Mtwara. Kundi la watu wasiofahamika wamevamia na kubomoa nyumba ya mgombea ubunge wa jimbo jipya la Nanyamba kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) lililogawanywa kutoka Jimbo la Mtwara Vijijini, Twahil Saidi kwa kile kilichodaiwa kuwa amekihujumu chama hicho baada ya kushindwa kurejesha fomu.
Hali hiyo imempa fursa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimboni humo kuwa mgombea pekee.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku. Inadaiwa kuwa mgombea huyo alipotafutwa na viongozi wa chama hicho juzi baada ya kushindwa kutokea katika ofisi za halmashauri alikopaswa kufika kurejesha fomu, hakupatikana na simu zake za kiganjani inadaiwa pia kuwa zilikuwa zimezimwa.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wafuasi wa CUF, walidai kuwa hatua hiyo imewapunguzia thamani ya chama chao, lakini wataendelea kumtafuta ili kujua sababu iliyomfanya ashindwe kurejesha fomu.
Mkazi wa Nanyamba, Ally Jumbe alisema tukio la kubomolewa kwa nyumba hiyo huenda likahusishwa na kushindwa kurejesha fomu. “Tunahisi labda waliofanya hivi ni wanachama wenzake na wale wa vyama shirika vya Ukawa. Lakini mpaka tunapozungumza sasa, hakuna mtu aliyefahamika.”
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Nanyamba, Osca N’gitu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mji wa Nanyamba, alisema kati ya wagombea watatu waliochukua fomu za kuomba kugombea nafasi ya ubunge, ni mmoja kupitia CCM ndiye aliyerejesha fomu.
“Tulikuwa na wagombea watatu kutoka CUF, Chadema na CCM na kazi ya urudishaji fomu ilikuwa jana (juzi), ilianza saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni na mpaka inamalizika ni mgombea mmoja tu wa CCM, Abdallah Chikota ndiye aliyefanikiwa kurejesha fomu zake,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo tuliendelea na utaratibu mwingine kama sheria zinavyoelekeza lakini leo (jana) asubuhi nikapata taarifa kuwa nyumba ya mgombea aliyechukua fomu kupitia CUF imebomolewa na watu wasiojulikana. Nilienda eneo hilo na kufanya kikao na viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, kata na viongozi wa CUF, kimsingi nimewaomba kufanya utafiti wa kina ili kubaini waliohusika na tukio hilo na pili, kubaini ni kipi kilichomsibu mgombea huyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe alipotafutwa alisema yuko nje ya ofisi ila ana taarifa ya kuwapo kwa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment