BAADA ya kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola, kuna uwezekano mkubwa kwa mabingwa wa Tanzania Bara, kupangwa
kundi moja na mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho, Etoile Sportive du
Sahel ya Tunisia katika hatua ya makundi.
Ingawa upangaji wa makundi unategemea zaidi upigaji wa kura, lakini
uwezekano uliopo ni kwamba, Yanga inaweza kuwa kwenye kundi la Etoile na wala
siyo kundi litakaloongozwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kanuni za mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF zinaeleza
kwamba, timu mbili ambazo zimefanya vizuri kwenye mashindano ya klabu ya CAF
kwa miaka mitano iliyopita, ndizo ambazo zinakuwa vinara wa makundi wakati timu
nyingine sita zilizosalia zitaungana nazo kwa njia ya kura (draw).
Kigezo kingine kinachoangaliwa ni ubora wa klabu husika katika
viwango vya CAF, ambao TP Mazembe na Etoile bado ziko juu kuliko timu zote
zilizofuzu kwa hatua ya makundi ya kombe hilo.
TP Mazembe, ambayo imeweza kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho, imefanya vizuri katika miaka iliyopita ikiwa ni pamoja na kutwaa taji
la Ligi ya Mabingwa Afrika ambalo imelitema mwaka huu.
Timu tano kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini (Maghreb), zikiwemo
mbili kutoka Morocco, zimefuzu kwenye hatua ya makundi ambazo ni mabingwa
watetezi Etoile du Sahel (Tunisia), FUS Rabat (Morocco), Kawkab Marrakech (Morocco),
MO Bejaia (Algeria), na Al Ahly Tripoli (Libya).
Yanga, TP Mazembe na Medeama ya Ghana ndizo timu pekee kutoka
nje ya ‘Uarabuni’ kufuzu kwenye hatua hiyo, ambapo zitachanganywa na ‘Waarabu
hao wa Afrika’ katika mseto ambao unaonyesha dhahiri kwamba, mashindano hayo
yametawaliwa na timu za Kaskazini mwa Afrika.
Yanga, licha ya kufungwa bao 1-0 na Sagrada Esperanca katika
mechi ya marudiano mjini Dundo, Angola jana, lakini imefuzu kufuatia ushindi
wake wa mabao 2-0 ilioupata Mei 7 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, TP Mazembe na Medeama zimefuzu kwa sharia
ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kulingana.
TP Mazembe awali ilishinda bao 1-0 dhidi ya Stade Gabesien ya
Tunisia, lakini jana ilifungwa 2-1 ugenini na kusonga mbele, wakati Medeama
jana ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika
Kusini na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3, hivyo kusonga mbele ya bao la
ugenini baada ya kufungwa 3-1 katika mechi ya kwanza.
FUS Rabat imesonga mbele kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya
Stade Malien ya Mali, ambayo katika mechi ya kwanza zilitoka suluhu mjini
Bamako.
Al-Merreikh ya Sudan, wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki
na Kati (CECAFA), wameyaaga mashindano hayo baada ya kufungwa jumla ya mabao
2-1 na Kawkab Marrakech ya Morocco licha ya kushinda mechi ya kwanza 1-0. Mechi
ya pili walifungwa 2-0.
Misr Elmaqasah, timu pekee ya Misri iliyokuwa imesalia kwenye
mashindano hayo – tena ikiingia baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa –
imeng’olewa kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare nyumbani ya 1-1 na
Al Ahly Tripoli ya Libya. Katika mechi ya kwanza mjini Tripoli, timu hizo
zilitoka suluhu.
MO Bejaia ya Algeria nayo ilitoka sare ya bao 1-1 Esperance jijini
Tunis, hivyo kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka suluhu
katika mechi ya kwanza.
Mabingwa watetezi, Etoile Sahel wamesonga mbele kwa ushindi wa
jumla ya mabao 2-1 dhidi ya CF Mounana ya Gabon. Timu hiyo licha ya kufungwa
1-0 ugenini jijini Libreville jana, lakini ushindi wake wa mabao 2-0 katika
mechi ya kwanza ulikuwa mkubwa kuiwezesha kutetea kwa muda taji lake.
Novemba 29, 2015 ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Orlando
Pirates ya Afrika Kusini bao 1-0 kupitia kwa Ammar Jemal, hivyo kupata ushindi
wa jumla ya mabao 2-1. Katika mechi ya kwanza Novemba 21, timu hizo zilifungana
1-1 mjini Johannesburg.
Utawala wa Kaskazini
Kombe la Shirikisho lina timu tano kutoka Afrika Kaskazini wakati
kwenye Ligi ya Mabingwa ziko nne, hatua inayoonyesha dhahiri kwamba, msimu huu
vikombe hivyo vinaweza kuzama Maghreb baada ya kushindikana mwaka 2015.
TP Mazembe ilivunja utawala wa timu za huko baada ya kuichapa
USM Alger ya Algeria jumla ya mabao 4-1, kwanza ikishinda 2-1 na baadaye 2-0,
huku Mtanzania Mbwana Samatta akiibuka shujaa kwa kufunga mabao muhimu ya
ushindi.
Katika Ligi ya Mabingwa mwaka huu, kuna timu za Al Ahly na
Zamalek za Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na Entente Sportif de Setif ya
Algeria.
Timu ambazo hazitoki Kaskazini ni Enyimba ya Nigeria, ASEC
Mimosas ya Ivory Coast, ZESCO United ya Zambia na AS Vita Club ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
No comments:
Post a Comment