Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Ndugu Idrisa
Kitwana wakati wa kilele cha sherehe za siku ya Kimkazi (Kizimkaziday) kwenye
kijiji cha Kizimkazi Mkunguni.
Mashindano ya kuvuta kamba
Vijana
wa Kiume wakishindana kukuna nazi ikiwa sehemu ya mashindano ya Siku ya
Kizimkazi (Kizimkazi Day).
Wakina Mama wakishindana kufunga kamba kwenye kilele cha
sherehe za Kizimkazi.
......................................................
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahimiza
wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kuunga mkono jitihada zinazofanywa na
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika mapambano dhidi ya rushwa,ufisadi kama hatua ya kukomesha tabia
hiyo ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 13-Aug-16 wakati anahitimisha kilele cha sikukuuu ya Kizimkazi
katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni wilayani ya Kusini Unguja – Zanzibar ambaye
yeye ni mwasisi wa sikukuu hiyo ambayo inatumiwa na wakazi wa maeneo hayo kufanya
michezo mbalimbali ya jadi pamoja na kujadili na kuweka mipango na mikakati ya
kujiletea maendeleo kwa ushirikiano na viongozi wao.
Makamu
wa Rais amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa
watendaji wanaorudisha nyuma maendeleo ya wananchi ikiwemo ubadhirifu wa fedha
za umma ili kukomesha tabia hiyo.
Amesema
kuwa ili wananchi waweze kupata maendeleo ya haraka ni muhimu wananchi
wakaimarisha ushirikiano miongoni mwao katika kubaini changamoto zinazowakabili
na kushirikiane na viongozi wao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Makamu
wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan amesema yeye kama kiongozi wa kwanza kupata wadhifa
huo kutoka kwenye kijiji cha Kizimkazi - Zanzibar ataendelea kushirikiana
wananchi hao kutatua matatizo yanayowakabili wananchi hao ikiwemo tatizo la
upatikanaji wa maji.
Makamu
wa Rais pia amehimiza wananchi wa Kizimkazi kutafuta eneo haraka kwa ajili ya
ujenzi wa shule ya awali ambayo bado ni tatizo kubwa katika eneo hilo ili aweza
kuwasaidia katika ujenzi wake kama hatua ya kuondoa kero ya watoto kushindwa kupata
elimu ya awali.
Katika
Risala maalum ya wananchi wa kijiji cha Kizimkazi na Katibu wa Sherehe hizo Said
Ramadhani Mgeni kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wamewapongeza viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada wanazofanya za
ukusanyaji wa mapato ya serikali na wamesema wanaimani kubwa kuwa fedha zinazopatikana
zitatumika katika kuinua uchumi na kujenga ustawi wa Jamii bora wananchi.
Wananchi
hao wameahidi kuwa watadumisha na kuimarisha ushirikiano kati yao na serikali
hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Baadhi
ya Viongozi wa wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja waliopata nafasi ya kuzungumza
katika hafla hiyo ya hutimisha sikukuu ya wakizimkazi wamewaomba wananchi
kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao.
Katika kilele cha sherehe hizo Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikabidhi zawadi
mbalimbali kwa washindi ambao walishiriki kwenye mashindano ya siku ya
Kizimkazi zikiwemo fedha taslimu.
No comments:
Post a Comment