Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 31 August 2015

OLE KWA WATANZANIA, SHERIA YA MAKOSA YA MITANDAO KUWAFUNGA WENGI

Maxence Mello, Mkurugenzi wa kampuni ya Jamii Media wamiliki wa JamiiForums na Fikra Pevu, akifafanua madhara ya Sheria ya Makosa ya Mtandao kwa wahariri na waendhsa blogu (blogger) wakati wa warsha ya siku moja iliyofanyika kwenye Hoteli ya Kebbys, Mwenge jijini Dar es Salaam Agosti 27, 2015. (Picha na Daniel Mbega).

Maxence Mello akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa washiriki (hawapo pichani). 
James Marenga, mwanasheria kutoka Nola, akifafanua kuhusu Sheria ya Takwimu ambayo itaanza kutumika Septemba Mosi, 2015. 
Washiriki wa warsha wakifuatilia.

Na Daniel Mbega
AGOSTI 27, 2015 Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) iliwaita baadhi ya wahariri na waendesha blogu (bloggers) nchini kujadili ujio wa sheria kadhaa zinazoonekana zitawabana, si waandishi tu, bali Watanzania wote wanaotumia mitandao ya kijamii.
Sheria ambazo zitawabana watumiaji wote wa mtandao wa internet ni ile ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu, ambazo zote zimepitishwa mwaka 2015 na zinaanza kazi rasmi Septemba Mosi, 2015 huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikitangaza kiama kwa wale wanaotumia vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini.
Wakati wa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na MISA-TAN, ilielezwa kwamba hakuna atakayekuwa salama katika sheria hizo mbili, hali ambayo inaifanya Tanzania kuingia kwenye orodha ya mataifa yenye sheria kali za utumiaji wa mtandao na kuunyonga kabisa uhuru wa kupashana habari.
“Lengo la Sheria ya Makosa ya Mitandao ni kuangalia makosa kama vile kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na pia kusambaza picha za utupu za watoto na hata marehemu,” alisema Maxence Mello, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media inayoendesha jukwaa maarufu duniani la JamiiForums pamoja na tovuti ya Fikra Pevu.
Maxence, mhandisi wa ujenzi ambaye kwa sasa amezama kwenye habari hususan katika upande wa uandishi wa mitandaoni, alisema ingawa Watanzania walio wengi hawafahamu ujio wa Sheria hiyo na inawahusu kwa namna gani, lakini kwa lugha rahisi ni kuwa itamuathiri mtu yeyote anatumia mtandao wa internet kwa kutimia kifaa chochote - iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta kama simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na hivyo.
Malengo ya Sheria hii ni kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
Matumizi ya mitandao yote mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na Sheria hii.
Hiyo inamaanisha kwamba, jitihada za kuufanya mtandao wa internet kuwa wazi ili kila mtu awe na uhuru wa kuunganishwa, kuwasiliana, kuandika, kusoma, kutazama, kuzungumza, kusikiliza, kujifunza, kuunda na kubuni nazo zinafikia kikomo.
Sheria hiyo haijaeleza kuhusu kulinda uhuru wa kugundua na kuunda bila kulazimika kuomba idhini, hatua ambayo itawafanya wanasayansi chipukizi kuogopa kufanya ugunduzi wowote kwa kuhofia kuingia matatani.
Maxence alisema hakuna anayepingana kuwepo kwa sheria ya mitandao ambayo kimsingi itadhibiti baadhi ya mambo, lakini akasema tatizo kubwa lipo kwenye adhabu zinazoendana na sheria hiyo.
“Sheria ni muhimu iwepo ili kudhibiti, hata hivyo adhabu zake ni kubwa kiasi kwamba hakuna Mtanzania wa kawaida, ambaye ndiye mtumiaji mkubwa wa mitandao hii, atakayemudu kulipa faini tajwa, vinginevyo mamia kwa maelfu wataishi gerezani.
“Sheria inapoeleza kwamba utalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu, au kifungo kisichopungua miezi sita, tafsiri yake halisi ya kisheria ni kwamba unaweza ama kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni hamsini au ukatumikia kifungo cha miaka 10 jela kwa sababu imeelezwa ‘isiyopungua’ na siyo ‘isiyozidi’,” alisema Maxence.
TCRA inasema Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha taarifa nyingi za mitandao kutoaminika hadi nje ya nchi kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.
Mamlaka hiyo inasema kwamba, pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi yake si mazuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kwa watu maarufu.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia ya kusambaza picha za ngono, matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Shs. 30 milioni au kutumikia kifungo kisichopungua miaka 10 au vyote.
James Marenga, Mwanasheria kutoka taasisi ya kisheria ya Nola, akielezea Sheria ya Takwimu, alisema nayo itawapeleka wengi gerezani hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Marenga, ambaye pia ni mwanahabari na wakili wa Mahakama Kuu, alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, hakuna takwimu ambazo zitatolewa bila idhini ya mamlaka husika, na endapo mtu atatenda kosa hilo ataingia matatani.
“Kwa mfano, tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, ile tabia iliyozoeleka ya kuandika kwamba ‘fulani anaongoza’ inaminywa na sheria hii, hakuna mtu anayeruhusiwa kutangaza matokeo – hata ya awali – isipokuwa msimamizi wa uchaguzi au Tume ya Taifa ya Uchaguzi makao makuu,” alisema.
Ofisa wa MISA-TAN, G.S. Gasirigwa, alisema ni vyema wanahabari wakawa makini katika ujio wa sheria hizo, kwani tayari zimekwishapita na hakuna namna ya kuzikwepa.
“Hata tufanye nini haiwezekani, sheria zimekwishapitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lazima tuziishi, hoja ni namna gani tunaziishi,” alisema.
Imeandaliwa na www.brotherdanny.com. Simu: 0656-331974

No comments:

Post a Comment