Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 13 March 2015

JAPAN YACHANGIA SH. MILIONI 160 SHULE YA MSINGI KAKUNI

DSC_0144
Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Kazuyoshi Matsunaga akisoma risala fupi mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kulia) wakati wa hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada wa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Awali ya Kakuni wilayani Mlele Machi 6, 2015 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).
 
*Waziri Mkuu aomba Watanzania wamuunge mkono

SERIKALI ya Japan imetoa msaada wa dola za Marekani 90,286 sawa na sh. milioni 160/- kusaidia ujenzi wa shule ya awali kwenye shule ya msingi Kakuni, iliyopo kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele, mkoa wa Katavi
Japan imetoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika shule mpya ya msingi Kakuni ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alianzisha wazo la kuijenga kama njia ya kumshukuru Mungu na kuwashukuru wananchi waliosaidia kumfikisha hapo alipo. Waziri Mkuu Pinda alisoma darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Kakuni mwaka 1957 hadi 1960.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada huo uliofanyika (Ijumaa, Machi 6, 2015) kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni na kushuhudiwa na Waziri Mkuu mwenyewe, Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Kazuyoshi Matsunaga alisema Serikali yake imeamua kutoa msaada huo kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 inayosema elimu ni haki ya kila mtoto.
Alisema sera ya elimu iliongezewa uzito na Mpango wa Kuendeleza Elimu ya Msingi Awamu ya Pili (PEDP II) ambao unasisitiza kwamba kila shule ya msingi ni lazima iwe na shule yake ya awali kama njia thabiti ya kuhimiza upatikanaji wa elimu ya awali hapa nchini.
“Mojawapo ya changamoto inayoikabili sekta ya elimu hapa Tanzania ni kukosekana kwa mazingira mazuri ya shule katika hatua za mwanzo za makuzi ya watoto wengi. Kwa mfano, kata ya Kibaoni ina shule tatu za msingi ambazo ni Kakuni, Ilalangulu na Milumba lakini hakuna shule ya awali hata moja, jambo ambalo hufanya watoto wote walundikane kwenye darasa mojawapo kwenye shule ya msingi Kakuni,” alisema.
Alisema anaamini mchango walioutoa utasaidia kuboresha viwango vya elimu ya awali katika kata ya Kibaoni. Mchango huo wa sh. milioni 160/- unatarajiwa kutumika kujenga madarasa mawili ya awali, ofisi ya walimu wa shule hiyo, eneo la michezo, bwalo dogo la chakula na jiko. “Natambua kuwa ujenzi wa shule peke yake hauinui kiwango cha elimu, bali kuongeza uandikishaji wa watoto, kuongeza walimu na kuboresha maslahi yao ni chachu nyingine muhimu katika kuinua kiwango cha elimu,” alisema.
DSC_0168
Baadhi ya watendaji ofisi ya Waziri Mkuu waliohudhuria hafla hiyo fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada na Ubalozi wa Japan wa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Awali ya Kakuni wilayani Mlele Machi 6, 2015 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam.
Utiaji saini huo ulifanywa na Kaimu Balozi huyo pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mlele, Bw. William Mwakalambile. Wengine waliokuwepo ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Ibrahim Msengi na Katibu Tawala wa mkoa huo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Waziri Mkuu Pinda aliishukuru Serikali ya Japan kwa msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi? Hakuna jambo ambalo naweza kufanya na kuisaidia jamii ya wanakijiji na kata nzima ya kwetu?,” alisema Waziri Mkuu katika mada fupi aliyoiwasilisha jana.
“Niliwaza pia kufanya ukarabati lakini nikabaini kuwa eneo la shule halitoshi kwani idadi ya wanafunzi waliopo ni kubwa kuliko eneo la shule hiyo. Hivi sasa shule ina wanafunzi wapatao 770. Madarasa yamechakaa na nyumba za walimu pia zimechakaa,” alisema.
DSC_0148
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Ibrahim Mzengi (wa kwanza kushoto) akiwa na watendaji wa mkoa wa Katavi na wilaya ya Mlele alioambatana nao kwenye hafla hiyo fupi. Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Kalobelo (wa pili kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mlele, William Mwakalambile (wa pili kulia) pamoja na Afisa Mipango wa wilaya ya Mlele, Seif Mohamed Makome (kulia).
Alisema alipeleka maombi kwenye Serikali ya Kijiji cha Kibaoni ambayo ilitoa ekari 65 kutoka eneo lililokuwa ni mashamba ya bega kwa bega na kisha akawasilisha ombi maalum kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (wakati huo) ambayo hivi sasa ni Mlele ili kuomba ushauri na usimamizi wa jumla katika kuisimamia ndoto hiyo.
Alisema aliishirikisha Halmashauri kuandaa michoro inayotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na OWM-TAMISEMI, na kuwataka waandae mapendekezo ya bajeti kwa kuzingatia taratibu za kiuhandisi na ujenzi na makisio ya awali yalikuwa sh. bilioni 1.3/-.
Alisema alipeleka barua kuomba michango kwa watu binafsi, mashirika ya umma, taasisi, mabenki na balozi mbalimbali ambao hadi sasa wamekwishamchangia sh. milioni 816.6 na dola za Marekani 210,000 na kwamba hadi sasa kwenye akaunti ya ujenzi amebakiza kiasi cha sh. milioni 182 na dola za Marekani 60,189.
“Katika kuanza zoezi la kukusanya fedha mwaka 2013, Ubalozi wa China ulikuwa wa kwanza kuitikia maombi yetu na ulitoa Dola za Marekani 200,000 ambazo zilikuwa sawa na sh. milioni 320. Pia ubalozi ukamteua mkandarasi wa barabara ya kutoka Nkasi – Kibaoni – Mpanda asaidie katika ujenzi wa shule ili kupunguza gharama,” alisema.
PG4A5435 (1)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akishuhudia utiaji saini mkataba wa msaada wa Japan wa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Awali ya Kakuni wilayani Mlele Machi 6, 2015 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam baina ya Kaimu balozi wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunaga (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mlele, William Mwakalambile (kulia). Waliosimama nyuma yao kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Ibrahim Mzengi, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Kalobelo na Kulia ni Afisa Mipango wa wilaya ya Mlele, Seif Mohamed Makome.
Hadi sasa majengo yaliyokamilika ni madarasa 14, jengo la utawala lenye ofisi za walimu na maktaba mbili (wanafunzi na walimu), jengo la TEHAMA la wanafunzi lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi ya mwalimu na jengo moja la choo lenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba sita za walimu uko kwenye hatua ya msingi. Nyumba hizo zinajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Waziri Mkuu aliwaomba Watanzania watakaoguswa na jambo hili wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani bado anakabiliwa na kazi ya kuweka umeme, maji, kujenga nyumba nane za walimu, choo kingine chenye matundu 48, bwalo na jiko, karakana nne za ufundi, vitabu na TABLETS za wanafunzi, kituo cha walimu cha mafunzo ya muda mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre), viwanja vya michezo vya kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa uvunaji maji ya mvua, mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za walinzi na uzio wa shule.
Alitaja vitu vingine ambavyo bado vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za ofisini na darasani, viti vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati ya shule ya msingi na ya awali, meza na viti vya maktaba zote mbili, meza na viti vya bwalo – shule ya msingi na shule ya awali.
DSC_0186
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akishuhudia tukio la kubadilishana hati za mkataba wa msaada baina ya Kaimu balozi wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunaga (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mlele, William Mwakalambile (kulia).
DSC_0134
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitoa neno la shukrani kwa Serikali ya Japan mara baada ya hafla ya utiaji saini wa mkataba wa msaada huo.
DSC_0215
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akifanya 'Power point presentation' ya hatua ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni aliyoijenga kutokana na michango ya wadau wa maendeleo kama kurudisha fadhila kwa jamii yake iliyomsomesha kijijini kwake.
DSC_0244
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Balozi wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunaga (kulia kwake) baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa msaada wa Japan wa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Awali ya Kakuni wilayani Mlele Machi 6, 2015 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Ibrahim Mzengi na wapili kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Kalobelo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele, William Mwakalambile.

No comments:

Post a Comment