Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 15 July 2016

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AUNGA MKONO JITIHADA ZA WANAWAKE KISARAWE KUSINDIKA MUHOGO


 Bi. Anna Salado, Mkurugenzi wa taasisi ya Women for Africa Foundation ya Hispania, akizungumza na akinamama wa kikundi cha Green Voices katika Kijiji cha Kitanga (hawako pichani) na kueleza jinsi alivyofurahishwa na mafanikio yao kwenye usindikaji wa zao la muhogo.


NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, ameunga mkono jitihada za wanawake wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe kusindika zao la muhogo.
Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe (CCM), amesema yuko tayari kushirikiana na wanawake wa kijiji hicho pamoja na wilaya nzima ya Kisarawe kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi kutokana na zao hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu na mshiriki kiongozi wa kikundi cha Kitanga Green Voices, Bi. Abia Magembe, mara baada ya ziara ya ujumbe wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kijijini hapo Julai 13, 2016, Mhe. Jaffo alimtaka kiongozi huyo kuwasiliana naye mara moja ili kuona ni namna gani anaweza kusaidia mradi huo ambao umeanza kuonyesha matunda mazuri kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Wakati wa ziara ya ujumbe wa taasisi ya WAF kutoka Hispania, Mhe. Jaffo hakuwepo kutokana na kutingwa na majukumu ya kazi, lakini kwa mujibu wa Bi. Magembe, amemtaka kuwasiliana naye haraka ili kuhakikisha jitihada za wanawake hao zinaendelezwa.
Ujumbe wa WAF ulioongozwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Anna Salado kutoka Hispania, pamoja na mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, ulijionea namna akinamama hao wanavyosindika bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo kijijini hapo.
 Bi. Anna Salado akicheza wakati akinamama wa Kitanga wakiimba.
Aidha, ujumbe huo ulielezwa kwamba, mpango wa akinamama hao kwa sasa ni kujenga viwanda vidogo kijijini hapo ili kusindika zao la muhogo ikiwa ni hatua mojawapo ya kuunga mkono kauli ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.
“Kwa kuwa serikali imekwishaahidi kwamba inataka kuona Tanzania ya viwanda ili kuongeza ubora wa thamani ya mazao yetu pamoja na kuzalisha ajira, sisi tumedhamiria kujenga viwanda vidogo hapa hapa kijijini ili iwe rahisi kwa akinamama kupata malighafi na kuwasaidia wengine kujifunza,” alisema Mama Magembe.
Mama Magembe, ambaye ni miongoni mwa akinamama 15 waliokwenda Hispania mapema mwaka huu kujifunza miradi mbalimbali inayolenga kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, alisema kwamba kujengwa kwa viwanda vidogo kijijini hapo kutakuwa ukombozi wa jamii nzima hasa kwa vile wilaya ya Kisarawe inalima sana muhogo, lakini wananchi wanapunjwa na walanguzi, hivyo zao hilo kuonekana kutowakwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Bi. Anna Salado, ambaye alimwakilisha Rais wa taasisi hiyo, Maria Tereza Fernandez de la Vega, alieleza kufurahishwa na jitihada za wanawake hao na akaahidi kwamba, mradi huo ni miongoni mwa miradi itakayopewa kipaumbele katika awamu ya pili.
Alisema kwamba, imekuwa vizuri kwa wananchi wenyewe kubuni miradi inayotekelezeka na yenye tija, na kwa namna walivyoweza kufanikiwa katika kipindi kifupi, wana matumaini makubwa wanawake hao na wanawake wengine nchini watafanya vizuri ikiwa watajifunza.
Aidha, Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia, alisema kwamba mradi wa kusindika muhogo utaikwamua jamii katika suala zima la kukabiliana na njaa, lakini pia utawasaidia wanawake kuongeza kipato kutokana na kuongeza mnyororo wa thamani.
“Mmefanya vizuri sana, tunawaongeza na tunaamini kwamba, katika awamu inayofuata mtafanya vizuri zaidi,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka wanawake wa kikundi hicho kuwa waalimu kwa wanawake wengine kwa kuwa lengo ni kuhakikisha wanawake wote wanapata elimu na ujuzi na wanatekeleza miradi inayoweza kuwakwamua kiuchumi na kuwaletea maendeleo.
 Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, akizungumza na akimama wa Green Voices katika Kijiji cha Kitanga, Kisarawe.
Bi. Secelela Balisidya, ambaye ni mratibu wa Green Voices Tanzania, aliwapongeza akinamama hao na kuwataka wasikate tamaa kwa kuwa mwanzo umeonekana.
Aliwaasa kudumisha umoja ili kikundi hicho kiwe cha mfano na kuwahimiza kukisajili haraka ili serikali iweze kukitambua.
“Dumisheni umoja, vikundi vingi huanza vizuri halafu vinasambaratika, tusingependa kuona hilo linatokea kwa sababu bado kuna fursa nyingi za kuwawezesha wanawake na umoja ndiyo nguzo muhimu,” alisema.
 Bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo ambazo zinazalishwa na akinamama wa Green Voices katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Zao la muhogo lina manufaa mengi kwani mbali ya kuutafuna mbichi, kuuchemsha au kuuchoma, kutengeneza mchanyato; unga wake hutumika kwa ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka hutumika kama kuni.
Lakini pia unga wa muhogo unatumika kutengeneza bidhaa nyingine kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, sambusa, maandazi, chapati, tambi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, huku maganda ya mihogo hutumika kama chakula bora cha mifugo.
Aidha,  muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.
Kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.
Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania. 
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya  mahindi.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.

Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.
 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kitanga, Wazir Yakoub Wazir, akisalimiana na Mkurugenzi wa taasisi ya Wanawake wa Afrika, Anna Salado.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia (kushoto) na Anna Salado wakipata msosi huku wakiwa na madafu yao wakati walipotembelea mradi wa kusindika muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe Julai 13, 2016.

No comments:

Post a Comment