Na
Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) kupitia programu yake ya Jukwaa la Sanaa wiki hii limetoa elimu kwa
wasanii kuhusu maudhui ya katiba inayopendekezwa hasa ibara ya 59 ya katiba hiyo
inayohusu sekta ya Sanaa.
Akizungumza katika programu
hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa BASATA ulioko Ilala Sharif
Shamba, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) aliyewakilisha wasanii Bw. Paul
Mtenda alisema kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania katiba
inayopendekezwa imeibeba tasnia ya Sanaa kitu ambacho ni mwanzo mzuri katika
kupata sera na sheria bora za kuisimamia sekta.
“ Kitendo cha katiba
pendekezwa kutambua uwepo wa Sanaa ni mwazo mzuri katika kupata sera, sheria na
kanuni zilizo bora za kuisimamia sekta hii. Maana kupitishwa kwa katiba lazima
kubadilishe sheria na kanuni mbalimbali zilizopo” alisema Mtenda.
Aliongeza kwamba, wasanii
hawana budi kuisoma katiba inayopendekezwa na kuelewa maudhui yaliyomo na
wasikubali kuwa wa kuhadithiwa na kuruhusu watu wengine kuwasemea na
kuwaamulia.
Katika hili alisema kwamba
wasanii toka mchakato wa kuandika katiba mpya ulipoanza wamekuwa wakipaza sauti
ili nafasi ya Sanaa itambuliwe kikatiba sasa ni wakati wa wao kuhakikisha wanayasoma
maudhui yote yaliyomo katika katiba inayopendekezwa na kuyaelewa vema ili kutumia
sanaa kuwaelimisha wengine.
“Tulipaza sauti sana ili
Sanaa itambuliwe na katiba inayopendekezwa, sasa tumefanikiwa. Kazi iliyopo ni
kuisoma na kuielewa vema ili sasa tuweze kuwaelimisha na wengine kuhusu maudhui
yaliyomo maana mwisho wa siku kila mmoja atakuwa na maamuzi yake kulingana na
uelewa” alisisitiza Mtenda.
Akizungumzia ibara ya 59
inayozungumzia hakimiliki, hataza na hakibunifu kwa wasanii, Mtenda alisema kwamba
bado kuna kazi kubwa ya kufanywa na wasanii pia wadau wa Sanaa ili kuhakikisha
kunakuwa na sera, sheria na kanuni bora zaidi katika kuisimamia sekta ya Sanaa.
“Kutambuliwa kwa Sanaa
katika katiba ni suala moja lakini suala la kuwa na sera, sheria na kanuni
zilizo bora ni suala jingine. Wasanii lazima tuendelee kuyapigania haya”
aliongeza.
No comments:
Post a Comment