Hayati Aboud Jumbe Mwinyi
Na Daniel Mbega
ABOUD
Jumbe Mwinyi (96) hatunaye tena. Naam, rais huyo wa pili wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar amefariki dunia nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni jijini
Dar es Salaam na amefariki akiwa mwingi wa siku.
Taarifa zaidi bado hazitatolewa, hivyo haijulikani kama kiongozi huyo aliyepata pia
kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati wa awamu ya kwanza atazikwa kiserikali au
la.
Hiyo
inatokana na wasia aliopata kuutoa mwenyewe mwaka 2000 baada ya kifo cha Rais
mwingine mstaafu wa nne wa Zanzibar, Idris Abdul-Wakil Nombe, aliyefariki Machi
15, 2000.
Katika
wasia huo, inaelezwa kwamba Alhaj Jumbe alieleza kwamba pindi mauti
yatakapomfika asingependa kuona bendi wala mizinga ikipigwa, na kwamba jeneza
lake lisifunikwe kwa bendera ya Taifa wala ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
"Sitaki
bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote lingine lenye hata chembe
ya kufuru,"
sehemu ya wasia huo iliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari huku akisisitiza
kwamba angependa kuzikwa Kiislamu: "Mimi Aboud Jumbe Mwinyi, namshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunibariki kuzaliwa ndani ya Uislamu na namuomba aniruzuku
kufa na kufufuliwa ndani ya Uislamu".
"Ni
matumaini yangu kwamba kama Mwenye Enzi Mungu alivyonirehemu kuwa Muislamu,
atanijaalia nikifa kukoshwa, kuvishwa sanda, kutiwa katika jeneza, kusaliwa na
kuzikwa kwa mujibu wa sunna ya Mtume Muhammad (s.a.w.).
"Nikiwa hai, dhamana ya vitendo vyangu inaniangukia mimi
mwenyewe, nikifa dhamana ikiwa vitendo vyema au vibaya nitakavyofanyiwa
itawaangukia waandalizi, watendaji na wenye kushiriki katika vitendo
hivyo", anadaiwa kusisitiza katika wasia huo uliosainiwa na Msaidizi wake
Bwana Abubakar.
Wasia huo
anadaiwa aliutoa mbele ya Mufti wa Zanzibar, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Naibu
Kadhi Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Sharrif Juneid, Masheikh wengine na wanawe.
Jumbe
ni nani?
Alhaj
Aboud Jumbe Mwinyi alizaliwa Juni 14, 1920 mjini Juba, Sudan Kusini. Alishika nafasi
mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na ndani ya Afro-Shiraz Party (ASP) na yeye na Mwalimu
Julius Nyerere ndio walioviunganisha vyama vya ASP na Tanu na kuzaliwa CCM
Februari 5, 1977.
Baada
ya kifo cha Sheikh Abeid Amaan Karume Aprili 7, 1972 yeye ndiye aliyeteuliwa
kuwa Rais wa SMZ na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati huo huo akiwa
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata baada ya
kuzaliwa kwa CCM, yeye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Yeye
ndiye aliyesimamia kupatikana kwa Katiba ya kwanza ya Zanzibar mwaka 1979 baada
ya Mapinduzi ya 1964.
Jumbe
alikuwa Rais wa SMZ kuanzia Aprili 11, 1972 hadi Januari 30, 1984 alipovuliwa
vyeo vyote mjini Dodoma.
Lakini
unapozungumzia kuhusu Muungano wa Tanzania, lazima pia umzungumzie Alhaj Aboud
Jumbe ambaye alikuwa sehemu kubwa ya utawala wa Visiwa vya Zanibar kwa
takribani miaka 12.
Jumbe
ana historia ndefu ya siasa za Visiwa hivyo, na mtazamo wake unawafanya mpaka
leo wengi wajiulize kama ni shujaa, mpinga Muungano ama mtu aliyekuwa amekata
tamaa.
Tukio
la kujiuzulu kwake kwa shinikizo miaka 32 iliyopita linaweza kuwa ni historia
nyingine ngumu kuelezeka kwa siasa za Tanzania. Nakumbuka hata mimi, ambaye
wakati huo nilikuwa shuleni, sikuweza kuelewa kiini hasa cha kujiuzulu kwa
kiongozi huyo mkubwa kabisa nchini.
Kwa
kipindi ambacho nchi nyingi zilikuwa ndiyo kwanza zimetoka katika makucha ya
ukoloni huku zikipigania kujenga chumi zao changa, tukio la kujiuzulu kiongozi
lilionekana geni sana, ingawa huko nyuma tulikuwa tumeshuhudia viongozi kadhaa
wakijiuzulu, akiwemo Alhaj Ally Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu mwaka 1978
kufuatia wimbi la mauaji ya watu, hasa vikongwe, kule Shinyanga.
Hata
hivyo, suala la kujiuzulu kwa Jumbe halikuweza kujadiliwa mitaani kwa kipindi
kile, tofauti pengine na kipindi hiki ambapo watu wangeweza hata kutoa hoja zao
nyingi kuhusiana na kiini cha kujiuzulu kwake.
Kwa
kipindi ambacho ilikuwa vigumu kunyoosha kidole hata kwa mtendaji wa kijiji,
hakika ingekuwa vigumu kama kuuhamisha Mlima Kilimanjaro kwenda Dodoma kuhoji
uamuzi wa kiongozi wa juu kama rais.
Jambo
la msingi kuhusiana na kujiuzulu kwake ni kutambua kwamba Jumbe alitaka, na
hata kesho angetaka, kuona Nyaraka za Muungano zinapitiwa upya ili kuleta usawa
wa pande zote mbili zilizounda Muungano huo, Bara na Visiwani.
Ingawa
yeye pia alishiriki katika maandalizi ya Nyaraka hizo, lakini hakuwa na mamlaka
ya juu kipindi hicho kwa vile alikuwa chini ya mtu, na miaka takribani 20
baadaye aliona kuna haja ya kufanya mapitio mapya kuona Zanzibar inapewa
heshima yake katika baadhi ya masuala yaliyoonekana kuingiliwa na Serikali ya
Muungano.
Ndiyo
maana hata katika kitabu chake cha Tanganyika and Zanzibar: The Partner-ship
alichokitoa mwaka 1994, miaka 10 baada ya kujizulu kwake, alielezea kwa kirefu
ni kwanini alitaka yafanyike mapitio ya Nyaraka za Muungano.
Anasema
alimweleza Mwalimu Nyerere wakati wa kuadhimisha miaka 20 ya Mapinduzi Januari
12, 1984 kwamba kulikuwa na kero ambazo Wazanzibari waliona zilistahili
kuzungumzwa ili kuimarisha Muungano huo.
Alikuwa
amejiandaa kuelezea kwa kirefu kero hizo kwenye vikao husika, lakini kabla ya
hapo akaandaa waraka uliopaswa kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere.
Kwa kuwa waraka ule ulikuwa umeandikwa kwa mkono, tena kwa lugha ya Kiingereza,
alimpa mtu kuuchapa. Ukapotea katika mazingira ya kutatanisha.
Lakini
ajabu ni kwamba, siku chache baadaye aliitwa Ikulu kwa Mwalimu Nyerere na
alipokwenda akashangaa kuukuta waraka ule ule aliouandika mwenyewe kwa mkono
wake ukiwa mkononi mwa Nyerere! Namna ulivyofika mimi, wewe na hata yeye
mwenyewe hatujui, lakini Mwalimu angekuwa hai leo angeweza kutueleza
aliupataje, kama tungekuwa na haja ya kujua hilo.
Na
kwa vile tayari Jumbe alikuwa ameonyesha nia yake ya kujiuzulu wadhifa wa Rais
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu alimwambia
kwamba kama isingekuwa kwa waraka aliokuwa nao mkononi, katu asingekubali
kujiuzulu kwake, lakini kwa yale aliyokuwa ameyaainisha kuhusu Muungano, naye
alikuwa radhi kuona anajiuzulu.
Ndipo
Januari 30, 1984, katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kule Dodoma, akaamua
kujiuzulu nyadhifa hizo. Ali Hassan Mwinyi, mtu aliyekuwa akiiunga mkono
Tanzania Bara, akachukua madaraka na watu kadhaa walioonekana kuwa wapinzani
wakakamatwa.
Mwinyi
akaanzisha mfumo wa usawa Visiwani na Bara kabla hajawa rais wa Muungano mwaka
1985 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka huku Zanzibar ikiongozwa na
Idris Abdul Wakil Nombe. Mwaka 1990 Dk. Salmin Amour Juma akachaguliwa Rais wa
Zanzibar; akarejea tena madarakani katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi
mwaka 1995 ambao unadaiwa haukuwa huru na wa haki.
Aboud
Jumbe alipochukua urais baada ya mauaji ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume
mwaka 1972, jamii yote ilitegemea kwamba mambo ya kale yalikuwa yamefikia
kikomo.
Na
kwa kiasi fulani ndivyo ilivyokuwa, kwani utawala wake ulilegeza baadhi ya
mambo kuliko ule uliotangulia, lakini kwa kuwa alikuwa chini ya Baraza la
Mapinduzi, alipaswa kutekeleza baadhi ya sera ngumu zilizokuwepo, pale
ilipobidi, kwa utashi wa washirika wake katika uongozi.
Wazanzibari
wanakumbuka kwamba mlongo mmoja wa utawala wake ulitawaliwa na hali ya Zanzibar
kuegemea zaidi Bara na mwaka 1977 akaongoza muungano wa vyama vya Afro-Shiraz
na kile cha Tanganyika African National Union (TANU) cha Bara kuzaa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), chama ambacho bado kinaendelea kushika hatamu za uongozi hata
leo.
Lakini
kwa kiasi kikubwa, chini ya Jumbe watu walikuwa na uhuru na waliweza kusafiri
ulimwenguni bila matatizo makubwa tofauti na serikali ya ‘mkono wa chuma’ ya
hayati Karume. Hali hii ikamfanya kuwa kipenzi cha Wazanzibari wengi.
Jumbe
huyu pia akafungua taasisi mbalimbali za elimu Tanzania Bara kwa ajili ya
Wazanzibari waliopenda kuchukua elimu ya juu. Hali hii iliwawezesha Wazanzibari
kufika mbali zaidi kielimu badala ya kusomea ualimu, taaluma pekee ambayo
walikuwa na uwezo wa kuipata.
Siku
za nyuma, nafasi za uongozi serikalini zilikuwa zikitolewa kwa watu waliokuwa
kwenye mfumo wa chama tu, na zaidi ya kazi ya ualimu hakukuwa na uwezekano
wowote wa watu kupata elimu ya juu zaidi.
Mnamo
mwaka 1979, Jumbe aliweka historia kwa kufungua taasisi ya kwanza ya
kidemokrasia, Baraza la Wawakilishi, lakini wajumbe wa baraza hilo walikuwa
wakiteuliwa badala ya kuchaguliwa na wananchi wenyewe. Pia alifungua utawala
wake kwa watu, ambao wangeweza kuwa pembeni kama kanuni ngumu za mapinduzi
zingezingatiwa kama ilivyokuwa awali.
Hatua
hii, ambayo baadaye alijikuta akiijutia, ndiyo iliyokuwa chanzo cha kuanguka
kwake. Alikuwa haelewani na wale waliojulikana kama ‘Kamati ya Watu 14’ ambayo
iliwahusisha watu wengi walioshiriki kwenye Mapinduzi. Ushawishi wao ulianza
kupungua na madaraka yao yakaanza kuhojiwa.
Katika
jaribio lake la kutaka kuokoa jahazi kutokana na matatizo hayo akawatema
wajumbe wengi katika serikali yake na kufanya jaribio la kujitenga kutoka
katika serikali moja kuu kwa Tanzania nzima. Lakini mwaka 1984 akalazimishwa na
Kamati Kuu ya CCM kujiuzulu.
Hatua
ya kujiuzulu kwake, kwa mwanamapinduzi inaweza kuchukuliwa kuwa ya kishujaa
kutokana na hoja zile alizokuwa akizitetea. Hakujutia uamuzi wake, ingawa
alisikitishwa kutokana na yale aliyokuwa ameyaainisha kushindwa kuwafikia
wananchi wengi, ambao ni dhahiri hata leo hii hawajui ni kipi hasa alichokuwa
akikipigia kelele.
‘Kwa shujaa huenda kilio,
kwa mwoga huenda kicheko’, ndivyo Waswahili wasemavyo. Wale ambao hatukumwelewa Jumbe
wakati huo tulimuona kama mtu aliyechanganyikiwa kueleza kasoro hizo ambazo
hazikuwa na mantiki yoyote kwa kipindi hicho huku tukiendelea kuimba na
kuzinadi sifa mbalimbali za viongozi wa chama na serikali.
Lakini
leo hii yale ambayo alikuwa akiyasema Jumbe na kuyapigania tumeyaona Zanzibar.
Kero za Muungano zimekuwa nyingi mno kiasi cha kuifanya hali ya amani Visiwani
kuwa tete tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ambapo baadhi ya
wachunguzi wa masuala ya siasa wanadai kura ziliibwa ili Chama cha Wananchi
(CUF) kisitawale.
Kero
hizo ndizo zinazozidi kujenga ufa mkubwa hata ndani ya CCM Visiwani humo, na
ingawa viongozi wake wanajitahidi kuficha, ukweli bado unaendelea kubaki pale
pale kwamba kuna tatizo, tena kubwa.
Ujio
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ukaibua mapya, kwa
sababu ulikuja na mapendekezo ambayo Jumbe alikuwa ameyaeleza – hata kwenye
kitabu chake. Na hoja ya kuwa na serikali tatu ikachukua nafasi.
Pengine
lingekuwa jambo la busara sasa kumpa heshima ya ushujaa Alhaj Jumbe kwa yale
yote aliyoyatenda enzi za utawala wake, pia hata kwa mawazo yake aliyokuwa
ameyaandika kwenye waraka ambao ulimfikia mhusika hata kabla ya kuusaini
mwenyewe.
Viongozi
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Muungano hawapaswi kupuuza kero
hizo kwa misingi ya kulinda chama, kwa sababu kama hazikutatuliwa siyo tu
zitauvunja Muungano wenyewe, bali hata mustakabali wa chama utakuwa mashakani.
Buriani Jumbe. Mungu akupe
pumziko la Amani!
No comments:
Post a Comment