Wakulima wa tumbaku wakiwa shambani
Na Hastin Liumba, Tabora
BAADHI ya Vyama vya Msingi vya Ushirika wa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora viko hatarini kufutiwa usajili sanjari na kuzuia uteuzi katika vyama hivyo lengo likiwa kuleta nidhamu katika sekta ya tumbaku.
Hatua hiyo ni kwa vitendo cha kujihusisha na wizi wa tumbaku, utoroshaji au kuuza kinyemelea kwa baadhi ya makampuni.
Akizindua Ofisi ya Association ya Block Farm Kalola, wilayani Uyui, mjumbe wa Bodi ya Tumbaku Nchini, Said Ntahondi, amesema wanataka zao la tumbaku liwe linalimwa na watu waliodhamiria na sio watu wanaotaka kugeuza tumbaku kuwa zao la wezi.
Ntahondi ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui, aliongeza kuwa wakulima wa zao la tumbaku kwa sasa wengi wao hawanufaiki na zao hilo lakini kama mikakati hii itazingatiwa na hatua kali chukuliwa kwa wanaoenda kinyume zao hilo litawanufaisha.
Aidha aliwataka wakulima binafsi maarufu kama IF, kujiepusha na malalamiko mbalimbali yanayotolewa dhidi yao kuwa wanatorosha tumbaku kutoka vyama vya msingi na kujifanya ni mali yao.
Mwenyekiti wa Association ya Block farm, Abdallah Koni alisema wameamua kujenga ofisi yao ili wanachama wao wapate sehemu ya kufanyia shughuli za chama badala ya kuhangaika.
Alieleza kuwa wamepania kuhakikisha wanachama wao wananufaika na zao la tumbaku huku malipo yao wakiwa wanayapata ndani ya wiki zisizodi mbili tangu wauze tumbaku yao sio kama ilivyo sasa kwa wanachama wa vyama vya msingi.
"Tumelenga kumnufaisha mkulima aliye mwanachama wetu kwa kupata malipo ndani ya muda mfupi tofauti na ilivyokuwa wakati tukiwa wanachama wa vyama msingi" alisema.
Aliongeza kuwa lengo la kuanzishwa kwa Association hiyo ni kuwainua wakulima wao kiuchumi ili waendane na soko la ushindani,.
No comments:
Post a Comment