Mheshimiwa
Spika, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji amewasilisha maombi ya Fedha
ili Bunge lako Tukufu limuidhinishie Jumla ya Tshs 82 Bilioni (Tshs 42 Bilioni
za Matumizi ya Kawaida na Tshs 40 Bilioni za Maendeleo). Waziri anaomba tumpe
idhini kutumia Fedha hizi ili aanze kutekeleza Mpango wa Pili wa Miaka Mitano
ambao lengo lake kubwa ni kuwezesha Tanzania ya Viwanda. Bajeti ya Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni sawa na 0.3% ya Bajeti nzima ya Serikali ya
mwaka 2016/17.
Mheshimiwa Spika, Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameibua hoja nzito sana kwenye hotuba yake ambazo naamini Serikali hainabudi kuzipatia majibu yanayostahili. Hoja kubwa ni ile inayohusu kuwepo kwa matamko 3 tofauti, yenye tarakimu tofauti kutoka Serikali moja. Mfano uliotolewa ni kufufua Kiwanda cha General Tyre ambapo Vitabu vya Bajeti vinaonyesha kutengwa tshs 150 milioni, randama za Wizara zinaonyesha tshs 500 milioni na mpango wa Maendeleo unaonyesha tshs 2 bilioni zimetengwa. Kisheria za Bajeti, kilichomo kwenye vitabu vya Bajeti ndio kitakachoidhinishwa na Bunge. Kwamba Serikali inataka kufufua Kiwanda cha General Tyre kwa kutenga tshs 150 milioni, ni kichekesho cha karne. Mambo haya yanadhihirisha kuwa Serikali hii haitembei kwenye maneno yake. Wananchi wapatiwe majibu ya uhakika kuhusu masuala haya. Ni muhimu sana Serikali kuhakikisha kuna uratibu miongoni mwa Wizara za Serikali ili kuwa na sauti moja inayokwenda kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameibua hoja nzito sana kwenye hotuba yake ambazo naamini Serikali hainabudi kuzipatia majibu yanayostahili. Hoja kubwa ni ile inayohusu kuwepo kwa matamko 3 tofauti, yenye tarakimu tofauti kutoka Serikali moja. Mfano uliotolewa ni kufufua Kiwanda cha General Tyre ambapo Vitabu vya Bajeti vinaonyesha kutengwa tshs 150 milioni, randama za Wizara zinaonyesha tshs 500 milioni na mpango wa Maendeleo unaonyesha tshs 2 bilioni zimetengwa. Kisheria za Bajeti, kilichomo kwenye vitabu vya Bajeti ndio kitakachoidhinishwa na Bunge. Kwamba Serikali inataka kufufua Kiwanda cha General Tyre kwa kutenga tshs 150 milioni, ni kichekesho cha karne. Mambo haya yanadhihirisha kuwa Serikali hii haitembei kwenye maneno yake. Wananchi wapatiwe majibu ya uhakika kuhusu masuala haya. Ni muhimu sana Serikali kuhakikisha kuna uratibu miongoni mwa Wizara za Serikali ili kuwa na sauti moja inayokwenda kwa wananchi.
Kufungamanisha Sekta ya Viwanda na
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa
Spika, adhma ya nchi yetu kuwa ya Viwanda ni adhma yetu sote. Jambo hili ni
jambo la Maendeleo na halina ushabiki wa kivyama. Tumepitisha Mpango wa
Maendeleo katika Bunge hili na kwa hiyo ni Mpango wa Nchi sio mpango wa vyama
tena. Hivyo sote kwa pamoja tunafanya kazi ya kuhakikisha tunafikia malengo.
Sisi tulio kwenye upinzani jicho letu pamoja na kushauri na kupendekeza ni
kukosoa pale ambapo walio kwenye Serikali wanakosea. Kukosoa ni tendo la
kizalendo na walio Serikalini wawe tayari kukubali kukosolewa ili kuboresha zaidi.
Kwa maoni yangu, kama tusipofanya marekebisho ya kimkakati mapinduzi ya Viwanda
itakuwa ni nyimbo na ngonjera za kisiasa. Watakaoumia ni Wananchi ambao
hawatapata ajira na Serikali yenyewe itakosa kodi kuweza kutoa huduma kwa
wananchi. Kama nilivyosema hapo awali Serikali inahitaji kufanya uratibu ili
kufikia malengo. Sekta ya Viwanda au Maendeleo ya Viwanda yanapaswa
kufungamanishwa na sekta nyengine za uchumi kwa sababu kuna kutegemeana. Kwa
Tanzania unahitaji Sekta ya Kilimo inayokua kwa kasi ili kuzalisha malighafi
kwenye viwanda. Sekta nyingine kama Elimu, Afya, Nishati, Mazingira nk
zinahusiana na Viwanda pia. Kwa leo tutazame Sekta Kilimo na Viwanda kwa
muktadha wa Hotuba ya Waziri wa Viwanda na kulinganisha na Hotuba ya Waziri wa
Kilimo.
Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Kilimo kwa pamoja zinachangia nusu ya Pato
la Taifa ( GDP) na nusu nyingine ni sekta ya Huduma. Nadharia za Uchumi
zinatuambia kuwa Tija ikiongezeka kwenye ya Kilimo inawezesha sekta ya Viwanda
kukua na kisha sekta ya Huduma. Hapa Tanzania na nchi nyengine nyingi za
Afrika, sekta ya huduma iliruka hatua hizi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa
sana kwenye Pato la Taifa. Ndio maana tuna Kitendawili nchini kwetu kuwa Uchumi
unakua lakini umasikini haupungui; ni kwa sababu sekta ya huduma haijiri watu
wengi kama sekta ya Kilimo na hivyo uchumi unaokuzwa na sekta ya huduma ni
nadra kuondoa umasikini. Tanzania bado inapambana na umasikini. Juhudi zote
tunazofanya lengo lake ni kuondoa umasikini kwa watu wetu. Sekta za kuondoa
umasikini ni Kilimo na Viwanda hivyo lazima mikakati ya Serikali iendane na
kufungamanisha haya. Ndio Maana Nchi nyengine Wizara ya Kilimo hujumuisha
uongezaji thamani ( Ministry of Agriculture and Agro-processing ). Hatuhitaji
kufanya hivyo, tunachohitaji ni kufungamanisha. Hata hivyo Serikali imeshindwa
kufanya hivyo katika mwaka wake wa kwanza tu wa Bajeti. Nitaeleza kwa kutumia
changamoto tuliyonayo kuhusu Sukari, Mafuta ya Kula na Nguo.
Mheshimiwa
Spika, Malengo ya Serikali kwenye Viwanda yapo uk.140 ibara ya 191 ya Hotuba ya
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Serikali imepanga kutekeleza mambo 9
na katika mambo yote hayo hakuna hata moja linalohusiana na Viwanda vya
kuzalisha bidhaa zinazohudumiwa na wananchi wengi zaidi kama Sukari na Mafuta
ya kula. Bidhaa hizi ni bidhaa zinazoleta maneno ya kisiasa ndani ya nje ya
Bunge. Nadhani baada ya madawa ya kulevya, bidhaa zenye mizengwe mingi zaidi
katika duru za kisiasa ni Sukari na Mafuta ya kula. Sukari na Mafuta ya kula
imeangusha Mawaziri kadhaa hapa nchini katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Hata hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara haina mkakati kabisa kushughulika na
Bidhaa hizi licha ya uwezo wake wa kutenegenza ajira na kuokoa fedha za kigeni
kuziagiza. Wizara imezungumza kuhusu viwanda vya nguo lakini haijafafanua
changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya nguo nchini na hasusan biashara haramu
ya magendo ya Nguo inayoathiri sana ukuaji wa sekta ya nguo nchini.
Mheshimiwa
Spika, hata hivyo, ukitazama hotuba ya Waziri wa Kilimo ambayo Bunge lako
tukufu limeshapitisha bajeti yake kuna ‘mikakati’ ya kulima Miwa kwa ajili ya
Sukari. Ukurasa wa 44 ibara ya 107 ya Hotuba ya Wizara ya Kilimo na ukurasa wa
25 ibara za 63 na 64 zinaeleza ‘mikakati’ ya kukabiliana na uhaba wa Sukari
nchini. Kiambatanisho namba 6 cha Hotuba hiyo kimeeleza kwa kina changamoto
nzima ya Sukari na miradi inayopaswa kutekelezwa ili kumaliza kabisa suala la
uhaba wa Sukari nchini. Nimejumlisha miradi ile kutoka kona mbalimbali za nchi
na nimekuta ni takribani Hekta 300,000 za kulima Miwa. Kwa Hesabu ya chini ya
wastani wa kuzalisha Sukari kwa kila Hekta, miradi hii ikitekelezwa Tanzania
itaweza kuzalisha Tani 1.5 milioni za Sukari. Ukiondoa Sukari tunayotumia
nchini, ziada itakayouzwa nje inaweza kuliingizia Taifa Fedha za Kigeni USD 500
milioni, sawa na 30% ya malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa sekta ya Viwanda
katika mapato ya Fedha za kigeni ya USD 3bn. Hapo sijaeleza kiwango cha Ajira
kitakachopatikana, ukuaji wa biashara kwenye sekta nyengine na Umeme
utakaozalishwa ( Multiplier effect ).
Mheshimiwa
Spika, swali la kujiuliza, chukulia Wizara ya Kilimo inalima hiyo miwa hekta
300,000 halafu Wizara ya Viwanda haina mpango wa hivyo viwanda, hii miwa
itakwenda wapi? Sio kwamba inapaswa kufungaminisha Kilimo cha Miwa na Viwanda
vya Sukari? Ni kwa nini Wizara 2 zilizo chini ya Serikali moja zinashindwa
kusomana? Baraza la Mawaziri linajadili nini? Ndio maana Rais anajikuta akitoa
matamshi ya Mawaziri barabarani. Suala la Rais kutoa matamko kuhusu Sukari sio
sawa, hii ni Kazi ya Mawaziri maana mnamuexpose Rais. Rais sio mtu wa
kuhangaika na masuala ya kunywa Chai na Uji.
Mheshimiwa
Spika, nashauri Bunge lako tukufu leo lisipitishe Bajeti ya Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji ili Wizara hii ikakae na Wizara ya Kilimo wawianishe
mipango hii na kisha walete hapa Bungeni ndio tupitishe. Sukari ni mfano mmoja
tu katika suala hili. Hebu tumuunge mkono Rais kwa kuwarejesha mezani Wizara
hizi mbili.
Mheshimiwa
Spika, kwenye sukari kuna suala la ‘low hanging fruits’. Hivi tunavyozungumza
kila Mwaka miwa yenye uwezo wa kuzalisha tani 50,000 ya Sukari huoza hapa
nchini uko Kilombero na Mtibwa. Wakulima wanalima miwa mingi kuliko uwezo wa
Viwanda kununua. Bodi ya Sukari inapaswa kutoa leseni ili vikundi vya wakulima
au wawekezaji wadogo wazalishe Sukari. Bodi ya Sukari haijatoa leseni na wala
Serikali haijahamasisha Watanzania kuwekeza kwenye viwanda vidogo vya Sukari
ili kuwezesha miwa yote inayozalishwa kutoa Sukari. Kama hili lingefanyika, leo
tusingekuwa na ukali huu wa uhaba wa Sukari. Waziri wa Viwanda, hii ni ‘low
hanging fruits’.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji wa bidhaa kama Sukari unahitaji vivutio maalumu kutoka
Serikalini. Kule Uganda, Rais Museveni tangu aingie madarakani aliweka vivutio
maalumu kwa Viwanda kama Kakira Sugar ili wazalishe Sukari ya kutosha. Viwanda
vya Sukari Uganda hata umeme hulipiwa na Serikali kwa Asilimia 50 ili kupunguza
gharama za uzalishaji na kuokoa kutokana na ushindani wa Sukari kutoka nje
inayotupwa nchini ( dumping). Subsidies kwa ajili ya kupunguza gharama za
uzalishaji ili kuwezesha kuzalisha Sukari, kutengeneza ajira na kupata faida
nyengine ni jambo ambalo Lazima Serikali ianze kulifikiria. Sisi Kigoma kuna
mtu anataka kuzalisha Sukari tani milioni 1 kwa mwaka. Wizara ya Fedha na
Wizara ya Viwanda wanabishana kuhusu vivutio. Rais anahangaika na kuwafanya
Watanzania wanywe Chai na Uji kwa bei rahisi, Mawaziri wake wanabishana kuhusu
vivutio vya mitambo ya kupanda miwa nakuzalisha Sukari na kuzalisha Umeme.
Serikali, hebu mtawale. Hebu muongoze. Utawala sio kutoa matamshi ya
barabarani. Uongozi ni kufanya maamuzi yanayomaliza shida za wananchi kwa muda
mrefu zaidi na sio matamko ya kupata Kurasa za Mbele za magazeti ya siku moja
au mbili.
Mheshimiwa
Spika, suala la Mafuta ya Kula halina tofauti na suala la Sukari. Ukipanda gari
ukapita njia ya Singida unaona wananchi wamepanga madumu ya mafuta ya Alizeti
wanauza. Nguvu kazi hii ya Wananchi inapotea kwa sababu Serikali imetoa unafuu
mkubwa wa kodi kwa wanaoagiza mafuta ya kula kutoka nje ya Nchi. Leo kodi
kwenye mafuta ya kula kutoka nje ni 18% tu. Tukiendelea hivi tutaendelea
kuwaona wananchi wetu wanapigwa na jua kuuza mafuta ya Alizeti. Tunaposema
mapinduzi ya Viwanda tunataka kumsaidia nani kama sio huyu Mwananchi
anayeshinda juani? Kama tunataka kubadilisha hali ya Wananchi ni lazima
tuwawekee mazingira mazuri. Ni Aibu kubwa nchi hii kuagiza mafuta ya kula
kutoka nje ya nchi. Tunatumia USD 340 milioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula
kutoka nje. Leo hii bei ya lita ya mafuta ya Alizeti ni kubwa kuliko bei ya
lita ya petroli kwenye soko la dunia. Lakini wazalishaji wetu, wananchi wetu
masikini tunawatazama tu tukipita na mashangingi yetu barabarani. Hali hii
lazima ibadilike. Serikali ndio yenye wajibu wa kubadili hali hii kwa kuweka
kodi kubwa zaidi dhidi ya Mafuta ya kula kutoka nje na kuwekeza kwenye viwanda
vya kukamua Mafuta kwa kutumia Alizeti na Mawese.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa wa Kigoma kuna Mradi tunaotaka kuanza wa kupanda Michikichi ili
kuzalisha Mafuta ya Mawese. Tuna mpango wa kila familia 1 kupanda hekta 1 ya
michikichi kwa lengo la kufikia familia 100,000. Uzalishaji huu wa Mawese
unaweza kuondoa kabisa suala la Tanzania kuagiza mawese kutoka nje maana
tutaweza kuzalisha Tani 200,000 za Crude Palm Oil (CPO) kwa mwaka, kuzalisha
ajira nyingi, kupandisha hali ya maisha ya wananchi wakulima na kukuza biashara
nyengine. Tunahitaji watu watakaowekeza kwenye Viwanda vya kuzalisha mawese.
Wizara ya Viwanda ishirikiane na Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha
tunazalisha mafuta ya Kula ya kutosha ili kuondokana na uagizaji huu. Mawese na
Alizeti ndio suluhisho la kudumu la suala la Mafuta ya kula. Bunge liitake
Serikali ikae upya kuandaa Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
ili kuifungamanisha na Bajeti ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa
Spika, Suala la Mwisho ni sekta ya Nguo. Nchi nyingi duniani ambazo
zimefanikiwa kuondokana na umasikini zimetumia sekta ya nguo ( textile
industry). Mnyororo wa thamani wa Sekta ya Nguo ni mrefu kuanzia kwa Mkulima
mpaka kwenye nguo tunazovaa. Hii inapaswa kuwa sekta ongozi kwenye suala zima
la uchumi wa viwanda. Hata hivyo tuna tatizo la Pamba.
Mheshimiwa
Spika, uzalishaji wa Pamba umeporomoka kwa asilimia 47. Tutapata wapi Pamba ya
kulisha viwanda vya nguo? Wizara ya Kilimo na Wizaara ya Viwanda lazima zikae
pamoja ili kuhakikisha kuwa tunafufua zao la Pamba. Vinginevyo nchi hii
itaishia kuagiza pamba kutoka nje au tutajikuta tunaunganisha nguo za kutoka
China tu.
Mheshimiwa
Spika, Viwanda vya Nguo nchini vinapata shida kubwa sana kutokana na magendo ya
nguo. Kuna ukwepaji mkubwa sana wa kodi kwenye bidhaa za nguo zinazoingizwa
hapa nchini na hivyo kuua viwanda vya ndani. Viwanda vinapata shida kubwa ya
matumizi ya Umeme maana umeme hauna uhakika na ni bei kubwa. Matokeo yake
viwanda vingi vinafungwa na watu wetu kukosa ajira. Serikali lazima ifanye kazi
ya ziada ya kuzuia magendo ya nguo vinginevyo viwanda vilivyopo vitakufa na
hakuna atakayekubali kujenga kiwanda hapa nchini kwani atajua kuwa Serikali
haifanyi ziada kuhakikisha tunalinda viwanda.
Mheshimiwa
Spika, hakuna nchi duniani isiyolinda viwanda vyake. Leo Taifa kubwa kama
Uingereza linahangaika na kiwanda cha Chuma na kutaka hata kuingiza mtaji wake
ili kulinda ajira za Wanananchi wake. Tujifunze kwa wenzetu. Kama tunataka
kupata ajira kwa watu wetu ni lazima kulinda viwanda vyetu. Viwanda vya nguo
nchini vipo kwenye tishio kubwa sana kutokana na magendo ya nguo. Serikali
ichukue hatua stahiki. Nguo "zitatutoa" kuanzia kwa mkulima mpaka kwa
wenye viwanda.
Mheshimiwa
Spika, Naomba kutoa hoja kwamba Tuahirishe mjadala wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji ili kuiruhusu Serikali kuwianisha mipango ya Wizara ya
Kilimo na Wizara ya Viwanda. Wakiwa tayari ndio Bunge lije kupitisha
Bajeti ya Wizara hiyo.
Zitto Zubeir Ruyagwa Kabwe
Mbunge Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Mei 9, 2016
No comments:
Post a Comment