Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua kongamano la vijana kutoka shule
na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa wiki
ya maadhimisho ya Umoja wa Mataifa unaofikisha miaka 71 tangu kuasisiwa kwake.
Maadhimisho ya hayo yanaongozwa na kaulimbiu kwa upande wa Tanzania inayosema “Jukumu
la Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.
Mwakilishi
wa Shirika Umoja wa Mataifa nchini linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria
Kiaga akimkaribisha Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kufungua kongamano la
vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18, 2016 jijini Dar es
salaam.
Mwanafunzi
Matilda Mashauri kutoka shule ya sekondari ya Gerezani akimuuliza swali Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
juu ya kusimamia maadili ya Kitanzania na kuwaelimisha wazazi namna bora ya
kusimamia malezi ya watoto wao Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa kongamano la vijana kutoka shule na
vyuo mbalimbali nchini leo jijini Dar es salaam lililoandaliwa na Shirika Umoja
wa Mataifa linalishughulikia Maendeleo (UNDP).
Na Eleuteri Mangi, WHUSM
Mataifa
wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) yanashiriki kwenye shughuli mbalimbali za
kijamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 71 ya umoja huo kinachofikia
Oktoba 24 mwaka huu baada ya kuasisiwa kwake mwaka 1945.
Tanzania
ambayo ni mwanachama hai wa UN imeungana na umoja huo kwa kushiriki katika
shughuli mbalimbali za kuunganisha nguvu za vijana na kuwajenga kimaadili,
kiuchumi ili waweze kujitambua na kujua mustakabali wao katika kujenga uchumi
wa nchi.
Kwa
kuwa vijana ni nguzo kuu ya kujenga taifa lolote duniani, Tanzania kwa kukushirikiana
Umoja wa Mataifa imeona umuhimu wa kuwashirikisha vijana kupitia kongamano la
vijana kutoka shule za sekondari na vyuo
vikuu nchini lililofanyika Oktoba 18 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es salaam.
Lengo
la kongamano hilo ni kuwashirikisha vijana kujadili namna watakavyoshiriki
katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kutafuta namna bora
ya kutatua changamoto zinazowakabili vijana nchini.
Vijana
hao wamepata fursa ya kukumbushana, kuelimishana na kubadilishana mawazo juu ya
namna bora inayowawezesha kutoa mchango wao katika masuala ya kiuchumi na
maendeleo ya kijamii nchini.
Kwa
mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Viana ya mwaka 2007, ujana ni kundi
mtambuka ambalo linajumuisha vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 ndio maana
wanaitwa ni nguvu kazi ya taifa kwa kuwa wengi wao kuanzia miaka 18, umri wa
mtu mwenye nguvu na uwezo mzuri wa kufikiri na kuchangia katika maendeleo ya
taifa kiuchumi na kijamii.
Akifungua
kongamano hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof.
Elisante Ole Gabriel amewaasa vijana
kuwa watakumbukwa kwa mchango wao watakaotoa kwa jamii na si kwa nafasi zao kwa
kuchangia uchumi na maendeleo ya nchi, hivyo ni wajibu watambue umuhimu wao kwa
taifa.
“Ikiwa
kijana huna mchango katika jamii, huna thamani yeyote, ni vema kujijengea uwezo
wa kukumbukwa kwa vitu ulivyofanya kwa taifa” alisema Prof. Ole Gabriel.
Akinukuu
maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Prof. Ole Gabriel aliwaasa
vijana kwa kusisitiza “Baba wa Taifa aliwahi kusema, ni vema tujiulize,
tumelifanyia nini taifa na si taifa limenifania nini”
Kaulimbiu
iliyoongoza kongamano hilo inawataka vijana watambue nafasi yao katika kujenga
uchumu wa nchi “Jukumu la Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na
kijamii”.
Kwa
kuthamini nafasi ya kijana katika taifa, Katibu Mkuu Profesa Ole Gabriel
amewahimiza vijana nchini kuwa na utamaduni wa kufanya kazi ili kuchangia
uchumi wa taifa na maendeleo ya jamii.
Profesa
Ole Gabriel amewahimiza vijana kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kushiriki kufanya kazi zitakazowaletea
maendeleo.
Kwa
mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) neno "haki za binadamu" limetajwa
mara saba katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambo ni ndio mwanzilishi na
unafanya kazi ya kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kuzingatia kuwa huo
ndio ufunguo huru wa Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha Serikali
zinawawajibika kwa haki za binadamu.
Kwa
miaka 15 iliyopita, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanaelezwa kufanikiwa
katika masuala mengi ambayo yalikuwa yakiathiri maisha ya watoto, vijana na
familia zao.
Mafanikio
hayo yameonekana katika kupunguza vifo vya mtoto, kuongezeka kwa idadi ya
wanafunzi wa kiume na wa kike katika shule za awali, msingi na sekondari pamoja
na vyuo vikuu, kupunguza umaskini, upatikanaji wa maji salama na chakula bora.
Pamoja
na mafanikio hayo, Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali duniani umekuja na malengo
mapya ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyowekwa Septemba ya mwaka 2015 na
viongozi wa dunia ili kuleta mageuzi ya masuala mbalimbali kwa mustakabali wa
maendeleo ya binadamu hadi ifikapo mwaka 2030.
Katika
kupanga malengo hayo, zaidi ya mamilioni ya watu walishiriki katika kuandaa
ajenda mpya ya maendeleo endelevu.
Washiriki
hao ni pamoja na Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, wasomi, mfumo wa
Umoja wa Mataifa na watu binafsi.
Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria
Kiaga anasema kuwa kila Oktoba 24, UN husherehekea kuanzishwa kwake ambapo
huandamana na shughuli mbalimbali kwa nchi wanachama pamoja na kukaa na wadau
ili kupata maoni yao yaweze kusaidia katika kuleta maendeleo.
Katika
Malengo Endelevu 17 yaliyoainishwa na Umoja wa Mataifa, malengo matatu yanampa
nafasi kijana kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Lengo
la 3 la SDGs linalenga kuhakikisha vijana wanapata maisha yenye afya na kukuza
ustawi wao kifamilia kwa kuzingatia mazingira ya asili kwa ajili ya ukuaji na
ustawi ya wanafamilia wake wote hasa watoto, kwa kuwapa ulinzi na msaada ili
waweze kupata mahitaji yao kikamilifu ndani jamii yao.
Mshiriki
wa kongamano hilo, mwananfunzi Matilda Mashauri kutoka shule ya sekondari ya
Gerezani jijini Dar es Salaam anaiomba Serikali iungane na jamii kuwaelimishe
wazazi na walezi katika kusimamia ipasavyo haki na huduma kwa watoto ili vijana
waweze kufikia malengo yao na taifa kwa ujumla.
Mawazo
hayo ya Matilda yanaendana na lengo la nne (4) SDGs ambalo linalenga kuhakikisha
umoja na usawa katika utoaji wa elimu bora pamoja na kukuza fursa sawa ya
kujifunza kwa watoto wote ambapo inatarajiwa ifikapo 2030 wasichana na wavulana
wote wapate elimu ya msingi bure, kwa usawa na ubora wenye kuleta ufanisi katika
kujifunza.
Zaidi
hayo, malengo ya maendeleo endelevu yanahakikisha wanafunzi wote wanapata
maarifa na stadi zinazohitajika kukuza maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na
haki za binadamu, usawa wa kijinsia, kukuza utamaduni wa amani, kuthamini
utamaduni na mchango wa utamaduni.
Ili
kujipambanua na mataifa mengine Prof. Ole Gabriel anasema kuwa changamoto
inayowakabili vijana wengi nchini Tanzania ni fikra ya namna ya kujiletea
maendeleo kwa kutumia utamaduni chanya wa kufikiri kwa kutumia rasilimali
zilizopo na anawatahadharisha juu ya uvamizi wa teknolojia ambayo isipotumika
vizuri itabomoa vijana ambao ni tegemeo la taifa.
“Nchi
yoyote duniani isiyokuwa na maadili imeparanganyika, tusipokuwa na utamaduni
mzuri taifa letu halitakuwa salama” alisema Prof. Ole Gabriel.
Katika
kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unadumishwa Prof. Ole Gabriel anasema kuwa
ni vema teknolojia itumike vizuri ili kuwaletea vijana na taifa maendeleo
endelevu ili kuendana na Sera ya Taifa ya Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Naye
Mjasiriamali kijana Abdul Faraji mzaliwa wa mkoani Tanga amemweleza Mgeni Rasmi
Prof. Ole Gabriel kuwa licha ya yeye kuwa na makazi yake jijini Dar es salaam,
ameamua kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa ukanda wa bahari waishio mkoani
Tanga kwa kuanzisha kituo kijulikanancho kama Vijana House ili kurasimisha kazi
zao za kiuchumi ziwe zenye tija kwa maendeleo yao.
Mawazo
ya kijana Abdul Faraji yamekuwa ni njia ya kulelekea kutekeleza lengo la tano
(5) la SDGs katika kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na
wasichana kutambua asili, hadhi na haki sawa ya wanafamilia wote kwa msingi wa uhuru,
haki na amani duniani ambapo taasisi yake itafanya kazi na vijana wote bila
kujali jinsia zao.
Akizindua
Malengo ya 17 ya Maendeleo Endelevu
(SDGs) Septemba 29, mwaka 2015 jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa
UNDP Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya
dunia, serikali zimekutana na kukubaliana kupeana malengo kwa ajili ya kila
mtu.
“Malengo
haya yatasaidia mataifa yote kushirikiana katika kuwezesha ustawi, kupunguza
matumizi na kuilinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika hilo
watashughulikia viashiria vinavyohusu maendeleo endelevu; ukuaji wa uchumi,
ustawi wa jamii na kulinda mazingira.” Amesistiza Bw. Alvaro.
Malengo
hayo 17 ya SDGs ni pamoja na kuondoa umasikini, kumaliza tatizo la njaa
duniani, afya njema na ustawi miongoni mwa jamii, utoaji elimu bora, kuwepo na usawa
wa kijinsia, upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira pamoja na uhakika
wa kuwa na nishati nafuu na salama.
Mengine
ni watu wapate kazi nzuri yenye kukuza uchumi, kukuza viwanda, kuwepo ubunifu katika
sekta mbalimbali, na kuboresha miundombinu, kupunguza ukosefu wa usawa, kuendeleza
miji na jamii, kuimarika uwajibikaji, utumiaji na uzalishaji, utunzaji wa hali
ya hewa, utunzaji wa maisha ya viumbe hai chini maji na maisha juu ya ardhi, kuwepo
amani na kuwa taasisi imara za kusimamia haki pamoja na uwepo wa ushirikiano kwenye
malengo thabiti miongoni mwa mataifa.
No comments:
Post a Comment