Hassan Rehani Bitchuka
Na Daniel Mbega
NI
Jumapili nyingine wapendwa wasomaji wa blogu hii ambapo wengi wetu tunapumzika
majumbani tukijiandaa kwa siku ya kesho (wale wa ofisini) kwenda kulijenga
taifa.
Karibuni tukumbushane
mambo mbalimbali ya kijamii yanayopatikana kwenye tungo za wanamuziki
mbalimbali. Ni tungo maridhawa ambazo pamoja na kuimbwa miaka mingi iliyopita,
lakini bado ujumbe wake ungali na mantiki kwa jamii yetu.
Leo nakiangalia
kibao cha Chatu Mkali, cha bendi ya
International Orchestra Safari Sound (IOSS) ukiwa ni utunzi wake Hassan Rehani
Bitchuka ambaye aliimba akishirikiana na Muhidin Maalim Gurumo, Skassy
Kasambula, Ali Akida, Dingituka Molay, Tchibanda Sony, Benno Villa Anthony,
Kabeya Badu, Numbi Kileba, Mobali Jumbe, na Deus Mugunda.
Solo katika
wimbo huu ilipigwa na ‘String Master’ Joseph Mulenga, rhythm alipiga Ally
Makunguru na gitaa la bass likaungurumishwa na Charles John 'Ngosha', Emanuel
Zagallo alipiga drums, Mbaraka Rajab alipiga tumba, Ngoie Mubenga na Ibrahim
Mwinchande kwenye trumpet, Saleh Maluu, Kimeza Abdalah na Majengo Suleiman
kwenye Sax (mnaweza kunisahihisha kama mahali nimesahau).
Ngoja niwarejeshe
nyuma kidogo. Hii ilikuwa ni awamu ya pili ya bendi hii ambayo ilikuja
kuimarishwa na Gurumo na Bitchuka pamoja na wapiga ala kama Joseph Mulenga na
Charles John ‘Ngosha’ waliotokea DDC Mlimani Park Orchestra (Sikinde) mwaka
1984.
Mmiliki wa
bendi hiyo, Hugo Kisima, aliamua kuwachukua wanamuziki hao kuimarisha bendi yake
ambayo awali ilikuwa chini ya Maestro Freddie Ndala Kasheba aliyetamba na
mtindo wa Dukuduku na kuleta upinzani
dhidi ya bendi ya Marquiz du Zaire.
Gurumo alipotua
hapo akaanzisha mtindo wa Ndekule na
sasa ushindani ukawa baina ya Sikinde na Ndekule.
Hata utunzi
wa kibao cha Chatu Mkali kinatajwa
kwamba yalikuwa majibu kwa Sikinde ambao walikuwa wametoa kibao cha M.V. Mapenzi 2 kikimponda Gurumo kwa
kuitosa Sikinde ‘Meli ya Wapendanao’.
Pamoja na
vijembe hivyo, lakini ujumbe huu bado ungali na maana kwa jamii yetu ya sasa.
Wapo wanajamii
ambao wana kawaida ya ‘kuwachokoza’ wenzao, kuwabeza na kuwafanyia mambo mengi
mabaya hasa wanapowaona wakimya.
Hivi inakuwaje
ukamfanyia hiyana ndugu ama jamaa yako ambaye mmeazimia kwa pamoja kufanya
jambo. Mnakuwa wote katika dhiki na taabu wakati mnalianzisha, wakati mwingine unatumia
hata rasilimali zako kufanikisha jambo hilo ukiamini kwamba ni lenu pamoja,
lakini mara mambo yanaponyooka ndugu huyu anakudhulumu na kukutelekeza?
Semeni ukweli
ndugu zangu, kama jambo hili halijakutokea wewe, basi limetokea ndugu, jamaa
ama hata jirani yako.
Wanaofanya
hivi wanadharau kwamba, “Aaah, hata nikimfanyia hivi, atanifanya nini?”
Wanasahau kwamba, ndugu hawa nao wana mioyo ya nyama na wana nyongo. Hata kama
hawataweza kulipiza, lakini kamwe hawawezi kukaa kimya, wanaweza kumlilia Mungu
naye akakuadhibu kwa aibu kubwa.
Wengi ambao
wamewatendea unyama wenzao mwisho wao ni mbaya.
Lakini kamwe
hupaswi kuwatendea wenzio ubaya, hasa wale wakimya. Bora hata mtu anayezungumza
ama kujibu mapigo papo hapo kuliko yule ambaye ni mkimya, maana anaweza ‘akakuvizia’
kama afanyavyo chatu, na kuvia kwake ni “kumshtakia Mungu…”
Narudia tena,
katu usimchokoze mtu mkimya, mtu mwema na asiyependa ugomvi, kwa sababu akiamua
kulipiza, utalia! Kamwe huwezi kushinda nakwambia na utaumbuka na kudhalilika
mbele ya jamii inayokuheshimu.
Tazama mashairi
ya kibao hiki:
Chatu mkali kwa nini wamuogopa!
Mnyama asiye kivuli hana mfupa !
Tena jabali awindapo hana pupa!
Apenda
machakani mjini hakuzoea
(repeat x
3)
Hutega njiani usiku amekusudia
Ni mwepesi kubaini adui kumfikia
Usimchezee ndugu utaangamia!
Ukufike mtukutu ujute kuzaliwa
(Chorus)
Usimchezee chatu ohoo! chatu ehee!
Dongo usimtupie, utaukosa ushindi! x 2
[Muhidin
Gurumo]
Natoa onyo kwa yeyote anayechezea chatu ni
hatari
Atakuwa asipate lolote la manufaa
Na ajali imkute bila ya kutegemea!
Atakuja adhirika ajute na Dunia
(Chorus)
Usimchezee chatu ohoo! chatu ehee!
Dongo usimtupie, utaukosa ushindi! x 2
0656-331974
No comments:
Post a Comment