Korongo Taji-kijivu (Grey Crowned Crane).
Na Daniel Mbega (Mhifadhi Asilia)
WATANZANIA wa sasa hawachoki kwa visa. Watakwambia mji una joto au baridi kali, mara watasema foleni zinachosha. Lakini hakuna hata mmoja anayewaza kubadili mazingira hayo yanayomchosha japo kwa muda.
Naam, sehemu pekee ambayo unaweza kupata mawazo mapya ni kwa kutembelea hifadhi zetu za taifa, ambazo ziko 16! Huko utakutana na mazingira ya asili kabisa, upepo mwanana ukivuma usio na vumbi wala moshi wa magari mabovu ya mitumba, mengi yakiwa ya mikopo ya Saccos.
Tunahitaji japo mara moja kwenye kuangalia hizi rasilimali zetu ambazo zimeendelea kuwa vivutio vya wageni kutoka nje kuliko sisi wenyewe. Ni aibu sana.
Hii inatokana na ukweli kwamba, mtaji uliopo ni wa asili kwani kuna vivutio vingi kama wanyama, ndege, mimea na mbuga nzuri ambazo macho ya binadamu yeyote anayependa kubadilisha mtazamo wake yangependa kuvinjari.
Hata hivyo, wananchi wengi wa Tanzania wameonekana kutokuwa na utamaduni kwa kwenda kutembelea vivutio vyetu vya asili vya utalii, badala yake wengi wao wako tayari kununua mikanda mingi ya filamu za Kimagharibi na kupoteza muda mwingi kuangalia.
Hii ni mbaya kwa sababu siyo tu tunawajengea utamaduni mbovu hata watoto wetu, bali tunaikosesha Tanzania mapato ya ndani huku tukijenga hisia mbovu kwamba mbuga za wanyama ziko kwa ajili ya Wazungu pekee, jambo ambalo siyo sahihi.
Tunatambua kwamba watalii kutoka nje wamekuwa wakivifuata vivutio hivi tunavyovielezea hapa, lakini kwa bahati mbaya wengi wetu tumekuwa hatuna utamaduni wa kwenda kutembelea wala kuvitazama vivutio hivyo, hususan katika mbuga za wanyama.
Hatuhitaji kuwa na fedha nyingi sana wala pasipoti au viza kwenda kwenye mbuga zetu za wanyama, bali kiasi kidogo tu kinatosha kabisa kutufikisha huko kama gharama za usafiri, chakula na gharama kidogo tu za kuingilia hifadhini ili kuchangia pato la taifa.
Kwenye hifadhi zetu wamejaa ndege hawa wanaoitwa Korongo, ambao unaweza kuwaita Storks au Cranes kwa jamii zao.
Korongo Domo-ngazi (Saddle-Billed Stork).
Korongo wamegawanyika katika makundi mawili –
wale wa familia ya Ciconiidae
wanaoitwa Storks wenye domo refu na nene. Pia wanafahamika
kama Kongoti, hususan korongo mfuko-shingo. Mabawa yao ni marefu sana ambapo
yale ya korongo mfuko-shingo yana urefu wa meta 3.2, ni marefu kuliko yale ya
ndege wote ghairi ya tumbusi wa Andes (Andean
condor). Spishi nyingine huishi mahali pa majimaji nyingine mahali
pakavu. Hula vyura, samaki, wadudu na nyungunyungu, hata ndege na
wanyama wadogo. Korongo hawa hawawezi kutoa sauti. Lakini kwa tago hupiga
kelele na midomo yao.
Spishi za Korongo wa Familia hii ambazo zinapatikana Afrika ni Korongo Domo-Wazi (African Openbill Stork), Korongo Samawati (Abdim’s Stork), Korongo Mweupe (White Stork), Korongo Shingo-Sufu (Woolly-Necked Stork), Korongo Mweusi (Black Stork), Korongo Domo-Ngazi (Saddle-Billed Stork), Korongo Mfuko-Shingo, Kongoti au Marabu (Marabou Stork) maarufu zaidi kama Ndege Mwarabu, na Korongo Domo-Njano (Yellow-Billed Stork).
Korongo Domo-Wazi (African Openbill Stork)
Korongo Mweupe (White Stork)
Korongo Samawati (Abdim’s Stork)
Korongo Shingo-Sufu (Woolly-Necked Stork)
Korongo Mweusi (Black Stork)
Korongo Mfuko-shingo, Kongoti au Marabu (Marabou Stork) maarufu kama Ndege Mwarabu
Korongo Domo-Njano (Yellow-Billed Stork)
Aina ya pili ya Korongo ni wale wa Familia ya
Gruidae wanaoitwa Cranes ambao pia wanajulikana kama Mana. Hawa wana midomo mifupi na
myembamba kuliko wale wa familia ya Ciconiidae.
Spishi nyingi hutembea kwa mikogo na madoido. Madume hubembeleza jike kwa mbwembwe
huku wakitoa sauti kubwa. Wakikubaliana huishi maisha yao yote. Makorongo hawa hupenda kuwa pamoja
na huhama kwa makundi makubwa. Hula kila kitu kinachopatikana, kama panya,
wadudu watambaao, amfibia au samaki, hata nafaka na matundamadogo. Spishi za
makorongo zinatokea mabara yote ghairi ya Amerika ya Kusini.
Spishi zinazopatikana Afrika ni Korongo Buluu (Blue Crane), Korongo Tumbo-Jeusi (Demoiselle Crane), Korongo Taji-Jeusi (Black Crowned Crane), Korongo Taji-Kijivu (Grey Crowned Crane), Korongo Ndevu (Wattled Crane), na Korongo Paji-Jeusi (Eurasian au Common Crane).
Korongo Buluu (Blue Crane)
Korongo Tumbo-Jeusi (Demoiselle Crane)

Korongo Ndevu (Wattled Crane)
Korongo Paji-Jeusi (Eurasian au Common Crane)
Ndege hawa wanaopatikana katika hifadhi zetu
nyingi nchini kitaalamu ama kisayansi wako katika Himaya ya Animalia (Wanyama), Faila ya Chordata (yaani Wanyama wenye ugwe wa
neva mgongoni), Nusufaila ya Vertebrata
(Wanyama wenye uti wa mgongo), Ngeli ya Aves
(Ndege), Oda ya Ciconiiformes (Ndege
kama makorongo), Familia ya Ciconiidae
na Gruidae, na Jenasi mbalimbali kama
zilivyotajwa hapo juu.
Jamani, nendeni kwenye mbuga za wanyama
mkatazame vivutio hivi, maana vipo kwa ajili yetu na siyo Wazungu tu peke yao
kuja kuangalia.
* Mwenye maoni, au anayewajua ndege hawa kwa
majina ya kienyeji, anitumie kupitia Simu/Whatsapp/Telegram 0656 331974, au e-mail:brotherdanny5@gmail.com.



No comments:
Post a Comment