Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers Ltd, Eric Shigongo James pamoja na mshindi wa nyumba Nelly Mwangosi wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa nyumba hiyo iliyopo Salasala.
Shigongo, Mwangosi na mume wa Nelly Mwangosi, Karolo Stephen Magani wakifungua bango lililopo katika nyumba hiyo.
Bango lililopo katika nyumba hiyo.
Shigongo akimkabidhi mshindi wa nyumba, Nelly Mwangosi ufunguo wake. Kushoto ni mume wa Mwangosi, Karolo Stephen Magani na katikati ni kijana wao, Emmanuel Karolo.
...Akimkabidhi mkataba wa makabidhiano ya nyumba hiyo.
Shigongo akimtaka Mwangosi kutokuwa na hofu kwani nyumba hiyo ni mali yake kuanzia leo na hakuna mtu yeyote atakayemsumbua.
Furaha ikiwa imetawala baada ya mshindi wa nyumba kuwasili kwenye nyumba yake.
Mshindi wa nyumba na familia yake wakikaribishwa kwenye nyumba yao.
Ndugu, jamaa na marafiki wa Nelly Mwangosi wakiwasili eneo la nyumba.
Shigongo akimkaribisha Mwangosi kwenye nyumba yake mpya Salasala.
Mwangosi, mumewe na kijana wao wakielekea kwenye nyumba yao.
Mshindi wa nyumba ya Global, Nelly Mwangosi (katikati) mara baada ya kuwasili kwenye nyumba yake Salasala. Kushoto ni mumewe Karolo Stephen Magani, wa pili kulia na kijana wao, Emmanuel Karolo na Mhariri wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Sifael Paul (kulia) aliyeambatana nao.
MSHINDI wa Shindano la Shinda Nyumba lililokuwa likiendeshwa na Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti yake ya Championi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Uwazi na Amani, Nelly Mwangosi leo amekabidhiwa rasmi mjengo wake huo.
Mwangosi ambaye ni mkazi wa mkoani Iringa aliibuka mshindi wa nyumba hiyo katika bahati nasibu iliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kukabidhiwa nyumba hiyo, Mwangosi (45) ambaye alikuwa ameambatana na mumewe, Karolo Stephen Magani (52) alitembelea makao makuu ya Global Publishers yaliyopo Bamaga jijini Dar es Salaam na kupokelewa kwa shangwe na vifijo na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Hali hiyo ilimfanya Mwangosi abubujikwe na machozi ya furaha kutokana na mapokezi makubwa ambayo hakutarajia kukutana nayo kutoka kwa wafanyakazi wa Global waliokuwa wakiongozwa na mkurugenzi wake mtendaji, Eric Shigongo James.
Akiwa ofisini hapo, Mwangosi alipata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi wa Global kuhusiana na nini alichokifanya mpaka akafanikiwa kuibuka mshindi wa bahati nasibu hiyo.
“Hakuna chochote nilichokifanya zaidi ya kukata kuponi za magazeti ya Championi, Uwazi, Amani, Ijumaa, Ijumaa Wikienda pamoja na Risasi na kumpatia mume wangu azipeleke kwa wakala wa Global Publishers aliyepo Iringa.
“Hata hivyo namshukuru sana Mungu kwani yeye ndiye kila kitu na yeye ndiye aliyepanga mimi niwe mshindi wa bahati nasibu hiyo, lakini pia nawapongeza sana Global Publishers kwa kuandaa shindano hili kwani mmeonyesha ni jinsi gani mlivyo karibu na watu, Mungu awabariki sana,” alisema Mwangosi ambaye ni mama wa watoto wawili.
Baada ya mazungumzo hayo na wafanyakazi wa Global, safari ya kwenda kwenye mjengo huo uliopo Salasala jijini Dar kwa ajili ya zoezi zima la kumkabidhi zawadi yake hiyo lilianza. Ilichukua takriban dakika 25 kufika kwenye mjengo wake huo mpya wa kisasa kabisa uliokuwa na kila kitu ndani.
Hata hivyo, Mwangosi alipouona mjengo huo kwa mara nyingine, alishindwa kujizuia na kujikuta akibubujikwa na machozi ya furaha yaliyomfanya mume wake aanze kumbembeleza.
Kitendo hicho pia kiliwatoa machozi baadhi ya ndugu zake aliokuwa ameambatana nao lakini baada ya kutulia alishuka katika gari aliyokuwa amepanda na kwenda moja kwa moja kukabidhiwa nyumba yake hiyo na Mkurugenzi wa Global, Eric Shigongo.
Baada ya zoezi hilo, Mwangosi aliishukuru kwa mara nyingine tena Global Publishers kwa zawadi hiyo ambayo hakuwa anaitarajia katika maisha yake.
“Nawashukuru sana Global Publishers kwani mmeyabadilisha maisha yangu hakika Mungu awabariki wote, pia nachukua nafasi hii kuwataka Watanzania wote kutopuuzia bahati nasibu yoyote inayoendeshwa na kampuni hii.
“Hakuna uongo wowote unaofanywa ila kila kitu wanachokifanya ni kweli kabisa, katika maisha yangu sikuwa na ndoto za kumiliki nyumba lakini kupitia gazeti moja tu la Sh 500 maisha yangu yamebadilika, nawaomba Watanzania wote kushiriki bahati nasibu zote zinazoendeshwa na Global, ipo siku nao watafanikiwa,” alisema Mwangosi.
Katika hatua nyingine, Shigongo alimtaka Mwangosi kutokuwa na hofu kwani nyumba hiyo ni mali yake kuanzia leo na hakuna mtu yeyote atakayemsumbua.
“Nyumba hii kuanzia sasa ni mali yako, hivyo kuwa na amani kabisa hakuna atakayekusumbua, ila jambo la msingi unapaswa kumshukuru Mungu kwani amekufuta machozi kutokana na shida mbalimbali ulizopitia katika maisha yako.
“Siku zote nilikuwa namuomba Mungu mshindi wa nyumba hii awe ni mama ambaye maisha yake ni ya chini na asiye na nyumba kabisa na hatimaye maombi yangu yamesikika,” alisema Shigongo.
Bahati nasibu ya shindano hilo iliendeshwa kwa takriban miezi sita kwa kujumuisha wakazi wa mikoa yote ya Tanzania.
Shindano hilo pia lilijumuisha droo ndogondogo kwa kutoa zawadi kwa wasomaji ambapo baadhi yao walibahatika kujishindia pikipiki za kisasa, vyombo vya jikoni, mashuka, televisheni za ‘flats creen’, ving’amuzi vya Ting, simu za ‘smartphone’ na kadhalika.
No comments:
Post a Comment