Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti, Richard Sinamtwa imebaini kasoro kwa Abajalo FC kumtumia mchezaji Laurent E. Mugia hivyo kuamua kumfungia mchezaji huyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa kanuni ya 36 (16) toleo la mwaka 2014 la Ligi Daraja la Pili kwa kosa la kuchezea klabu mbili katika msimu mmoja.
Kwa kuwa kanuni za Ligi Daraja la Pili mpaka Ligi Kuu zina upungufu unaofanyiwa mapitio pale kiongozi wa timu anapofanya udanganyifu wa usajili wa mchezaji bila kumshirikisha mchezaji, Kamati sasa imelazimika kutumia kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Ibara ya VII (10) ikinukuu:
“A team which will have committed a fraud on the identity of player or which will have allowed a suspended or non-qualified player to take part in match shall, lose the match and shall be completely eliminated from the competition as soon as the incriminating fact are clearly established by CAF organizing committee.” Mwisho wa kunukuu.
Kwa maelezo hayo, timu ya Abajalo FC inanyang’anywa pointi sita. Timu za Pamba SC na The Mighty Elephant wanapewa pointi tatu kila timu na magoli matatu.
Kamati inaagiza Sektretarieti kuwachukulia hatua na kuwapeleka katika vyombo vya Serikali viongozi wote wa timu ya Abajalo walioshiriki kubadilisha jina la mchezaji alilotumia akiwa na timu ya Kagera Sugar ili kufanikisha usajili wao na pia kwa kubadilisha tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa za mchezaji ili kufanikisha usajili wao kwa msingi kwamba waligushi.
Uamuzi huu, ni wa mwisho na kwamba kama kuna ambaye hajaridhika, ana nafasi ya kukata rufaa kwenye CAS - Mahakama ya Mashauri ya Soka ya FIFA iliyoko Geneva, Uswisi.
Awali kwa nyakati tofauti, Pamba SC ya Mwanza na The Mighty Elephant ya Songea zilikata rufaa kuilalamikia Abajalo FC kwa kumtumia mchezaji wa Kaliua City ya Tabora, Laurence Mugia kutoka Kagera Sugar katika michezo ya mtoano wa Ligi Daraja la Pili kwa ajili ya kupanda daraja la kwanzaa huku wakijua kuwa ni kosa kwa mujibu wa kanuni.
No comments:
Post a Comment