Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 26 March 2015

LUKUVI: NUNUENI NYUMBA ZA NHC, UJENZI BINAFSI NI GHARAMA KUBWA SANA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa mkandarasi anayejenga nyumba za NHC (Town Houses) katika eneo la Jangwani, Manispaa ya Sumbawanga. Kulia kwake ni Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Sebastian Katepa, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ntendo. (Picha zote na brotherdanny5.blogspot.com).

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu (wa tatu kutoka kulia) akifafanua jambo kwa Waziri Lukuvi kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akimsikiliza mkandarasi anayejenga nyumba za NHC Sumbawanga mjini. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, na anayemfuatia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya, alishindwa kujizuia na kwenda kushiriki ngoma ya Vingwengwe ya kabila la Wafipa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la nyumba za gharama nafuu za NHC leo hii. Hapa anaonekana akiwa amembeba mwanasesere. 
 Diwani wa Kata ya Katandala, Mhe. Kisabwite (kushoto), anaonekana akifuatilia kwa makini shughuli hiyo.
 Waziri Lukuvi akiteta jambo la Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya.

Na Daniel Mbega, Sumbawanga
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Vangimembe Lukuvi, amewataka wananchi kununua nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) badala ya kujenga wenyewe, kwani gharama ni kubwa.
Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa nyumba za makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga leo hii, Mhe. Lukuvi amesema nyumba zinazojengwa na NHC ni za gharama nafuu na zenye ubora, hivyo ni vyema kila mwananchi akanunua nyumba hizo kuliko kujenga kwa kuwa zinaweza kuchukua muda mrefu, kutumia gharama kubwa na ubora hafifu.
“Hizi nyumba, ambazo zinajengwa nchi nzima, ziko wazi kununuliwa na kila mwananchi, njooni mnunue kwa kuwa mkijenga ninyi wenyewe gharama yake ni kubwa zaidi na haziwezi kukamilika kwa wakati,” alisema na kuongeza kwamba, heshima ya mtu, mbali ya kazi na kipato, ni nyumba bora.
Lukuvi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya, kwa kutenga maeneo kwa ajili ya miradi ya NHC ya nyumba za gharama nafuu huku akisisitiza kwamba ni vyema maeneo hayo yawe na watu, kwani shirika hilo linafanya biashara ili kuongeza pato la taifa.
Amezitaka halmashauri zote kutenga maeneo kwa miradi hiyo ili kujenga nyumba za watumishi wao na wananchi kwa ujumla.
“Tengeni maeneo ili kujenga nyumba za watumishi wenu, lakini hata wananchi wa kawaida wanaruhusiwa kununua nyumba hizi,” alisema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Manyanya, alisema kwamba serikali yake imetenga eneo la ekari 25 katika mji wa Matai kwa ajili ya mradi wa nyumba hizo za NHC ambazo hazitalipiwa fidia.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, amesema mradi wa nyumba (town houses) uliozinduliwa ulibuniwa na shirika hilo kwa lengo la kuwapa fursa watu wa kipato cha kati katika miji mbalimbali kumiliki nyumba.
“Mradi huu ulianza Julai 2014 na utakamilika Julai 2015 ambao utakuwa na nyumba 10 za kuishi familia 20 na zina vyumba vitatu, jiko na sebule, ambapo utagharimu Shs. 1,532, 872,000,” alisema Mchechu.
Alisema shirika lake lina miradi mbalimbali katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo limenunua pia ekari 21 wilayani Kalambo na linakamilisha kulipia ekari tisa wilayani Nkasi kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama nafuu.
“Katika Mkoa wa Katavi tumeshajenga nyumba za gharama nafuu 70 zilizogharimu Shs. 2,346,937,089 katika eneo la Ilembo, Mpanda na tunaendelea kujenga nyumba 24 kwa gharama ya Shs. 1,212,467,364 za aina hiyo mjini Inyonga katika wilaya mpya ya Mlele.
“Shirika pia linajenga jengo kubwa la kisasa mjini Mpanda kwa ajili ya kufanyia shughuli za biashara kwa gharama ya Shs. 3,167,781,000,” alisema.


No comments:

Post a Comment