PRESS RELEASE
BASATA
YAMFUNGULIA NAY WA MITEGO, YAMWEKA KWENYE UANGALIZI
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungulia Msanii
wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego kuendelea
na shughuli za Sanaa baada ya kuwa ametekeleza adhabu (maagizo) zote alizopewa kama
masharti ya kumfungulia.
Aidha, BASATA kama mlezi wa wasanii linamfungulia
kufuatia yeye mwenyewe (Nay wa Mitego) kujutia na kukiri kwamba amejifunza na
yuko tayari kubadilika na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya
Hata hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na
shughuli za Sanaa Baraza linamweka kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama
sehemu ya kuhakikisha anaendesha shughuli za Sanaa kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu sambamba na kuzingatia maadili katika kazi zake.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 27/07/2016 Baraza
lilimfungia Msanii Nay wa Mitego kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka
kutekeleza maagizo yafuatayo:
1.
Kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa
2.
Kulipa faini ya shilingi milioni moja
(1,000,000/-)
3.
Kuomba radhi watanzania kupitia mkutano na
waandishi wa habari na kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii
4.
Kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale
Kati’ ili ubebe maudhui yenye
maadili
Msanii Nay wa Mitego ametekeleza adhabu zote tajwa
hapo juu. Leo hii tunamkabidhi rasmi cheti chake cha usajili na kibali cha BASATA.
Hata hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara
mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’ Baraza bado halijaridhishwa na marekebisho hayo
hivyo linaendelea kuufungia wimbo huu hadi hapo litakapojiridhisha umekidhi
vigezo vya kimaadili.
Katika kikao na Msanii Nay wa Mitego cha kufanya
tathimini ya utekelezaji wa adhabu yake kilichofanyika tarehe 12/08/2016 Ofisi
za BASATA ameagizwa kuendelea kuufanyia marekebisho wimbo wake huo kama bado
anaona anauhitaji.
Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na
watanzania kwa ujumla kuacha kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa
vinginevyo. Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha
habari kitakachokiuka agizo hili.
Aidha, katika kikao hicho cha tathimini ilibainika
kwamba Msanii Nay wa Mitego kwa taarifa potofu alizopewa alipanda Jukwaani
kwenye tamasha la Mwendo Kasi la tarehe 30/07/2016 akiwa katika adhabu. Kwa
kosa hili ameandika barua ya kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za
kuchukua kwa waandaaji wa tamasha hili.
Baraza linatoa wito kwa wasanii kuendelea
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za Sanaa sambamba
na kuhakikisha wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili kuepuka
matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa sana.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment