Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 1 March 2016

TRAFIKI WASIPONGEZWE, FEDHA HIZI ZILIKUWA ZIKIINGIA MIFUKONI MWAO!

WAKATI nikiwa katika mkoa mmoja wa Kanda ya Ziwa nilikutana na kisa hiki ‘laivu’ katika maeneo ya kituo kimoja cha polisi.
Askari mmoja wa kike (WP) alikuwa akilia na wenzake wakijitahidi kumbembeleza, lakini nilipowauliza baadaye wenzake wakasema: “Analia kwa sababu ameondolewa kwenye kitengo.”
Awali sikuelewa, lakini wakanielewesha kwamba, askari huyo alikuwa wa usalama barabarani na sasa ameondolewa na kurejeshwa kwenye dawati la kawaida (General Desk au GD), ambako aliona kama ‘ametupwa’.
Ilinishangaza kuona askari, ambaye wakati anaajiriwa hakuomba kupangiwa kitengo chochote, leo analalamika na kumwaga machozi kwa kuhamishwa kitengo cha trafiki ambacho alipangiwa kutokana na utaratibu wa kazi.
“Wanapata fedha nyingi sana, siyo sisi ambao tuko hapa kwenye madawati…” alisema mmoja wa askari hao wa kike baada ya mwenzao kuondoka.
Mwingine akadakika: “Yule mwenzetu lazima amwage machozi, alikuwa na mikopo mingi mno licha ya kujenga nyumba mbili, sasa anapiga hesabu atalipaje fedha hizo.”
Nimekumbuka kisa hiki baada ya kutolewa kwa taarifa kwamba katika mwezi Februari 2016 pekee, kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kimefanikiwa kukusanya kiasi cha Shs. 1.9 bilioni zikiwa ni malipo ya faini mbalimbali zilizotokana na makosa ya barabarani.
Watanzania wengi walipongeza hatua hiyo ya ukusanyaji wa mapato kupitia jeshi hilo wakilinganisha na kasi ya Serikali ya sasa katika kuhakikisha kwamba kila idara inayohusika inakusanya kodi na mapato kwa ukamilifu.
Lakini wakati watu wengi wanalipongeza jeshi hilo, hakuna anayejishughulisha kuangalia ufanisi wa kikosi cha usalama barabarani katika kusimamia na kutekeleza majukumu yao kama inavyopasa.
Wanashindwa pia kukumbuka matukio na utendaji kazi wa askari wa kitengo hicho katika awamu tatu zilizotangulia, hasa kutokana na ukweli kwamba, ndicho kitengo kinachoongoza kwa rushwa ndani ya jeshi hilo.
Pengine wangewapongeza kwa kuacha kupokea rushwa na kuiibia serikali mapato katika mazingira ambayo pia yanawafanya wenyewe wavunje sharia na kuchochea makossa ya bararabani.
Kwa miaka mingi sasa askari wa kitengo hicho wamekuwa wakilalamikiwa kwa uzembe, rushwa na ufisadi wa hali ya juu huku hali ya usalama barabarani ikiendelea kutia mashaka kutokana na wimbi kubwa la ajali linalosababishwa na askari hao kuacha kazi yao na kufanya kazi ya kukamata magari hovyo.
Fikra Pevu kwa muda mrefu umeandika makala na kuendesha mijadala kupitia mtandao dada wa Jamii Forums kuhusiana na matatizo ya usalama barabarani, hususan suala la askari wa usalama barabarani kujikita katika ukusanyaji wa mapato badala ya kulinda usalama.
Operesheni mbalimbali za kukamata madereva wa magari wanaofanya makosa ya barabarani ambayo daima huendana na utozaji wa tozo za faini, mara nyingi huwaondoa askari hao kwenye majukumu yao ya msingi ya kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Mbinu ya kuotea (off-side trick) ndiyo imekuwa ikitumiwa na askari hao kwani hata kama wataona dereva anakosea hawawezi kumuonya bali wanasubiri atende kosa na kumwajibisha kwa kumlipisha faini, ambazo mara nyingi huwa siyo timilifu kwa sababu hupokea fedha kidogo wanazoziweka mifukoni na hata kama faini ni timilifu, huwa hazifikishwi mahali kunakotakiwa.
Licha ya kuwepo kwa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2011, lakini askari hao wamekuwa hawaizingatii na badala yake kuwalipisha madereva faini hata kwa makosa ambayo wanapaswa kuelekezwa tu.
Fikra Pevu ilipata kufanya mahojiano na baadhi ya askari wa kikosi hicho ambao walijitetea kwamba, wanalazimika kukusanya fedha kwa kila hali kutokana na maelekezo ya wakubwa wao.
“Kila mkoa wa kipolisi jijini Dar es Salaam, kwa mfano, kila askari wa usalama barabarani amepangiwa kukusanya kati ya Shs. 5 milioni na Shs. 10 milioni kwa mwezi… usipotimiza malengo unaondolewa kwenye ‘kitengo’”, askari mmoja alipata kuliambia Fikra Pevu.
Inaelezwa kwamba, kila askari wa usalama barabarani anapaswa kuwasilisha Shs. 150,000 kwa siku kwa makossa matano, kwa kila siku anayokuwa barabarani.
Kwa maana nyingine, askari hao wa usalama barabarani wanajitahidi ‘kutengeneza’ makosa ili waweze kutimiza malengo, lakini pia wanapaswa kupata ziada ili nao wafaidike.
Katika tukio moja, nikiwa nimepanda gari la ofisa mkubwa wa polisi ambaye alikuwa akiendesha mwenyewe, tulisimamishwa ghafla jijini Mwanza na askari wapatao watano. Hawakuweza kumtambua kwa sababu alikuwa katika nguo za kiraia na hakuwa wa mkoani humo.
Askari hao walianza kudai hiki na kile, walipoona hakuna kosa lolote wakampelekea msimamizi wao aliyekuwa na cheo cha Sajini Meja na kutumia takriban dakika kumi wakijadiliana wenyewe kwa wenyewe.
Baada ya ofisa huyo wa polisi, ambaye alikuwa na cheo cha juu kuliko hata msimamizi wao, kujitambulisha, askari wale walihamanika sana maana walikuwa wanatumia mbinu ya kuchelewesha ili ‘kumlazimisha’ mhusika atoe chochote baada ya kutokuwa na kosa.
Mapato makubwa
Kulisifu jeshi la polisi kukusanya mapato hayo siyo sahihi kwa sababu ninaamini hata hayo yaliyowasilishwa ni madogo.
Walichokifanya tu sasa polisi hao ni kwamba, wameogopa ‘kutumbuliwa majipu’, hivyo badala ya kuzifutika mifukoni fedha hizo kama wanavyofanya siku zote, sasa wameamua kuzipeleka mahali stahiki, yaani serikalini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wananchi, askari wengi walio katika kikosi cha usalama barabarani ni matajiri, wana majumba makubwa na vitega uchumi vingi ambavyo haviendani na vipato vyao halali.
Tunaambiwa kwamba, katika miji mingi askari hao wanamiliki vyombo vya usafiri kama daladala na mabasi ya masafa marefu, na mengi kati ya hayo ndiyo yamekuwa yakihusika na makossa ya usalama barabarani lakini madereva wake wamejaa kiburi kwa kuwa vyombo hivyo vya usafiri ni vya ‘wakubwa’.
Matukio kadhaa ya ajali yanatajwa kusababishwa na askari hao hao, ambao katika barabara kuu mara nyingi hujificha vichakani na kukurupuka ghafla kusimamisha magari yaliyo kwenye mwendo kasi na gari linapomshinda dereva matokeo yake ni ajali ambayo huondoa roho za watu wengi wasio na hatia.
Mara nyingi askari hao wamekuwa wakilalamikiwa kwa ‘kulazimisha’ makosa ilimradi tu wahalalishe kupata ‘kitu kidogo’.
Katika matukio ambayo kweli madereva huwa wamefanya makosa, ama magari yenyewe yana kasoro za kiusalama, askari hao wamekuwa wakiyafumbia makosa hayo ili kupata chochote au kwa sababu magari hayo ni ya ‘wakubwa’.
Jambo la kusikitisha ni kwamba, licha ya ‘kitengo’ hicho cha usalama barabarani kuwa na mapato makubwa, askari wamefanya kama mgodi wao wa kuchuma fedha na ndiyo maana wamejilimbikizia mali nyingi zisizoendana na vipato vyao.
Hali hiyo ndiyo inayowafanya askari wengi, wakiwemo wale waajiriwa wapya, kukimbilia kwenye ‘kitengo’ hicho badala ya vitengo vingine ndani ya jeshi hilo kama FFU, anti-robbery, anti-terrorism, homicide, fraud na kadhalika.
Hawataki mikiki mikiki ya kukimbizana na wahalifu wanaotumia silaha, bali madereva ambao wakinyooshewa mkono tu wanaegesha magari pembeni, wanafungua pochi na mambo yanakwisha.
Malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa yanaonyesha wazi kwamba, baadhi ya madereva na makondakta ni mithili ya miungu watu kwa sababu wanafanya watakavyo, hawafuati sheria na taratibu zilizopo katika kuendesha biashara ya usafirishaji.
Katika tukio mojawapo kati ya mengi niliyoyashuhudia, dereva mmoja alikamatwa mapema asubuhi na kutozwa faini ya Shs. 60,000 kwa makossa mawili – kupiga u-turn sehemu isiyostahili na kushusha na kupakia abiria sehemu isiyostahili pia.
Baada ya kupewa adhabu hiyo, dereva yule akasema: “Sasa hapa ni mwendo mdundo, silipi tena faini kwa sababu kila atakayenikamata nitamwonyesha notification hii…”
Katika nchi inayofuata utawala wa sheria, hatua ya madereva kama hawa inaonyesha kiburi, lakini msingi wake mkubwa ukiwa utendaji mbovu wa askari wa usalama wa barabarani.
Madereva wengine wanalalamika kwamba, wamekuwa wakiandikiwa stakabadhi feki zisizo na alama maalum, hatua inayoonyesha kwamba fedha hizo hazifikishwi serikalini bali zinaishia kwa wakubwa wachache pamoja na askari hao.
Suala hili liliwahi kutolewa ufafanuzi na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, ambaye alisema: “Wapo baadhi ya wananchi wanaoamini kuwa fedha zao zinakwenda mifukoni mwa askari kwa sababu hiyo ya kutopewa stakabadhi. Kile kitabu cha notification kimekidhi matakwa yote ya kisheria kupokelea fedha za Serikali kwa sababu stakabadhi anaweza akafoji.”
Akaongeza: “Ni kweli viko (vitabu) vya aina mbili, vipo ambavyo karatasi zake ukiziangalia zina ‘watermark’ ya Serikali ya Tanzania na vipo vitabu ambavyo havina hiyo watermark. Ni makosa yaliyofanyika wakati wa uchapaji. Ninachoomba Fikra Pevu mtusaidie, ni kwamba kama mtaona nakala mbili kwenye kitabu zinazotofautiana namba tupigieni picha mtuletee nasi tutalishughulikia ikiwemo kumchukulia hatua askari wa usalama barabarani anayehusika.
“Inawezekana watu wakatumia mwanya huo kuingiza kitabu chao kwa maana Watanzania wanafanya vitu visivyo na maana, na ilishawahi kutokea huko nyuma, lakini nakuhakikishia kwamba mitandao ya kihalifu ya aina hiyo inapotokea tunaisambaratisha.”
Kwanini sasa?
Jambo ambalo liko wazi ni kwamba, hivi sasa trafiki wameanza kuwasilisha mapato serikalini kwa sababu ya mashine mpya ambazo askari wa kitengo hicho wamepewa.
Mashine za sasa hazidanganyi, kama alivyokiri askari mmoja katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam.
“Kaka mambo yote yako wazi, hakuna kutafuta carbon paper wala nini, nikibonyeza vibaya tu inakula kwangu, kwa sababu inarekodi kila kitu – ni kama zile mashine za wafanyabiashara (EFD),” anasema ofisa huyo.
Kwa hali hiyo ni vigumu kutumia ujanja ujanja kukwepa kuwasilisha mapato serikalini, labda pale ‘wanapokubaliana’ na dereva atoe ‘chochote alichonacho’ katika utaratibu ule wa kizamani, bila kuandikiwa.
Hali hii ndiyo inayofanya niseme kwamba hakuna haja ya kuwapongeza askari hao wa usalama barabarani kwamba wamekusanya fedha nyingi, bali tunapaswa kuwalaani kwa kuwa wameiibia serikali mabilioni ya fedha kwa miaka mingi.
Kama kwa mwezi Februari 2016 tu wamekusanya Shs. 1.9 bilioni, maana yake katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita serikali imepoteza Zaidi ya Shs. 200 bilioni ambazo zilikuwa zikiwanufaisha askari hao wanaolilia kukaa kwenye ‘kitengo’ kwa gharama yoyote.
Lakini kwa upande mwingine, kitendo cha askari wa usalama barabarani kukusanya mapato mengi kwa makosa ya barabarani kinadhihirisha kwamba, bado kuna tatizo kubwa katika usimamizi wa sheria za usalama wa barabarani.
Hatuwezi kufurahia mapato makubwa wakati kila siku tunashuhudia na kusikia ajali nyingi zikitokea kana kwamba hakuna wasimamizi wa usalama.
Mapato wanayokusanya ni kwa wale ambao wameangukia kwenye mikono ya sheria, lakini naamini wapo wengi wanaokiuka na kufanya makossa ambayo ndiyo yanayosababisha hata wimbi la ajali nyingi.
Tutawapongeza Zaidi wakati tutakapoona mapato hayo yanapungua kwa haki, siyo yaingie mifukoni mwao, bali kuona hali ya usalama barabarani imetengemaa na madereva wanazingatia sheria ikiwa ni pamoja na kupungua kwa makosa ya barabarani.
Hili litawezekana ikiwa kutakuwepo na mkakati wa makusudi kabisa na endelevu wa kuwapa elimu watumiaji wa barabara – hususan madereva wa magari na bodaboda – ambao utasaidia kuwapa uelewa wa sheria za usalama barabarani na kuzingatia.
Watumiaji wengine, wakiwemo waenda kwa miguu na abiria wa vyombo vya usafiri, nao wanapaswa kuelimishwa kwa sababu wakati mwingine wanachangia kutokea kwa ajali kwa kuwahimiza madereva waende mwendo kasi ama kuchepuka kwa kuwa tu ‘wanataka kuwahi’.
Ni heri kuchelewa katika ulimwengu huu, kuliko kuwahi katika ulimwengu ujao. Ajali ni janga la kitaifa, lakini uzembe wa askari wa usalama barabarani ni janga kubwa zaidi. 


CREDIT: FIKRA PEVU



No comments:

Post a Comment