Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce
Ndalichako akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara
hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Na Aron Msigwa - DODOMA.
Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya
kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote
walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia.Aidha,
imewataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na
mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma
yanayokuja nchini.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako wakati wa majumuisho
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya
mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha kuwa Elimu
inayotolewa katika shule, vyuo na taasisi mbalimbali inazalisha wahitimu wenye
sifa na ubora kwa maslahi ya Taifa .
Amesema katika kulitimiza hilo Serikali itawachukulia hatua
kali za kinidhamu na kisheria watendaji wote walioshiriki na wale wanaoendelea
kushiriki kwa namna moja au nyingine kukwamisha maendeleo ya elimu nchini ikiwa
ni pamoja na wale waliohusika katika udahili wa wanafunzi wasio na sifa katika
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.
"Serikali ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati
kabisa kuboresha kiwango cha elimu yetu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika
mfumo wa elimu, naomba niwahakikishie kwamba pale panapohitajika kufanyika
mabadiliko tutayafanya bila woga" Amesisitiza.
Amesema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali
za elimu hapa nchini, serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa elimu ambao
umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko hayo yatafanyika kwa
kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.
" Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa
elimu tumekubali tumekubali kwamba tuna changamoto, katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali
pa kuanzia hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono"
Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Prof.Ndalichako Amesema lengo la Serikali kupitia Wizara
yake ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa hapa nchini kwa kuendelea kutoa
wahitimu bora wanaokidhi vigezo na viwango katika soko la ajira.
Amesisitiza kuwa mkakati wa Serikali ni kuanza kuwafuatilia
wahitimu wote wasio na viwango ambao wako katika maeneo mbalimbali ya ajira
huku akisisitiza kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na kiwanda kinahitaji
malighafi nzuri ili kitoe bidhaa bora.
Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuvikagua vyuo
vyote vinavyotoa elimu ya juu kuona kama vinakidhi sifa na vigezo vya
kiutendaji ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote wanaowadanganya
wananchi na kuwapotezea muda vijana
wanaowadahili bila kuzingatia sifa.
"Wizara yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta
hii muhimu, tulichofanya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo
vingine"
Akizungumzia suala la Ada elekezi amefafanua kuwa suala
hilo linaendelea kutazamwa kwa umakini mkubwa kwa kuwashirikisha wadau husika
wa sekta hiyo kwa kulifanyia utafiti kwa kuzingatia changamoto zinazojitokeza.
Ili kukidhi matarajio ya wananchi kuhusu suala la ada
elekezi amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kwa kulifanyia utafiti
kuliangalia na madaraja ya shule binafsi na kuongeza kuwa serikali itaendelea
kutumia taratibu zilizowekwa na Ofisi ya Kamishna wa Elimu nchini.
Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu
inaendelea kulifuatilia kwa karibu suala la ada na michango mingine kwa kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara ili kuona kama michango na ada zinazotozwa
zinazingatia maslahi ya Taifa.
Prof. Ndalichako amebainisha kuwa ukaguzi utakaofanywa
katika shule hizo utajielekeza katika kuangalia uhalali wa michango inayotozwa
kwa wanafunzi ikiwemo michango ya kila muhula ya majengo, ulinzi na mingineyo
ambayo imekuwa kero kwa wananchi.
" Kama Serikali hatuwezi kukubali wananchi kuendelea
kutozwa michango ya majengo wakati kigezo kimojawapo cha mtu kuruhusiwa kutoa
elimu ni kuwa na majengo, hili halikubaliki na hatutalifumbia macho" Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Amewataka wananchi kuelewa kwamba serikali kutotoa ada
elekezi haina maana kwamba imejitoa kabisa katika kufuatilia masuala ya elimu
hapa nchini bali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha watanzania
kupata elimu bora kwa gharama nafuu.
Kuhusu ujenzi wa maabara amesema kuwa Serikali imetenga
kiasi cha shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwa
shule zote 1536 ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya maabara kote nchini.
Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali katika mwaka wa
fedha wa 2016/2017 itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii kote
nchini ili majengo ya vyuo hivyo yaweze
kutumika kuanzishia vyuo vya Ufundi Stadi VETA katika wilaya na mikoa
ili kuwapatia stadi za kazi vijana waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wao baadhi ya Wabunge waliopata nafasi ya
kuchangia wakati wa Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo wameiomba Serikali kuweka
mkazo katika usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili shule, Taasisi na vyuo vya
Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya Taifa.
Aidha, wameiomba Serikali kupitia Bajeti hiyo itenge fedha
za kutosha kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa shule, kuboresha
maslahi na kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha Mamlaka za Udhibiti wa
Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment