu zilivyoboreshwa kwa kuondoa zaidi ya maneno 1,000 ili kuja kusimamia vema michezo wa soka huku akiwataka kuwa mahiri wakati wote. Henrique anafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Mark Mzengo kutoka Malawi, Felix Tangawarima wa Zimbabwe na Gladys Onyago kutoka Kenya.
Kozi za Waamuzi wa Mpira wa Miguu wa Tanzania sasa ilianza jana Julai 25, 2016 kwa waamuzi wenye Beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) na waaamuzi waandamizi wanaotarajiwa kuveshwa beji hizo kwa majina yao kupendekezwa FIFA kama watapata matokeo mazuri kwenye kozi inayoendelea.
Kozi ilianza kwa ratiba ya waamuzi wote kuchukuliwa vipimo (physical fitness test) kwa kila mwamuzi chini ya wakufunzi hao kutoka FIFA. Baada ya vipimo, darasa la waamuzi hao litaanza kwa nadharia na vitendo. Darasa hilo litafikia mwisho Julai 29, 2016 kabla ya kuanza darasa la waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) na makamishna wa michezo kwa msimu wa 2016/2017.
No comments:
Post a Comment