Twitter Buzz
....
...
IMETOSHA!
Featured post
KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO
Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...
Sunday, 23 August 2015
ALICHOSEMA NYERERE: VIONGOZI WA SERIKALI SI WAJINGA KUIKUBALI HOJA YA TANGANYIKA, WANAOGOPA KUWAUDHI WAZANZIBARI!
(Inaendelea kutoka jana)
Kwa kuwa tabia ya Serikali ya Zanzibar ya kupuuza vifungu fulani vya Katiba ya Muungano ndiyo iliyokera watu wengi na hatimaye ikazua hoja ya kutaka Serikali ya Tanganyika, nilidhani kuwa baada ya Zanzibar kukiri kosa lake na kutoka katika OIC, Serikali zote mbili zingekaa pamoja na kutazama sehemu nyingine za Katiba zinazopuuzwa ama na Serikali ya Zanzibar au Serikali ya Muungano.
Badala yake Serikali ya Muungano ikiendekeza Utanganyika, na ikakubali hoja ya Serikali Tatu. Sasa naamini kuwa Serikali ya Muungano haiwezi tena kufuatilia kwa makini mazungumzo yake na Serikali ya Zanzibar kuhusu Katiba ya Nchi yetu. Kwa sababu zifuatazo:
Sababu moja kubwa iliyofanya Viongozi wetu wasitake kuwaudhi "Wazanzibari" katika suala la OIC na uchaguzi wa Makamu wa Rais, ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi ye yote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi "Wazanzibari" ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia Ndiyo maana Viongozi wa Zanzibar walipoomba nia yao ya kuingia katika OIC izungurnzwe na Kamati Kuu, na baadaye na Halmashauri Kuu ya Taifa, Viongozi wetu waheshimiwa hawakupenda hata kidogo suala hilo lizungumzwe. Walijua kuwa Zanzibar haiwezi kuingia katika OIC bila kuvunja Katiba ya Nchi yetu; na kwamba suala hilo Iikizungumzwa katika vikao hivyo vya Chama, wako Viongozi watakaolipinga, na wataka urais watapata tatizo: Kupinga au kutopinga, litakuwa suala gumu! Kwa hiyo wakamshauri Rais lisizungumzwe katika vikao vya Chama, ila yeye mwenyewe achukue jukumu la kulizungumza na Viongozi wa Zanzibar, Suala likiwa gumu, usimsaidie Rais, mtupie!
Zanzibar wakaingia katika OIC. Viongozi wetu wakafanya kila njia ya kufanya kitendo hicho kisijulikane, au baadaye kushindwa kukificha kipuuzwe. Haikuwezekana. Kikafichuliwa, na ngoma zikaanza. Hatimaye "Watanganyika" wakachoka na wakaanza kudai Serikali ya Tanganyika. Kwa mtaka urais hii ilikuwa balaa mpya; maana si 'Wazanzibari" peke yao ambao wanazo kura za uteuzi wa wagombea urais na baadaye uchaguzi venyewe;
"Watanganyika" nao wanazo, tena nyingi zaidi. Kwa Kizungu hali hii huitwa "dilemma"; ni utatuzi wa uamuzi, kama penye njia panda:
Kifo cha maji kushoto,
Kulia kifo cha moto:
Kukubali, kukataa,
Kila moja ni balaa!
Kote uko hatarini,
Hujui ufanye nini.
Kwa hiyo Waziri Mkuu alipomwambia Rais kwamba hoja ya Serikali Tatu ikijadiliwa Bungeni, yeye mwenyewe atakuwa na utatuzi wa uamuzi, alikuwa anajisemea kweli yake. Alikuwa katika hali hii ya "dilemma". Baadaye, kama tunavyojua, alipoambiwa kuwa asipokubaliana na wenzake ataachwa katika mataa, aliamua kusarenda na wote wakaunga mkono hoja ya Utanganyika.
Hawa si watu wajinga, na wala si wapumbavu; wanajua wafanyalo. Wamefanya uamuzi huu wakijua matokeo yake. Kwa hawa sasa, makosa ya "Wazanzibari", yawe ya kuvunja Katiba au ya aina nyingine, kwao sasa ni faraja; ni hoja ya kudai Utanganyika. Hawa hawawezi tena kutaka makosa hayo yazungumzwe, na yasahihishwe; maana yakisahihishwa, kama lilivyosahihishwa lile la OIC, msingi wale wa hoja yao utabomoka. Katika hili, "Wazanzibari" na "Watanganyika", ni mbuya wakuu; ni washiriki na wabia kwenye mradi ule ule wa kutaka kuvunja Tanzania.
Lakini hata kama wangekuwapo mawaziri ambao si "Watanganyika", bali ni Watanzania halisi wanaopenda kukaa na Watanzania wenzao wa Visiwani ili kuzungumza masuala ya Katiba, hawawezi kufanya hivyo chini ya uongozi wa sasa wa Serikali ya Muungano. Katiba inayozungumzwa ni Katiba hii ya sasa, ya muundo wa Serikali Mbili. Hoja ya Utanganyika ilipoletwa Bungeni Serikali ilikuwa tayari imeteua, au inakusudia kuteua, Kamati ya kutazama migogoro ya Katiba iliyopo hivi sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, na kufanya mapendekezo ya kuiondoa.
Tulitazamia kuwa serikali ya Muungano itapinga hoja ya Utanganyika, na kuwaarifu Wabunge kwamba Kamati hiyo itapokamilisha kazi yake Serikali itafikisha mapendekezo yake Bungeni. Badala ya kufanya hivyo, Serikali ya Muungano ikaamua kuwa mfumo wa Serikali Mbili haufai, kinachofaa ni mfumo wa Serikali Tatu. Hivi sasa sera ya Serikali ya Muungano ni muundo wa Serikali Tatu.
Itawezekanaje Serikali hiyo hiyo ikae chini na Serikali ya Zanzibar kuzungumzia umuhimu wa kutii, au jinsi ya kurekebisha muundo wa Serikali Mbili? Kwao Katiba hiyo inachongojea ni kufutwa tu. Mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Shellukindo na wenzake hayana maana tena kwa Serikali hii. Serikali ya sasa inachosubiri na inachokishughulikia ni Shirikisho la Serikali Tatu- kwa kweli kufa na kuzikwa kwa Tanzania. Hawana uhalali, wala uwezo, wala nia ya kuzungumza Muungano wa Serikali Mbili. Kwa kweli jambo moja ambalo waheshimiwa hawa wamefaulu ni kufanya watu waache kabisa kuzungumza Katiba ya sasa na mambo mengine yale muhimu, na wabaki kumkimbiza sungura wa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano".
Maadamu matatizo halisi ya Muungano hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa Bara na Visiwani, wanaopenda kuitumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya hivyo. Na wale, wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na hiyo inawafanya hata watu wasio na nia mbaya, ila ni wajinga tu, waamini kuwa inafaa wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania imevunjika na tumeachwa katika mataa! Anayedhani kuwa viongozi wetu ni wajinga yafaa akachunguzwe akili zake! Wanajua wafanyalo.
Nimesema awali kwamba "Wazanzibari" na "Watanganyika" ni marafiki wakuu. Matendo ya "Wazanzibari" ni kisingizio kizuri cha matendo ya "Watanganyika": na matendo ya "Utanganyika" ni kichocheo cha ukabila wa upande wa pili. Wenyewe wanauita "Utaifa", na ni sawa maana ni wa kupinga Utanzania. Serikali yenye msimamo wa Utanganyika haiwezi kukaa na Serikali ya Zanzibar kuzungumza katiba hii ya Serikali Mbili. Hilo linaweza kufanywa na Serikali mpya y a Jamhuri ya Muungano: Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo.
Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo. Selikali ya sasa haina uhalali wala uwezo wala nia ya kuizungumza, ukiacha mazungumzo ya kuitia maji ili kuwafurahisha "Wazanzibari", au kuifuta ili tulete Shirikisho la Serikali Tatu na hivyo kuwafurahisha "Watanganyika".
Itaendelea kesho...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment