Na Beatrice Lyimo- MAELEZO
05/05/2016
Dar es Salaam
Msanii wa kizazi kipya Snura Mushi amewaasa wasanii nchini kujisajili katika mamlaka zote zinazosimamia kazi za sanaa ili waweze kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa, kutambulika na kuiendeleza tasnia ya Sanaa nchini.Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam alipokuwa akiomba radhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa sekta zinazosimamia Sanaa nchini na Watanzania kwa ujumla kwa kutokufuata Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika uendeshaji wa Sanaa nchini.
“Tunaomba radhi kwa Serikali, Umma na Watanzania kwa ujumla kwa kosa la kutengeneza, kuzindua na kuweka mtandaoni Video ya udhalilishaji wa wanawake na isiyozingatia maadili ya kitanzania ya muziki unaoitwa Chura” alisema Msanii huyo
Aidha Msanii huyo ameahidi kuwa mfano katika jamii na kwa wasanii wenzake katika masuala yahusuyo kutunza na kufuata maadili na utamaduni wa kitanzania pamoja na sheria za nchini.
Mbali na hayo ameahidi kutekeleza maazimio na maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, BASATA na mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuhusu video ya chura, ambayo ni kuitoa video ya Chura kwenye mtandao wa You Tube, kujisajili BASATA na kuifanya upya video hiyo.
Aprili 4, 2016 Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliifungia video ya muziki wa Chura kutokana na video hiyo kumdhalilisha mwanamke pamoja na tasnia ya muziki kwa kutozingatia maadili na utamaduni wa mtanzania.
No comments:
Post a Comment