Wakurugenzi
wa Halmashauri zinazotekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (ULGSP)
wametakiwa kuangalia maeneo yote yanayokwamisha utekelezaji wa mradi na
kuyafanyia kazi kwa kuyaboresha ili kuweza kwenda sambamba na muda uliopangwa
kukamilisha utekelezwaji wa mradi huo.
Akifungua
Mkutano wa siku tatu wa kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania
jijini Arusha, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhandisi Mussa Iyombe alisema katika mkutano amegundua kuwa utekelezaji wa
mradi wa ULGSP umechelewa kutekelezwa na hivyo aliwataka Wakurugenzi kuangalia
maeneo yanayokwamisha utekelezaji na kuyatafutia ufumbuzi ili mradi uweze kukamilika
kwa wakati.
“
Katika mkutano huu nimegundua kuwa bado tupo nyuma, tumechelewa katika
utekelezaji hivyo ninaagiza katika mapitio ya mradi yanayofanywa, kuondoa
vikwazo vyote vinavyotuchelewesha ili tuweze kufikia malengo katika miaka
miwili ya utekelezaji wa miradi iliyobakia”Alisema Mhandisi Iyombe.
Alisema
ana Imani kuwa vikwazo vikiondolewa na mradi kutekelezwa vizuri Benki ya Dunia
itatoa fedha nyingine ya kufanyia kazi katika awamu nyingine ya programu na hatimaye mradi huu kuweza kufanyika kwenye
halmashauri zingine.
Akiwasilisha
mada katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mipango Miji wa Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Hante alisema yapo mambo kadhaa yaliyopelekea
miradi ya Uboreshaji Miji Tanzania kukwama yakiwepo masuala ya ucheleweshwaji
wa fedha pamoja na mchakato wa upitishaji wa fedha za manunuzi.
Katika
kutatua changamoto moja ya chanagamoto iliyokuwa ikizikabili halmashauri katika
mchakato wa manunuzi, Serikali sasa imeruhusu Halmashauri katika vikao vyake
vya kisheria kupitisha fedha isiyozidi bilioni moja badala ya Shilingi milioni
50 iliyoruhusiwa awali.
Awali
kabla serikali haijabadili sheria ya manunuzi halmashauri zilitakiwa kuomba
kibali cha kupitisha fedha za matumizi zinazozidi milioni 50 kwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali hali ambayo ilipelekea kuwepo kwa ucheleweshwaji wa
utekelezaji wa mradi.
Wakizungumza
katika kikao hicho baadhi ya Wakurugenzi walioshiriki katika mkutano huo wa
mapitio wamepongeza hatua iliyofanyika katika kuboresha mchakato wa manunuzi kwa kuruhusu Halmashauri kwa kupitia vikao
husika kupitisha fedha isiyopungua bilioni moja badala ya Tsh. Milioni 50
iliyokubaliwa awali.
"Awali
Wakurugenzi walipata taabu kusimamia miradi mbalimbali katika halmashauri zetu
kwasababu mchakato wa sheria
za manunuzi, lakini hivi sasa miradi inayofadhiliwa na benki ya Dunia
itatekelezwa kwa wakati kutokana na serikali kurahisisha mchakato huu wa
manunuzi ". walieleza.
Akifungua
mkutano huo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe aliwasihi
Wakurugenzi wa Halmashauri 18 ambazo zinatekeleza mradi wa ULGSP kuhakikisha
wanatumia fursa hiyo kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na kuainisha
vipaumbele vya miradi ili kutatua
changamoto zilizokuwa zikiwasumbua wananchi kwenye halmashauri zao.
Naye
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Bwana Marx Kamaoni aliishukuru serikali kwa
kuwezesha kuiboresha sheria hiyo ya manunuzi kwani awali mradi huo ulianza
mwaka 2013 lakini ulikumbana na changamoto mbalimbali katika sekta ya manunuzi ingawa licha ya changamoto hizo halmashauri
hizo 18 zilishaanza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara,
vituo vya mabasi, vituo vya malori, machinjio na ukarabati wa sehemu za utupaji
wa taka ngumu.
Naye
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Bibi Jenifa Omolo alisema mradi wa ULGSP umeleta
maendeleo kwa Manispaa ya Songea kwani umewezesha ujenzi wa stendi ya mabasi ya
kisasa inayotarajia kuzinduliwa mwezi huu.
Naye
Mhandisi wa mradi huo, Gilbert Mfinanga ambaye ndiye Msimamizi Msaidizi wa
Mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (ULGSP), alisema mradi huo ulianza mwaka 2013
na unatarajia kumalizika mwaka 2018, utagharimu dola za Kimarekani milioni 255.
Washiriki wa mkutano huo ni
pamoja na Wakurugenzi, Wahandisi, Wachumi, Maafisa Mazingira, Maafisa Maendeleo
ya Jamii, Watunza Hazina wa Halmashauri 18 pamoja na ujumbe kutoka nchini
Uganda wakiongozwa na Waziri wa Nchi Maendeleo ya Miji Bibi Rosemary Najemba.
No comments:
Post a Comment