Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 26 August 2015

ALICHOSEMA NYERERE: UBOVU WA UONGOZI NDANI YA CCM NDIO ULIOFANYA NIKAPENDEKEZA TUANZISHE VYAMA VINGI

Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake akiwa na Rais wa sasa Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo akiwa Waziri. 

(Inaendelea kutoka jana)
Tarehe 24:8: 1993, siku kumi tu baadaye, viongozi wetu wakuu wanapata ndoto nzuri zaidi, wanasarenda na kupitisha Bungeni hoja "muafaka" ya kuleta Serikali ya Tanganyika "ndani ya Muungano". Miezi miwili baadaye, Oktoba, 1993, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, inaandaa mapendekezo na kuyafikisha mbele ya Halmashauri ya Taifa, kuitaka ikubali pendekezo la Serikali la kuunda Shirikisho la Serikali Tatu. Abautani zote mbili, ya Serikali na ya Kamati Kuu, zinafanyika kana kwamba ni mambo ya kawaida tu: .Bila swali, bila maelezo!
Kukubali kufanywa vikaragosi vya viongozi ni dalili ya woga, si dalili ya heshima; na woga na heshima ni vitu viwili mbali mbali. Maadili mema hayatudai tuwaogope viongozi wetu. Na viongozi makini hupenda kupata heshima ya wananchi wenzao, lakini hawapendi kuogopwa. Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta, viongozi halisi hawapendi kuishiriki. Kujenga mazoea ya kutii viongozi hata katika mambo haramu ni dalili ya woga, ni kukaribisha udikteta.
Kamati Kuu ikishakuwa na mshikamano katika jambo lo lote, hata kama mshikamano huo ni wa bandia, na umetokana na woga, matokeo yake ni yale yale katika vikao vingine vya Chama. Ni vigumu sana kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kupinga Kamati Kuu yenye msimamo mmoja, kwa sababu zile zile zinazofanya iwe vigumu sana kwa Kamati Kuu kupinga viongozi wakuu wenye msimamo mmoja katika suala lolote. Kupinga viongozi wenye msimamo mmoja kunataka ujasiri mkubwa sana, maana anayethubutu kufanya hivyo huonekana kama mwasi au msaliti.
Ndiyo maana katika suala la utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais, nilipotambua kuwa Kamati Kuu itakuwa na msimamo mmoja katika kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba utaratibu wa sasa uendelee, niliomba nipatiwe nafasi nami nikatoe maoni yangu mbele ya kikao hicho. Inawezekana kuwa tatizo la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa kengele shingoni: taabu ni kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo. Na panya watakuwa wajinga sana wakidhani kuwa paka watajifunga au watafungana kengele shingoni!
Hatuwezi kuachia utamaduni wa woga ukawa ni mbinu au sifa mpya ya uongozi. Na sasa lazima tukiri kwamba utamaduni huu wa woga unaanza kuwa ni sehemu ya tatizo letu la kitaifa.
Nilisema awali kwamba nilionana na baadhi ya wabunge wenye hoja ya Utanganyika. Wale walipokwisha kutoa dukuduku zao kuhusu madhambi ya Serikali, niliwaambia: "Waheshimiwa wabunge, yale mliyoyasema ni sababu nzuri za kuchukua hatua za kuwadhibiti viongozi wahusika; kwa nini badala ya kufanya hivyo mnachukua hatua za kutaka kuigawa nchi yetu?" Jibu lao: "Viongozi wakisemwa wanakuwa wakali sana!" Viongozi wetu nao nilipowauliza: "Kwa nini hamkupinga hoja ya wabunge kama tulivyokuwa tumekubaliana, na badala yake mkaamua kuikubali?" Jibu lao; "Wabunge hao walipotoka kwako Msasani walikuwa wakali kama mbogo!" Na wajumbe wa Kamati Kuu ukiwauliza: "Kwa nini hamkukataa pendekezo la Serikali la kukubali hoja ya SerikaIi Tatu?" Jibu lao: “Wakubwa walikwisha kukubaliana, sisi tungeweza kufanya nini?" Hata mtu mmoja hakuweza kupaza sauti na kusema: hivi sivyo? Hii ndio demokrasia mpya na mbinu mpya ya kukabiliana na Mfumo wa Vyama Vingi? Huko ndiko kwenda na wakati?
Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoa nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM au ambacho kingekilazimisha Chama Cha Mapmduzi kusafisha uongozi wake kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao.
Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani; wala dalili zozote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Chama hili kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini, hili si jambo la kutarajia bila ya hofu na wasi wasi! Wazalendo Watanzania hawana budi wapende kuona demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi: Hii ina sura mbili.
Kwanza, ni lazima kurudisha tena uhuru na utaratibu wa kujadili masuaIa yote makubwa na kufikia uamuzi baada ya mjadala. Viongozi wetu hivi sasa wanaogopa kutumia nguvu za hoja ili kutoa maamuzi muhimu. Kwa sasa wanatumia hila zaidi kuliko hoja; vitisho kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha ya kutumia akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala. Viongozi hawa wakipewa nafasi watatumia hoja ya nguvu tu; na hawatakuwa na haja ya kutumia akili. Kichini chini baadhi yao tayari wameanza kutumia hoja ya vitisho. Na kama tukiacha utamaduni wa woga ukazagaa tutakuwa tunakaribisha udikteta.
Uhuru hauji wala haudumishwi bila kuwa tayari kulipa gharama zake; na vitu vile vyenye thamani kubwa gharama yake ni kubwa. Chama Cha Mapinduzi lazima kiendelee kujenga utaratibu na utamaduni wa kuchambua masuaIa makubwa katika mijadala, na kufikia uamuzi baada ya uchambuzi na mijadaIa ya kidemokrasia na ya wazi wazi. Na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo vyao lazima waanze kupiga vita utamaduni wa woga na fidhuli ya viongozi.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi hakina budi kitazame upya utaratibu wake wa kuchagua viongozi wake wakuu. Na muhimu zaidi na la haraka zaidi, Chama Cha Mapinduzi hakina budi kitazame upya utaratibu wake wa kuteua mgombea wake wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano. Nasema hili ni jambo muhimu na la haraka zaidi kwa sababu uchaguzi wenyewe ni mwakani tu. Hili lisipofanyika upesi na kwa makini, yanaweza yakafanyika makosa yatakayofuta kabisa uwezo wetu wa kufanya hivyo baadaye.
Nina hakika kwamba utaratibu wetu wa sasa wa kuteua mgombea kiti cha urais sasa umekwisha kupitwa na wakati. Mimi nilikuwa nikiteuliwa na HaImashauri Kuu ya Taifa baada ya kupendekezwa na Kamati Kuu bila mshindani. Na ndugu Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa katika mazingira ya siasa ambayo hayakuwa tofauti sana. Hapakuwa na washindania urais. Ni Kamati Kuu yenyewe iliyoamua ni nani wafikiriwe; na mmoja wao, nakumbuka, alikuwa hataki hata kidogo; tukalitoa jina lake.
Lakini sasa mambo ni tofauti. Washindania urais wapo, tena moto moto. Chama kinajua hivyo, na wananchi wanajua hivyo. Chama Cha Mapinduzi hakina budi kitafute utaratibu mzuri wa kuwashindanisha wataka urais hawa kwa njia ya wazi wazi. Tutafanya makosa makubwa tukikubali kuteua mgombea urais kwa kutumia mzengwe. Njia ya mzengwe ilitufaa tu wakati tulipokliwa hatuna washabiki wa urais. Na inaweza kufaa kama mnataka kumteua mwenzenu ambaye mnaamini kuwa ndiye anayefaa, lakini hapendi misukosuko ya kushindania uongozi.
Hivyo sivyo mambo yalivyo sasa. Sasa tunao washabiki, tena washabiki wa kweli kweli! Kwa hiyo hali ya sasa inataka ushindani wa wazi wazi, na ni vema Chama Cha Mapinduzi kitafute utaratibu mzuri wa kuwashindanisha hivyo. Ni muhimu zaidi kuwataka wanachama wa CCM watoe maoni yao kuhusu Rais wetu wa baadaye, kuliko kuwataka watoe maoni yao kuhusu Serikali ya Tanganyika, jambo ambalo walikuwa wala hawaIifikirii. Chama kisisite kutafuta utaratibu wa kushirikisha wanachama katika suala hili, kabla vikao vya juu havijafanya uamuzi wa mwisho.
Ni vizuri katika suala kama hili mwongozo wa awali ukatokana na wanachama wenyewe baada ya kupitiwa na wataka urais. Katika uchaguzi wa madiwani, chama kimeanza kutumia utaratibu wa kutafuta kwanza maoni ya wanachama kabla ya kuomba vikao vya juu kufanya uteuzi wa mwisho. Utaratibu huu ni muhimu zaidi kwa kutupatia mgombea urais kuliko mgombea udiwani.
Nchi yetu bado changa. Tusione haya kuendeleza taratibu ambazo zinaonekana kuwa zinafaa, na wala kubadili zile ambazo japokuwa huko nyuma zimetufaa, lakini sasa "zimepitwa na wakati." Ndivyo tulivyofanya kuhusu mfumo wa chama kimoja; tusiogope kufanya hivyo kuhusu mageuzi ya kuleta demokrasia zaidi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Inawezekana kwamba demokrasia peke yake ambayo kwa sasa itaendelea kuwa na maana kwa nchi hii wakati tunasubiri kupata mpinzani mzuri na makini nje ya CCM, ni demokrasia ndani ya CCM. Wanachama wa CCM wana wajibu wa kukitazama upya chama chao na kuona jinsi ya kuongeza demokrasia ndani yake. Wajibu huu si kwa chama chao tu, ni wajibu wa uzalendo kwa manufaa ya Tanzania nzima.
Ole wake Tanzania
Tusipoisaidia!
Niwezalo nimefanya:
Kushauri na kuonya.

Nimeonya: Tahadhari!
Nimetoa ushauri:
Nimeshatoka kitini;
Zaidi nifanye nini.

Namlilia Jalia
Atumulikie njia;
Tanzania ailinde,
Waovu wasiivunde.

Nasi tumsaidie
Yote tusimwachie!
Amina, tena Amina!
Amina tena na tena!

REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)

No comments:

Post a Comment