Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 20 May 2016

TFF YAJISHTUKIA, YATOA ONYO KALI KUHUSU KUPANGA MATOKEO LIGI KUU

Jamal Malinzi, Rais wa TFF

Wakati pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara likitarajiwa kufungwa Jumapili Mei 22, 2016 kwa michezo minane, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa onyo kali kwa timu zote kutojiingiza kwenye mtego wa aina yoyote wa kupanga matokeo.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameziasa timu zote za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kucheza mechi hizo kwa kufuata taratibu, kanuni za Ligi Kuu kadhalika sheria 17 zinazoongoza mchezo huo ambao unapendwa na mamilioni ya watu Tanzania na dunia nzima.“Nimefanya tathmini yangu na kubaini kwamba, inawezekana kukawa na mipango ya kupanga matokeo. Nichukue nafasi hii kuzionya timu zote kutojiingiza hulo. TFF iko makini, tena makini sana na ina watu wake kila mkoa ambako michezo hiyo itafanyika, sasa basi naziasa timu kufuata taratibu, kanuni na sheria,” alisema Malinzi.
Mbali ya Malinzi, pia Bod ya Ligi nayo imetoa onyo ikisema michezo yote haina budi kuanza saa 10.00 jioni hata kama kutakuwa na hali ya mvua katika viwanja husika lengo likiwa ni kukabiliana na upangaji wa matokeo.
Baada ya michezo 29 kwa kila timu, tayari Coastal Union ya Tanga ikiwa imeaga rasmi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania 2015/16 na kwamba kuna timu tano ambazo baadhi yake (timu mbili) zikipata matokeo mabaya zitaungana na Wagosi wa Kaya kushuka daraja msimu wa 2015/16. Coastal Union yenye pointi 22 na hata ikishinda mchezo wa mwisho, haiwezi kuzifikia timu zilizo juu yake.
Timu ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15); Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao wakishinda.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Toto Africans itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Stand United, wakati JKT Ruvu mgeni wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wenyewe Kagera Sugar watamaliza na Mwadui FC watakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga wakati Mgambo wataalikwa Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ilihali African Sports ‘Wanakimanumanu’ wataifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi nyingine ya kukunja jamvi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom zitakuwa kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Yanga itakayokuwa mgeni wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine wenye presha utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48 ambayo licha ya kucheza na Coastal Union ambayo imeshuka daraja kwenye Uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi ya nne. Mtibwa Sugar ina pointi 47.
Tanzania Prisons itacheza na timu ambayo haina nafasi katika Ligi Kuu msimu huu. Presha kubwa ni kwa Simba na Azam ambazo zina tofauti ya pointi moja katika msimamo wa ligi hiyo iliyoshirikisha timu 16.
Azam FC ina pointi 63 ikishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga huku Simba inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 62. Mvutano wa Tanzania Prisons, Mtibwa ni wa nafasi ya tatu na nne hasa ukirejea kwenye zawadi za Vodacom ka timu vinara kama ilivyo kwa Azam na Simba.
Yanga ambayo imetwaa ubingwa, tayari imepewa taji na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji Jumamosi iliyopita na inachusubiri ni fedha Sh 81,345,723 wakati Azam na Simba zinawania zawadi ya mshindi wa Pili Sh 40,672,861 na Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 huku Prisons na Mtibwa Sugar zikichuana kupata zawadi ya Mshindi wa Nne ambayo ni Sh 23,241,635.
Pia timu zote zinawania zawadi ya Mchezaji Bora ambayo ni Sh 5,742,940 kiwango kinachofanana na atakachopewa Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa Bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom wakati Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 kiwango kinachofanana atakachopewa Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.

No comments:

Post a Comment