Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na waandishi wa habari leo mjini Bukoba
alipokuwa akitoa taarifa ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kurejesha
hali baada ya maafa ya tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba
Serikali inaendelea na
juhudi za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko ili kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za msingi za kijamii ikiwemo shule za msingi,
sekondari, barabara na vituo vya afya.
Akitoa taarifa ya
urejeshwaji wa hali baada ya tetemeko la ardhi la Septemba 10 mwaka huu kwa
waandishi wa habari leo mjini Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Kagrea Meja Jenerali
Mstaafu Salum Kijuu amesema kuwa Kamati
ya Maafa tayari imetoa vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha hali ya miundombinu
inarejea na kuwahudumia wananchi.
Aidha, Watanzania walioguswa
na janga tetemeko wametakiwa kuendelea kuwachangia Wanakagera ili kuwarejeshea
maisha yao ya kawaida.
Katika kurejesha hali,
tayari vifaa mbalimbali vimetolewa ikiwemo mabati 4,496 ya geji 30, mbao 98,
misumari ya bati kilo 110 na misumari mchanganyiko kilo 558 ili kurekebisha na
kujenga miundombinu kulingana na uharibifu uliotokea.
“Tumetoa kipaumbele
katika kurejesha miundombinu ya huduma za kijamii kwenye halmashauri za wilaya
zilizoathirika ili kamati za maafa za wilaya ziweze kukarabati miundombinu ya
kutolea huduma za kijamii kama shule za sekondari na msingi, vituo vya kutolea
huduma za afya vilivyoharibiwa na tetemeko ili huduma hizo muhimu ziweze
kurejea mara moja na kutoa huduma kwa wananchi” amesema Meja Jenerali Mstaafu
Kijuu.
Katika kuhakikisha
wananchi wananchi wanapata mahitaji muhimu, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema
kuwa Kamati ya Maafa imeendelea kugawa mahitaji kwa wananchi walioathirika na
tetemeko kadri inavyoyapokea kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mahitaji yaliyogawiwa
kwa wananchi ni pamoja na unga wa sembe kilo 4,350, sukari mifuko 1,014, mchele
kilo 103,400, maharagwe kilo 5,753, mahindi kilo 50,000 majani ya chai tani 3,
maji katoni 850, mafuta ya kula lita 249, sabuni katoni 26, mashuka 90,
mablanketi ya watu wazima na watoto 2,680, vyandarua 1,274, sare za wananfunzi
570, magodoro 694, mahema 127 na matrubali 5,760.
Kuhusu watu waliopata
majeraha, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema wamebakia majeruhi sita, ambapo katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera wamebakia majeruhi wawili, Hospitali ya
Mugana majeruhi mmoja, na Hospitali ya Rufaa ya Bugando majeruhi watatu na
majeruhi wote wanaendelea kupata huduma za matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa
amesema kuwa awali baada ya tetemeko la ardhi kulikuwa na majeruhi 440 ambapo
tayari majeruhi 434 wametibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa
na vituo mbalimbali vya afya kwenye mkoa huo.
Kwa upande wa misaada
iliyopokelewa na kamati ya maafa, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa kamati
ya maafa imepokea misaada ya mahitaji mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya
shilingi 1,094,478,950 ambayo imeendelea kugawiwa kwa wananchi kadiri
ilivyokuwa inaletwa na wananchi na wadau wengine.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa
amewashukuru wananchi pamoja na wadau mbalimbali ambao wameendelea kutuchangia
kwa fedha taslimu na hundi katika akaunti maafa inayojulikana kwa jina la
“Kamati Maafa Kagera 0152225617300 CRDB BUKOBA.” ambapo hadi Oktoba 03 mwaka
huu zimepokelewa jumla ya shilingi bilioni 3,481,069,473.43 na kuwaasa wananchi
wasikatishwe tamaa kuchangia kutokana na tukio la hivi karibuni la kufunguliwa
akaunti nyingine ambayo siyo halali na kuwahakikishia kuwa suala hilo limedhibitiwa
na hakutakuwepo na udokozi wala matumizi mabaya ya fedha zinazochangwa wala
vifaa vinavyochangiwa.
Wakati huo huo, Mkuu wa
mkoa amesema kuwa mitandao ya simu ya M-pesa 0768196669, Tigo Pesa 0718069616,
na Airtel Money 0682950009 hadi kufikia Oktoba 03 2016 zimepokelewa jumla ya
shilingi milioni 4,750,927.
Zaidi ya hayo Meja
Jenerali Mstaafu Kijuu aesema kuwa Kamati ya Maafa inaendelea kuwahudumia
wananchi walioathirika na tetemeko mkoani Kagera wanaotoa malalamiko, ushauri,
maoni na taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi waloathirika katika tetemeko.
Malalamiko yanaweza
kuletwa kwa kamati kupitia za namba za simu zilizotolewa katika Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa 0621155777 na Ofisi ya Waziri Mkuu 0621155888 na kujibiwa au kuelekezwa wanachotakiwa
kufanya ili kupata huduma ya misaada.
Kupitia namba hizo za
simu kamati imepokea jumla ya simu 82 kutoka maeneo mbalimbali na wananchi kuhudumiwa
na kupata misaada waliotarajia na kuwataka wananchi kuendelea kutumia simu hizo
ili kutatuliwa kero zao hasa kuhusu misaada.
Mkuu wa mkoa alitumia
nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote ambao waliathirika na tetemeko la ardhi na
nyumba zao kuharibiwa wahakikishe wanaanza kurejesha miundombinu ya nyumba zao
kama baadhi yao walivyokwisha kufanya wasisubiri kujengewa na kuongeza kuwa Serikali
inajenga miundombinu iliyoharibiwa ya kutolea huduma za jamii.
No comments:
Post a Comment