Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam imewatahadharisha wanaouza kazi feki za wasanii mbalimbali hapa nchini kuachana na mfumo huo kwa sababu kuanzia mwezi huu watawakamata wanaofanya biashara hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama alisema wametoa siku 30 kwa wanaofanya biashara hiyo kuachana nayo kabla hawajawashukia.
“Tunatoa siku 30 kwa wanaofanyabiashara ya kazi feki za wasanii, hiyo biashara waachane nayo kwa sababu inapoteza pato la Taifa,” alisema Msama.
Msama alisema kwa kuanzia watapita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na mkoa kwa mkoa ili kusaka computer zinazotumika kuiba kazi za sanaa.
Msama alisema ili kufanikisha kazi hiyo wanashirikiana na Jeshi la Polisi, Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo sambamba na Kampuni ya Msama Promotions ili kufanikisha zoezi hilo ambalo litakuwa ni la kusafisha tatizo hilo.
Aidha Msama alisema ili kukomesha zoezi hilo wakikuta kazi feki kwenye duka wanabeba mzigo mzima wa kazi za sanaa.
Naye Inspekta Jenera wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu alisema jamii inatakiwa kutoa ushirikiano na Polisi katika jambo hilo ambalo linaumiza nguvu kazi ya Taifa.
IGP Mangu alisema wananchi wanatakiwa kutoa taarifa kwa Polisi ili kazi ifanyike inavyotakiwa kwa lengo la maendeleo ya wasanii ambao wanasaka namna ya kuendeleza maisha yao.
No comments:
Post a Comment