Na Immaculate Makilika, MAELEZO
Utafiti
ulofanywa mwaka 2009 na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya watoto hapa nchini
ulionyesha kuwa kuna kiwango kikubwa cha
ukatili dhidi ya watoto.
Hata
hivyo, pamoja na kuwa ni utamaduni wa kigeni kuripoti matukio mbalimbali
kupitia namba za simu na kwenye mitandao, matumizi ya namba 116 (Child
helpline) hapa nchini yamesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa
za ukatili dhidi ya watoto. Kama anavyoeleza
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, Bwana. Benedict Missari kuanzia mwezi Juni 2013 hadi mwezi Juni
2014, Wizara hiyo ilipokea jumla ya simu
tulipokea jumla ya simu 16000 kati ya hizo1659 zilielezea ukatili dhidi ya
watoto.
Kati ya simu hizo 1659,
“simu 107 zilikuwa za ‘physical violence’, 23 za ubakaji, 23 za unyanyasaji
mwingine wa kingono, 69 ni za kutelekezwa, 6 za utekwaji wa watoto, 12 zilihusu
mimba kwa watoto huku 21 ni za uuzwaji wa watoto kwenda maeneo mbalimbali mfano
Zanzibar na nchi za Uarabuni”.
Watoto walio
na umri wa chini ya miaka 18 nchini Tanzania ni sawa na asilimia 51 ya jumla ya
idadi ya wananchi wote nchini.
Matukio
mengi ya ukatili dhidi yao yamekuwa yakifanyika ama shuleni au nyumbani
yakiwemo ya kubakwa, kukeketwa, kutelekezwa, kuchomwa moto, kutumikishwa kazi
chini ya umri mdogo pamoja na ukatili mwingine wa aina hizo ambao huathiri
maendeleo ya mtoto.
Ili
kukabiliana na hali hiyo, mnamo tarehe 3 Januari, 2013 Serikali chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto kwa kushirikiana na Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya C-Sema chini ya Child
Helpline International(CHI) ilianzisha na kuendesha mtandao wa mawasiliano ya
simu katika maeneo ya majaribio (Pilot Areas) katika wilaya sita ambazo ni
Wilaya/Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu na Hai
ili kupata taarifa za ukatili wa watoto kwa kupiga simu bure kwa kutumia namba
116(Child helpline).
Mtandao huo wa
mawasiliano unatoa fursa kwa watoto na
au watu wazima kwa niaba ya watoto kutoa taarifa za ukatili unaofanywa kwa
watoto katika eneo fulani ili kuwezesha wahusika kufuatilia kwa karibu na kutoa
msaada kwa mtoto/watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili kwa kuwachukulia hatua
wahusika wa vitendo hivyo vya ukatili.
Kupokelewa kwa taarifa ukatili
dhidi ya watoto kumeweza kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
ikiwemo makampuni ya simu kwa kumwezesha mtoa taarifa kupiga simu hiyo bure,
Polisi kwenda kukamata wahusika na kuwafikisha sehemu husika kulingana na
Sheria na taratibu za nchi, na hospitali
kutoa huduma kwa wahusika wa matatizo mbalimbali yanayohitaji huduma za
kiafya.
Kuhusu uelewa wa wananchi
juu ya matumizi ya simu 116 (Child helpline), kuripoti taarifa za ukatili kwa
watoto katika maeneo yao, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Mtoto, anasema
wananchi wa Wilaya zile sita zilizo kwenye mradi wa majaribio (Wilaya/ Manispaa
za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu na Hai) wameonyesha uelewa wa kutosha na wamekua watumiaji wazuri
tu wa namba hiyo. Hali hii imepunguza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
katika maeneo yao.
Anataja sehemu ambazo
kumekua na changamoto ya matumizi ya simu katika Wilaya hizo teule kuwa ni hasa
zile sehemu za ndani zaidi ama vijijini na kusema bado kupitia wadau mbalimbali
wameweza kusaidia watoto wanaokutwa na ukatili dhidi yao.
“Kumekuwa na uelimishwaji
hadi ngazi ya kata na mtaa juu ya
kuripoti taarifa za ukatili dhidi ya watoto pamoja na ushirikiano wa kazi wa karibu kati yao na maafisa maendeleo ya jamii
na wadau wengine wakiwemo Wanasheria, Maafisa Ustawi wa Jamii, Halmashauri za
Wilaya pamoja na Taasisi za Elimu.”Anasema Missari.
Mpango
wa kuripoti taarifa za ukatili dhidi ya watoto umekuwa na mafanikio mengi
ikiwemo, kusaidia watuhumiwa wa watoto waliopata madhara mbalimbali kutokana na
ukatili dhidi yao kufikishwa katika vyombo vya sheria mfano wa kesi ya hivi
karibuni ya mtuhumiwa aliyembaka mtoto alihukumiwa kwenda kifungo cha miaka 30
gerezani na mtoto aliyetoroshwa toka Musoma kuweza kurudishwa kwa wazazi wake.
Bwana
Missari anasema “mfano tulipata taarifa kutoka kwa jirani kuwa mtoto Nasra ameafanyiwa
ukatili kwa kuwekwa ndani ya boksi kwa muda wa miaka minne huko mkoani
Morogoro. Taarifa hizo tulizifanyiakazi na kufanikiwa kumpeleka mtoto kutibiwa
katika hospitali ya Taifa Muhimbili. Bahati mbaya mtoto Nasra alifariki dunia
Juni mosi mwaka 2014.”
Mtoto
Shabani Abdalah mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la tano katika shule
ya Msingi Temeke katika Manispaa ya Temeke jijini Dar salaam ameeleza namna
alivyosaidiwa na matumizi ya namba 116.
“Kwa
vile nilisikia shuleni kuhusu namba 116, niliamua kupiga simu na kuwaeleza
namna ambavyo mlezi wangu ananitesa kwa kunifanyisha kazi ngumu, kuninyima
chakula na kunipiga mara kwa mara, nafurahi kwani nilipata msaada na aliacha
kunifanyia vitendo hivyo”
Pamoja
na hayo, fanikio kubwa kabisa la matumizi ya namba 116 katika kuripoti taarifa
za ukatili dhidi ya watoto ni kuanzishwa kwa ‘One Stop Centre’ iliyopo katika
hospitali ya Amana wilaya ya Ilala mahali
ambapo mtoto aliyefikwa na tatizo la ukatili hukuta huduma zote mahali pamoja
kwa maana ya polisi, mwanasheria, daktari pamoja maafisa maendeleo ya mtoto.
Pia,
kumekuwapo na mafunzo kuhusiana na sheria za mtoto na namna ya kulinda mtoto
ikiwa ni sambamba na kuanzishwa kwa dawati la mtoto katika vituo vya polisi
sehemu mbalimbali nchini.
Pamoja na mafanikio, Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Mtoto Missari anasema
kwamba baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika kuendesha mtandao huu ni
pamoja na kupokea simu kutoka karibia mikoa yote ya nchi tofauti na matarajio
na maandalizi yetu ya kupokea simu kutoka kwenye wilaya ambazo zina mfumo wa
ulinzi na usalama wa mtoto.
Tatizo la baadhi ya wilaya
na Kata kutokuwa na maafisa ustawi wa jamii au mfumo wa ulinzi na usalama wa
mtoto. Hili swala linatusababisha kupata kigugumizi pale ambapo unahitaji
kufanya rufaa ya kesi kwa maafisa ustawi wa jamii kwa msaada zaidi, kwani kwa
mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009, maafisa ustawi wa jamii ndio
wanajukumu la kuhakikisha usalama na ustawi mzuri wa mtoto na kuhakikisha
watoto wote wanaishi katika mazingira rafiki na salama.
Changamoto nyingine ni
uhaba wa wafanyakazi wa kupokea simu hizo hasa wakati wa usiku lakini pia kukosekana
‘call centre’ za kutosha kuhudumia nchi nzima pamoja na uelewa mdogo wa
wananchi dhidi ya mtandao.
Uanzishaji wa Mtandao wa
Mawasiliano wa Kusaidia Watoto ni mojawapo ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja
wa Mataifa wa Haki za Watoto (The UN
Convention on the Rights of the Child – UN CRC) ambao Tanzania iliusaini na
kuuridhia mara baada ya kupitishwa kwake.
Kwa kiasi kikubwa kama
mtandao utatumiwa kwa malengo haya, ni imani yangu kuwa itasaidia kupunguza
ukatili dhidi ya watoto na vile vile kuhakikisha kuwa watoto wanapata msaada
stahiki na kwa wakati.
Kwa
bahati mbaya watoto kama Ndyimiake Kiswigo mwenye umri wa miaka tisa anayesoma
darasa la pili na Subilaga Kiswigo mwenye umri wa miaka nane anayesoma darasa
la kwanza wote katika shule ya Msingi Chemuchemu katika Manispaa ya Iringa
mjini, mkoani Iringa wanasema hawajui chochote kuhusu namba 116, licha ya kuwa
wanasikia watoto wenzao wakifanyiwa vitendo vya ukatili katika mazingira yao.
Pia, mtu kama Avelina Mushi mwenye umri wa miaka
60, mkazi wa Kibosho Kirima mkoa wa Kilimanajro, wilaya ya Moshi vijijini,
anasema hawajawahi kusikia namba 116 kuhusu kutoa msaada kwa watoto, lakini anaipongeza
Serikali kwa juhudi hizi za kutafutia ufumbuzi tatizo la ukaliti na unyanyasaji
kwa watoto, huku akiitaka itoe elimu kwa wananchi wengi kuhusu matumizi ya
namba hiyo ili waweze kuwaokoa watoto katika matatizo mbalimbali.
Child
Helpline International (CHI) ni Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na
uanzishaji wa mitandao ya mawasiliano ya kusaidia watoto. Tanzania ni moja ya nchi zinazotumia
mitandao yenye kuhudumia watoto zikiwemo Afrika ya kusini, Kenya na Swaziland.
No comments:
Post a Comment