Esther Bulaya - Bunda Mjini
Ansbert Ngurumo - Muleba Kaskazini
Fred Mpendazoe - Kishapu
Njelu Kasaka - Lupa
Said Nkumba - Sikonge
Mwita Mwikwabe Waitara - Ukonga
Na Daniel Mbega
CHADEMA
imekifanya kile ambacho imekuwa ikituhumu kufanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM)
– upendeleo na kushindwa kukubali maoni ya wananchi walio wengi.
Chama hicho
kimewabwaga makada 12 walioshinda kura za maoni na kuwapitisha wengine ambao
walishindwa, uamuzi ambao umechukuliwa na wachambuzi wa mambo ya siasa kama wa ‘upendeleo’
na hauna tofauti na utaratibu wa CCM wa miaka yote wa kuangalia pia sifa
mbalimbali ikiwemo mchango wao kwa chama, uadilifu na uwezo katika utendaji.
Baadhi ya
waliobebwa na ‘mbeleko ya chuma’ ya Chadema ni Esther Bulaya, Fred Mpendazoe,
Njelu Kasaka, Mwita Mwikwabe Waitara, Michael Aweda na Ansbert Ngurumo ambao
wamekuwa miongoni mwa wateule 138 waliosimamishwa na chama hicho baada ya
mgawanyo wa majimbo kwa vyama vyote vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Idadi hiyo
ni asilimia 54 ya majimbo 253 ambayo umoja huo umesimamisha wagombea kati ya
majimbo yote 265 nchini.
Mgawanyo
huo unaonyesha kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kimesimamisha wagombea 99 sawa
na asilimia 29 (yakiwemo majimbo 49 ya Zanzibar), NCCR-Mageuzi yenyewe imesimamisha
wagombea 14 (sawa na asilimia 5.5) na NLD imesimamisha wagombea watatu (sawa na
asilimia 1.2).
Uchunguzi uliofanywa
na www.brotherdanny.com unaonyesha
kwamba, katika Mkoa wa Mara, Chadema imembeba aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum
(Vijana) wa CCM, Esther Bulaya kwa kumteua kugombea Jimbo la Bunda Mjini licha
ya kushindwa vibaya katika kura za maoni kwa kushika nafasi ya tatu.
Katika uchaguzi
huo wa kura za maoni Chadema, Bulaya alipata kura 37 nyuma ya mshindi Pius Masururi
aliyepata kura 61 na Magembe Makoye aliyepata kura 40. Wengine walikuwa Frank
aliyepata kura 35, Maganja (5) na Jane na Chacha Nyamhanga ambao hawakuambulia hata
kura moja.
Lakini Bulaya
alikuwa ameshinda kwenye Viti Maalum katika jimbo hilo kwa kupata kura 71 na
kuwazidi Godliver Masamaki (31), Joyce Sokombi (4), Minza Shani (3), Dk. Jane
Nyamsenda (1) na Alice Wandya (0).
Baadhi ya
wanachama wa Chadema mkoani humo walikuwa wakipinga uamuzi wa chama hicho ‘kumzawadia’
Bulaya ubunge wakati kuna watu ambao walifanya kazi kubwa kukijenga chama.
Bulaya
sasa atapambana na ‘babu’ Steven Wasira katika jimbo hilo, ambalo wachunguzi wa
siasa wanaeleza kwamba ‘lilitengenezwa’ kwa ajili yake akiwa CCM, na kuondoka
kwake kunaonekana kama ni ‘ukorofi’ ambao utakuwa mtaji wa chama chicho tawala.
Mkoani Simiyu
katika Jimbo la Kisesa, Chadema imemteua mshindi wa pili wa kura za maoni
Masanja Manani badala ya William Masanja aliyeshinda kwa kupata kura 270.
Manani yeye alipata kura 219 wakati wagombea wengine walikuwa Masunga Ndemela (47),
Sendama W. Hunge (16), Matondo Sebastian (4), Nkwabi Mahona (3), Erasto Kassanga
Tumbo na Simon Jilala walioambulia kura mbili kila mmoja.
Katika Jimbo
la Itilima mkoani humo, Martin Makondo aliyeshinda kwa kupata kura 377 amepigwa
chini na Chadema kumpitisha Martine Magile aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata
kura 153. Wagombea wengine jimboni humo walikuwa Lucas (18), Mchungaji Machimu
(10) na Bahati (8).
Katika Mkoa
wa Shinyanga, Chadema imempitisha Fred Tungu Mpendazoe kuwania Jimbo la Kishapu
licha ya kushika nafasi ya nne kwenye kura za maoni kwa kuambulia kura 11 tu
kati ya wagombea watano waliojitokeza. Mshindi wa jimbo hilo alikuwa Kahema
ambaye alipata kura 291, Edmund akapata kura 76 na Pius Singiri alipata kura
27, wakati aliyeshika nafasi ya mwisho alikuwa Dk. Bundu aliyepata kura 6.
Ni Mpendazoe huyu aliwahi kutolewa kafara na kundi la wapinga ufisadi na kutangulizwa kama chambo katika chama ambacho hakikuwa na usajili - Chama cha Jamii (CCJ) - mwaka 2010, akajiuzulu ubunge miezi michache kabla ya Bunge kuvunjwa, CCJ ilipokosa usajili akakimbilia Chadema na kugombea Jimbo la Segerea ambako alishindwa na Dk. Milton Makongoro Mahanga wa CCM. Sasa wanataka 'kumrejeshea jimbo lake'.
Mkoani Mwanza,
Chadema imempiga chini Shejamabu aliyeshinda kura za maoni katika Jimbo la
Sengerema kwa kupata kura 182 na kumpitisha mshindi wa pili, Hamis Tabasamu
aliyeambulia kura 85.
Katika Mkoa
wa Kagera, Chadema imefanya kile ambacho kilishaelezwa kupitia kwenye mitandao
ya kijamii kwamba Kamati Kuu ingempitisha mwanahabari Ansbert Ngurumo ‘iwe-isiwe’
licha ya kudondoka vibaya kwenye kura za maoni kwenye Jimbo la Muleba
Kaskazini.
Kwenye uchaguzi
wa kura za maoni, Ngurumo alipata kura 55 tu wakati Najim Kasange alishinda kwa
kupata kura 247! Mgombea mwingine, Christina Mwainunu alijitoa kabla ya
uchaguzi.
Katika
Jimbo la Lupa mkoani Mbeya, Chadema imetumia mbeleko ya chuma kumbeba
mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Edward Mlugale Kasaka licha ya kushika nafasi
ya pili kwenye kura za maoni kwa kupata kura 45 nyuma ya Miraji Hussein
aliyepata kura 65 huku Filipo Mwakibinga akipata kura 32.
Njelu, muasisi
waHoja ya Serikali ya Tanganyika Bungeni mwaka 1993, amekuwa akitangatanga
tangu aliposhindwa kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2010, ambapo alikimbilia
CUF, akarudi CCM na baadaye amekimbilia Chadema.
Kwenye
Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Chadema imepiga ‘ana-ana-do’ na kumpitisha
Mussa L. Mdede na kumwacha Sinkala Lucas kufuatia wagombea hao wawili kupata
kura 64 kila mmoja wakati wa kura za maoni. Grace Tendega, ambaye mwaka 2014
aligombea katika uchaguzi mdogo jimboni humo, alishika nafasi ya tatu kwa
kuambulia kura 27 na Mwanahamisi Muyinga akapata kura 16.
Huko
mkoani Manyara, Chadema pia imecheza tik-tak kwa kumpitisha kada wake wa
mirandaoni Michael Petro Aweda badala ya Amani Paul Gaseri.
Kura za maoni za awali zilionyesha kwamba
Gaseri alishinda kwa kupata kura 76 na Aweda akapata 75, lakini katika hali ya
kushangaza, ‘eti’ ikabidi uchaguzi urudiwe kwa wagombea hao wawili tu kwa
maelezo kwamba Katiba ya chama hicho Ibara ya 6.3.1 (c) inasema: Majina ya wagombea
wote wenye sifa zilizotakiwa yatapigiwa kura za siri na kikao kinachohusika na
mshindi atapatikana kwa uwingi wa kura usiopungua 50% ya wapiga kura halali
waliohudhuria kiako cha uchaguzi!
Ajabu ni
kwamba, kati ya waliopitishwa kuwania majimbo hayo, wapo ambao hawakufika hiyo
asilimia 50, na kuna wengine ambao walipata kura sawa.
Lakini waliporudia
kwa shinikizo na njama za wasimamizi wa uchaguzi huo jimboni humo, Aweda
akapata kura 163 na Gaseri 120.
Kwenye uchaguzi
wa awali, wagombea wengine na kura zao kwenye mabano walikuwa James Gitonge
Sombi (52), Emmanuel Darabe Tippe (39), Michael Tarimo Lorri (29), Yuda Qoryo
Gurty (16) na Paschal Awaki Side (0).
Mkoani Dar
es Salaam, Chadema iliendelea na sera zile ambazo imekuwa ikiikosoa CCM za
kuwabeba watu walioshindwa kwenye kura za maoni kwa kigezo cha kuangalia mchango
wao kwenye chama na siyo matakwa ya watu.
Kwenye Jimbo
la Ukonga, chama hicho kimempitisha Mwita Mwikwabe Waitara aliyeshika nafasi ya
pili kwa kupata kura 49 badala ya Nickson Tugara alishinda kwa kura 59. Wagombea
wengine walikuwa Elly Dallas (15), Deogratias Munishi (8), Lucas Otieno (6),
Asia Msangi na Deogratias Mramba waliopata kura tano kila mmoja na Gasto
Makwetta (1). Wengine saba hawakuambulia kura hata moja.
Aidha,
katika Jimbo la Ilala, pia wamembwaga Naomi Kaihula aliyepata kura 34 na
kumpitisha Muslim Hassanali Haiderali aliyeshika nafasi ya pili kwa kura 20.
Bi. Kaihura ndiye aliyegombea jimbo hilo mwaka 2010 na kushindwa na mgombea wa
CCM, Mussa Azzan Zungu.
Katika Mkoa
wa Pwani mambo hayakuwa na tofauti pia hasa katika Jimbo la Chalinze ambapo
mshindi wa kura za maoni, Chacha Machera aliyepata kura 69 ametemwa na nafasi
yake kuchukuliwa na aliyekuwa mshindi wa pili, Mathayo Torongey aliyepata kura 53.
Torongey ndiye aliyegombea kwenye uchaguzi mdogo jimboni humo mwaka 2014 na
kushindwa na Ridhiwani Kikwete wa CCM.
Huko
Morogoro katika Jimbo la Mvomero, Chadema imempitisha mshindi wa pili wa kura
za maoni Oswald Mlay aliyepata kura 181 badala ya Owden aliyepata kura 185.
(Imeandaliwa
na www.brotherdanny.com. Simu:
0656-331974)
No comments:
Post a Comment