Frank Mvungi-MAELEZO
Taasisi
ya kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) yabaini kuwepo kwa sukari iliyofichwa
tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kwa
mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU Valentine Mlolowa Taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea
maghala yaliyopo Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.
TAKUKURU tayari imetembelea Maghala ya
mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem
yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa
sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hiyo. Ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Aidha
uchunguzi uliofanywa na Taasisi hiyo ulibaini
kuwepo kwa njama za dhati za kutouza sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa
na mfanyabiashara huyo kwani hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa
na dalili za upakiaji wa sukari hiyo ili
iweze kusambazwa.
Taarifa
hiyo imeendelea kufafanua kuwa katika eneo la Kitumbini kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
Katika
uchunguzi wake TAKUKURU pia imebaini
kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyo kwa
kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa
hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa
kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.
Kuficha
bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza
Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali
haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya
mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii.
TAKUKURU
imetoa wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha
sukari na vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote
atakayebainika kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
No comments:
Post a Comment