Sikika
inasikitishwa na taarifa za kukosekana kwa damu salama katika vituo vya kutolea
huduma za afya nchini. Damu salama ni moja kati ya dawa muhimu kwa kuwa
inakidhi vipaumbele vya afya katika jamii kama ilivyobainishwa na Shirika
la Afya Duniani (WHO).
Ni dawa muhimu na ya kipekee kwa kuwa pindi
inapohitajika kutumika hakuna mbadala wala haiwezi kutengenezwa kiwandani.
Hivyo, uwepo wa damu salama katika hospitali zetu ni jambo la lazima.
Nchini
Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) uliopo chini ya Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, una wajibu wa kuhamasisha watu ili kujitolea damu. Vile
vile, mpango huu una wajibu wa kuhakikisha kuwa damu salama pamoja na bidhaa
zitokanazo na damu zinapatikana katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za
damu.
Ijapokuwa
NBTS imeweza kuongeza upatikanaji wa damu salama kutoka chupa 12,500
(2005) hadi chupa 160,000 (2013) kwa mwaka, hata hivyo, ukusanyaji wa damu bado
upo chini ya mahitaji halisi ya nchi ambayo ni kati ya chupa 400,000 hadi
450,000 kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani. NBTS imekuwa
ikikusanya takribani asilimia 38 tu ya mahitaji ya damu salama nchini kwa
mwaka, hivyo kusababisha upungufu wa kudumu wa damu salama katika vituo vyenye
dhamana ya kutoa huduma za damu nchini.
Kumekuwepo
na taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa majuma kadhaa sasa, kuhusu
upungufu mkubwa wa damu katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu
nchini. Uhitaji wa damu salama nchini ni mkubwa kutokana na kuongezeka kwa
tatizo la upungufu wa damu mwilini unaosababishwa na malaria na matatizo ya
uzazi hasa wakati wa ujauzito na kujifungua. Tanzania ni moja kati ya nchi
zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zenye idadi kubwa ya vifo vya watoto na
wanawake. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 28-30 ya vifo vya kina mama
vinatokana na upungufu wa damu mwilini. Hii inaweza kuonekana katika matumizi
ya damu salama nchini ambayo karibu asilimia 80 ya damu inayokusanywa inatumika
kwa wanawake na watoto, wakati asilimia 20 inatumika kwa matumizi mengine kama
upasuaji, ugonjwa wa selimundu (sickle cell anaemia) na tiba ya saratani. Kwa
hiyo upatikanaji wa damu salama kwa wakati unazuia kuongezeka kwa ugonjwa na
hata vifo na hivyo kuboresha afya za wananchi.
Ni kutokana
na umuhimu huu wa damu salama, Sikika iliamua kuangalia kwa undani ukubwa wa
tatizo hili, sababu na namna linavyoweza kutatuliwa ili kuboresha upatikanaji
wa damu salama nchini.
Katika
utafiti wetu tulibaini kuwa, kuna upungufu mkubwa wa damu salama katika vituo
vingi vya kutolea huduma hiyo. Kwa mfano katika wilaya ya Simanjiro, mahitaji
ya damu salama kwa mwaka ni chupa 145 hata hivyo wamekuwa wakipokea chini ya
nusu ya mahitaji yao. Mwaka 2013 walipokea chupa 74 tu, na kati ya mwezi
Februari na Machi mwaka huu hawakuwa na akiba kabisa kwani mara ya mwisho
kupokea damu ilikuwa mwezi Septemba mwaka 2014.
Hali hiyo
pia ilionekana katika wilaya ya Mpwapwa, ambapo kati ya mwezi Februari na Machi
2015 hawakuwa na akiba ya damu salama. Mahitaji yao kwa mwaka ni chupa 1,400,
hata hivyo wamekuwa wakipokea wastani wa chupa 20 kwa mwezi ambazo ni sawa na
chupa 240 tu kwa mwaka ikiwa ni mara 6 pungufu ya mahitaji yao.
Kwa
mkoa wa Dar es salaam, hali ni kama ilivyo katika mikoa mingine ambapo,
vituo vyote vilivyotembelewa vilikutwa na upungufu mkubwa wa damu salama
kutokana na kupatiwa damu pungufu na NBTS. Kwa mfano, hospitali ya Wilaya ya
Temeke imekuwa ikipokea damu salama inayokidhi mahitaji ya hospitali kwa
asilimia 20% tu kwa mwaka, huku hospitali ya Amana ikiwa inapatiwa asilimia 40%
tu ya mahitaji yake. Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambayo imekuwa
ikishugulikia mgonjwa makubwa na sugu, nayo imekuwa ikipatiwa damu
salama kwa takribani asilimia 50 - 60 ya mahitaji yake. Uhaba wa damu salama
umekuwa sugu nchini kote kutokana na kuwa vituo vyote vinategemea NBTS katika
kupatiwa bidhaa hiyo.
Sikika
inatambua na inaamini Serikali inatambua kuwa, chanzo kikubwa cha uhaba
sugu wa damu salama nchini ni upungufu wa fedha unaoikabili NBTS. Hii
inasababisha NBTS kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu kama vile kufanya
kampeni za kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa hiari pamoja na kununua
vitendanishi vya kutosha kwa ajili ya kupima, kuhifadhi na kutengeneza bidhaa
zingine zitokanazo na damu salama. Kwa takribani miaka 10, bajeti ya NBTS
kwa zaidi ya asilimia 80% imekuwa ikitoka kwa wafadhili, hususani
Serikali ya Marekani, kupitia Mpango wa dharura wa UKIMWI (PEPFAR) ambao
wamekuwa wakipunguza ufadhili wao unaofikia kikomo mwaka huu 2015.
Serikali imekuwa ikichangia asilimia 20 tu ya bajeti ya NBTS huku
ikishindwa kuziba pengo lililokuwa linaachwa na wafadhili, jambo ambalo ndio
chanzo kikubwa cha NBTS kushindwa kukusanya damu salama ya kutosha nchini. Kwa
mfano, Mahitaji ya damu salama nchini ni chupa 100,000 hadi 112,000 kwa muhula
kiasi ambacho NBTS imeshindwa kukusanya hata nusu ya kiasi hicho. Mathalani,
katika kipindi cha mihula miwili iliyopita (Oktoba – Disemba 2014 na Januari –
Machi 2015), NBTS imeweza kukusanya kiasi cha chupa 34,000 tu ambacho ni sawa
na asilimia 17 ya mahitaji ya damu salama kwa kipindi hicho.
Kushindwa
kwa NBTS kukusanya damu salama ya kutosha, kumepelekea baadhi ya vituo vya
huduma kutumia damu wanayoikusanya kutoka kwa familia, ndugu na jamaa za
wagonjwa badala ya kuipeleka katika vituo vya kanda au taifa kwa ajili ya
kupima, kuhifadhi na kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu salama. Hii
ni hatari kiafya, kwani huweza kusababisha maambukizi ya magonjwa na pia
kuchangia matumizi mabaya ya damu kwa kuwa vituo vya huduma havina
mashine na utaalamu wa kutosha hususani katika kutengeneza bidhaa zingine
zitokanazo na damu.
Kama ilivyo
kwa bidhaa zingine, uhaba wa damu salama kwa kiasi kikubwa umekuwa
ukisababisha baadhi ya watoa huduma za afya kujihusisha na vitendo vya rushwa -
‘’kuuza damu kwa wagonjwa’’ kutokana na ongezeko la mahitaji ya damu huku
upatikanaji wake ukiwa ni mdogo.
Sikika,
tumefurahishwa na tunapongeza jitihada za wadau mbalimbali kama taasisi za
kidini na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuandaa kampeni za kukusanya damu.
Jitihada hizi ni nzuri katika kutatua tatizo kwa muda mfupi lakini kunahitajika
mpango endelevu ambao utaiwezesha NBTS kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Tunaitaka
Serikali kuwajibika katika kutatua tatizo la damu salama nchini. Ni jukumu la
Serikali kuiwezesha NBTS kifedha badala ya kutegemea wafadhili na watu
binafsi. Serikali ipange bajeti inayotosha pamoja na kutoa fedha kwa wakati kwa
Mpango huu ili kuuwezesha kukusanya na kusambaza damu salama inayokidhi
mahitaji ya nchi. Tunaamini kuwa, iwapo Mpango wa Taifa wa Damu Salama utakuwa
na fedha za kutosha na zinazotolewa kwa wakati hakutakuwa na Upungufu wa damu
salama nchini.

Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183
Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi:
2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika
Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment