Na Immaculate Makilika, MAELEZO
RAIS wa Serikali ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame amesema nchi yake inapata amani kuona kuwa Tanzania iko tayari kufanya nao biashara.
Hayo yamesemwa leo, wakati Rais Kagame alipokuwa akifungua maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa katika viwanja vya Mwl. Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
“Inatupa amani kuona Tanzania iko tayari kufanya biashara na Rwanda, naahidi kuwa tutaendelea kujifunza zaidi na kufanya biashara zaidi” amesema Rais Kagame.
Rais Kagame, ameendelea kwa kusema kuwa “ sote ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na nchi za Ukanda wa kati, zenye lengo moja, hivyo wananchi wetu watafaidika kwa kuwa na miundombinu itakayosadia kukuza biashara zetu”.
Aidha, amewataka washiriki wa maonesho hayo kuwa na mawazo mapya ya biashara yatakayosaidia kuona fursa za biashara zilizopo katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema, katika bara la Afrika kumekuwepo na changamoto nyingi za biashara kama kutokuwa na ushirikiano baina ya nchi na nchi na kutojitangaza kibiashara. Hivyo kufanya kiwango cha biashara kati ya nchi na nchi kuwa chini.
Rais Magufuli, ameongeza kuwa kupitia soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki lenye nchi sita, na soko la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) lenye watu zaidi ya milioni 40, iwe fursa ya watu kushirikiana na kujitangaza kibiashara.
Maonesho hayo ya 40 ya biashara ya kimataifa, yamekuwa na mafanikio kwa kuwepo na ushiriki wa nchi 30 kutoka sehemu mbalimbali duniani, ikiwa ni zaidi ya nchi zilizoshiriki mwaka jana. Aidha, kumekuwepo na mabanda zaidi ya 650 na wajasiriamali 2000 ambao wanashiriki kwa kuonesha bidhaa mbalimbali, huku yakiwemo makampuni 15 kutoka nchini Rwanda.
No comments:
Post a Comment