Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 30 July 2016

AfDB YAAHIDI KUENDELEA KUIPIGA JEKI TANZANIA KUKUZA UCHUMI WAKE

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) akiwa kwenye majadiliano na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Frannie Leutier (katikati) na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia  Kandiero. (Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango).
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akifafanua jambo mbele ya Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier, kulia kwa Dkt. Leutier, ni Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia  Kandiero na watendaji wa Wizara.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, akitoa ufafanuzi kuhusu vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano kwa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier (Hayupo pichani). 
Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia  Kandiero (wa kwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango. Kutoka kushoto kwake ni Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja (anayeandika).
Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier akitoa ufafanuzi wa namna ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo benki hiyo imewekeza Dola za Marekani Bilioni 2 hadi sasa nchini Tanzania.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia  Kandiero.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier.

Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier akisoma jambo kwenye kompyuta ndogo wakati akieleza jambo kwa Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye ofisini kwake Jijini Dar es salaam.
Na Benny Mwaipaja, MoFP

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya  mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Frannie Leautier, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo ameishukuru Benki hiyo kuwa mojawapo ya mashirika ya kimataifa yanayoisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Benki hiyo imewekeza hapa nchini kiasi cha dola Bilioni 2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni  4.4 kama ruzuku na mikopo yenye riba nafuu ili kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo barabara, elimu, kilimo, nishati ya umeme, na viwanda.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Mpango, ameelezea kufurahishwa kwake na Dira ya AfDB ambayo inafanana na vipaumbele vya serikali, kupitia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao umelenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Dira ya Benki hiyo imejikita katika malengo matano ambayo ni kuwekeza katika nishati ya umeme, uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda, kuiunganisha Afrika kwa mtandao wa barabara na kuboresha maisha ya watu.  
Mhe. Dkt. Mpango, amesema kuwa uwekezaji katika sekta hizo utasaidia mpango mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu kama vile kujenga viwanda kwa kuhusisha sekta ya umma na binafsi-PPP, umeme wa kutosha kuendesha viwanda, barabara ambazo zitaunganisha nchi zote  za Afrika.
“AfDB wametusaidia sana katika ujenzi wa barabara nyingi nchini Tanzania ikiwemo barabara ya kutoka Tanga kwenda Horohoro, ambayo imerahisisha usafiri wa kwenda nchini Kenya.  Barabara nyingine zitajengwa kutoka mpakani Kagera kupitia Kigoma kwenda Katavi, Dodoma hadi Iringa.  Hili ni jambo kubwa” Alisema Dkt. Mpango
Dkt. Mpango amemweleza Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt.  Frannie Leautier juu ya mpango wa serikali wa kuimarisha sekta ya usafirishaji ikiwemo kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (standard gauge) ambapo kiasi cha shilingi Trilioni 16 kinahitajika kukamilisha mradi huo.
Ameeleza kuwa tayari serikali imetenga kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika bajeti yake ya mwaka huu 2016/2017 kwaajili ya kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa unaohusisha njia ya reli yenye urefu wa kilometa 2,190.

Ameitaja Sekta nyingine ya kipaumbele kuwa ni kilimo kwaajili ya kuzalisha chakula kwa wingi kwaajii ya kutosheleza matumizi ya ndani na ziada yake kuuzwa nje ya nchi huku ikitiliwa mkazo uzalishai wa malighafi zitakazotumika katika viwanda.
Katika mazungumzo hayo Waziri wa Fedha na Mipango alimpongeza Dkt. Leautier, ambaye ni raia wa Tanzania, kwa kupata nafasi ya Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, kuwa ni faraja na kielelezo kizuri kwa akina mama wa Kitanzania kuwa wanaweza.
Kwa upande wa Makamu wa Rais wa AfDB Dkt. Frannie  Leautier Dkt. Leautier, ambaye aliambatana na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo hapa nchini, Bi. Tonia Kandiero, amesema kuwa AfDB imesaidia na itaendelea kusaidia  miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo ya barabara, elimu, kilimo, afya, sekta ya umeme ili Tanzania iwe na umeme wa kutosha kuendesha viwanda.
“Kwa kufanya hayo uchumi wa nchi utaimarika, vijana watapata ajira, wananchi watakuwa na maisha bora, chakula kitazalishwa cha kutosha na kingine kuuzwa nje ya bara la Afrika, Viwanda vitasaidia sana kiumarisha uchumi wa nchi kwani bila viwanda ni vigumu sana kuendelea” alisema Dkt. Leautier
Ameahidi kuwa Benki yake itaendelea kusaidia kuinua sekta ya kilimo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kutoa mkopo wenye masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima wakubwa, wa kati na wadogo kupata fursa ya mikopo hiyo itakayosaidia uzalishaji wa mazao.
Dkt. Leautier amesema kuwa atawasilisha kwenye bodi ya benki hiyo wazo la Tanzania kutaka kupigwa jeki katika ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa kwa kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa si tu kwa Tanzania, bali kwa nchi zote zinazoizunguka zikiwemo zile ambazo hazina bahari.
“Mradi huo ukikamilika utasaidia pia kunusuru barabara ambazo zimekuwa zikiharibika kutokana na kupitishwa mizigo mingi mizito ambayo ingefaa kusafirishwa kwa njia ya reli ili kuzifanya barabara hizo zidumu muda mrefu” aliongeza
Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, kupitia mfuko wake wa Maendeleo-African Development Fund (ADF),  imeahidi kutoa kiasi cha Dola Milioni 200, sawa na shilingi 433.6 bln,  kama ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu kwenye Mfuko Mkuu wa Bajeti wa serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018

Imetolewa

Benny Mwaipaja
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Fedha na Mipango

No comments:

Post a Comment